ترجمة معاني القرآن الكريم - الترجمة السواحلية - علي محسن البرواني * - فهرس التراجم

XML CSV Excel API
تنزيل الملفات يتضمن الموافقة على هذه الشروط والسياسات

ترجمة معاني سورة: الجاثية   آية:

سورة الجاثية - Surat Al-Jathiyah

حمٓ
H'a Mim .
H'a Mim. Hizi ni harufi mbili katika harufi za kutamkwa, zimeanzia Sura hii kama ada ya Sura nyingi katika Qur'ani ambazo zimeanzia kwa harufi kama hivi ili kuashiria kuwa washirikina wameshindwa kuleta mfano wake, ijapo kuwa hii Qur'ani imeundwa kwa harufi hizi hizi wanazo zitumia katika maneno yao.
التفاسير العربية:
تَنزِيلُ ٱلۡكِتَٰبِ مِنَ ٱللَّهِ ٱلۡعَزِيزِ ٱلۡحَكِيمِ
Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Huu mteremsho wa Qur'ani umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Asiye shindika, Mwenye hikima katika kupanga kwake na kuendesha kwake.
التفاسير العربية:
إِنَّ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِ لَأٓيَٰتٖ لِّلۡمُؤۡمِنِينَ
Hakika katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini.
Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi ni katika ufundi wa namna ya pekee wa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka ni dalili zenye nguvu kabisa katika Ungu wake na Upweke wake, ambao wanauamini wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu kwa maumbile yao yaliyo sawa.
التفاسير العربية:
وَفِي خَلۡقِكُمۡ وَمَا يَبُثُّ مِن دَآبَّةٍ ءَايَٰتٞ لِّقَوۡمٖ يُوقِنُونَ
Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini.
Na vile Mwenyezi Mungu kukuumbeni nyinyi, enyi watu, kama mlivyo, mna sura nzuri, na umbo la peke yenu, na mnavyo khitalifiana baina ya wanaadamu na wanyama na mkaenezwa ulimwenguni, na manufaa mbali mbali, bila ya shaka ni Ishara zenye nguvu na ziwazi kwa watu wanao tafuta yakini ya mambo yao kwa kuzingatia na kufikiri.
التفاسير العربية:
وَٱخۡتِلَٰفِ ٱلَّيۡلِ وَٱلنَّهَارِ وَمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مِن رِّزۡقٖ فَأَحۡيَا بِهِ ٱلۡأَرۡضَ بَعۡدَ مَوۡتِهَا وَتَصۡرِيفِ ٱلرِّيَٰحِ ءَايَٰتٞ لِّقَوۡمٖ يَعۡقِلُونَ
Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya upepo, ni Ishara kwa watu wenye akili.
Na katika kukhitalifiana usiku na mchana, kwa urefu na ufupi, na mwangaza na giza, na kupeana zamu kwa nidhamu iliyo thibiti, na katika mvua anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, akaihuisha ardhi kwa mimea baada ya kufa kwake kwa ukame, na kuziendesha pepo pande mbali mbali nazo zinakhitalifiana kwa ubaridi na joto, na nguvu na udhaifu, ni alama zilizo wazi za kuonyesha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa watu wenye kufikiri kwa akili zao, wakafikilia yakini yao.
التفاسير العربية:
تِلۡكَ ءَايَٰتُ ٱللَّهِ نَتۡلُوهَا عَلَيۡكَ بِٱلۡحَقِّۖ فَبِأَيِّ حَدِيثِۭ بَعۡدَ ٱللَّهِ وَءَايَٰتِهِۦ يُؤۡمِنُونَ
Hizi Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi hadithi gani watakayo iamini baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake?
Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo eleza uumbaji alio ufanya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu. Tunakusomea wewe katika Qur'ani kwa ulimi wa Jibrili, nazo Aya hizo ni za haki. Ikiwa hao hawaziamini hizi basi maneno gani watayasadiki baada ya maneno ya Mwenyezi Mungu, nayo ni Qur'ani na Aya zake
التفاسير العربية:
وَيۡلٞ لِّكُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٖ
Ole wake kila mzushi mwenye dhambi!
Atapata maangamizo makubwa kila anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo mbaya, na mwenye kukithiri madhambi yake kwa kitendo hicho!
التفاسير العربية:
يَسۡمَعُ ءَايَٰتِ ٱللَّهِ تُتۡلَىٰ عَلَيۡهِ ثُمَّ يُصِرُّ مُسۡتَكۡبِرٗا كَأَن لَّمۡ يَسۡمَعۡهَاۖ فَبَشِّرۡهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٖ
Anaye sikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha anashikilia yale yale aliyo katazwa, na anajivuna, kama kwamba hakuzisikia. Basi mbashirie adhabu chungu!
Mzushi kama huyu husikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, nazo zinasema haki tupu. Kisha yeye huendelea na ukafiri wake kwa kutakabari, akaikataa Imani. Hali yake ni hali ya asiye pata kuzisikia Aya. Basi ewe Nabii! Mbashirie, kwa kumkejeli, kuwa atapata adhabu chungu kwa huko kushikilia kwake kitendo kitacho mletea adhabu hiyo.
التفاسير العربية:
وَإِذَا عَلِمَ مِنۡ ءَايَٰتِنَا شَيۡـًٔا ٱتَّخَذَهَا هُزُوًاۚ أُوْلَٰٓئِكَ لَهُمۡ عَذَابٞ مُّهِينٞ
Na anapo kijua kitu kidogo katika Aya zetu hukifanyia mzaha. Watu hao ndio watakao kuwa na adhabu ya kufedhehesha.
Na huyu mwenye inda, akijua kitu kidogo katika Aya za Mwenyezi Mungu huzifanya Aya zote za Mwenyezi Mungu ni kitu cha kufanyia maskhara na mzaha. Wazushi hao wingi wa madhambi watapata adhabu ya kuwadhalilisha kwa kiburi chao.
التفاسير العربية:
مِّن وَرَآئِهِمۡ جَهَنَّمُۖ وَلَا يُغۡنِي عَنۡهُم مَّا كَسَبُواْ شَيۡـٔٗا وَلَا مَا ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِ ٱللَّهِ أَوۡلِيَآءَۖ وَلَهُمۡ عَذَابٌ عَظِيمٌ
Na nyuma yao ipo Jahannamu. Na walio yachuma hayatawafaa hata kidogo, wala walinzi walio washika badala ya Mwenyezi Mungu. Na watapata adhabu kubwa.
Nyuma yao ipo Jahannamu inawangojea, na walicho kichuma duniani hakitawapunguzia hata chembe ya adhabu yake. Wala hiyo miungu ya uwongo walio ifanya ndio ya kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu, haitawakinga na chochote katika adhabu yake. Na wao watapata mateso makubwa, kwa kitisho chake na ukali wake.
التفاسير العربية:
هَٰذَا هُدٗىۖ وَٱلَّذِينَ كَفَرُواْ بِـَٔايَٰتِ رَبِّهِمۡ لَهُمۡ عَذَابٞ مِّن رِّجۡزٍ أَلِيمٌ
Huu ni uwongofu. Na wale wale walio zikataa Ishara za Mola wao Mlezi watapata adhabu inayo tokana na ghadhabu iliyo chungu.
Hii Qur'ani ni ushahidi kaamili wa Haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na hao wanao zikataa hoja zilio kusanywa na Qur'ani zilizo toka kwa Muumba wao na Mlezi wao watapata adhabu kali mno miongoni mwa namna za adhabu.
التفاسير العربية:
۞ ٱللَّهُ ٱلَّذِي سَخَّرَ لَكُمُ ٱلۡبَحۡرَ لِتَجۡرِيَ ٱلۡفُلۡكُ فِيهِ بِأَمۡرِهِۦ وَلِتَبۡتَغُواْ مِن فَضۡلِهِۦ وَلَعَلَّكُمۡ تَشۡكُرُونَ
Mwenyezi Mungu ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili humo zipite marikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.
Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ikutumikieni bahari ili marikebu zipate kwenda juu yake kwa idhini yake, na uwezo wake, zikikubebeni nyinyi na bidhaa zenu, na ili mtafute kutokana na fadhila za Mwenyezi Mungu mali ya baharini kwa kupata manufaa ya ujuzi, na biashara, na jihadi, na zawadi, na uvuvi, na kutoa vyombo, na ili mpate kushukuru neema zake kwa kumsafia Dini Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَمَا فِي ٱلۡأَرۡضِ جَمِيعٗا مِّنۡهُۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَأٓيَٰتٖ لِّقَوۡمٖ يَتَفَكَّرُونَ
Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa watu wanao fikiri.
Na akakudhalilishieni vyote viliomo mbinguni, nyota zenye kung'ara na sayari, na vyote viliomo kwenye ardhi, makulima, mifugo, maji, moto, hewa, na jangwa, vyote hivyo vinatokana na Yeye Mtukufu, ili akuenezeeni manufaa ya uhai. Hakika katika hizo neema zilizo tajwa zipo Ishara zenye kuonyesha kudra yake kwa watu wenye kuzingatia Ishara.
التفاسير العربية:
قُل لِّلَّذِينَ ءَامَنُواْ يَغۡفِرُواْ لِلَّذِينَ لَا يَرۡجُونَ أَيَّامَ ٱللَّهِ لِيَجۡزِيَ قَوۡمَۢا بِمَا كَانُواْ يَكۡسِبُونَ
Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku za Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
Ewe Mtume! Waambie wanao msadiki Mwenyezi Mungu na wanakufuata wewe, wasamehe maudhi yanayo wafikia kutokana na watu ambao hawataraji kuja siku za Mwenyezi Mungu za kuwalipa watu kwa kheri na shari kwa mujibu walivyo.
التفاسير العربية:
مَنۡ عَمِلَ صَٰلِحٗا فَلِنَفۡسِهِۦۖ وَمَنۡ أَسَآءَ فَعَلَيۡهَاۖ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمۡ تُرۡجَعُونَ
Mwenye kutenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kutenda uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu Mlezi.
Mwenye kutenda mema atapata ujira wake na thawabu mwenyewe; na mwenye kutenda uovu basi dhambi za kitendo chake zitamuangukia mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Muumba wenu kwa ajili ya malipo.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ ءَاتَيۡنَا بَنِيٓ إِسۡرَٰٓءِيلَ ٱلۡكِتَٰبَ وَٱلۡحُكۡمَ وَٱلنُّبُوَّةَ وَرَزَقۡنَٰهُم مِّنَ ٱلطَّيِّبَٰتِ وَفَضَّلۡنَٰهُمۡ عَلَى ٱلۡعَٰلَمِينَ
Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu wote.
Ninaapa kwa hakika tumewapa Wana wa Israili Taurati, na hukumu iliomo ndani yake, na Unabii ulio funuliwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na tumewaruzuku kheri namna mbali mbali, na tumewafadhilisha wao katika neema nyingi juu ya viumbe vyote.
التفاسير العربية:
وَءَاتَيۡنَٰهُم بَيِّنَٰتٖ مِّنَ ٱلۡأَمۡرِۖ فَمَا ٱخۡتَلَفُوٓاْ إِلَّا مِنۢ بَعۡدِ مَا جَآءَهُمُ ٱلۡعِلۡمُ بَغۡيَۢا بَيۡنَهُمۡۚ إِنَّ رَبَّكَ يَقۡضِي بَيۡنَهُمۡ يَوۡمَ ٱلۡقِيَٰمَةِ فِيمَا كَانُواْ فِيهِ يَخۡتَلِفُونَ
Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliyo kuwa baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa wakikhitalifiana.
Na tumewapa dalili wazi katika mambo ya Dini yao. Basi haikutokea khitilafu baina yao ila baada ya kwisha wajia ujuzi wa hakika ya Dini na hukumu zake. Na hayo ni kwa uadui na uhasidi tu ulio baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atapambanua baina ya hao wanao khitalifiana Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa wamekhitalifiana.
التفاسير العربية:
ثُمَّ جَعَلۡنَٰكَ عَلَىٰ شَرِيعَةٖ مِّنَ ٱلۡأَمۡرِ فَٱتَّبِعۡهَا وَلَا تَتَّبِعۡ أَهۡوَآءَ ٱلَّذِينَ لَا يَعۡلَمُونَ
Kisha tukakuweka wewe juu ya Njia ya haya mambo, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu.
Tena tukakujaalia wewe, ewe Muhammad, baada ya khitilafu za Watu wa Kitabu (yaani Mayahudi na Wakristo), kuwa ni Mtume wa kwenda Njia iliyo wazi katika mambo ya Dini tuliyo kuwekea wewe na walio kuwa kabla yako miongoni mwa Mitume. Basi ifuate Sharia yako ya Haki, yenye kuthibiti imara kwa hoja na dalili, wala usifuate matamanio ya watu wasio ijua Njia ya Haki.
التفاسير العربية:
إِنَّهُمۡ لَن يُغۡنُواْ عَنكَ مِنَ ٱللَّهِ شَيۡـٔٗاۚ وَإِنَّ ٱلظَّٰلِمِينَ بَعۡضُهُمۡ أَوۡلِيَآءُ بَعۡضٖۖ وَٱللَّهُ وَلِيُّ ٱلۡمُتَّقِينَ
Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni rafiki wa wamchao.
Hakika hao waongo wenye tamaa ya kuwa ati wewe utawafuata wao, hawatoweza kukuondolea hata chembe ya adhabu pindi ukiwafuata. Na hakika wenye kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu husaidiana wao kwa wao katika upotovu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuwasaidia wale wanao mcha, basi hao haitawafikia dhulma ya wenye kudhulumu.
التفاسير العربية:
هَٰذَا بَصَٰٓئِرُ لِلنَّاسِ وَهُدٗى وَرَحۡمَةٞ لِّقَوۡمٖ يُوقِنُونَ
Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao yakinisha.
Hii Qur'ani ulio teremshiwa wewe ni dalili kwa watu kuwaonyesha Dini ya Haki, na uwongofu wa kuwaongoza kwenye njia za kheri, na neema kwa watu wenye kuyakinisha thawabu na adhabu za Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
أَمۡ حَسِبَ ٱلَّذِينَ ٱجۡتَرَحُواْ ٱلسَّيِّـَٔاتِ أَن نَّجۡعَلَهُمۡ كَٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّٰلِحَٰتِ سَوَآءٗ مَّحۡيَاهُمۡ وَمَمَاتُهُمۡۚ سَآءَ مَا يَحۡكُمُونَ
Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama walio amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya wanayo ihukumu!
Bali wanadhani hao walio chuma yanayo chusha katika ukafiri na maasi kwamba tutawafanya kama walio muamini Mwenyezi Mungu na wakatenda vitendo vyema, na hivyo tuwafanye sawa baina ya makundi mawili hayo katika uhai na katika kufa? Hukumu yao ni mbaya mno, ikiwa wanahisi kuwa wao ni sawa na Waumini.
التفاسير العربية:
وَخَلَقَ ٱللَّهُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ بِٱلۡحَقِّ وَلِتُجۡزَىٰ كُلُّ نَفۡسِۭ بِمَا كَسَبَتۡ وَهُمۡ لَا يُظۡلَمُونَ
Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na ili kila nafsi ilipwe yale iliyo yachuma. Nao hawatadhulumiwa.
Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa mujibu wa hikima na nidhamu, ili zidhihiri dalili za Ungu wake na uwezo wake, na apate kulipwa kila mtu kwa alilo tenda, ikiwa kheri au shari. Na wao hawatapunguziwa chochote katika malipo yao.
التفاسير العربية:
أَفَرَءَيۡتَ مَنِ ٱتَّخَذَ إِلَٰهَهُۥ هَوَىٰهُ وَأَضَلَّهُ ٱللَّهُ عَلَىٰ عِلۡمٖ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمۡعِهِۦ وَقَلۡبِهِۦ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِۦ غِشَٰوَةٗ فَمَن يَهۡدِيهِ مِنۢ بَعۡدِ ٱللَّهِۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ
Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?
Ewe Mtume! Umeangalia, ukamwona huyo mwenye kufanya matamanio yake ndiye mungu wake wa kumuabudu, akamnyenyekea, na akamt'ii, na akaiacha Njia ya Haki na hali anaijua, na akaziba masikio yake asisikie waadhi, na moyo wake asiamini Haki, na akabandika vitanga vya macho asione ya kuzingatiwa? Basi nani wa kumwongoa mtu huyu baada ya kwisha puuzwa na Mwenyezi Mungu? Je! Mnaacha kutazama ili msipate kukumbuka?
التفاسير العربية:
وَقَالُواْ مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا ٱلدُّنۡيَا نَمُوتُ وَنَحۡيَا وَمَا يُهۡلِكُنَآ إِلَّا ٱلدَّهۡرُۚ وَمَا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنۡ عِلۡمٍۖ إِنۡ هُمۡ إِلَّا يَظُنُّونَ
Na walisema: Hapana ila huu uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana kinacho tuhiliki isipo kuwa dahari. Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu.
Na walisema wenye kukanya kufufuliwa: Hapana uhai ila huu uhai wa duniani tu tulio nao sasa. Tunaishi na tunakufa. Na hapana nyuma ya hayo uhai baada ya kwisha kufa. Na hapana cha kututeketeza isipo kuwa kupita dahari, yaani zama na wakati. Wala wao hawasemi hayo kwa ujuzi na kuwa na yakini, bali ni kwa kudhania na kukisia tu.
التفاسير العربية:
وَإِذَا تُتۡلَىٰ عَلَيۡهِمۡ ءَايَٰتُنَا بَيِّنَٰتٖ مَّا كَانَ حُجَّتَهُمۡ إِلَّآ أَن قَالُواْ ٱئۡتُواْ بِـَٔابَآئِنَآ إِن كُنتُمۡ صَٰدِقِينَ
Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasemao kweli.
Na ukiwasomea Aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi zenye kuonyesha uwezo wake wa kufufua, huwa hawana hoja ila kusema - kwa kuikimbia haki : Wafufueni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasema kweli katika kudai kuwa kupo kufufuliwa.
التفاسير العربية:
قُلِ ٱللَّهُ يُحۡيِيكُمۡ ثُمَّ يُمِيتُكُمۡ ثُمَّ يَجۡمَعُكُمۡ إِلَىٰ يَوۡمِ ٱلۡقِيَٰمَةِ لَا رَيۡبَ فِيهِ وَلَٰكِنَّ أَكۡثَرَ ٱلنَّاسِ لَا يَعۡلَمُونَ
Sema: Mwenyezi Mungu anakuhuisheni, kisha anakufisheni, kisha anakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu wengi hawajui.
Ewe Muhammad! Waambie: Mwenyezi Mungu amekupeni uhai duniani nanyi hamkuwa chochote, kisha anakufisheni unapo timia wakati wenu. Kisha atakukusanyeni Siku ya Kiyama, na hapana shaka ya kukusanywa huko. Lakini wengi wa watu hawaujui uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, kwa sababu ya mapuuza yao kuzingatia dalili ziliopo. Na huyo Muweza wa hayo pia ni Muweza wa kuwaleta baba zenu.
التفاسير العربية:
وَلِلَّهِ مُلۡكُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۚ وَيَوۡمَ تَقُومُ ٱلسَّاعَةُ يَوۡمَئِذٖ يَخۡسَرُ ٱلۡمُبۡطِلُونَ
Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na siku itapo simama Saa ya Kiyama, siku hiyo wataangamia wenye kushikamana na upotovu.
Na ni wa Mwenyezi Mungu pekee ufalme wa mbingu na ardhi, kwa kuumba, kumiliki, na kupanga. Na itapo fika Saa ya Kiyama, siku hiyo watakhasiri wenye kufuata upotovu.
التفاسير العربية:
وَتَرَىٰ كُلَّ أُمَّةٖ جَاثِيَةٗۚ كُلُّ أُمَّةٖ تُدۡعَىٰٓ إِلَىٰ كِتَٰبِهَا ٱلۡيَوۡمَ تُجۡزَوۡنَ مَا كُنتُمۡ تَعۡمَلُونَ
Na utauona kila umma umepiga magoti, na kila umma utaitwa kwenda soma kitabu chake: Leo mtalipwa mliyo kuwa mkiyatenda.
Ewe unaye semezwa! Utawaona siku itapo fika Saa watu wa kila dini wamekalia magoti kwa khofu waliyo nayo kungojea kuitikia wito. Kila umma utaitwa kwenye daftari la vitendo vyao, na wataambiwa: Leo mtalipwa sawa malipo ya mliyo kuwa mkiyatenda duniani.
التفاسير العربية:
هَٰذَا كِتَٰبُنَا يَنطِقُ عَلَيۡكُم بِٱلۡحَقِّۚ إِنَّا كُنَّا نَسۡتَنسِخُ مَا كُنتُمۡ تَعۡمَلُونَ
Hichi kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyo kuwa mkiyatenda.
Na wataambiwa: Hichi hapa kitabu chetu tulimo sajili vitendo vyenu, nanyi mmekichukua kwa mikono yenu, kinataja juu yenu yale mliyo yatenda kwa ushahidi wa kweli. Hakika Sisi tulikuwa tukiwataka Malaika waandike, ili tupate kukuhasibieni yaliyo tokana nanyi.
التفاسير العربية:
فَأَمَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّٰلِحَٰتِ فَيُدۡخِلُهُمۡ رَبُّهُمۡ فِي رَحۡمَتِهِۦۚ ذَٰلِكَ هُوَ ٱلۡفَوۡزُ ٱلۡمُبِينُ
Ama walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawatia katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi.
Basi ama walio amini na wakatenda vitendo vyema, Mola wao Mlezi atawatia katika Pepo yake. Malipo hayo ndio kufuzu kulio bainika, kulio wazi.
التفاسير العربية:
وَأَمَّا ٱلَّذِينَ كَفَرُوٓاْ أَفَلَمۡ تَكُنۡ ءَايَٰتِي تُتۡلَىٰ عَلَيۡكُمۡ فَٱسۡتَكۡبَرۡتُمۡ وَكُنتُمۡ قَوۡمٗا مُّجۡرِمِينَ
Na ama walio kufuru, wataambiwa: Kwani hamkuwa mkisomewa Aya zangu nanyi mkapanda kichwa, na mkawa watu wakosefu?
Na ama walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake wataambiwa kwa kuwahizi: Kwani hawakukujilieni Mitume wangu? Hamkusomewa Aya zangu, nanyi mkajiona bora hamfai kuikubali haki, na mkawa kaumu ya makafiri?
التفاسير العربية:
وَإِذَا قِيلَ إِنَّ وَعۡدَ ٱللَّهِ حَقّٞ وَٱلسَّاعَةُ لَا رَيۡبَ فِيهَا قُلۡتُم مَّا نَدۡرِي مَا ٱلسَّاعَةُ إِن نَّظُنُّ إِلَّا ظَنّٗا وَمَا نَحۡنُ بِمُسۡتَيۡقِنِينَ
Na ikisemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, na Saa haina shaka, nyinyi mkisema: Hatuijui hiyo Saa, tunadhania dhana tu, wala hatuna yakini.
Enyi mnao kanya kufufuliwa! Akikwambieni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba agano la Mwenyezi Mungu la kuwalipa ni haki yenye kuthibiti, na Saa haina shaka itakuja, nyinyi mkisema: Sisi hatujui chochote khabari ya hiyo Saa ya Kiyama, wala ukweli wake; na sisi ni dhana ya kudhania tu kuwa hiyo Saa itakuja, wala hatuna yakini kuwa itatokea.
التفاسير العربية:
وَبَدَا لَهُمۡ سَيِّـَٔاتُ مَا عَمِلُواْ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُواْ بِهِۦ يَسۡتَهۡزِءُونَ
Basi ubaya wa waliyo yatenda utawadhihirikia, na yatawazunguka waliyo yafanyia maskhara.
Na utawadhihirikia hawa makafiri ubaya wa vitendo vyao, na itawateremkia jaza ya maskhara yao waliyo kuwa wakizifanyia Ishara za Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
وَقِيلَ ٱلۡيَوۡمَ نَنسَىٰكُمۡ كَمَا نَسِيتُمۡ لِقَآءَ يَوۡمِكُمۡ هَٰذَا وَمَأۡوَىٰكُمُ ٱلنَّارُ وَمَا لَكُم مِّن نَّٰصِرِينَ
Na itasemwa: Leo tunakusahauni kama nyinyi mlivyo sahau mkutano wa siku yenu hii; na mahali penu ni Motoni, wala hamna wa kukunusuruni.
Na wataambiwa hawa washirikina kwa kuwahizi: Leo hii tunakuacheni katika adhabu kama nyinyi mlivyo acha kujitayarisha kukutana na Mola wenu Mlezi katika siku hii kwa ut'iifu na vitendo vyema. Na pahala penu pa kukaa ni Motoni, na wala hamna wa kukunusuruni akakuokoeni na adhabu yake.
التفاسير العربية:
ذَٰلِكُم بِأَنَّكُمُ ٱتَّخَذۡتُمۡ ءَايَٰتِ ٱللَّهِ هُزُوٗا وَغَرَّتۡكُمُ ٱلۡحَيَوٰةُ ٱلدُّنۡيَاۚ فَٱلۡيَوۡمَ لَا يُخۡرَجُونَ مِنۡهَا وَلَا هُمۡ يُسۡتَعۡتَبُونَ
Hayo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu; na maisha ya dunia yakakudanganyeni. Basi leo hawatatolewa humo wala hao hawatakubaliwa udhuru wao.
Adhabu hiyo imekuteremkieni kwa sababu ya ukafiri wenu, na maskhara yenu kuzifanyia Ishara za Mwenyezi Mungu, na mlivyo khadaika na maisha ya dunia kwa mapambo yake. Basi leo hapana yeyote awezaye kuwatoa hawa kwenye Moto, wala hawatakikani kumtaka radhi Mola wao Mlezi kwa kutafuta udhuru.
التفاسير العربية:
فَلِلَّهِ ٱلۡحَمۡدُ رَبِّ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَرَبِّ ٱلۡأَرۡضِ رَبِّ ٱلۡعَٰلَمِينَ
Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mbingu, na Mola Mlezi wa ardhi, na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Basi ni za Mwenyezi Mungu pekee sifa njema, Muumba mbingu na ardhi, na Muumba wa viumbe vyote. Kwani hivi kuwa ni Mola Mlezi wa kila kitu unawajibika uhimidiwe kwa neema zote.
التفاسير العربية:
وَلَهُ ٱلۡكِبۡرِيَآءُ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۖ وَهُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡحَكِيمُ
Na ukubwa ni wake Yeye tu, mbinguni na katika ardhi, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Na ni wake Yeye, Subhanahu, utukufu na utawala katika mbingu na ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, asiye shindika, Mwenye hikima, asiye kosea katika hikima yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote.
التفاسير العربية:
 
ترجمة معاني سورة: الجاثية
فهرس السور رقم الصفحة
 
ترجمة معاني القرآن الكريم - الترجمة السواحلية - علي محسن البرواني - فهرس التراجم

ترجمة معاني القرآن الكريم إلى اللغة السواحلية، ترجمها علي محسن البرواني.

إغلاق