HII NI SURA Tuliyo iteremsha na tukailazimisha; tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.
Sura hii tumeifunua na tumewajibisha hukumu zake, na tumeteremsha ndani yake dalili zilizo wazi za kuthibitisha uwezo wa Mwenyezi Mungu na upweke wake, na kwamba Kitabu hichi kinatoka kwake, ili mpate kuwaidhika.
Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini.
Na miongoni mwa hukumu hizo ni hukumu ya mwanamke na mwanamume wenye kuzini. Basi kila mmoja wao mpigeni fimbo mia. Wala huruma kwao isikuzuieni kutimiza hukumu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Kwani yanayo takikana na Imani ni kukhiari kumridhi Mwenyezi Mungu kuliko kuwaridhi watu. Na wahudhurie baadhi ya jamaa Waumini waone hiyo adhabu inavyo tekelezwa, ili adhabu hiyo iwatishe wenginewe wasitende hivyo.
Mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo ya. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke meharimishwa kwa Waumini.
Mwanamume muovu aliye zoea uzinifu hapendi kumwoa ila mchafu anaye zini au mshirikina. Na mwanamke mchafu ambaye kazi yake ni uzinifu hapendelei kuolewa ila na mchafu anaye zini;au mshirikina. Na ndoa namna hii haiwaelekei Waumini, kwa kuwa imeshabihi fiski na kupelekea kutuhumiwa. Haya ikiwa haikupita toba. Na tafsiri ya haya ni kuwa inabainishwa tabia za washirikina au wazinifu kuwa wao hawapendi ila mambo ya ufisadi tu. Na kwa mujibu wa maoni ya Hambali na Ahli-Dhaahir (na pia Ibadhi) haisihi ndoa ya mwanamume mzinifu au mwanamke mzinifu kabla ya toba.
Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu .
Na wanao watuhumu wanawake wenye hishima zao wasio na makosa kwa tuhuma ya uzinzi bila ya kuleta mashahidi wane wa kuthibitisha tuhuma yao, waadhibuni kwa kuwapiga fimbo thamanini, na wala ushahidi wao usikubaliwe tena kwa jambo lolote muda wa uhai wao. Basi hawa ndio wanao faa kuitwa kwa jina la walio toka vibaya kwenye mipaka ya Dini. Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 2-4 " Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo yameharimishwa kwa Waumini. Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu." Makosa katika Sharia ya Kiislamu ni mambo yaliyo harimishwa na Mwenyezi Mungu akayakemea kwa kuyawekea adhabu au izara ya kufedhehesha. Na maharimishwa hayo ama ni kutenda kilicho katazwa kukitenda, au kuacha kutenda kilicho amrishwa na Sharia kutendwa. Na sababu ya kuharimishwa haya yaliyo katazwa ni kuwa hayo ni kupiga vita moja katika maslaha yanayo kubaliwa katika Uislamu. Na maslaha hayo yanayo kubaliwa ni matano, nayo ni: 1. Kuhifadhi nafsi. 2. Kuhifadhi Dini. 3. Kuhifadhi akili. 4. Kuhifadhi mali 5. Kuhifadhi hishima. Kuuwa kwa mfano ni kuipiga vita nafsi. Na kurtadi, kutoka katika Uislamu, ni kuipiga vita Dini. Na kutumia vinavyo levya ni kuipiga vita akili. Na wizi ni kuyapiga vita mali. Na uzinzi ni kuipiga vita hishima. Na wanazuoni wa ilimu ya Fiqhi (Sharia) wameyagawa makosa sehemu mbali mbali. Lakini sisi yatutosha kwa sababu ya kueleza Aya hizi kugawa kwa mujibu wa uzito wa adhabu zake, na namna ya kiasi chake. Nayo yamegawika mafungu matatu: 1. H'udud, yaani Adhabu. 2. Kisasi au Diya 3. Izara, au Fedheha. Ama H'udud, au Adhabu, ni makosa ambayo yanaonekana kuwa yanaingilia kuvunja Haki ya Mwenyezi Mungu, au kuwa Haki ya Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi ndani yake kuliko haki ya binaadamu. Na kwa hivyo ndio Mwenyezi Mungu akaiwekea MIPAKA ndio maana khasa ya H'udud. Kaiwekea mipaka adhabu yake katika Qur'ani au katika Sunna za Mtume s.a.w. Ama makosa ya Kisasi na Diya ni makosa ambayo baadhi kubwa yake yamewakhusu wenyewe waja. Mwenyezi Mungu amewekea adhabu za baadhi yake katika Qur'ani au katika Sunna za Mtume s.a.w., na amewaachilia mengine wapime wenyewe wenye madaraka. Mfano wa hayo makosa ya kumwaga damu, kama kuuwa na kukata viungo, na kujuruhu. Ama makosa ya Izara, Uislamu umejitosheleza kwa kutaja mwisho wa ukali na mwisho wa upole katika adhabu zao, na kuachia yaliyo baki wenye kutawala wahukumie kwa kila kosa kwa mujibu wa hali na zama yanapo tokea makosa. Makosa ya H'udud ni saba: 1. Uzinzi. 2. Kuzulia wanawake mahashumu wasio na makosa. 3. Udhalimu. 4. Wizi. 5. Uharamia. 6.Ulevi. 7. Kurtadi. (Kutoka katika Uislamu). Mwenyezi Mungu ameyawekea mipaka yote makosa hayo na ameyaleta kwa hisabu yake katika Qur'ani, kama alivyo wekea adhabu zake katika Qur'ani vile vile, isipo kuwa adhabu ya mwenye kuzini naye amewahi kuoa, yaani Zaani Muh's'an, ambaye hupigwa mawe, na mlevi na adhabu yake ni fimbo thamanini, na adhabu ya mwenye kurtadi ambaye jaza yake ni kuuwawa. Hayo yamekuja katika Sunna. Na zimezoea hizi kanuni za kuundwa na watu katika kupinga makosa ya uzinzi kwa adhabu khafifu kama vile kifungo, hata ndio uchafu ukaenea kati ya watu, na fiski na ukahaba ukazagaa, na hishima zikapotea, na maradhi yakakithiri, na nasaba za ukoo zikachanganyika. Katika jambo la ajabu ni kuwa hizi kanuni za kisasa za nchi zinazo ambiwa za kistaarabu ndio zinazo yalinda makosa haya. Katika kanuni za adhabu za Kifaransa, kwa mfano, wazinzi wasio oa wala kuolewa hawapati adhabu yoyote maadamu wao wakiwa wamekwisha fikilia utu uzima. Kwa kuwa ati uhuru wao wa binafsi unataka waachiliwe wajifanyie wenyewe watakalo. Ama mzinzi mwanamume aliye na mke, au mwanamke mwenye mume, basi huyo adhabu yake ni kifungo. Lakini mwana sharia wa serikali haingii kuchunguza ila akipata mashtaka kutokana na mume au mke. Na inaonyesha kuwa ni haki ya mume tu kuwa hilo kosa limetokea au la, kwani ikiwa yeye ndiye aliye fikisha mashtaka, basi yeye anaweza kuyafuta pia, na uchunguzi utasita. Na yeye anaweza kumsamehe mkewe akatoka gerezani kabla ya kutimiza muda wa kifungo chake ijapo kuwa hukumu ilikuwa ni juu yake huyo mwanamke mwishoni. Na wapo baadhi ambao ati wanaushutumu Uislamu kwa ukali wake kushadidia kwake kuadhibiwa wazinifu. Yaliyo elekea zaidi ni kuwa lau wangeli zingatia kuwa kama ilivyo kuwa adhabu ni kali, hali kadhaalika umeshadidiwa ushahidi kwa jambo hili. Kwani ijapo kuwa katika kosa la mauwaji yatosha ushahidi wa mashahidi wawili waadilifu, katika uzinzi ni lazima wapatikane mashahidi wane waadilifu walio ona kitendo hicho kwa macho yao, au aungame mkosa! Hayo, na tunaona kuwa Qur'ani Tukufu imelazimisha kuwa kupigwa hizo fimo kuwe jahara ili mkosa ajuulikane, na iwe ni onyo kuwakhofisha wenginewe.
Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
Lakini mwenye kutubu katika wao akajuta kwa maasi yake, na akaazimia kuwa mt'iifu na kuonyesha ukweli wa toba yake kwa kwenda kwake mwendo mwema, basi Mwenyezi Mungu atamsamehe kumuadhibu.
Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
Na hao wanao watuhumu wake zao kuwa wamezini na hawana mashahidi wanao takikana kushuhudia ukweli wa tuhuma yao, basi anatakikana mmoja wa hao kama anataka isimpate adhabu, ashuhudie kwa Mwenyezi Mungu mara nne kuwa yeye ni mkweli katika hiyo tuhuma yake.
Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyu mume ni miongoni mwa waongo.
Baada ya haya mwanamke akinyamaza kimya itampasa kupata adhabu ya uzinzi. Ili kujikinga na adhabu yampasa ashuhudie kwa Mwenyezi Mungu mara nne kwamba mumewe ni mwongo kumtuhumu yeye kwa uzinzi.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni fadhila na akakurehemuni, na kuwa Yeye ni Mwingi wa kukubali toba za waja wake, na Mwenye hikima katika vitendo vyake vyote, asingeli kufanyieni sharia za hukumu hizi, na angeli fanya haraka kukuadhibuni duniani kwa maasia.
Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyo yachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa.
Hakika hao walio zua uwongo ulio potoka na kila uwongofu kumzulia Aisha, mke wa Nabii s.a.w. walipo mtangazia uzushi, ni kikundi wanao ishi pamoja nanyi. Msidhani kituko hichi ni shari kwenu, bali ndiyo kheri yenu; kwa sababu kimewapambanua baina ya wanaafiki na Waumini wa kweli. Na ukadhihiri ukarimu wa walio wema na wenye kuingiwa na uchungu. Na kila mtu katika hawa walio tuhumu watapata malipo yao kwa mujibu wa kadri alivyo shiriki katika uzushi huu. Na mkuu wa kikundi hichi ndiye ataye pata adhabu kubwa kwa ukubwa wa makosa yake.
Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
Ilikuwa inavyo takikana kwa Imani ni kuwa wakati wa kusikia huu uzushi, ni Waumini wanaume na wanawake wajidhanie nafsi zao kheri ya usafi na unadhifu, na waseme kwa kupinga: Huu ni uwongo ulio wazi umezuliwa, kwa kuwa haya yamemkhusu bora ya Mitume na bora ya wanawake walio wa kweli.
Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo.
Je! Hao wazushi walileta mashahidi wane wa kushuhudia hayo waliyo yasema? Hawakufanya hayo...Na ikiwa hawakufanya basi hao kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu ni waongo.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyo jiingiza.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni fadhila kwa kubainisha hukumu, na hakukurehemuni duniani kwa kuacha kuleta adhabu kwa haraka, na Akhera kwa kukusameheni, angeli kuteremshieni adhabu kubwa kwa sababu ya kujiingiza kwenu katika uzushi huu.
Mlipo yapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa.
Mmezichukua khabari hizo kwa ndimi zenu na mkazieneza kati yenu. Wala nyinyi hamkujua kuwa hizo ni khabari za kweli, na mkaona jambo hili ni dogo si la kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu, au sana adhabu yake ni ndogo; na ilhali ni jambo kubwa kweli la kuadhibiwa adhabu kali na Mwenyezi Mungu.
Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!
Yanayo faa ni kuwa baada ya kusikia maneno haya ya uwongo ni kuambizana msiyazungumze, kwa sababu si laiki yenu, na mustaajabie kuzuliwa uwongo muovu wa namna hii wa khatari.
Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!
Na hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni msirudie tena kufanya maasi namna hii kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini wa kweli. Kwani sifa za Imani zinapingana na mwendo huu.
Na Mwenyezi Mungu anakubainisheni Aya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
Na Mwenyezi Mungu anakuteremshieni Aya zenye kuonyesha hukumu kwa uwazi dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa Ujuzi, hapana asicho kijua katika vitendo vyenu. Naye ni Mwenye hikima kwa kila anacho kitungia sharia na kukiumba. Kwani kila sharia zake na uumbaji wake ni kwa mujibu wa hikima.
Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
Hakika hao wanao penda kutangaza machafu, wakayatangaza baina ya Waumini watapata adhabu yenye kutia uchungu duniani kwa mateso yaliyo kwisha pasishwa, na Akhera watatiwa Motoni ikiwa hawato tubu. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zenu zote, za dhaahiri na zilizo fichikana. Na nyinyi hamjui anayo yajua Yeye.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake kwenu, na kuwa Yeye ni Mwingi wa upole, Mkunjufu wa rehema, asingeli kubainishieni hukumu, na angeli kuleteeni mateso kwa haraka hapa duniani kwa maasi yenu.
Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Enyi mlio amini! Hifadhini nafsi zenu kwa Imani. Wala msimfuate Shetani anaye kuvutieni kwenda tangaza uchafu na maasi baina yenu. Na mwenye kumfuata Shetani basi huyo amekwisha a'si, kwani Shetani anaamrisha madhambi makubwa makubwa na maasi mabaya. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake kwenu kwa kubainisha hukumu na kukubali toba ya wenye kuasi asinget'ahirika hata mmoja wenu na uchafu wa maasi. Lakini Mwenyezi Mungu anamsafisha mwenye kumuelekea Yeye kwa kumwezesha kuwa mbali na maasi, au kwa kumsamehe kwa kutubu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia kila kauli, Mwenye kujua kila kitu, na atakulipeni kwayo.
Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa jamaa zao na masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Wala wasiape wema wenu wenye nafasi kuwa watazuia kuwafanyia hisani jamaa zao na masikini na walio hama makwao katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wengineo kwa sababu za kibinafsi, kama vile kuwa wamewatendea uovu fulani. Lakini inatakikana wawasamehe na wayaachilie mbali makosa yao. Na ikiwa mnapenda Mwenyezi Mungu akusameheni maovu yenu basi wafanyieni wanao kufanyieni mabaya mfano wa anavyo kufanyieni nyinyi Mola wenu Mlezi. Na fuateni mwendo wake kwani Yeye ni Mkunjufu wa kusamehe na kurehemu. Aya hii imeteremka pale Abu Bakar r.a. alipo apa kumkatia msaada jamaa yake Mist'ah bin Uthaathah hapo alipo ingia Mist'ah katika uzushi alio zuliwa bibi Aisha r.a.
Hakika wanao wasingizia wanawake, wanao jihishimu, walio ghafilika, Waumini, wamelaaniwa duniani na Akhera, nao watapata adhabu kubwa.
Hakika hao wanao wasingizia wanawake wema walio safi, ambao hawadhaniwi hayo, bali wao kwa kumshughulikia Mwenyezi Mungu hata wameghafilika na hayo wanayo singiziwa, Mwenyezi Mungu atawatenga mbali na rehema yake katika dunia na Akhera, na watapata adhabu kubwa ikiwa hawatotubu.
Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
Adhabu hiyo itakuwa Siku ya Kiyama ambapo itakuwa hapana njia ya kuikataa. Bali waliyo yatenda yatathibiti juu yao, kwa kuwa zitawashuhudia ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao, kwa madhambi yote waliyo yatenda. Na hayo ni kwa kudhihiri athari ya vitendo vyao juu ya viungo hivyo, au kwa kutamkishwa na Mwenyezi Mungu ambaye anatamkisha kila kitu.
Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki Iliyo Wazi.
Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iliyo kwisha hukumiwa wapewe kwa ukamilifu wake bila ya upungufu. Na hapo wataujua kwa ujuzi wa yakini Ungu wa Mwenyezi Mungu na hukumu za Sharia yake, na ukweli wa ahadi yake na kitisho chake. Kwani yote hayo yatakuwa wazi hayana kificho.
Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.
Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na kadhaalika wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Basi yamkini vipi kuwepo uwovu katika wema ulio hifadhiwa nao ni mke wa mwema muaminifu Mtume Mtukufu s.a.w.? Na wema hawa wamehifadhika na tuhuma wanazo wasingizia hao waovu. Na wao wana maghfira ya Mwenyezi Mungu kwa vijidhambi vidogo vidogo ambavyo mwanaadamu hakosekani kuwa navyo. Na watapata ukarimu mkubwa wa kupata neema za Peponi.
Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka.
Enyi mlio amini! Msiingie katika nyumba zisio kuwa zenu ila baada ya kutaka idhini kwa wakaazi wake na mkaruhusiwa kuingia, na baada ya kuwatolea salamu wakaazi wake - na salamu ni bora kwenu kuliko kuingia tu bila ya kutoa salamu. Na Mwenyezi Mungu amekuwekeeni sharia hii ili mpate kunasihika na muifuate.
Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda.
Na ikiwa katika hizo nyumba hamkumkuta mtu wa kukupeni idhini basi msiingie mpaka aje wa kukuruhusuni. Na ikiwa hakukuruhusuni na akakutakeni mrudi nyuma, basi rudini; wala msishikilie kutaka ruhusa ya kuingia. Kwani kurejea nyuma ni hishima zaidi na usafi zaidi kwa nafsi zenu. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zenu zote na atakulipeni, basi msende kinyume na uwongozi wake.
Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisio kaliwa ambazo ndani yake yamo manufaa yenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yadhihirisha na mnayo yaficha.
Na mkitaka kuingia nyumba za umma zisio kaliwa na watu makhsusi na ndani yake zipo haja zenu, kama vile maduka, mahoteli, nyumba za ibada, hapana ubaya kuingia bila ya kutaka ruhusa. Na Mwenyezi Mungu anajua kwa ujuzi wa timamu kabisa vitendo vyenu vyote vya dhaahiri na vilivyo fichikana. Basi tahadharini na kwenda kinyume naye.
Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za wanayo yafanya.
Ewe Nabii! Waambie Waumini katika yanayo pelekea zina na kutilisha shaka, wasitazame yanayo harimishwa kutazama, nayo ni tupu za wanawake na sehemu za uzuri wao, na wanaume wahifadhi tupu zao kwa kuzisitiri na kuto zitumilia kwa njia isiyo ruhusiwa na Sharia. Adabu hiyo ndio ina hishima zaidi na safi zaidi kwao wasiingie katika maasi na tuhuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua baraabara yote wayatendayo, na atakuja walipa kwayo.
Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.
Vile vile ewe Nabii, waambie wanawake Waumini, wanaamrishwa waache kutazama yaliyo harimishwa, na wazihifadhi tupu zao kwa kuzisitiri na kutoingiliwa ila kwa njia ya Kisharia. Na wasiwaonyeshe wanaume ya kuwavutia katika uzuri wa umbo lao na mapambo, kama kifua, mabega, vidani, isipo kuwa yale tangu hapo yamedhihiri, kama uso na mikono. Na ewe Nabii! Watake hao wanawake wajisitiri mwahali zilipo funuka nguo, kama shingo na kifua. Na hayo kwa kuteremshia vitambaa vya kichwani. Na wasiachilie kuonekana uzuri wao ila kwa waume zao, na jamaa ambao ni haramu kuoana nao milele, kama baba zao, au baba za waume wao, au watoto wao, au watoto wa waume zao kwa wake wengine, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao. Na mfano wa hawa ni wanawake wenzao, sawa sawa wakiwa waungwana au wajakazi, na wanaume wanao ishi nao na hawana tena haja ya wanawake kwa ukongwe. Na kadhaalika watoto wadogo ambao hawajafikilia miaka ya kutamani. Na pia watake wanawake wasifanye vituko vya kutaka kuwavutia wanaume kama kugonga miguu chini ili isikilizane milio ya mitali na kugesi iliyo fichikana ndani ya nguo. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, kwa mlivyo iacha amri ya Mwenyezi Mungu. Na shikamaneni na adabu za Dini mpate kuongokewa katika dunia na Akhera yenu.
Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.
Na saidieni katika kujitenga na zina na yanayo pelekea zina, kwa kuwaoza ambao bado hawajaoana miongoni mwa wanaume wenu na wanawake wenu, na walio kuwa wanafaa kwa hayo katika watumwa wenu. Na wala umasikini usiwe sababu ya kuzuilia kuoa. Kwani Mwenyezi Mungu atasahilisha njia za maisha mazuri kwa mwenye kutaka kuishi maisha safi. Na fadhila za Mwenyezi Mungu ni kunjufu, na Yeye anajua kabisa niya za watu, na kila lipitalo katika ulimwengu.
Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Na ambao hawakupata uwezo wa fedha za kuolea basi wafuate mojapo wa njia nyengine kama saumu na riyadha na kazi za kutumia akili . Kwa hayo hujikurupusha mpaka Mwenyezi Mungu akawafungulia kwa fadhila zake zitakazo wawezesha kuoa. Na watumwa ambao wanataka kuandikiana nanyi ili wapate uhuru wao ni waajibu juu yenu kuwakubalia walitakalo, mkijua kuwa watatimiza kutekeleza na wanaweza. Na juu yenu kuwasaidia waweze kutimiza walio andikiana nanyi, na hayo ama ni kwa kuwapunguzia shuruti mlizo andikiana nao, au kwa kuwapa mali katika mali aliyo kuneemesheni Mwenyezi Mungu, mkawapa katika Zaka au Sadaka. Na ni haramu juu yenu kuwafanya vijakazi vyenu njia ya pato la duniani rakhisi kwa kuwafanya makahaba, na mkawalazimisha kwa hayo. Na vipi mnakwenda kumlazimisha uchafu anaye taka kuwa safi? Na mwenye kuwalazimisha, basi Mwenyezi Mungu humsamehe mwenye kulazimisha pindi akitubu kwa dhambi zake za kulazimisha. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema. Haya yanaelezwa na kauli ya Mtume s.a.w.: "Enyi vijana! mwenye kuweza kuwoa na aoe kwani hivyo linalindwa jicho, unahifadhiwa utupu. Asiye weza na afunge, kwani hivyo ni kinga yake."
Na kwa yakini tumekuteremshieni Ishara zilizo wazi na mifano kutokana na walio tangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu.
Na Sisi tumekuteremshieni katika Sura hii na nyenginezo Aya zilizo wazi zenye kubainisha hukumu. Na tumekuteremshieni mifano ya hali mbali mbali za walio tangulia, na uwongozi, na mawaidha ambayo kwayo watapata faida wenye kumkhofu Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha Nuru ya katika mbingu na ardhi. Yeye ndiye Mwenye kunawirisha vyote hivyo kwa nuru yote tunayo iona na tukenda ndani yake, na ya maana, kama Nuru ya Haki na uadilifu, na ilimu, na fadhila, na uwongofu, na Imani, na kwa ushahidi na athari kama alivyo waahidi viumbe vyake, na kwa vyote vinavyo onyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, na vikalingania Imani kumuamini Yeye Subhanahu. Na mfano wa Nuru yake Tukufu na dalili zake zilizo zagaa kwa uwazi ni kama mfano wa Nuru ya taa yenye kung'aa kwa ukali kabisa, iliyo wekwa kwenye shubaka la ukutani ili kuukusanya mwangaza wake na kuzidi kuupa nguvu. Na taa hiyo imevikwa tungi la kigae safi linameremeta kama inavyo meremeta nyota. Na taa ile inawaka kwa mafuta ya mti wenye baraka nyingi, ulio pandwa kwenye udongo mzuri na pahali pazuri. Mti huu ni mzaituni unao mea pahala pa kati na kati. Basi huo si wa mashariki ukakosa joto la jua wakati wa alasiri, wala si wa magharibi ukakosa joto la jua wakati wa asubuhi. Bali huo uko juu ya kilele cha mlima, au katika uwazi wa ardhi unao patisha jua mchana kutwa. Mafuta ya mti huu yanakaribia kutoa mwanga kwa ubora wa usafi wake hata ikiwa hayajaguswa na moto wa taa. Mambo haya yote yanazidisha mwangaza wa hiyo taa juu ya mwangaza wake, na Nuru juu ya Nuru. Na namna hii ndio zinakuwa dalili zilizo enea katika ulimwengu, za kuonekana na kupimika kwa akili; ni Ishara zilizo wazi hazitaki kutiliwa shaka yoyote kwa kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwajibikia Imani kumuamini Yeye, na Risala za Mitume aliyo waleta. Na Mwenyezi Mungu humwezesha kufikia Imani amtakaye kwa njia ya dalili hizi ikiwa huyo mtu atajaribu kunafiika na nuru ya akili yake. Na Mwenyezi Mungu ameleta mifano ya kuweza kuhisiwa na kuonekana ili iwe wepesi kuelewa mambo ya kiakili. Na Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, anawajua wenye kuangalia Ishara zake na wenye kuzipuuza na wakapanda kiburi. Naye atawalipa kwa hayo.
Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni
Hakika wapo watu wanao mtakasa Mwenyezi Mungu na wanamuabudu misikitini ambayo Mwenyezi Mungu ameamrisha ijengwe na iamirishwe kwa kudhukuriwa Mwenyezi Mungu, nao wameshughulikia hayo asubuhi na jioni.
Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.
Dunia na yaliomo duniani ya kuuza na kununua hayawashughulishi wakaacha kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kumzingatia. Wao wanashika Swala, na wanatoa Zaka, na huku wakiikhofu Siku ya Kiyama ambapo nyoyo zitakuwa hazina utulivu kwa sababu ya wasiwasi na hamu, na kungojea matokeo, na macho yatadahadari kwa mhangaiko na kushtuka kwa vituko vigeni wanavyo viona, na wingi wa vitisho.
Ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo yatenda, na awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
Na malipo ya vitendo vyao ni kulipwa sawa sawa kwa ubora wa malipo kwa vitendo vyao vyema, na watapata fadhila kwa kupewa zaidi kuliko wanavyo stahiki. Kwani Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa fadhila, humpa amtakaye katika waja wake wema kipao kikubwa, asichoweza mtu kukihisabu wala wenye kuhisabu hawawezi kukisia.
Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
Na hao walio pinga na wakakanya wanadhani wenyewe kuwa wamefanya vizuri, na kwamba vitendo vyao vizuri vitawaletea faida Siku ya Kiyama. Lakini hao wamekosea katika dhana yao hiyo. Kwani mfano wa vitendo vyao katika upotovu wake na kukosa maana ni kama mmetuko unao tokea unapo angukia mwako wa jua wakati wa adhuhuri juu ya ardhi tambarare jangwani. Mwenye kiu hudhania kuwa ni maji. Hata akiyafikia asikute chochote chenye manufaa kama alivyo dhania. Hali kadhaalika vitendo vya makafiri siku ya malipo vitakuwa vumbi lilio tawanyika. Na kafiri ataikuta adhabu ya Mwenyezi Mungu inamngojea kwa utimilivu wake bila ya nuksani. Hakika hisabu ya Mwenyezi Mungu hapana shaka inakuja. Na Yeye, Aliye takasika, ni Mwepesi katika kuhisabu kwake, hachelewi wala hakosei.
Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru.
Na huu mfano mwengine wa vitendo vya makafiri. Mfano wake ni mfano wa giza la bahari kubwa iliyo tanda yenye kina kirefu. Mawimbi yake yanapigana na kusukumana wenyewe kwa wenyewe. Nayo yamefunikwa na mawingu mazito meusi hayapitishi mwangaza. Katika giza hili lililo rundikana msafiri wa baharini hawezi kuuona mkono wake hata akiukurubisha machoni. Basi anabaki ameduwaa amebabaika hajijui. Na vipi ataona kitu atokane na butaa hili bila ya kupata Nuru ya kumwongoa katika mwendo wake, na kumwokoa na kugongana na kuhiliki. Na basi kama hali hiyo hiyo makafiri hawapati faida katika vitendo vyao, wala hawatoki katika upofu wao na upotovu wao, wala hawajiokoi nafsi zao, ila kwa Nuru ya Imani. Kwani hana Nuru ya kumwongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. Basi atakuwa katika walio teketea. "Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu." Sarabi si chochote ila mandhari ya mwangaza yanayo sabibishwa na marejeo (reflection) ya miale inayo toka kwenye vitu vyenye kutoa mwanga. Na hiyo hurejeshwa tena kutokana na ardhi pana tupu, yaani uwanda, na kupanda kidogo kidogo mkabala na uso wa ardhi, na joto linapo panda wakati wa mchana, basi miale hiyo inayo rejea ikifika kwa jicho la mwenye kuangalia huona vile vitu vimegeuka juu chini kama kwamba kwenye kiyoo kikubwa kilicho tanda. Na kadhaalika mbingu safi ya rangi ya kibuluu huonekana kama kwamba ni ziwa la maji juu ya uso wa ardhi. Na vile vitu vingine kama miti miti na mitende iliyo onekana juu chini inazidi kuonyesha kama kwamba ni vivuli kwenye maji. Na hii Sarabi huzidi kudhihiri kwa uwazi kabisa inapo kuwa khitilafu ni kubwa baina ya joto la uso wa ardhi na angani katika hewa. Na hayo huonekana zaidi majangwani na nyandani na kwenye barabara za jangwani za lami zilio nyooka. Kwa maelezo hayo inaonekana kuwa Sarabi ni kiini macho tu. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 40: " Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru." Aya hii tukufu imekusanya yaliyo muhimu kabisa katika midharuba ya baharini. Ni maarufu kuwa midharuba ya bahari kuu huwa na mawimbi yanayo khitalifiana urefu wao na ukubwa wao au mnyanyuko wao, hata inaonekana kama kwamba hayo mawimbi yanapandana moja juu ya mwenzie, na kwa hivyo yakaziba mwangaza wa jua kwa vile hiyo midharuba inasabibisha kurundika kwa mawingu mazito ambayo nayo huuziba mwangaza wa jua, na kwa hivyo husabibisha giza mtu asiweze kuona kitu juu ya kuwa macho yake mazima. Na ilivyo kuwa Mtume s.a.w. kazaliwa na kakulia jangwani, kuja maelezo kama haya ya undani ya ki-ilimu kwa ulimi wake kuwa ni ufunuo ulio tokana na Mwenyezi Mungu, ni ushahidi kuwa Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na kuwa ni muujiza wa Mtume huyu mtukufu.
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua wayatendayo.
Ewe Nabii! Hujui kwa yakini kwamba kwa Mwenyezi Mungu hunyenyekea kila kiliomo mbinguni na duniani? Na wanamnyenyekea ndege vile vile, nao wamekunjua mbawa zao? Basi viumbe vyote hivi vinanyenyekea amri ya Mwenyezi Mungu na mipango yake. Vinamtakasa na washirika na kila lisio na laiki naye. Na kila kimojawapo kinajua kwa kujaaliwa na Mwenyezi Mungu yaliyo kiwajibikia katika unyenyekevu na kutakasa na kutimiza wadhifa wa maisha. Na Mwenyezi Mungu nyuma yao anajua kwa utimilivu wa kujua Swala ya kila mwenye kusali, na kusabihi kwa mwenye kusabihi, na yote wayafanyayo waja. Basi huwaje makafiri wakawa hawaamini?
Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya wote.
Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi na viliomo ndani yao, na ndiye Mwenye madaraka juu yao, na wote watarejea kwake Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo.
Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho.
Ewe Nabii! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyavuta mawingu, kisha huyakusanya na kuyarindika moja juu ya moja. Utaona mvua inatoka kwenye mawingu. Na Mwenyezi Mungu huteremsha kutokana na mawingu yaliyo rindikana yanayo shabihi milima kwa ukubwa wake, vipande vya barafu kama changarawe, vikawaangukia watu vikawaletea manufaa au madhara, kufuatana na kanuni zake na matakwa yake, wala asiwateremshie wenginewe kwa mujibu apendavyo Yeye Subhanahu, Mtendaji, Mwenye kukhitari. Mwangaza wa umeme unao tokea kwa kugongana mawingu hukaribia kutia upofu kwa ukali wake. Na mambo kama haya ya kuonekana ni dalili za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu ambao unao wajibisha kuleta Imani ya kumuamini Yeye. Hajui kushabihiana baina ya mawingu na milima ila mwenye kupanda ndege (eropleni) inayo ruka juu ya mawingu, akayaona kutoka huko juu kama ni milima na vilima. Ilivyo kuwa ndege hizo hazijawa bado zama za Mtume s.a.w. basi hii inakuwa ni dalili kuwa maneno haya yanatokana na Mwenyezi Mungu anaye jua ya juu na chini. "Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho." Aya hii tukufu imeutangulia msafara wa sayansi. Kwani hii yaeleza daraja za kuundika mawingu yanayo rindikana, na sifa zake, na yaliyo juulikana hivi karibuni ki-sayansi ya kwamba mawingu ya mvua huanzia kwa sura ya moja moja kisha yakajumuika yakawa kikundi, ndiyo hayo mawingu yaliyo rindikana, yaani mawingu yanayo endelea kukua kwa kuelekea utosini. Hayo hukua kimo chake hata kufikia urefu wa kilomita 15 au 20, na hapo huonekana kama ni milima mikubwa iliyo nyanyuka. Na yajuulikanayo ki-sayansi ni kuwa mawingu yaliyo rindika yanapitia daraja tatu, nazo: Daraja ya kukusanyika na kukua. Daraja ya kunyesha. Na mwisho daraja ya kumalizikia. Kama ilivyo kuwa mawingu hayo - nayo ni peke yao - yenye mvua ya mawe na inabeba nguvu za umeme (electricity, Kahrabaa) , huweza kuwa yakashika mfululizo wa umeme na radi, hata huweza ikawa ni miripuko karibu 40 kwa dakika moja, hata mtu anaye tazama akawa hawezi tena kuona kwa ukali wa mwanga wake. Na haya ndiyo khasa yanayo wapata marubani wa meli na ndege wakati wa midharuba ya radi.
Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye kuona.
Mwenyezi Mungu huzigeuza hali za usiku na mchana kwa urefu na ufupi, na kwa kuanzia na kumalizikia, kwa mizunguko ya falaki. Hakika katika hayo pana mazingatio kwa wenye akili zilio nzima zenye busara, na kwa njia hiyo wakamuamini Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na ndiye aliye anzisha kila kitu kwa kupenda kwake. Na akaumba kila kilicho hai kutokana na asili moja ya shirika, nayo ni maji. Na kwa hivyo kila kihai hakiachi kuwa na maji. Kisha zinawakhitalifisha khitilafu nyengine kwa namna, na uwezo, na sura, na kadhaalika. Katika wanyama wapo wanao tambaa kwa matumbo yao, kama samaki, na nyoka. Na wapo wanao kwenda kwa miguu miwili kama wanaadamu na ndege. Na wapo wanao kwenda kwa miguu mine kama mahayawani wengi wa kufugwa na wa mwituni. Mwenyezi Mungu huumba apendavyo kwa njia mbali mbali, kuonyesha uwezo wake na ujuzi wake. Kwani ni Mwenye kutaka atakacho, na Mwenye kukhitari apendacho. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu. "Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu." Maji katika Aya hii tukufu ni maji ya uzazi, yaani vinyama vinavyo toa manii. Na Aya hii si kama imetangulia msafara wa sayansi katika kubainisha kuzalikana mtu kutokana na tone la manii, kama ilivyo kuja katika kauli yake Aliye tukuka: "Hebu naajitazame mtu, ameummbwa kwa kitu gani? Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa." (Sura Att'ariq 5,6), bali imetangulia pia katika kubainisha kwamba kila kinyama kinacho kwenda kwenye ardhi kimeumbwa kwa njia ya kuzalikana na vinyama vya manii, na vinga khitalifiana hivyo vinyama vya manii na sifa zao katika kila namna mnamo hizo namna za vinyama. Katika maana za kisayansi ambazo zaweza kuwa nazo hii Aya ni kuwa maji ni msingi wa kila kiumbe kilicho hai. Kwa mfano mwili wa mtu umekusanya 70% ya uzito wake kuwa ni maji. Yaani mtu mwenye uzito wa kilo 70, kiasi kilo 50 ni maji. Na kabla ya kuteremka Qur'ani haya hayakuwa yakijuulikana kabisa ya kuwa mtu ana sehemu hii kubwa ya mwili wake kuwa ni maji. Na maji ndio chakula cha dharura kabisa kwa mwanaadamu. Kwani hali mtu yamkini aishi siku 60 bila ya kula chakula chochote, hawezi kuishi bila ya maji kwa zaidi kuliko siku 3 mpaka 10 mwisho wake. Na maji ndio msingi wa kufanyika damu, na maji ya limfo, na ya katika ubongo wa mifupa, vimwagavyo na mwili, kama mkojo, na jasho, na machozi, na mate, na nyongo, na maziwa, na maji yanayo patikana katika viungo, na ambayo ndiyo sababu ya ulaini wa mwili. Na yakikosekana 20% ya maji yake basi mwanaadamu hukabiliwa na mauti. Na maji huyayusha vyakula vikasahilika kufyonzeka. Na kadhaalika huyayusha makombo yenye asili ya vilivyo hai au maadini katika mkojo na jasho. Na kwa namna hii maji yana sehemu kubwa zaidi na muhimu kabisa katika kuumbwa kwa mwili. Na kwa hivyo yamkini kusema kwamba kila kiumbe kilicho hai kimeumbwa kutokana na maji.
Kwa yakini tumeteremsha Ishara zinazo bainisha. Na Mwenyezi Mungu hummwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Na hakika Sisi tumeteremsha kwa wahyi Aya zilizo wazi za kubainisha hukumu na mawaidha, na zinazo piga mifano. Na Mwenyezi Mungu humwezesha kwenye kheri ampendaye katika waja wake ambao wapo tayari kuziangalia na kufaidika nazo.
Na wanasema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tumet'ii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye kuamini.
Na wanaafiki husema kwa ndimi zao: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tunazifuata amri zao. Na wanapo tiwa mtihanini kikundi kati yao hukataa kushirikiana na Waislamu katika kazi ya kheri, kama Jihadi na nyenginezo, baada ya kauli yao hii. Na watu hawa si Waumini wa kweli, wala hawastahiki kutumiliwa jina la Waumini kwao.
Na wanapo itwa kumuendea Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, kipo kikundi katika wao kinakataa.
Na katika hali zao ni kuwa wakitakiwa kuhukumiwa mbele ya Mtume kwa jambo alilo literemsha Mwenyezi Mungu, unaafiki wa baadhi yao hudhihiri, na wao hukataa kuhukumiwa wakijua kuwa haki ni ya wale makhasimu zao.
Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wanaona shaka, au wanaogopa ya kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali hao ndio madhaalimu.
Na kwa nini wanasimama msimamo huu katika kushitakiana mbele ya Mtume? Ni kwa sababu nafsi zao zimesibiwa na maradhi ya upofu, na kwa hivyo haziridhiki na hukumu yako ya haki? Au ni kwa kuwa wao wanatilia shaka uadilifu wa Muhammad s.a.w. katika kuhukumu? Si lolote katika hayo kabisa. Lakini hao ni madhaalimu walio dhulumu nafsi zao na wengineo kwa sababu ya ukafiri wao na unaafiki wao na kuiacha kwao haki.
Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa.
Hakika kauli ya haki ifaayo kwa Waumini wa kweli wanapo itwa wahukumiwe kwa mujibu wa yaliyo kuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kuwa waseme kwa kukubali na kunyenyekea: Tumesikia wito wako, ewe Muhammad! Na tumeridhia hukumu yako. Na hao ndio watao kuwa watu wa kufanikiwa katika dunia yao na Akhera yao.
Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.
Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na kuridhia anayo yaamrisha Mtume s.a.w. na wakaiogopa dhati ya Mwenyezi Mungu Tukufu, na wakaukumbuka Utukufu wake, na wakaikhofu ghadhabu yake, hao ndio watakao pata radhi ya Mwenyezi Mungu na mapenzi yake, na neema za Pepo, na ndio wenye kupata kheri tupu.
Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kiapo chao ya kwamba ukiwaamrisha kwa yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajuulikana. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Na wanaafiki wanaapa kwa ukomo wa nguvu za viapo vyao, kwamba wewe, Muhammad, ukiwaamrisha watoke nawe kwenda vitani watakut'ii. Waambie: Msiape! Kwani mambo yatakikanayo kwenu mnayajua, hapana hata mmoja wenu asiye yajua. Wala yamini zenu za uwongo haziondoi ujuzi huo. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua baraabara kila linalo tokana nanyi, na Yeye atakulipeni kwayo.
Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu yake ni aliyo bebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyo bebshwa nyinyi. Na mkimt'ii yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe wazi wazi.
Waambie: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume kwa ut'iifu wa kweli wenye kuonyesha vitendo vyenu. Wanaafiki wakipuuza wasifuate, basi juu ya Muhammad ni waajibu wa aliyo twishwa tu na Mwenyezi Mungu, nayo ni amri ya kufikilisha Ujumbe, wala hakukalifishwa uwongofu wao. Na nyinyi juu yenu ni hayo aliyo kutwikeni Mwenyezi Mungu nayo ni kufuata na kut'ii. Na mtapata adhabu ikiwa mtaendelea na uasi. Na mkimt'ii Mtume mtaongoka kwenye kheri. Na yeye haimpasi ila kufikisha kwa uwazi mukimti au mukiamsi na yeye akaisha fikisha
Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.
Mwenyezi Mungu amewahidi katika nyinyi, walio sadiki haki na wakaifuata, na wakatenda vitendo vyema, kwa ahadi ya kutia mkazo. Yakwamba atawafanya makhalifa, (wafuatizi) warithi wa wale walio tangulia wawarithi katika kuhukumu na utawala katika nchi, kama ilivyo kuwa hali kwa walio tangulia. na atawasimamishia Uislamu kuwa ndio Dini yako, alio wapendekezea, basi watakuwa na heba na madaraka. Na atabadilisha hali yao ya khofu iwe ya amani, wawe wananiabudu mimi, nao wametua hawanishirikishi mimi na chochote kile katika ibada. Na wenye kukhiyari ukafiri baada ya ahadi hii ya kweli au wakaritadi wakaacha Uislamu, basi hao ndio waliotoka nje walioasi wapizani
Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na mt'iini Mtume, ili mpate kurehemewa.
Na shikeni Swala kwa ukamilifu wa nguzo katika utulivu na unyenyekevu, ili ipate kuwa inazuia uchafu na mambo mabaya. Na wapeni Zaka wanao stahiki. Na mt'iini Mtume kwa yote anayo kuamrisheni, ili mpate kutaraji rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi yake.
Msiwadhanie walio kufuru kwamba watashinda katika nchi. Na makaazi yao ni Motoni, na hakika ni maovu kweli marejeo yao.
Ewe Nabii! Usidhani kuwa makafiri wataweza kumkwepa Mwenyezi Mungu asiwashike kwa madhambi yao, au watu wa Haki wasiwaone pahala popote pale katika ardhi. Bali Yeye ni Muweza, na marejeo yao Siku ya Kiyama ni Motoni. Na marejeo maovu kabisa ni marejeo yao.
Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
Enyi mlio amini! Yakupaseni muamrishe watumishi wenu na vijana wenu ambao bado hawajabalighi wasikuingilieni vyumbani mwenu ila baada ya kutaka idhini katika nyakati tatu, nazo ni kabla ya Swala ya alfajiri, na pale mnapo punguza nguo zenu wakati wa kupumzika mchana, na baada ya Swala ya Isha mnapo jitayarisha kulala. Kwani nyakati hizi mtu hubadilisha mavazi ya kulalia badala ya mavazi ya kutokea, na huonekana sehemu za mwili ambazo hazifai kuonekana. Wala hapana ubaya kwenu wala kwao kuingia bila ya ruhusa nyakati nyenginezo, kwa sababu ni jamba la ada watu wa nyumbani kupitiana kwa maslaha yao. Na kwa uwazi wa namna hii Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya za Qur'ani ili akuwekeeni wazi hukumu. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, Mkubwa wa hikima, anajua yanayo silihi kwa waja wake, na anawatungia Sharia zinazo wanasibu, na kwa kadri ya haja yao. "Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamikiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Swala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Swala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima." Aya hii tukufu ni moja katika Aya zinazo elekeza nadhari ya watu wazingatie yaliyo laiki katika jamii za watu khasa ndani ya ukoo. Nayo kuwa kuchanganyika kwa watumishi na watoto katika aila yao huenda kukapindukia mipaka ya hishima za maingiano, wakawa wanawaingilia wenginewe bila ya kutaka idhini katika nyakati maalumu zilizo tajwa katika Aya. Na kwa kuwa nyakati hizo ni nyakati za faragha na uhuru wa binafsi, na kuvua nguo nzito nzito, Aya hii imekusudia kuweka Sharia ya kutaka idhini katika nyakati hizo kutokana na watumishi na vijana ili wasione ambayo yanahisabiwa kuwa ni siri, ambayo ni kama utupu ambao wapasa kusitiriwa. Na kwa hivyo wanaelekezwa watu wa ukoo wavae mavazi yanayo kuwa laiki ya kukabiliana hata wao kwa wao, ili hishima yao ibaki imehifadhika, na uhuru wao umedhaminika, na adabu zao zimechungika. Na Qur'ani ndio inaayo faa khasa kutuongoza tufuate mwendo ulio bora na wa juu. (Ikiwa watoto wa nyumbani haiwafalii kuwaingilia watu katika nyakati hizo za faragha zilizo tajwa, seuze watu mbali!)
Na watoto wanapo fikilia umri wa kubaalighi basi nawatake ruhusa, kama walivyo taka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyo kubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
Na vijana vyenu wakifikilia umri wa kubalighi inawapasa watake ruhusa ya kuingia kila nyumba, na kila wakati, kama ilivyo wapasa wenzao wa kabla yao. Na kwa mfano wa uwazi kama huu Mwenyezi Mungu anakuwekeeni wazi Aya zake alizo ziteremsha. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, Mkubwa wa hikima. Anajua linalo wasilihi waja wake, na anawaatungia Sharia zinazo wanasibu, na kwa kadri ya haja yao.
Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Na wanawake wakongwe ambao hawatumai kuolewa, hawalaumiwi wakipunguza baadhi ya nguo zao, kwa sharti wasiwe wanajishauwa kwa kuonyesha uzuri wa mwili wao ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha usitiriwe. Lakini kujihishimu kwa kujisitiri kwa ukamilifu ni bora kwao kuliko kujifunua. Na Mwenyezi Mungu anawasikia wayasemayo, na anayajua makusudio yao, na atawalipa kwa hayo.
Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, (baba mdogo) au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Aya zake mpate kuelewa.
Wenye udhuru kama vile vipofu, viguru, wagonjwa hawana lawama, bali hata nyinyi wazima hamna lawama kula katika nyumba za watoto wenu, kwani hizo ni nyumba zenu. Wala kula katika nyumba za baba zenu, na mama zenu, na ndugu zenu wanaume na ndugu zenu wanawake, au nyumba za ami zenu, au mashangazi zenu, au wajomba zenu, au mama wadogo, dada wa mama zenu, au nyumba ambazo mmewakilishwa kuzitazama, au nyumba za rafiki zenu mnao changanyika nao, ikiwa hamna yaliyo harimishwa humo. Na hayo ikijuulikana kuwa mwenye nyumba ameruhusu yeye au mkewe. Wala hapana ubaya kula humo pamoja au mbali mbali. Na muingiapo katika nyumba toeni salamu kwa waliomo ambao hao ni baadhi yenu kwa umoja wa Dini na ujamaa. Kwani hao ni kama nyinyi. Na maamkio haya ni maamkio yaliyo wekewa Sharia, yenye baraka na thawabu, na pia ndani yake nyoyo hupoa. Na kwa mfano kama huu Mwenyezi Mungu anazifafanua Aya kwa ajili yenu mpate kuelewa waadhi na hukumu ziliomo ndani yake, na mpate kuzifahamu na mzitende.
Hakika Waumini wa kweli ni walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na wanapo kuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka wamtake ruhusa. Kwa hakika wale wanao kuomba ruhusa, hao ndio wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao, mruhusu umtakaye miongoni mwao, uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemmu.
Hakika Waumini wenye kusadiki ni wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wala hawamwachi Mtume peke yake katika jambo muhimu linalo hitajia wajumuike pamoja kwa ajili yake, kama mfano wa Jihadi. Ila baada ya kumtaka ruhusa ya kuondoka na wakakubaliwa, hakika wanao kukadiri wewe, ewe Nabii, kama unavyo stahiki, na wanatambua umuhimu wa huo mkusanyiko hawaondoki ila baada ya wewe kukubali. Hao ndio wenye kusadiki katika Imani yao kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi wakikutaka ruhusa hawa kwenda kufanya baadhi ya maslaha yao mpe ruhusa umtakaye katika wao, pindi ukimwona kuwa ana haja kweli ya kuondoka, na si dharura kwa mkutano kuwapo yeye. Juu ya hivyo waombee maghfira kwa Mwenyezi Mungu kwa kuondoka kwao, ambako kwa hakika hakuelekei kabisa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema.
Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao ondoka kwa uficho. Basi nawatahadhari wanao khalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu.
Fanyeni hima kuhishimu wito wa Mtume kukuiteni kukusanyika kwa mambo muhimu. Na muitikieni huo wito wake, wala msifanye wito huo kama mnavyo itana nyinyi kwa nyinyi, kuwa inafaa kupuuza na kuondoka mpendavyo. Wala msiondoke ila baada ya kutaka ruhusa na mkakubaliwa, na tena iwe katika mipaka ya ufinyo kabisa, na dharura za shida. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu anawajua wanao ondoka bila ya idhini wakijificha ficha kati ya watu ili ati Mtume asiwaone. Na watahadhari wanao kwenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu asije Subhanahu akawapatiliza kwa uasi wao wakapata mateso makali duniani kama ukame na mitetemeko, au akawapa adhabu yenye wingi wa uchungu aliyo waandalia Akhera, nayo ni ya Motoni.
Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika Yeye anajua mlio nayo. Na siku mtapo rudishwa kwake atawaeleza waliyo yafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Zindukaneni enyi watu! Mjue kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi, na viliomo ndani yao. Anayajua mlio nayo, ukafiri wenu na Uislamu wenu, na uasi wenu, na ut'iifu wenu. Basi msiende kinyume na amri yake. Na Yeye atawapa khabari watu, watapo rejea kwake Siku ya Kiyama, kwa yote waliyo yatenda duniani, na atawalipa kwayo. Kwani Yeye amekizunguka kila kitu kwa ujuzi wake.
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
Sakamakon Bincike:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".