Alif Lam Mim: Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala ameanzia kwa harufi hizi kuashiria moja katika miujiza ya Qur'ani Tukufu iliyo tungwa kwa harufi zile zile ambazo Waarabu wakitungia maneno yao, na juu ya hivyo wao wameemewa hawakuweza kuleta kitu mfano wa Qur'ani hii. Pia juu ya hivyo hizi harufi zinazindua ili upate kuzingatia yasemwayo.
Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu,
Hichi ndicho Kitabu kilicho kamilika, kisicho kuwa na dowa, nacho ni Qur'ani tunayo iteremsha isiyo tiliwa shaka yoyote na kila mwenye akili na mwenye insafu akajua kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Wala haitilii shaka kuwa yasemwayo juu ya mambo na hukumu ni ya kweli tupu. Ndani ya Kitabu hichi upo uwongofu ulio kamilika kwa walio kuwa tayari kuitafuta Kweli, na wanajikinga na madhara na mambo ya kuwaletea adhabu.
Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa katika tuliyo wapa.
Na hawa ndio ambao, kwa kuazimia na kunyenyekea, wanayasadiki yale ya ghaibu wasio yaona kwa macho, wala kuyahisi kwa viungo, ambayo ni ya kuitakidiwa na kuaminiwa, kama mambo ya Malaika, Siku ya Akhera. Kwani msingi wa kushika Dini ni kuamini yaliyo ya ghaibu. Pia wakashika Swala vilivyo, kwa kumwelekea Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea kikweli, na wale ambao wanatoa katika yale alio waruzuku Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mambo ya kheri na mema.
Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo.
Na wale wanao isadiki Qur'ani ulio teremshiwa wewe (Muhammad) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na yote yaliomo ndani yake katika mambo ya hukumu na khabari, na wakatenda yatakikanayo, na wakavisadiki Vitabu vya Mwenyezi Mungu walivyo teremshiwa Manabii na Mitume wa kabla yako, kama Taurati na Injili na vyenginevyo. Kwani risala za Mwenyezi Mungu zote zina asli moja, na hao wanatambulikana kuwa wanaamini Imani moja isiyo legalega ya Siku ya Kiyama na yatayo tokea ya Hisabu na Thawabu na Adhabu.
Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio walio fanikiwa.
Hawa walio sifiwa kwa sifa zilizo tangulia, wamekua kwa kupata sababu za uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na wamekaa imara juu ya hayo. Wao peke yao ndio walio fuzu watakao pata wayatakayo, na wayatamaniayo, nayo ni malipwa kwa kazi yao na juhudi yao, na kutimiza amri na kuepuka waliyo katazwa.
Hakika wale walio kufuru ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawaamini.
Hii ndiyo hali ya waongofu. Ama wajinga, majaahili, walio acha kujitayarisha kwa Imani kwa mapuuza na kufanya inda, wasimwitikie Mwenyezi Mungu, basi ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye.
Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao, na juu ya macho yao pana kifuniko. Basi watapata adhabu kubwa.
Ukafiri umesaki kwa watu hao, hata imekuwa kama nyoyo zao zimetiwa muhuri, zimezibwa kwa vizibo, haziingii kitu chochote zaidi ya kiliomo ndani yake. Na kama kwamba masikio yao pia yamezibwa, hayasikii onyo lake la kweli, na kama kadhaalika wamefunikwa kwa vitanga vya macho. Hawazioni ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuonyesha Imani. Kwa hivyo basi imekuwa wanastahiki kuwafikilia adhabu iliyo kali.
Na katika watu, wako wasemao: Tumemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wala wao si wenye kuamini.
Na miongoni mwa makafiri wapo watu ambao husema kwa ndimi zao yasiyo kuwamo nyoyoni mwao. Hudhihirisha imani na kusema: "Sisi tunamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama," na wala hawasemi kweli. Basi hao hawaingii katika kundi la Waumini.
Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui.
Hao makafiri wadanganyifu huwakhadaa Waumini kwa wanayo yafanya, na wao hudhania kuwa wanamdanganya Mwenyezi Mungu. Wanafikiri kuwa Yeye hayajui wanayo yaficha, na kumbe Yeye anayajua ya siri na yanayo non'gonwa. Basi wao kwa hakika wanajikhadaa wenyewe, kwa sababu madhara ya vitendo vyao yatawapata wao, sasa au baadae. Mwenye kumkhadaa mtu, na akadhani kuwa huyo mtu hajui naye kumbe anajua, basi inakuwa anajikhadaa mwenyewe nafsi yake.
Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi. Basi watakuwa na adhabu chungu kwa sababu ya kusema kwao uwongo.
Katika nyoyo za watu hawa mna maradhi ya uhasidi na chuki kwa watu wenye imini, na itikadi zao zimefisidika. Mwenyezi Mungu basi anawazidishia hayo maradhi yao, kwa ajili ya kuinusuru Haki, kwani hayo yanawaudhi wao kwa sababu ya uhasidi wao, na chuki yao, na inadi yao. Watu hao watapata adhabu iliyo chungu Duniani na Akhera kwa sababu ya uwongo wao na upinzani wao.
Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni watengenezaji.
Na pindi mmojawapo wa walio ongoka akiwaambia hawa wanaafiki: "Msifanye uharibifu katika nchi kwa kuipinga Njia ya Mwenyezi Mungu, na kueneza fitna, na kuwasha moto wa vita," wao hujitoa makosani mwa uharibifu, na husema: "Kee sisi ndio tunao tengeneza." Na hayo ni kwa kuwa ghururi yao imepita mpaka. Huu ndio mwendo wa kila mharibifu, khabithi mwenye ghururi. Yeye hudai kuwa ule uharibifu wake ndio matengenezo na maendeleo.
Enyi Waumini! Amkeni, mtanabahi, muwatambue kuwa hao ndio mafisadi wa kweli, lakini wenyewe hawautambui ufisadi wao kwa ajili ya ghururi walio nayo, wala hawaitambui adhabu kali watakayo ipata kwa unaafiki wao huu.
Na wanapo ambiwa: Aminini kama walivyo amini watu. Husema: Tuamini kama walivyo amini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini hawajui tu.
Akitokea mtu kuwanasihi na kuwaongoza kwa kuwaambia:"Kubalini yalio waajibu." Nako ni kuwa muamini Imani safi kama wanavyo amini watu wakamilifu wanao itikia wito wa akili, wao hufanya maskhara na kejeli na husema: "Si laiki yetu sisi kuwafuata hawa wajinga, wapungufu wa akili." Mwenyezi Mungu anawarudi kwa ule ubishi wao na kuwahukumia kuwa ni wao tu ndio wajinga, wapumbavu, lakini wao hawajui kwa ujuzi wa yakini kuwa ujinga na kukosa kuelewa ni kwao wao tu.
Na wanapo kutana na walio amini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao na mashet'ani wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki tu.
Hawa wanaafiki wakiwakuta Waumini wa kweli husema: "Sisi tunaamini hayo hayo mnayo amini nyinyi," yaani kumkubali Mtume na wito wake, "na sisi tu pamoja nanyi katika itikadi." Wakisha ondoka wakakutana na wenzao wanao shabihiana na mashetani kwa fitina na ufisadi, huwaambia: "Sisi tu pamoja nanyi katika njia yenu na kazi yenu, lakini tukiwaambia yale hao Waumini kwa ajili ya kuwalazia na kuwadhihaki tu."
Mwenyezi Mungu atawadhihaki wao na atawawacha katika upotofu wao wakitangatanga ovyo.
Mwenyezi Mungu Subhana atawalipa kwa huko kudhihaki kwao, na atawaandikia uangamifu unao lingana na hayo maskhara yao na dharau zao. Atawatendea inavyo stahili kutendewa mwenye kudhihaki, na anawapa muhula tu katika dhulma yao iliyo ovu, inayo watia upofu wasiione haki. Kisha khatimaye ndipo atapo watia mkononi kwa adhabu yake.
Hao ndio walio nunua upotofu kwa uwongofu; lakini biashara yao haikupata tija, wala hawakuwa wenye kuongoka.
Na hawa (wanaafiki) kwa kukhiari upotofu badala ya uwongofu wamekuwa kama mfanya biashara aliye khiari kwa biashara yake bidhaa mbovu ya kuchina, basi hafanikiwi kupata faida yoyote. Hupoteza rasilmali yake. Na wao basi hawaongokewi katika 'amali yao.
Mfano wao ni kama mfano wa aliye koka moto, na ulipo tanda mwangaza wake kote kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawawacha katika giza, hawaoni.
Hali ya watu hawa katika unaafiki wao ni kama hali ya mwenye kuwasha moto apate nafuu yeye na watu wake. Moto ukisha waka ukatoa mwangaza kunawiri kote, Mwenyezi Mungu huwaondolea Nuru wenye kuwasha wakawa katika giza zito, hawaoni chochote. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwatunukia sababu za kuongoka, nao hawakuzishika. Kwa hivyo macho yao yakazibwa, wakastahiki kubaki katika kuemewa na upotovu.
Watu hawa ni kama viziwi, kwani wamepoteza manufaa ya kusikia; hawaisikii Haki kwa msikio wa kuikubali na kuitikia. Nao ni kama bubu, kwa sababu hawatamki la uwongofu au la Haki. Na wao kama vipofu, kwani hawanufaiki kwa macho yao. Hawazingatii na kujikataza. Basi hao hawaachi upotovu wao.
Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na radi na umeme; wakawa wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya mingurumo, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.
Au mfano wa hali yao katika kubabaika kwao, na hadi ya mambo yanavyo waemea, na kutokufahamu nini liwafaalo na nini linalo wadhuru, ni kama hali ya watu walio teremkiwa na mvua kutoka mbinguni, yenye radi na mingurumo, wanatia ncha za vidole vyao masikioni mwao ili ati wasisikie sauti za mingurumo, na huku wanaogopa kufa, wakidhani kuwa kule kujiziba kwa vidole kutawalinda na mauti. Watu hao ikiteremka Qur'ani - na ndani yake ikabainisha giza la ukafiri na ikatoa maonyo ya juu yake, na ikabainisha Imani na mwangaza wake unao meremeta, na yakabainishwa mahadharisho na namna mbali mbali za adhabu - wao hujitenga nayo na wakajaribu kuepukana nayo kwa kudai kuwa ati kwa kujitenga nayo wataepukana na adhabu. Lakini Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri kila upande kwa ujuzi wake na uwezo wake.
Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea mwangaza huenda, na unapo wafanyia giza husimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu angeliondoa kusikia kwao na kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Huu umeme mkali wa kuonya unakaribia kunyakua macho yao kwa ukali wake, nao kwa hakika unawamurikia njia kidogo ili wapate kwenda khatua chache kwa mwangaza wake, na unapo katika umeme kiza kinazidi, basi wao husimama hawajui watendeje, wamepotea. Basi hawa wanaafiki dalili na ishara zinapo watolea mwangaza huwa na hamu ya kutaka kuongoka, lakini mara punde hurejea kule kule kwenye ukafiri na unaafiki. Mwenyezi Mungu, Mkunjufu wa uwezo akitaka kitu hukitenda tu, haemewi na chochote katika ardhi wala katika mbingu.
Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka.
Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuanzeni, akakuumbeni akakuleeni, kama alivyo waumba walio kutangulieni. Kwani Yeye ndiye Muumba wa kila kitu. Haya ni hivyo ili mpate kuzitayarisha nafsi zenu, na mzitengeneze kwa ajili ya utukufu wa Mwenyezi Mungu na uangalizi wake. Kwa hivyo nafsi zenu zitahirike na zipate kuifuata Haki, na ziogope mwisho muovu.
(Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe riziki zenu. Basi msimfanyizie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua.
Ni Yeye Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye itandika ardhi kwa kudra yake, na akaikunjua ili isahilike kwenu kuweza kuikalia na kunafiika kwayo. Akajaalia juu yenu mbingu zilio nyanyuka na sayari zake mfano wa jengo lililo jengwa vilivyo, na akakuleteeni njia za uhai na neema - nayo ni maji - aliyo yateremsha kutoka mbinguni, akayafanya ndiyo sababu ya kutoa mimea na miti ya matunda ambayo amekuruzukuni faida yake. Basi haifai baada ya haya mkawaza kuwa Mwenyezi Mungu ana washirika mkawaabudu kama kumuabudu Yeye, kwani Yeye hana mfano wake wala mshirika. Na nyinyi kwa maumbile yenu mnajua kwa yakini kuwa Yeye hana mfano wala mshirika. Basi msiyaharibu maumbile haya. Katika Aya hii ipo sehemu ya kuonesha muujiza wa Qur'ani Tukufu: nayo ni kauli yake Mtukufu "mbingu kama paa". Haya asingeyajua Nabii asiyejua kusoma ila kwa ufunuo wa Mwenyezi Mungu, nayo ni kuwa mbingu kwa kisayansi ni kila kilicho izunguka dunia pande zote, na kwa ukomo wowote, na kwa sura yoyote katika anga, mpaka huko juu kabisa kwenye sayari nyenginezo, zilizoenea zisio na mwisho. Zote hizo zinazunguka kwa mpango wa ajabu, na sisi tunapata uvukuto na mn'gao wake, nazo zinakwenda kwa nguvu ya mvutano kama smaku. Katika sehemu ya mwanzo ya mbingu iliyo tuzunguka lipo anga linalo tukinga kama paa na mianga inayo dhuru kutokana na hizo sayari. Na tabaka hizo huachilia mianga yenye faida tu, ndipo penye mawingu yaletayo mvua.
Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.
Na ikiwa mna shaka kuisadiki hii Qur'ani tunayo mteremshia mja wetu Muhammad, basi mnayo hoja iliyo dhaahiri itayo kubainishieni haki: jaribuni kuleta sura kama hizi za Qur'ani katika ufasihi wake, na hukumu zake, na ilimu zake, na uwongofu wake wote, na muwaite watakao shuhudia kwamba mmeleta sura mfano wake, mtake msaada kwao, na wala hamtowapata. Na mashahidi hao ni mbali na Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu anamuunga mkono mja wake kwa hichi Kitabu chake, na anamshuhudia kwa vitendo vyake. Haya ikiwa ni kweli nyinyi mnaitilia shaka hii Qur'ani.
Na mkitofanya - na wala hamtofanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe walio andaliwa hao wanao kanusha.
Basi ikiwa hamtoweza kuleta sura moja mfano wa hizi sura za Qur'ani - na kabisa hamtoweza kwa njia yoyote, kwani viumbe hawawezi hayo kwa kuwa Qura'ani ni maneno ya Muumba - basi waajibu wenu mziepuke sababu zitazo kuleteeni adhabu ya akhera, nayo ni Moto ambao utakuwa kuni zake za kuwashia ni hao makafiri na masanamu yao. Moto huu umetengenezwa kwa ajili ya kuwaadhibu wapinzani wenye inda.
Na wabashirie walio amini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake; kila watapo pewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo pewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyo fanana; na humo watakuwa na wake walio takasika; na wao humo watadumu.
Ikiwa hizi ni adhabu za waovu wapinzani, basi Pepo ndio makao ya Waumini. Waambie wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu chake, na wakaikubali haki bila ya kutia shaka au wasiwasi, na wakatenda vitendo vyema - waambie khabari ya kuwafurahisha na kukunjua vifua vyao; nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaandalia mabustani yenye mazao, yapitayo mito chini ya miti yake na majumba yake. Kila Mwenyezi Mungu akiwaruzuku matunda ya hizo bustani wao husema: "Haya yamefanana na yale tuliyo pewa kabla." Kwani matunda haya yanashabihiana kwa sura, lakini yanakhitalifiana kwa utamu na ladha. Na watakuwa nao humo pia wake walio kamilika walio safi, wasio kuwa na ila yoyote. Na katika Pepo hii wataishi maisha ya milele wala hawatotoka humo.
Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu,
Mwenyezi Mungu huwaletea mifano watu kueleza hakika ya mambo yalivyo juu, kwa kufananisha na vidudu vidogo na pia vitu vikubwa. Wasio amini waliikejeli hiyo mifano ya vijidudu vidogo kama nzi na buibui. Basi Mwenyezi Mungu aliye takasika haoni aibu kama wanavyo aibika watu kwa kuona haya. Hana la kumzuia asiwape waja wake mfano wowote autakao hata ukiwa mdogo vipi. Kwa hivyo ni sawa kabisa kupiga mfano wa mbu na kilio zaidi kuliko hivyo. Na walio amini wanajua kuwa hii ni mifano, na kuwa huu ni ukweli utokao kwa Mwenyezi Mungu. Ama walio kufuru hawapendi hayo, na husema: "Mwenyezi Mungu anataka nini kwa mfano huu?" Na mfano kama huu huwa ni sababu ya kupotea wale wasio tafuta haki wala hawaitaki, na huwa ni sababu ya kuwaongoa wenye kuamini na kuitaka haki. Basi hawapotei ila waasi walio kwisha potea.
Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye khasara.
Na hao walio kwisha potea ni wale ambao wanaivunja ahadi ya Mwenyezi Mungu, na wao ndio wasio ishika vilivyo ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo iweka katika nafsi zao tangu kuumbwa, kuwa ni fungamano la akili yenye kutambua na yenye kuunga mkono Utume, na wakayakata yale aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, kama vile kuwaangalia jamaa, na kupendana na kutendeana mema, na kuoneana hurumu watu kwa watu; na wakafanya fisadi katika nchi kwa mambo maovu na kuzua fitna na kuchochea vita na kuharibu majenzi. Hao ndio wenye kuleta khasara kwa kufisidi khulka yao walio umbwa nayo, na wakawagawa watu mapande mapande, badala ya kuleta mapenzi na kuoneana huruma kama inavyo stahiki. Kwa vitendo vyao hivyo watapata hizaya duniani na adhabu huko Akhera.
Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu akakufufueni! Kisha atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?.
Hakika hali yenu instaajabisha! Vipi mnakufuru na wala hapana sababu yoyote ya kutegemewa katika kukufuru kwenu? Ukiangalia hali yenu utaona inakataa ukafiri huu wala hamna udhuru wowote. Kwani nyinyi mlikuwa maiti, hamna uhai, akakuumbeni Mwenyezi Mungu na akakupeni uhai na umbo zuri. Kisha ni Yeye atakaye kurejezeni muwe maiti baada ya kutimia wakati wenu. Kisha atakufufueni muwe hai mara nyingine kwa ajili ya hisabu na malipo. Kisha mtarejea kwake, wala hamwendi kwa mwenginewe, mtarejea, kwa ajili ya hisabu na malipwa kwa vitendo vyenu.
Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi. Tena akazielekea mbingu, na akazifanya mbingu saba. Naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.
Mwenyezi Mungu anaye pasa kuabudiwa na kut'iiwa ndiye aliye kufadhilini. Akaumba kwa ajili ya manufaa na faida yenu kila neema inayo patikana duniani, kisha baadae akazielekea mbingu akaziumba mbingu saba kwa mpango. Katika hayo yapo mnayo yaona na msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote, na anavijua vyote.
Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua.
Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye Takasika, amebainisha kuwa ni Yeye ndiye aliyempa uhai mtu, na akamweka duniani. Kisha amebainisha vile vile asli ya kumweka mwanaadamu na ujuzi aliyo mpa, na akakumbushwa hayo. Basi kumbuka, ewe Muhammad, neema nyingine ya Mola wako Mlezi kumpa mtu, nayo ni pale alipo waambia Malaika: Mimi nitajaalia awepo katika ardhi mfwatizi, ambaye nitamweka hapo, na nimpe madaraka, naye ni Adam na vizazi vyake. Mwenyezi Mungu atamweka kama Khalifa, au naibu wa kuimarisha dunia, na kutekeleza amri, na kuzitengeneza nafsi. Malaika wakauliza kutaka kujua nini siri ya hayo, wakasema: Je, utaweka katika Ardhi atakaye leta uharibifu humo kwa maasi, na atakaye mwaga damu kwa uadui na mauwaji kwa kufuata tabia yake ya matamanio, na ilhali sisi tunakutakasa na yasiyo laiki na utukufu wako, na tunasafisha kumbusho lako, na tunakutukuza? Mola wao Mlezi akajibu: Mimi ninajua maslaha ya hayo msiyo yajua nyinyi.
Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli.
Na baada ya Mwenyezi Mungu kwisha kumuumba Adam na akamfundisha majina ya vitu vyote na sifa zao ili atue katika ardhi na anufaike navyo, aliwaletea hivyo vitu Malaika na akawaambia: Niambieni majina ya vitu hivi na sifa zao kama kweli nynyi ndivyo kama mnavyo dhani kuwa mnastahiki kupewa madaraka katika Ardhi, na kuwa hapana aliye bora kuliko nyinyi kwa sababu ya ut'iifu wenu na ibada zenu.
Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima.
Malaika wakatambua upungufu wao, wakasema: Sisi tunakutakasa Ewe Mola wetu Mlezi kwa mtakaso ulio laiki nawe. Tunakiri kuwa tumeshindwa, na hatuwezi kupinga. Kwani hatuna ilimu kuliko uliyotupa Wewe, na Wewe ndiye Mjuzi wa kila kitu, na Mwenye hikima na hukumu katika kila jambo ulitendalo.
Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipo waambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha?
Mwenyezi Mungu alimwambia Adam: Watajie Malaika khabari za vitu hivi. Akataja; na ukadhihiri ubora wake juu yao. Na hapo Mwenyezi Mungu akawaambia kuwakumbusha vipi ujuzi wake ulivyo enea: Sikukwambieni kuwa Mimi ninajua siri za mbingu na ardhi, na hapana ajuae hayo isipo kuwa Mimi, na Mimi ninajua mnayo yadhihirisha katika kauli yenu, na mnayo yaficha katika nafsi zenu.
Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri.
Na kumbuka Ewe Nabii! Tulipo waambia Malaika: Mnyenyekeeni Adamu kwa kumwamkia na kuukiri ubora wake. Wakat'ii Malaika wote ila Iblis. Yeye alikataa kusujudu akawa miongoni mwa walio asi, walio zikataa neema za Mwenyezi Mungu, na hikima yake, na ujuzi wake.
Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu.
Kisha Mwenyezi Mungu alimuumba Adam na mkewe, na akawaamrisha wakae katika Bustani ya neema. Akamwambia: Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii na kuleni humo mtakavyo vya kutosha bila ya kutaabika, na kaeni mtakapo, mle mtakacho. Lakini Mwenyezi Mungu aliwatajia mti maalumu na akawahadharisha wasiule, na akawaambia: Msiukaribie mti huu, wala msile matunda yake. Mkifanya hivyo mtakuwa miongoni mwa walio dhulumu, na mtakuwa waasi.
Lakini Shet'ani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyo kuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda.
Lakini Iblis, anaye mhusudu na kumchukia Adam, alimfanyia vitimbi, akawadanganya mpaka wakateleza wakala mti walio katazwa. Mwenyezi Mungu akawatoa katika ile neema na ukarimu walio kuwa nayo. Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaamrisha washukie kwenye Ardhi waishi humo wao na vizazi vyao, na wawe na uadui baina yao kwa wao kwa sababu ya ushindani na kupotozwa na Shetani. Na huko kwenye Ardhi pawe pahali pa kukaa kwao na kupata maisha, na kustarehe kutako kwisha kwa kutimia wakati.
Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu.
Adam na mkewe walitambua makosa yao na kujidhulumu nafsi zao. Mwenyezi Mungu Mtukufu alimfunza Adam baadhi ya maneno ya kutubia na kuomba msamaha na akayasema. Mwenyezi Mungu alimkubalia toba yake, na akamsamehe, kwani Yeye ni mwingi wa kukubali toba, naye ni Mwenye kuwarehemu waja wake wanyonge.
Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni uwongofu utokao kwangu, basi watakao fuata uwongofu wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
Tukamwambia Adam na mkewe na vizazi vyao vijavyo na Iblis: Shukeni katika Ardhi, na huko mtalazimishwa mambo. Yakikujieni hayo kutokana na Mimi - na hapana shaka yatakujieni - basi wale watakao itikia amri yangu, na wakafuata uwongofu wangu hawataona khofu yoyote, na hawatopata huzuni, kwa kukosa thawabu, kwa sababu Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa atendaye mema.
Na wenye kukufuru na kuzikanusha ishara zetu, hao ndio watakao kuwa watu wa Motoni, humo watadumu.
Na wale ambao watapinga na watawakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu na Vitabu vyake, hao ni watu wa Motoni, watabaki huko milele, wala hawatatoka wala hawatakufa.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo kuneemesheni, na timizeni ahadi yangu, na Mimi nitatimiza ahadi yenu, na niogopeni Mimi tu.
Enyi Wana wa Israili kumbukeni neema zangu nilizo kutunukieni nyinyi na wazee wenu kwa kuzifikiri na kushukuru na kutimiza agano langu nililo lichukua kwenu, na nyinyi nafsi zenu mkalikiri, nalo ni Imani, na Vitendo vyema, na kuwasadiki Manabii wajao baada ya Musa, ili Nami nitimize ahadi yangu kwenu, nayo ni kukulipeni malipo mema, na neema ya kudumu. Na wala msimwogope mtu yeyote isipo kuwa Mimi, na tahadharini na kufanya mambo yatakayo nifanya nikasirike nanyi. Aya hii inaonyesha kuwa ahadi, au agano, ni waajibu wa pande zote mbili zilizo ahidiana kutimiza lilio lazimika. Akiacha mmojapo basi haimlazimu wa pili kutimiza agano lake.
Na aminini niliyo yateremsha ambayo yanasadikisha mliyo nayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze Ishara zangu kwa thamani ndogo. Na niogopeni Mimi tu.
Na isadikini Qur'ani iliyo teremshwa kusadikisha vile vitabu mlivyo navyo, na kufunza Tawhidi (kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja) na kumwabudu Mwenyezi Mungu, na uadilifu baina ya watu. Wala msikimbilie kutaka kuipinga Qur'ani msije mkawa ndio wa mwanzo kuikana, na ilhali ifaavyo ni nyinyi ndio muwe wa mwanzo kuiamini. Wala msiziache Ishara za Mwenyezi Mungu mkenda badala yake mkachukua chenginecho kipitacho njia katika starehe za uhai wa dunia. Na niogopeni Mimi tu, na fuateni Njia yangu, na wacheni upotovu.
Wala msichanganye kweli na uwongo na mkaificha kweli nanyi mnajua.
Wala msichanganye Haki iliyo toka kwangu na upotovu mlio uzua nyinyi, hata ikawa halijuulikani la kweli na la uwongo. Wala msiifiche Haki, na katika hiyo Haki ni kumsadiki Muhammad, na nyinyi mnajua kuwa yeye ni wa kweli na wa kusadikiwa.
Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na wanao inama.
Itikieni Imani. Shikeni Swala yenye nguzo zilizo simama baraabara. Na toeni Zaka muwape wanao stahiki. Na salini pamoja na jamaa wa Kiislamu ili mpate malipo ya Swala na thawabu za kusali jamaa. Na haya yanalazimu kuwa muwe Waislamu.
Je! Mnawaamrisha watu mema na mnajisahau nafsi zenu, na hali nyinyi mnasoma Kitabu? Basi je, hamzingatii?
Je, mnawataka watu wafanye kheri, na wajilazimishe ut'iifu, na waache maasia, kisha nyinyi hamtendi myasemayo, wala hamjilazimishi nafsi zenu kwa yale myatakayo? Kwa hivi mnajipoteza nafsi zenu, kama kwamba mmezisahau, na ilhali nyinyi mnasoma Taurati na ndani yake pana maonyo na mikemeo kwa mwenye kusema asilo litenda. Basi nyinyi hamna akili ya kukuzuieni na kwenda mwendo huu wa kutukanisha?
Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu,
Na tafuteni msaada wa kutekeleza waajibu kwa subira na kuizuia nafsi isitende yanayo udhi. Katika hayo ni kwa kufunga Saumu, na kwa Swala ambalo ni jambo kubwa lenye kuusafisha moyo na kuzuia kutenda machafu na maovu, na kwa hivyo ndio yakawa mazito ila kwa wenye kupenda ut'iifu ambao nyoyo zao zimetulia kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
Ambao wana yakini kuwa hakika watakutana na Mola wao Mlezi na ya kuwa hakika watarejea kwake.
Hao ndio wanyenyekevu walio tulia nyoyo zao, ambao wanaiamini Siku ya mwisho, na wana yakini kuwa watakutana na Mola wao Mlezi wakati wa kufufuliwa, na kwake Yeye pekee ndio watarejea ili awahisabie kwa yale waliyo yatenda na awalipe kwayo.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni zile neema zangu nilizo kuneemesheni, na nikakuteuweni kuliko wote wengineo.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema zangu nilizo kuneemesheni kwa kukutoeni katika dhulma ya Firauni, na nikakuongoeni na nikakuwekeni imara katika nchi baada ya kuwa mlikuwa mkionewa humo. Mshukuruni kwa kumt'ii Mwenye kukutunukieni hayo. Na kumbukeni kuwa Mimi niliwapa baba zenu mlio zalikana kutoka kwao nisiyo wapa wowote wengineo wakati wenu. Haya wanaambiwa taifa la Mayahudi walio kuwako zama za Mtume.
Na iogopeni Siku ambayo mtu hatomfaa mtu kwa lolote, wala hayatakubaliwa kwake maombezi, wala hakitapokewa kikomboleo kwake; wala hawatanusuriwa.
Iogopeni Siku ya Hisabu kali, Siku ya Kiyama, siku ambayo hapana mtu ataeweza kumtetea mtu, na wala hapana mtu ataye mfaa mtu, wala hakubaliwi mtu kuleta mwombezi, kama ilivyokuwa hatokubaliwa mtu kutoa fidia ya dhambi, wala hapana mtu ataye weza kuizuia adhabu isimpate mwenye kustahiki.
Na vile tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya, wakiwachinja wana wenu wa kiume na wakawawacha hai wanawake; na katika hayo ulikuwa ni mtihani mkubwa ulio toka kwa Mola wenu Mlezi.
Na kumbukeni katika neema zetu juu yenu kuwa tumekuokoeni kutokana na mateso ya Firauni na wasaidizi wake walio kuwa wakikuonjesheni adhabu kali kabisa, kwa kuwa wakiwachinja wana wenu wanaume - kwa khofu kuwa miongoni mwao atatokea wa kupindua utawala wa Firauni - na wakiwabakisha wanawake ili wawafanye wajakazi wao wa kuwatuma. Na katika adhabu hizi na uteketezaji huu wa umma ni majaribio makuu kutokana kwa Mola wenu, na ni mtihani mkuu kwenu.
Na tulipo ipasua bahari kwa ajili yenu na tukakuokoeni, tukawazamisha watu wa Firauni, na huku mnatazama.
Kumbukeni vile vile katika neema alizo kuneemesheni Mwenyezi Mungu pale tulipo kupasulieni bahari - na tukayagawa maji katikati ili mpate kupita - mkaokoka, Firauni na askari wake wasikupateni. Na kwa fadhila yetu mkavuka na tukawapatiliza adui zenu kwa sababu yenu, tukawazamisha mbele ya macho yenu. Nyinyi mkawa mnawaona wanazama, na bahari ikiwafunika baada ya nyinyi kwisha vuka salama.
Na tulipo muahidi Musa masiku arubaini, kisha mkachukua ndama (mkamuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
Na kumbukeni wakati Mola wenu alipo agana na Musa muda wa masiku arubaini kwa ajili ya mazungumzo. Alipo kwenda walipo agana na akarejea alikukuteni mmekwisha geuka, na mkamfanya ndama aliye muunda Saamiriyu ndiye wa kuabudiwa. Mkawa kwa hivyo ni wenye kudhulumu kwa kumfanyia Mwenyezi Mungu aliye kuumbeni na kukuokoeni ana mshirika wake. ("Masiku" ni wingi wa Usiku. Wingi wa siku ni siku, kama ilivyo sahani, sabuni, silaha, sinia, sungura, saa. Ni makosa kwa Kiswahili kusema "masiku" kuwa ni wingi wa siku; "Masiku" ni wingi wa "Usiku". Kutumia "Masaa" kuwa ni wingi wa "Saa" ni makosa.)
Kisha tukakusameheni baada ya hayo, ili mpate kushukuru.
Kisha tukakusameheni na tukaifuta adhabu yenu mlipo tubu na mkapata msamaha kwa dhambi zenu, ili mpate kumshukuru Mola Mlezi wenu kwa huko kufuta kwake makosa yenu, na kusamehe kwake, na fadhila zake.
Na tulipo mpa Musa Kitabu na pambanuo ili mpate kuongoka.
Na kumbukeni tulipo kuneemesheni kwa kukumteremshia Nabii wenu Musa Kitabu chetu Taurati, Kitabu ambacho kinafarikisha baina ya Haki na baat'ili, na kinabainisha baina ya Halali na Haramu, ili mpate kupata uwongozi kwa nuru yake na muongoke kutokana na upotovu kwa kuzingatia yaliyomo ndani yake.
Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmezidhulumu nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu. Naye akapokea toba yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba na Mwenye kurehemu.
Ikumbukeni siku alipo kwambieni Mtume wenu Musa: Enyi watu wangu! Mmejidhulumu kwa kumchukua ndama wa Saamiriyu mkamuabudu. Basi tubuni kwa Mola wenu aliye kuumbeni kabla hamjawa kitu, kwa kuzighadhibikia nafsi zenu ovu zenye kuamrisha maovu, na zifanyeni hizo nafsi ziwe nyonge, ili mpate nafsi mpya zilio safi. Mwenyezi Mungu alikusaidieni kwa hayo na akakuwezesheni mkaweza, na hiyo ni kheri itokayo kwa Muumba wenu. Na haya ni kabla ya kutubu kwenu, Naye akakusameheni. Kwani Yeye ni mwingi wa kukubali toba kwa waja wake, na mwingi wa kuwarehemu.
Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi. Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia.
Na kumbukeni kauli yenu mlio mwambia Musa: Kwamba sisi hatukukubali wewe mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi hivi hivi kwa macho bila ya kificho. Ikakuchukueni radi na moto kutoka mbinguni, ikakutikiseni kuwa ni malipo ya inadi yenu na dhulma zenu, na kutaka kwenu jambo ambalo ni muhali kutokea kwenu. Nanyi mnaiona hali yenu na balaa na adhabu zilizo kusibuni kwa mpigo wa radi hiyo.
Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate kushukuru.
Kisha tukakuzindueni kutokana na huko kudawaa kwenu na kupwelewa, na tukakufundisheni ili mpate kuishukuru neema yetu kwa hayo, na mpate kuiunga mkono Haki ya Mwenyezi Mungu kwa kupitia njia ya shukrani hii.
Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na tukakuteremshieni Manna na Salwa; tukakwambieni: Kuleni vitu vizuri hivi tulivyo kuruzukuni. Nao hawakutudhulumu Sisi lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao.
Na katika fadhila zetu juu yenu ni kuwa tumekuleteeni mawingu yawe kama ni kivuli kukulindeni na mwako wa jua kali, na tukakuteremshieni Manna, nacho ni kitu kitamu kama asali kinaanguka juu ya miti linapo chomoza jua. Kadhaalika tumekuteremshieni Salwa, naye ni ndege aliye nona, nao wakikujieni kwa makundi asubuhi na jioni ili mle mstarehe. Na tukakwambieni: Kuleni vilivyo vyema katika riziki yetu. Hawa watu wakaikufuru neema. Na haya hayakutudhuru Sisi, lakini wamejidhulumu nafsi zao. Kwani madhara ya uasi unawarejea wao watendao. Katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tukakuteremshieni Manna na Salwa" imetajwa kwa uhakika wa kisayansi, kwani hivi mwishoni imevumbuliwa kuwa madda za "Protein" zenye asli ya vinyama kama vile nyama na ndege ni bora kumfaa mtu kwa chakula kuliko "Protein" zinazotoka katika mimea na mboga. Na katika Manna mna sukari ya kumpa mtu nguvu na uchangamfu wa kufanyia kazi na kutaharaki huku na huku.
Na tulipo sema: Ingieni mji huu, na humo mle mpendapo maridhawa, na ingieni katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni: Tusamehe! Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.
Na kumbukeni enyi Wana wa Israili! Tulipo kwambieni: Ingieni katika mji mkubwa aliyo kutajieni Nabii wenu Musa na mle katika viliomo humo kama mnacho kitaka, kwa wingi na kwa wasaa, kwa sharti lakini kuwe kuingia kwenu kwa upole na unyenyekevu, kupitia mlango aliyo utaja Nabii wenu. Na kwamba hapo mumuombe Mwenyezi Mungu akusameheni makosa yenu. Kwani mwenye kufanya hayo kwa ikhlasi, usafi wa niya, tunamfutia makosa yake. Na mwenye kuwa mtenda mema aliye mt'iifu tunamzidishia thawabu na ukarimu juu ya kumsamehe na kumfutia dhambi.
Lakini walio dhulumu waliibadili kauli isiyo kuwa waliyo ambiwa. Kwa hivyo tukaiteremsha juu ya wale walio dhulumu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya walivyo kuwa wamepotoka.
Lakini walio dhulumu walikwenda kinyume na amri za Mola wao Mlezi, wakasema sio walio amrishwa wayaseme, kwa kudhihaki na kuasi. Basi jaza yao ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwateremshia juu yao adhabu kuwa ndiyo malipo ya ukosefu wao na kuzivunja amri za Mola wao Mlezi.
Na Musa alipo omba maji kwa ajili ya watu wake, tulimwambia: Lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatimbuka chemchem kumi na mbili; kila kabila ikajua mahali pake pa kunywea. Tukawaambia: Kuleni na mnywe riziki ya Mwenyezi Mungu, wala msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.
Na kumbukeni, enyi Wana wa Israili, siku Nabii wenu Musa alipo taka maji kutokana na Mola wake Mlezi kiliposhtadi kiu jangwani, Nasi tukakurehemuni. Tukamwambia Musa: Lipige jiwe kwa fimbo yako, yakatimbuka maji kutoka chemchem kumi na mbili. Kila kikundi na chemchem yake, na walikuwa makundi thinaashara Kumi na mbili. Basi kila kabila ikawa na pahala pake pa kunywea. Na tukakwambieni: Kuleni Manna na Salwa, na kunyweni maji haya yanayo timbuka, na muwache mlio nayo, wala msipite mipaka kwa uharibifu katika nchi, bali wacheni maasia.
Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu, basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyo mea katika Ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyo viomba. Na wakapigwa na unyonge,na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyo asi na wakapindukia mipaka.
Na kumbukeni pia, enyi Mayahudi, pale wale wazee wenu walio tangulia walipo zidi jeuri zao, wasiipe neema ya Mwenyezi Mungu haki yake, wakamwambia Musa: Sisi hatutovumilia chakula hicho kwa hicho (nacho ni Manna na Salwa). Basi muombe Mola wako atutolee katika ardhi mboga, na matango, na adasi, na thom na vitunguu. Musa aliyastaajabia haya na wala hakupendezewa nayo. Akawaambia: Hivyo nyinyi mnafadhilisha vyakula namna hii kuliko vilivyo kuwa bora zaidi na vizuri zaidi, navyo ni Manna na Salwa? Basi shukeni kutoka Sinai, na ingieni katika mji mmojawapo na huko mtapata hivyo mnavyo vitaka. Na kwa sababu ya kutoridhika kwao huko na inda yao hao Mayahudi walipigwa na madhila, na ufakiri na unyonge, wakastahiki kupata ghadhabu ya Mwenyezi kwa ule mtindo wao wa inda na uasi, kukanusha ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa Manabii. Kwa haya ikawa wanaacha Haki iliyo kwisha thibiti na kukubalika. Yaliyo wapelekea hata wakaingia katika ukafiri ule na mauwaji yale ni kule kuziachia nafsi zao kupanda maasi na kufanya uadui na kupindukia mipaka katika maasia.
Hakika Walio amini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
Wale walio amini, nao ni Manabii wa zamani, na Mayahudi, na Wakristo, na wanao tukuza nyota na malaika, na wanao uamini ujumbe wa Muhammad baada ya kuteuliwa kuwa ni Mtume, na wakaamini kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mmoja wa pekee, na wakaamini kuwa kupo kufufuliwa na kuhisabiwa Siku ya Kiyama, na wakatenda vitendo vyema duniani, basi watu hawa wana malipwa yao yaliyo wekewa kwa Mola wao Mlezi. Wala haitowapata khofu ya kuadhibiwa, na wala haitowafika huzuni kwa kukosa thawabu. Na Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa mwenye kutenda mema.
Na tulipo chukua ahadi yenu, na tukaunyanyua mlima juu yenu (tukakwambieni): Shikeni kwa nguvu haya tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kujilinda.
Kumbukeni pale tulipo chukua ahadi na agano juu yenu, tukaunyanyua mlima wa T'uur, tukaufanya kwa uwezo wetu kama kivuli juu yenu mpaka mkaogopa mkanyenyekea, tukakwambieni: Shikeni uwongofu na uwongozi tulio kupeni kwa nguvu na jitihadi, na mkumbuke kwa kutekeleza na kutenda yaliyo tajwa ndani ili mpate kujilinda nafsi zenu msipate adhabu.
Kisha mligeuka baada ya haya. Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema zake, mngeli kuwa miongoni mwa wenye kukhasirika.
Tena baada ya hayo yote mkageuka. Na lau kuwa si fadhila na rehema ya Mwenyezi Mungu juu yenu kuiakhirisha adhabu kwenu mngeli kwisha kuwa miongoni walio potea na kuangamia.
Na hakika mlikwisha yajua ya wale miongoni mwenu walio ivunja Sabato, (siku ya mapumziko, Jumaa Mosi) na tukawaambia: Kuweni manyani wadhalilifu.
Na nyinyi bila ya shaka mliwajua wale walio pindukia mipaka katika siku ya Sabato, siku ya ibada na mapumziko, siku ya Jumaamosi. Pale walipo kwenda kuvua samaki siku hiyo na ilhali siku hiyo ilikuwa imetengwa iwe ni siku ya mapumziko na siku kuu, na kufanya kazi siku hiyo ilikatazwa. Mwenyezi Mungu alizipotoa nyoyo za wakosefu wale, wakawa kama manyani katika pumbao lao na matamanio yao. Tukawaweka mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu, wakifukuzwa kama mijibwa, watu hawataki kukaa nao, na wanawanyanyapaa kuchanganyika nao.
Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale walio kuwa katika zama zao na walio kuja baada yao, na mawaidha kwa wachamngu.
Mwenyezi Mungu ameifanya hali yao namna hii waliyo ifikia ili iwe ni kama funzo na onyo kwa wengineo, wasitende kitendo kama hichi. Ameyafanya haya ili yazingatiwe na watu wa nyakati zao na watakao kuja baada yao, kama tulivyo yafanya kuwa ni mawaidha kwa wale wanao mcha Mola wao Mlezi, kwani wao ndio wanao nafiika kwa maonyo ya mawaidha na mazingatio.
Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje Ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Audhubil lahi! Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga.
Na kumbukeni pale alipo uliwa mtu na asijuulikane muuwaji, Musa akawaambia watu wake: Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje Ng'ombe ili iwe ndio ufunguo wa kumgundua muuwaji. Lakini wakaona hayo ni mageni, baina ya yale mauwaji na kumchinja ng'ombe. Wakasema: Unatufanyia maskhara wewe Musa? Yeye akawajibu: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu asinipatilize kwa kuwa katika wajinga wanao wadhihaki waja wake.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni Ng'ombe gani? Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba Ng'ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.
Tena wakamwambia Musa wakirejea lile shauri la ng'ombe: Tutakie kwa Mola wako Mlezi atubainishie sifa za huyo ng'ombe. Akawaambia: Mwenyezi Mungu ameniambia huyo Ng'ombe si mkubwa wala si mdogo, bali yu katikati baina ya upevu na uchanga. Basi hebu tekelezeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie nini rangi yake? Akasema: Yeye anasema, kuwa Ng'ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza wanao mtazama.
Lakini walikakamia katika kutaradadi kwao, wakasema: Tutakie kwa Mola wako Mlezi atupambanulie nini rangi yake. Akawajibu: Mwenyezi Mungu anasema: Ng'ombe huyo ni wa rangi ya manjano iliyo koza, na safi. Ukimtazama anapendeza kwa usafi wa rangi yake ilivyo zagaa.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni yupi? Hakika tunaona ng'ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, tutaongoka.
Tena wakashikilia kuuliza kwao, wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie khasa huyo ni yupi? Kwani ng'ombe wanatudanganyikia sisi, hatujui. Na Inshallah, Mwenyezi Mungu akipenda, sisi tutaongokewa tumjue.
Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni Ng'ombe asiye tiwa kazini kulima Ardhi wala kumwagia maji mimea, mzima, hana baka. Wakasema: Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye hayo.
Musa akawambia: Mwenyezi Mungu anasema kuwa Ng'ombe huyo bado hajatiwa kazini kwa kulima wala kumwagia maji shambani kwa ajili ya makulima. Naye hana ila yoyote, mzima kabisa, wala katika mwili wake hana kibaka chochote, wote ni wa rangi moja. Hapo tena wakamwambia: Sasa umepambanua vilivyo. Wakamtafuta Ng'ombe mwenye sifa hizo wakamchinja. Na walikuwa wamekaribia wasifanye hayo kwa kukithiri masuala yao na wingi wa kushikilia kwao.
Na mlipo muuwa mtu, kisha mkakhitalifiana kwayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha.
Na kumbukeni siku mlipo muuwa mtu, mkakhasimiana wenyewe kwa wenyewe, mkautetea ukhalifu, mkawa mkituhumiana kwa mauwaji, na hali Mwenyezi Mungu anaijua hakika, na ataikashifu na kuidhihirisha juu ya kuificha kwenu.
Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo Ng'ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Ishara zake ili mpate kufahamu.
Tukakwambieni kwa ulimi wa Musa: Chukueni kipande cha nyama ya huyo Ng'ombe mumpige nacho, nanyi mkafanya hivyo. Mwenyezi Mungu akamfufua huyo aliye uliwa akataja jina la aliye muuwa, na kisha akafa tena. Na huo ulikuwa ni muujiza wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Musa. Kwani Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, na kwa uwezo wake huu ndivyo anavyo huisha maiti Siku ya Kiama. Na anakuonyesheni dalili za uwezo wake ili mpate kufahamu na kuzingatia haya. Mwandishi mmoja wa zama zetu, marehemu Sh. Abdul Wahhab Annajjar ametaja kwamba kauli ya Mwenyezi Mungu: "Mpigeni kwa kipande chake" maana yake kipande cha aliye uwawa. Na makusudio ya kufufuka kwake ni kumtolea kisasi, kwa kuwa kupigwa kwa kiungo cha mwenye kuuliwa humpelekea muuwaji kuungama, na mara nyingi kumwona tu aliye uwawa humpelekea mwenye kuuwa kuungama. Na inakuwa kisa hichi ni mbali na lile jambo la kuchinja, na kuamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kuchinja; na kwamba kuamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu wamchinje Ng'ombe ni kwa ajili ya kumla. Na katika haya pana mafunzo ya nafsi kwao, kwani hawa walikuwa pamoja na Wamisri ambao wakimwona Ng'ombe ni mtakatifu, na yalikuwa kwao mabaki ya haya ya kumtukuza Ng'ombe kwa dalili ya kuwa waliabudu sanamu la ndama baada ya hayo. Ikawa hapana budi kung'oa mabaki yake katika nafsi zao kwa kuwalazimisha kumchinja Ng'ombe. Ndio ikawa ile amri ya kuchinja, na yakatokea majadiliano na kukawa kule kusitasita kwao, na mwisho wakamchinja, na walikaribia wasichinje.
Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, hata zikawa kama mawe au ngumu zaidi; kwani kuna mawe yanayo timbuka mito, na kuna mengine yanayo pasuka yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine huanguka kwa sababu ya khofu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yafanya.
Tena nyinyi baada ya miujiza na ishara hizi zote hamkukubali wala hamkunyooka, wala nyoyo zenu hazikulainika na kunyenyekea. Bali zikawa zimekacha na ngumu, na zikabakia vile vile na ugumu wake na ushupavu wake, kama jiwe gumu katika ule ukakamavu wake, bali hizo nyoyo zenu zimeshinda jiwe kwa ugumu. Kwani yapo mawe yanayo athirika na kulainika. Yapo mawe yanayo timbuka maji yakawa mito, na yapo mawe yanayo pasuka na yakatoka maji kama chemchem, na yapo mawe kwa uwezo wa Mwenyezi yanayo nyenyekea kufuata mapenzi ya Mwenyezi Mungu yakaporomoka kutoka juu ya milima kama apendavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ama hizo nyoyo zenu,nyinyi Mayahudi, haziathiriki wala hazilainiki. Ole wenu kwa hayo! Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na vitendo vyenu, naye atakupeni adhabu kwa namna mbali mbali za adhabu, ikiwa hamtoshukuru kwa neema mlizo pewa.
Mnatumai watakuaminini na hali baadhi yao walikuwa wakisikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha wakayabadili baada ya kuwa wameyafahamu, na hali wanajua?
Haikufaliini enyi Waumini kutumai ya kuwa Mayahudi wataiamini Dini yenu na wakufuateni nyinyi, na ilhali katika makundi yao mbali mbali zimekusanyika sifa mbovu zinazo waweka mbali na kuiamini Haki. Walikuwapo baadhi miongoni mwao (nao ni wale Makohani) walio kuwa wakiyasikia maneno ya Mwenyezi Mungu katika Taurati, na wakiyafahamu vilivyo, kisha makusudi wakiyageuza na hali wanajua kuwa ni kweli, na kuwa vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyo teremshwa haijuzu kuvigeuza.
Na wanapo kutana na wale walio amini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao, wao kwa wao, husema: Mnawaambia aliyo kufunulieni Mwenyezi Mungu ili wapate kukuhojieni mbele ya Mola wenu Mlezi? Basi hamfahamu nyinyi?
Na kilikuwapo kikundi kingine miongoni mwa wanaafiki wao wakikutana na walio amini husema kwa kuwakhadaa: Tunaamini kuwa nyinyi mnafuata Haki, na kuwa Muhammad ni Nabii aliye tajwa sifa zake katika Taurati. Na wakiwa peke yao na wenzao hulaumiana kwa kughafilika kwa baadhi yao, kwa vile ndimi zao zilivyo teleza katika kuwakhadaa Waumini kuwapa maneno ambayo yatawapa faida makhasimu zao, na wala si lazima katika udanganyifu, wakawatajia yaliyomo katika Taurati ya kueleza kwa sifa kuja kwa Muhammad na kwa hivyo itakuwa hoja juu yao Siku ya Kiyama.
Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza?
Hivyo basi haiwapitikii watu hawa na wale kuwa Mwenyezi Mungu hana haja ya kupata hoja kama hizo? Kwani Yeye anajua wanacho kificha na wanacho kidhihirisha.
Na wako miongoni mwao wasio jua kusoma; hawakijui Kitabu isipo kuwa uwongo wanao utamani, nao hawana ila ni kudhania tu.
Na miongoni mwa Mayahudi kipo kikundi cha wajinga wasio jua kusoma, wasio jua chochote kutokana na Taurati ila uwongo unao wafikiana na matamanio yao, wanao wapachikia pachikia makohani wao, na wakaona katika mawazo yao kuwa hayo ni kweli iliyotoka Kitabuni.
Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyo andika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayo yachuma.
Basi hao makohani wataangamia na watapata adhabu kwa vile wanavyo andika vitabu kwa mikono yao, kisha wakawaambia wajinga wasiojua kusoma kuwa: Hii ni Taurati iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Kusudi lao ni kuwa wapate kwa hayo pato la upuuzi la kidunia, wanunue upuuzi huu kwa kuuza Haki na Kweli. Basi ole wao kwa wanayo mzulia Mwenyezi Mungu, na ole wao kwa yale matunda wanayo yachuma kwa uzushi wao!
Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu hatokwenda kinyume na ahadi yake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua?
Na katika khitilafu zao ni haya wanayo yapata kwa makohani ya kuwa Moto hautawagusa Mayahudi hata wakifanya maasia namna gani ila kwa muda wa siku chache tu. Basi waambie ewe Muhammad!: Nyinyi mmeagana na Mwenyezi Mungu kwa hayo, hata mkawa mmetumaini kuwa Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake, au mnamzulia uwongo tu?
Naam, anaye chuma ubaya - na makosa yake yakamzunguka hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.
Ukweli wa mambo ni kuwa nyinyi mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo. Kwani hukumu ya Mwenyezi Mungu inapitishwa kwa viumbe vyake vyote sawa sawa, hapana farka baina ya Yuhudi na asiye kuwa Yahudi. Wenye kutenda maovu, na maovu yakawazunguka hao waovu mpaka njia za kuokoka zote zikazibwa, basi hao ndio watu wa Motoni na huko watudumu milele.
Na wale walio amini na wakatenda mema, hao ndio watu wa Peponi, humo watadumu.
Na wale walio amini na wakatenda mema hao ndio watu wa Peponi, kwa sababu wao wameamini na wakatimiza iliyo wajibisha Imani yao, nayo ni vitendo vyema, basi wao watakaa Peponi daima milele.
Na tulipo funga agano na Wana wa Israili: Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Swala, na toeni Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.
Mbali na haya yote, nyinyi jamaa wa Kiyahudi, mnaendelea kuyashughulikia madhambi na kuvunja ahadi, na kupindukia mipaka aliyo kuwekeeni Mwenyezi Mungu. Kumbukeni tulipo chukua ahadi kwenu katika Taurat kuwa hamtamuabudu ila Mwenyezi Mungu, na mwatendee wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na mnapo zungumza na watu mtumie maneno mazuri ya kuleta masikilizano baina yenu nao wala sio ya kukutenganisheni, na mtimize yaliyo kuwa waajibu juu yenu, nayo ni Swala, na Zaka. Na kumbukeni ulikuwaje mwendo wenu katika ahadi hiyo? Vipi mlivyo ivunja na mkajipuuza nao, isipo kuwa wachache tu ndio walio ifuata Haki?
Na tulipo chukua agano lenu kuwa hamtamwaga damu zenu, wala hamtatoana majumbani mwenu; nanyi mkakubali nanyi mnashuhudia.
Na kumbukeni tulipo chukua ahadi kwenu katika Taurat kuwa hamtakuwa mkimwaga damu zenu, wala hamtafukuzana katika majumba yenu. Na ahadi hiyo mnakubali kuwa ipo katika Kitabu chenu na mnashuhudia kuwa ni kweli.
Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani kwao, mkisaidiana kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni mateka mnawakomboa, na hali kuwatoa mmekatazwa. Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda.
Nanyi wenyewe kwa wenyewe mnauwana, na mnatoana majumbani, nyinyi kwa nyinyi: hawa wanawauwa hawa na hawa wanawauwa hawa; hawa wanawafukuza hawa majumbani mwao na hawa wanawafukuza hawa. Na huku mkisaidiana katika vitendo vya dhambi na uadui. Baada ya hayo wakitokea baadhi yenu wakatekwa na hao mnao shirikiana nao mnajishughulisha kwenda kuwakomboa hao mateka. Mkiulizwa nini kilicho kupelekeeni kuwakomboa, mnajibu kuwa vitabu vyenu vinakuamrisheni kukomboa mateka wa Kiyahudi. Jee, vitabu hivyo havikukuamrisheni msimwage damu ya ndugu zenu? Havikukuamrisheni msiwatoe watu majumbani mwao? Hivyo nyinyi mnat'ii sehemu ya yaliyo kujieni katika Kitabu na mnayakataa mengineyo? Basi jaza ya mwenye kutenda hayo katika nyinyi si lolote ila kupata hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu, anaye vijua vyema vitendo vyao na siri zao, atawapeleka kwenye adhabu iliyo kali kabisa. Kabla ya Uislamu zilikuwapo katika mji wa Madina kabila mbili za Kiarabu ambazo zilikuwa na uadui baina yao, nazo ni Aus na Khazraj. Na pia zilikuwako kabila za Kiyahudi nazo ni Banu Quraidha na Banu Nnadhir. Banu Quraidha walifungamana na Aus, na Banu Nnadhir walifungamana na Khazraj. Ilikuwa kabila mbili za Kiarabu zikipigana, zile kabila za Kiyahudi nazo huingia vitani, kila kabila upande wa rafiki zake, na zikiuwana na wenzao wa dini moja nao, na wakifukuzana makwao. Lakini kila moja katika kabila mbili hizo za Kiyahudi zikishughulika baadaye kuwakomboa mateka walio tekwa na rafiki zao wa Kiarabu. Wakiulizwa kwa nini mnawakomboa na hao walikuwa wakipigana nanyi upande wa maadui zenu? Wao wakisema: Mwenyezi Mungu ametuamrisha katika Taurati tuwakomboe mateka wa Kiyahudi. Na wanajifanya hawajui kama Mwenyezi Mungu amewaamrisha vile vile wasiuwane wala wasitoane majumbani mwao. Kwa hivyo ndio wanaamini sehemu ya Kitabu na wanaikataa nyengine.
Hao ndio walio nunua uhai wa dunia kwa (uhai wa) Akhera; kwa hivyo hawatapunguziwa adhabu wala hawatanusuriwa.
Na hayo ni kwa kuwa wamekhiari mapato ya hii dunia ipitayo kuliko neema za Akhera zitakazo dumu. Katika haya wamekuwa kama mtu aliye uza Akhera yake kwa ajili ya kununua dunia. Basi hawatapunguziwa adhabu ya Jahannam, wala hawatapata wa kuwaokoa nayo.
Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.
Enyi Mayahudi, kumbukeni vile vile, ule msimamo wenu wa upotovu na wenye dhambi kwa mnasaba wa Musa na Mitume mingine tulio watuma. Kwani tulimtuma kwenu Musa na tukampa Taurati, na kumfwatia yeye tuliwaleta Mitume kadhaa wa kadhaa wengineo. Miongoni mwao ni: Isa bin Maryamu ambaye tulimpa miujiza na tukamuunga mkono kwa Roho Mtakatifu, naye ni Jibril Mjumbe muaminifu wa Ufunuo. Nanyi kila akikujilieni Mtume asiye wafikiana na matamanio yenu mnatakabari na hamtaki kumfwata. Mitume wengine mliwakataa na kuwaambia waongo, na wengine mliwauwa khasa.
Na walisema: Nyoyo zetu zimefunikwa. Bali Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru zao: kwa hivyo ni kidogo tu wanayo yaamini.
Hali kadhaalika msimamo wenu kwa Mtume wetu Muhammad, Nabii wa mwisho. Mlimwambia alipo kuiteni msilimu: Nyoyo zetu zimefunikwa kwa vifuniko visivyo achilia kupenya huo wito wako. Basi sisi hatuelewi kitu chochote unacho sema! Wala nyoyo zao hazikufunikwa kama wanavyo dai, lakini wamepanda kiburi tu, na wakakhiari upotovu kuliko uwongofu. Basi Mwenyezi Mungu amewalaani kwa ukafiri wao, na amedhoofisha yakini yao na imani yao.
Na kilipo wajia Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kinacho thibitisha waliyo nayo - na wao walikuwa wakitafutia ushindi kuwashinda makafiri - yalipo wajia yale waliyo kuwa wakiyajua waliyakanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu juu ya wakanushao!
Na Mtume wetu alipo wajia na Qur'ani, nayo ni Kitabu kilicho toka kwa Mwenyezi Mungu kinacho thibitisha Taurati walio teremshiwa wao, na wakajua kutokana na hiyo Taurati ukweli uliomo katika Kitabu hichi (Qur'ani) walikataa kwa inadi na uhasidi tu, kwa sababu yamekuja hayo kutokana na Mtume asiye kuwa wa taifa lao la Wana wa Israili, juu ya kuwa kabla yake walipo kuwa wakipambana na makafiri washirikina ikiwa mpambano wa vita au majadiliano, wakitaja kuwa Mwenyezi Mungu atakuja wanusuru wao kwa kumtuma Nabii wa mwisho aliye bashiriwa katika Kitabu chao, na ambaye sifa zake zimewafikiana kabisa moja kwa moja na sifa za Muhammad. Jueni basi laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya watu wa namna hii wenye inda na ukanushi. (Mwenyezi Mungu alimwambia Musa: "Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe...mtu asiye sikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake." --Kumbukumbu la Torati 18.18-22. Maana ya haya ni: Taurati inasema kwamba Nabii Musa aliambiwa na Mungu kwamba atawaletea Nabii kutokana na ndugu za Wana wa Israili, yaani Waarabu. Na asiye mfuata Nabii huyo Mwenyezi Mungu atamuadhibu.)
Kiovu kweli walicho jiuzia nafsi zao, nacho ni kule kukataa kwao aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kuona maya kwa kuwa Mwenyezi Mungu humteremshia fadhila yake amtakaye miongoni mwa waja wake. Basi wamejiletea wenyewe ghadhabu juu ya ghadhabu. Na makafiri watapata mateso ya kudhalilisha.
Kiovu mno walicho ziuzia nafsi zao na roho zao! Na hayo ni kwa udhalimu wao, na kuona maya na kufanya uadui tu. Matamanio yao na chuki zao za kikabila, na ugozi walio nao, ndio ulio wapelekea kukataa tulio yateremsha Sisi, kwa kuonea uchungu vipi Mwenyezi Mungu kumpa ujumbe wake Mtume asiye tokana na wao. Wanamkatalia Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kukhiari atakavyo nani wa kumteremshia fadhila yake miongoni mwa waja wake. Kwa hivyo wamejipalilia wenyewe ghadhabu juu ya ghadhabu kwa kufuru zao na inadi zao na uhasidi wao. Na makafiri kama hawa watapata adhabu ya kuwadhalilisha na kutia uchungu.
Na wanapo ambiwa: Yaaminini aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu. Wao husema: Tunaamini tuliyo teremshiwa sisi. Na huyakataa yasiyo kuwa hayo. Na hali ya kuwa hii ndiyo Haki inayo thibitisha yale waliyo nayo wao. Sema: Mbona mliwauwa Manabii wa Mwenyezi Mungu hapo zamani ikiwa kweli mlikuwa Waumini?
Hizi ndizo dhamiri walizo nazo ndani ya nafsi zao. Lakini mbele za watu wakijitetea kuwa wao hawaiamini Qur'ani wanapo takiwa waamini, kwa kuwa wao hawaamini ila yale walio teremshiwa wao tu, na wanayakataa mengineyo. Na hakika wanasema uwongo kwa hayo madai yao kuwa wanaamini yaliyomo katika Taurati, kwani kwa kukitaa Kitabu hichi cha Qur'ani kinacho thibitisha Kitabu chao, ndio kuwa maana yake wanakataa Kitabu chao chenyewe, na kwa kuwa wao waliwauwa Manabii walio kuwa wanawaitia yale walio teremshiwa. Na wao kuwauwa hao ni dalili ya kukata kuwa hawauamini Ujumbe wao.
Na alikufikieni Musa na hoja zilizo waziwazi, kisha mkamchukua ndama (kumuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
Bali hakika nyinyi Mayahudi mlikanusha kwa uwazi Vitabu vyenu, na mkarejea katika ushirikina katika zama za Musa mwenyewe. Kwani Musa alikujieni na hoja zilizo wazi, na miujiza inayo hakikisha ukweli wake, lakini kiasi ya kukupeni mgongo tu alipo kwenda kusema na Mola wake Mlezi nyinyi mkaingia kuabudu ndama, na mkarajea katika ukafiri wenu wa kuabudu masanamu, na nyinyi mkawa mlio dhulumu mlio potea.
Na tulipo chukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu (tukakwambieni): Kamateni kwa nguvu haya tuliyo kupeni na sikieni. Wakasema: Tumesikia na tumekataa! Na wakanyweshwa nyoyoni mwao (imani ya) ndama kwa kufuru yao. Sema: Ni uovu mno iliyo kuamrisheni imani yenu ikiwa ni wenye kuamini.
Na alipo kuleteeni Taurati mkaziona amri ngumu ziliomo ndani yake, mkaona mizito mizigo yake na mkaitilia shaka, Mwenyezi Mungu alikuonyesheni Ishara ya ukweli wa Kitabu hicho na faida ya mafunzo yake kwenu. Akaunyanyua Mlima wa T'uur juu ya vichwa vyenu hata ukawa kama kiwingu, na mkadhani kuwa utakuangukieni. Hapo mkaonyesha kukubali na kut'ii. Tukachukua ahadi yenu kuwa hamtaghurika na pumbao katika kufuata yaliyomo katika Kitabu hichi. Mkasema: Tumeamini na tumesikia. Lakini vitendo vyenu vimefichua uasi wenu, na kwamba imani haijaingia katika nyoyo zenu. Wala hayumkini kuwa imani imeingia katika nyoyo za watu walio shughulishwa na mapenzi ya kumuabudu ndama. Imani yenu hiyo mnayo dai basi imekusozeni kwenye maovu.
Sema: Ikiwa nyumba ya Akhera iliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni yenu tu bila ya watu wengine, basi tamanini mauti kama nyinyi mnasema kweli.
Na nyinyi mmedai kuwa Mwenyezi Mungu atakupeni nyinyi tu neema za Pepo baada ya kufa, wasipate watu wote wengineo. Ikiwa basi kweli mnaamini hayo myasemayo basi yafaa myapende mauti. Hebu yatamanini myapate upesi zisije kutaakhari hizo starehe mnazodai.
Wala hawatayatamani kamwe kwa sababu ya yale yaliyo tangulizwa na mikono yao; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua vyema wanao dhulumu.
Lakini kwa hakika mambo yalivyo, wao hawayatamani mauti kabisa kwa dhulma walio ifanya, ambayo haifichikani kwa Mwenyezi Mungu. Yeye anawajua kuwa wao ni waongo kwa hayo wanao dai. Neema za Siku ya Kiyama zitakuwa ni za wachamngu, si za wafanyao maovu kama wao.
Na hakika utawaona ni wenye kuwashinda watu wote kwa pupa ya kuishi, na kuliko washirikina. Kila mmoja wao anatamani lau angeli pewa umri wa miaka elfu. Wala hayo ya kuzidishiwa umri hayamuondoshei adhabu; na Mwenyezi Mungu anayaona wanayo yatenda.
Bila ya shaka yoyote utawakuta wao ndio wamewashinda watu wote kwa pupa waliyo nayo kuwania maisha ya dunia ya kila namna, ya utukufu na unyonge. Na hiyo pupa yao inashinda ya makafiri washirikina (mapagani) wasio amini kufufuliwa wala Pepo. Kwa hivyo wanapenda lau kuwa wangelizidishiwa umri wakaishi hata miaka elfu. Na hata wangeliishi vipi hawawezi kuepuka adhabu ya Mwenyezi Mungu inayo wangojea. Kwani Yeye ni Mjuzi wa hao madhaalimu, na atawaonjesha malipo ya vitendo vyao wanavyo vitenda
Sema: Aliye kuwa ni adui wa Jibril, basi huyo ndiye aliye iteremsha Qur'ani moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu inayo thibitisha yaliyo kuwa kabla yake, na ni uwongofu na bishara njema kwa Waumini.
Na baadhi yao wanadai kuwa wanakupinga na wanakikataa Kitabu chako kwa kuwa ati wao ni maadui wa Jibril anaye kufikishia hichi Kitabu. Basi sema ewe Nabii uwaambie: Anaye kuwa Jibril ni adui wake, basi vile vile huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Jibril haji na Kitabu hichi kwa nafsi yake, bali anakiteremsha kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Na Kitabu hichi kinathibitisha Vitabu vilivyo tangulia kutoka mbinguni.. na kinathibitisha Kitabu chenu wenyewe..na hii Qur'ani (inayo teremshwa na Jibril kutoka kwa Mwenyezi Mungu) ni Uwongofu na Bishara njema kwa Waumini.
Aliye kuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika wake na Mitume wake na Jibril na Mikail, basi hakika Mwenyezi Mungu ni adui wa makafiri.
Basi yeyote anaye kuwa ni adui wa Jibril, au Mikail, au Malaika yeyote au Mtume yeyote, miongoni mwa Malaika na Mitume wa Mwenyezi Mungu, ambao hawafanyi kitu wala hawapeleki ujumbe ila kama vile Mwenyezi Mungu anavyo waamrisha, basi mtu huyo anakuwa ni adui wa Mwenyezi Mungu, na anakuwa kafiri anamkataa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni adui wa makafiri.
Hakika tumekuteremshia Ishara zilizo wazi na hapana wanao zikataa ila wapotovu.
Na Jibril hateremshi kwenye moyo wako kila Ishara na hoja zilizo wazi, ambazo haiwezekani kwa mwenye kutafuta haki kikweli ila aziamini tu. Na hapana mwenye kuzikataa Ishara kama hizo ila wale wafanyao inda na inadi, ambao wametokana na mwenendo wa maumbile walio umbwa nao.
Je! Ati ndio kila wanapo funga ahadi huwapo kikundi miongoni mwao kikaivunja? Bali wengi wao hawaamini.
Na kama (hawa Wana wa Israili) walivyo kuwa vigeugeu katika itikadi na imani, hali kadhaalika walikuwa vigeugeu katika ahadi na mapatano wanayo choka nayo. Walikuwa kila wanapo fungamana na Waislamu au wengineo kwa maagano hutokea kikundi miongoni mwao wakavunjilia mbali maagano hayo. Kwani wengi wao hawaamini utukufu wa ahadi na utakatifu wa maagano.
Na alipo wajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwenye kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale walio pewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui.
Na alipo wajia Mtume aliye toka kwa Mwenyezi Mungu aliye wafikiana sawa sawa na sifa zilizo tajwa katika Vitabu vyao, naye ni Muhammad, rehema na amani iwe juu yake, kikundi kimojapo kutokana nao kilikataa hayo yaliyo tajwa katika Vitabu vyao kumkhusu Mtume huyu, kama kwamba halikutajwa jambo hilo humo wala wao hawajui lolote katika hayo.
Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani kuuzulia ufalme wa Su leiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani ndio walio kufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyo teremshwa kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua kwamba aliye khiari haya hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walicho jiuzia nafsi zao laiti wangelijua.
Na wao hakika waliyasadiki waliyo yazua mashetani wao na wapotovu wao juu ya ufalme wa Suleiman, walipo dai kuwa Suleiman hakuwa Nabii wala si Mtume aliye teremshiwa ufunuo (Wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bali alikuwa ni mchawi tu anaye tegemea msaada wa uchawi wake. Na kwamba ni uchawi wake huu ndio ulio mjengea ufalme wake na ukamwezesha aweze kuwatawala majini, na ndege, na upepo. Kwa hivyo walimsingizia ukafiri Suleiman, na hali Suleiman hakukufuru, lakini hao mashetani waovu ndio walio kufuru. Wao ndio walio zua uzushi huu, wakaingia kuwafunza watu uchawi wao na walio pokea katika mabaki yaliyo teremka katika Baabil (Babilonia) kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta. Na hawa Malaika wawili hawakuwa wakimfundisha mtu yeyote mpaka wamwambie: Sisi ni mtihani uwe ni majaribio kwenu, tunakufundisha mafunzo ambayo yanaweza kuleta fitna na ukafiri, basi jifunze lakini tahadhari usiitumie ilimu hii. Na lakini watu hawakunasihika kwa nasiha hii, na wakatumia hayo waliyo jifunza kwa hao Malaika wawili ya kumgombanisha mtu na mkewe. Naam, hawa mashetani waovu wamekufuru walipo zua katika uzushi wao na hadithi zao za uwongo wakafanya hayo ndio wasila na udhuru wa kuwafundishia Mayahudi uchawi. Na wao hao wachawi hawawezi kumdhuru yeyote, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Yeye anayeweza kumletea mtu madhara pindi akipenda. Na hayo ya uchawi wao yanawadhuru hao wanao jifunza katika dini yao na dunia yao, na wala hawapati faida yoyote. Na wao wanajua kweli ya kujua ya kwamba anaye elekea upande huu hana sehemu yoyote katika neema za Akhera. Na kama wamebakia na ujuzi wowote yafaa wajue kuwa haya waliyo yakhiari kwa ajili ya nafsi zao ni hadi ya kuwa maovu.
Na lau kuwa wangeamini na wakaogopa, bila ya shaka malipo yatokayo kwa Mwenyezi Mungu yange kuwa bora. Laiti wangeli kuwa wanajua!
Na lau kuwa wao wameiamini Haki na wakauogopa ufalme na uwezo wa Mola wao Mlezi, basi Mwenyezi Mungu angeli walipa malipo mema, na hayo bila ya shaka yoyote yangeli kuwa ni bora zaidi kuliko wanayo yapata katika hadithi zao za uwongo na dhamiri zao mbovu wanazo zidhamiria, lau kuwa wanabagua linalo kuwa na manufaa wakaacha lenye madhara.
Enyi mlio amini! Msiseme: "Raa'ina", na semeni: "Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.
Enyi mlio amini! Tahadharini na hawa Mayahudi. Msimwambie Mtume pale anapo kusomeeni ufunuo: "Raa'ina" kwa kukusudia akuwekeni pahala pa uangalizi wake, yaani (Tuchunge, Turai), na akupeni muda katika kusoma kwake mpaka mzingatie na mhifadhi. Kwani watu makhabithi miongoni mwa Mayahudi husaidiana kutaka kukuigeni na kupindua ndimi zao kwa neno hilo mpaka likawa neno la matusi wanalo lijua wao. Na wao humkabili Mtume kwa neno hilo kwa kumfanyia maskhara. Lakini nyinyi tumieni neno jingine wasilo weza Mayahudi kulipatia njia ya kufanya ukhabithi wao na maskhara yao. Tumieni neno: "Ndhurna" yaani "Tuangalie". Na sikilizeni vyema anayo kusomeeni Mtume. Na Mwenyezi Mungu anawadundulizia adhabu kali kwa Siku ya Kiyama hawa wanao mfanyia maskhara Mtume. Katika lugha ya Kiyahudi ya Kiebrania lipo neno "Rai'nu" ambalo limejengwa na neno "Ra'" kwa maana ya "Shari" na neno "nu" linaonesha jamii, wingi. Na maana ya neno lote ni kuwa "Wewe ni shari yetu", wakikusudia kumwambia Mtume hayo.
Walio kufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na washirikina hawapendi mteremshiwe kheri yoyote kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa rehema yake ampendaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.
Na yafaa mjue kuwa hawa makafiri wa Kiyahudi na washirikina waabuduo masanamu hawakutakieni ila mdhurike tu, wala hawapendelei iteremke kheri yoyote kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na Mwenyezi Mungu hathamini chochote wanacho kipenda wala wanacho kichukia. Kwani Mwenyezi Mungu humteua amtakaye kwa kumkhusisha kumpa rehema yake, na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.
Ishara yoyote tunayo ifuta au tunayo isahaulisha tunailetea iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu?
Nao walikutaka wewe Muhammad, uwaletee miujiza, ishara, ile waliokuja nayo Musa na Manabii wa Wana wa Israili. Sisi yatutosha kuwa tumekutia nguvu kwa kukuletea Qur'ani. Na Sisi tunapo acha nguvu kumpa Nabii anaye kuja nyuma kwa muujiza wa Nabii aliye tangulia, au tukawasahaulisha watu athari za muujiza ule, basi Sisi humletea huyu Nabii aliyekuja baadaye muujiza, kuwa ni Ishara, au Aya, iliyo bora zaidi au mfano wa ile ili kuwa ni dalili ya ukweli wake. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. (Na hapana Ishara, Muujiza au Aya, iliyo kubwa na bora na yenye kudumu kuliko hii Qur'ani.)
Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa Mbingu na Ardhi? Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
Na Yeye, Mwenyezi Mungu, ndiye mwenye ufalme wa Mbingu na Ardhi katika mikono yake. Na nyinyi watu hamna mlinzi wa kukusaidieni, wala tegemeo la kukunusuruni isipokuwa Yeye.
Au mnataka kumwomba Mtume wenu kama alivyo ombwa Musa zamani? Na anaye badilisha Imani kwa ukafiri bila ya shaka huyo ameipotea njia iliyo sawa.
Na kwa kule kumtaka kwenu Mtume wenu Muhammad miujiza fulani pengine ilikuwa mnawaiga Wana wa Israili wa zama za Musa, walipo mtaka awaletee miujiza maalumu. Kutaka kwenu huku kunaficha nyuma yake inda na kumili kwenye ukafiri, kama kulivyo kuwa kule kutaka kwa Wana wa Israili kumtaka Mtume wao. Na mwenye kufuata nyayo za inda na ukafiri akaacha usafi wa kutaka Haki na Imani basi huyo ameipotea Njia iliyo sawa iliyo nyooka.
Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wange kurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwisha wapambanukia Haki. Basi sameheni na wachilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu atapo leta amri yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Na wengi miongoni mwa Mayahudi wametamani kukurejesheni, enyi Waislamu, kwenye ukafiri baada ya kuwa nyinyi mmekwisha amini. Na haya juu ya kuwa wao imekwisha wadhihirikia kutoka na hicho hicho Kitabu chao kuwa nyinyi mpo juu ya Haki. Na hayakuwa hayo ila ni kuwa wanakuhusuduni na wanaogopa utawala usiwatoke mikononi mwao mkapewa nyinyi. Basi nyinyi wapuuzeni, na wasameheni, na waachilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu akuonyesheni lipi jengine la kuwafanyia, kwani Yeye ni Muweza wa kukupeni ushindi juu yao, na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Na shikeni Swala na toeni Zaka; na kheri mtakazo jitangulizia nafsi zenu mtazikuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yafanya.
Na hifadhini mambo ya Dini yenu: Shikeni Swala, toeni Zaka, na vitendo vyote vyema mnavyo fanya kujitangulizia nafsi zenu, na sadaka mnazo toa, malipo yake mtayakuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua vyema myatendayo; ujuzi wake ni ujuzi wa mwenye kutazama akaona.
Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa Yahudi au Mkristo. Hayo ni matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni wasema kweli.
Na katika upotovu wa Mayahudi na Wakristo na matamanio yao ya uwongo, ni yale madai yao kila mmoja wao kuwa hataingia Peponi ila mwenye kufuata dini yao. Hebu watakeni wa kutoleeni ushahidi wa hayo madai yao kama kweli wanasema kweli.
Sivyo hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
Na wala hawatapata ushahidi wa hilo. Kwani kweli ilivyo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaandalia neema za Pepo, na atawalipa malipo Siku ya Kiyama, na atawalinda na khofu na huzuni, hao ambao wanao msafia niya Mwenyezi Mungu na wanafuata Haki, na vitendo wavitendavyo ni vyema.
Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo. Na Wakristo husema: Mayahudi hawana lao jambo. Na ilhali wote wanasoma Kitabu hicho hicho (Biblia). Na kadhaalika walisema wale wasio jua kitu mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitilafiana.
Na ajabu iliyopo ni kuwa kama wanavyo fanyia uadui Uislamu, wanafanyiana uadui wenyewe, wao kwa wao. Mayahudi husema: Wakristo hawana lolote la haki. Na Wakristo nao wanasema mfano wa hayo, na huku wote wawili wanatoa ushahidi wao kutoka hivyo hivyo vitabu vyao vya Biblia wanavyoviamini wao wote. Na wale washirikina wa Kiarabu wasio jua chochote katika vitabu vilivyo teremshwa kwa Mayahudi na Wakristo husema maneno kama hayo. Na kwa hakika wote hao pamoja wamesema kweli, kwani hapana kikundi kimojapo katika wao kilicho kuwamo katika Haki. Na hayo yatabainika pale Mwenyezi Mungu atapo wahukumu Siku ya Kiyama katika zile khitilafu zao wanazo khitilafiana.
Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye zuia misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa ndani yake jina lake na akajitahidi kuiharibu? Watu hao haitawafalia kuingia humo ila nao wanaogopa. Duniani watapata hizaya na Akhera watapata adhabu kubwa.
Katika yanayo dhihirisha uadui wa wao kwa wao na uadui wao wote kwa Waislamu, ni kule baadhi ya mataifa yao yalivyo kuwa yakiharibu pahala mwa ibada ya mataifa mengineo, na vile wale washirikina walivyo kuwa wakiwazuia Waislamu wasiingie Msikiti Mtakatifu wa Makka. Na hapana kabisa mwenye kudhulumu zaidi kuliko azuiaye asitajwe Mwenyezi Mungu katika pahala pa ibada, na akafanya juhudi kutaka kupaharibu. Watu hao watapata hizaya duniani, na Akhera watapata adhabu kubwa. Haiwafalii wao kufanya ukhalifu kama huu muovu, bali iwapasavyo ni kulinda utakatifu wa pahala pa ibada, wala wasiingie humo ila kwa unyenyekevu na kukhofu, wala wasizuilie kutajwa jina la Mwenyezi Mungu ndani yake. (Na ufisadi kama huu, bali ni mkubwa zaidi, ni wa wale wanao ghusubu (kuiba) mali za wakfu ya misikiti.)
Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnako elekea, huko Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa na Mjuzi.
Ikiwa washirikina waliwazuia Waislamu kusali katika Msikiti Mtakatifu wa Makka, hawatoweza kuwazuia kusali na kumuabudu Mwenyezi Mungu. Kwani jiha zote na pande zote za dunia ni za Mwenyezi Mungu. Na hakika bila ya shaka Mwenyezi Mungu anampokelea Muislamu Sala zake, na anamkabili kwa radhi yake pande zote anapo fanya ibada yake. Kwani Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa, hawadhikishi waja wake, na Yeye ni Mwenye kuijua vyema niya ya mwenye kumuelekea.
Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu! Ametakasika na hayo. Bali vyote viliomo mbinguni na duniani ni vyake. Vyote vinamt'ii Yeye.
Basi huyo ambaye mambo yake ni kama hivi, na vyote viliomo ulimwenguni vinat'ii amri yake, vinanyenyekea kwa atakalo, basi Yeye huyo yuko juu mno, na mtukufu mno hata hahitajii kuwa na dhuriya au kujipa wana, kama wanavyo zua hawa Mayahudi na Wakristo na washirikina mapagani.
Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza; na anapo taka jambo basi huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa.
Vipi awe na haja ya uzazi au atafute mwana huyo aliye anzisha kuumba Mbingu na Ardhi bila ya kuwa na kiigizo chochote kabla yake, na akavifanya vyote viliomo humo vimt'ii Yeye kwa kila atakalo, na visiweze kumuasi? Yeye akitaka kitu basi husema tu: Kuwa! Kikawa.
Na walisema wale wasio jua kitu: Mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi au zikatufikia Ishara. Kama hivyo walisema wale walio kuwa kabla yao mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka wazi Ishara kwa watu wenye yakini.
Washirikina wa Kiarabu walikakamia katika inadi yao kumfanyia Muhammad, wakamtaka kama wale kaumu zilizo tangulia zilivyo wataka Manabii wao. Wakasema kuwa hawatomuamini ila Mwenyezi Mungu aseme nao, na awaletee ishara, au muujiza wa kuuona utakao onesha ukweli wake. Haya ni kama walivyo sema Wana wa Israili kumwambia Musa: Hatukuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu na aseme nasi. Na kama masahaba (wanafunzi) wa Isa walipo mtaka awateremshie chakula kutoka mbinguni. Na haya yote ni kuwa nyoyo za makafiri na wapinzani wenye inda katika kila umma zimefanana. Haki haidhihiriki ila kwa wale ambao kuona kwao kumesafika, na akili zao zimeelekea kufuata Yakini, na kuitaka Haki.
Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki uwe mbashiri, na mwonyaji. Na wala hutaulizwa juu ya watu wa Motoni.
Na Sisi tumekutuma ufikishe Haki iliyo yakini ili uwape bishara njema Waumini, na uwaonye makafiri. Na waajibu wako ni kufikilisha tu ujumbe wetu, wala wewe hutosailiwa kwa kukosa Imani hao wasio kuamini, ambao wataingia Motoni.
Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata mlinzi wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.
Basi usijikere nafsi yako kwa kutaka kuwaridhi hao wapinzani wa Kiyahudi na Wakristo. Kwani hao hawatakuwa radhi nawe mpaka ufuate mila yao hao ambao wanadai ati ndio wenye uwongofu. Na kabisa hapana uwongofu ila uwongofu wa Mwenyezi Mungu ulioko katika Uislamu. Na mwenye kufuata matamanio ya watu hawa baada ya kuijua Haki tuliyo kuteremshia wewe, basi Siku ya Kiyama hatapata mlinzi wa kumsaidia mbele ya Mwenyezi Mungu, wala hatapata wa kumnusuru na adhabu.
Wale tulio wapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini. Na wanao kikataa basi hao ndio wenye kukhasiri.
Tena kipo kikundi katika Mayahudi na Wakristo walio wataalamu katika vitabu vyao vya asli, na wakavisoma vilivyo, na wakafahamu mageuzo yaliomo ndani yake, hao wanauamini ukweli wa mambo, na kwa hivyo wanaiamini hii Qur'ani. Na wenye kukikataa Kitabu kilicho teremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu hao ndio wenye kukhasiri.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo kuneemesheni, na hakika Mimi nikakufadhilisheni kuliko wengineo wote.
Enyi Wana wa Israili! Aminini na mkumbuke neema kubwa niliyo kupeni kwa nilivyo kutoeni kwenye dhulma ya Firauni na nilivyo mzamisha baharini, na nilivyo kupeni Manna na Salwa, na nikakuleteeni Manabii kutokana miongoni mwenu, na nikakufunzeni Kitabu, na mengi mengineyo ya utukufu niliyo kupeni. Pia nikakunyanyueni kwa wakati fulani kuliko watu wote kwa vile nilivyo wateuwa Manabii kadhaa kutokana nanyi.
Na iogopeni siku ambayo hatamfaa mtu mwenziwe kwa lolote, wala hakitakubaliwa kwake kikomboleo, wala maombezi hayatamfaa, wala hawatanusuriwa.
Na iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu katika siku ambayo hapana mtu ataye weza kumtetea mwenziwe kwa lolote, wala fidia haitakubaliwa, wala maombezi hayatafaa kitu, wala makafiri hawatapata mtu wa kuwanusuru na Mwenyezi Mungu.
Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi wa watu. Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu.
Na kumbukeni pale Mwenyezi Mungu alipo mjaribu babu yenu Ibrahim kwa kumtwisha amri fulani. Naye Ibrahim alizitimiza hizo amri vilivyo. Mwenyezi Mungu akamwambia: Mimi nataka kukufanya wewe uwe Imamu, yaani Mwongozi, wa watu, nao wawe wakikufuata wakishika nyayo zako. Ibrahim akamtaka Mola awajaalie katika vizazi vyake wawe pia Maimamu kama yeye. Mwenyezi Mungu akamjibu kuwa haya hawatayapata wanao dhulumu, na hivyo kaashiria kuwa mnamo dhuriya za Ibrahim watatokea walio wema na walio wabaya.
Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipo kuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu na wanao jitenga huko kwa ibada, na wanao inama na kusujudu.
Na kadhaalika kumbukeni hadithi ya Ibrahim na mwanawe Ismail walipo ijenga ile Nyumba Takatifu ya Makka, Alkaaba. Katika kisa hichi pana funzo linalo fika mbali kwa mwenye moyo wa kuzingatia. Basi kumbukeni tulipo ifanya Nyumba hii ni pahala wanapo kwenda viumbe kutoka kila pahala duniani na kukusanyika. Na tukaifanya kuwa ni pahala pa usalama na amani kwa kila mwenye kutaka hifadhi. Na pia tulivyo amrisha kuwa pahala alipo kuwa akisimama Ibrahim kuijenga hiyo Nyumba pafanywe ni msala, yaani pahala pa kusalia. Na tukaagana na Ibrahim na Ismail waihifadhi Nyumba hiyo isipate kitu ambacho hakistahiki na utakatifu wake, na waitayarishe kwa matayarisho yanayo silihi kwa wanao kusanyika huko, wale wanao kwenda kut'ufu, na wanao kaa kwa ibada ya ii'tikafu, na wanao sali.
Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya Moto, napo ni pahala pabaya mno pa kurejea.
Na kumbukeni Ibrahim alipo mwomba Mola wake Mlezi ajaalie mji utakao kuwapo hapo kwenye nyumba ya Alkaaba uwe mji wa amani, na awaruzuku matunda ya ardhi na kheri zake watu wake watao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya mwisho. Mwenyezi Mungu alimjibu kuwa hatamnyima riziki hata kafiri muda wa uhai wake mfupi, kisha Siku ya Kiyama atakwenda ingia katika adhabu ya Jahannam, na mwisho wa watu hao ni muovu mno.
Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe ndiye Msikizi Mjuzi.
Na alipo kuwa Ibrahim na mwanawe Ismail wananyanyua misingi ya Alkaaba na huku wakimwomba Mwenyezi Mungu: Mola Mlezi wetu, Ewe Muumba wetu, na Muanzishi wetu! Tupokelee hii kazi yetu tuifanyayo kwa usafi wa niya kwa ajili yako, kwani Wewe ni Mwenye kusikia maombi yetu, ni Mwenye kujua ukweli wa niya yetu.
Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Mola Mlezi wetu! Tuwezeshe na utujaalie tuwe wenye kukusafia niya Wewe, na miongoni mwa vizazi vyetu wajaalie watoke watu wenye kukusafia Wewe. Na tufundishe njia za ibada yetu kukuabudu Wewe katika Nyumba hii takatifu na pembezoni mwake, na pokea toba yetu tunapo sahau au tunapo kosea. Hakika Wewe ni mwingi wa kupokea toba za waja wako, na Msamehevu kwao kwa fadhila yako na rehema yako.
Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anaye tokana na wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Mola Mlezi wetu! Waletee kutokana na vizazi vyetu Mtume miongoni mwao atakaye wasomea Aya zako na atawafundisha yale utakayo mfunulia yeye katika Kitabu na ilimu zenye manufaa na sharia zenye hikima, na awatakase kutokana na tabia mbovu. Hakika Wewe ndiye Mwenye kushinda, Mwenye nguvu, Mwenye hikima katika uyatendayo na unayo yaamrisha na unayo yakataza. Mwenyezi Mungu hakupeleka Mtume kutokana na vizazi vya Ismail ila Muhammad s.a.w. Kwake yeye ndiyo dua hii imepokelewa na Mwenyezi Mungu kwa kutumwa kwa vizazi vya Ismaili na wanaadamu wote.
Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipo kuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini Sisi tulimteuwa yeye katika dunia; na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
Aliyo yafanya Ibrahim na aliyo yaomba kwa Mwenyezi Mungu ni mambo mazuri mno. Hali kadhaalika mila aliyo ifuata ni mila iliyo kwenda sawa kabisa. Na hapana anaye jitenga na mila ya Ibrahim ila mwenye kuudharau utu wake mwenyewe na akili yake. Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa yeye Ibrahim katika dunia, na pia Akhera ni miongoni mwa watu wema walio karibishwa.
Na Mola wake Mlezi alipo mwambia: Silimu, Nyenyekea! Alinena: Nimesilimu, nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu wote.
Yeye Ibrahim aliitikia amri ya Mola wake Mlezi pale alipo mtaka asilimu, yaani anyenyekee. Akasema: Namnyenyekea Mola Mlezi wa walimwengu wote, majini, watu na Malaika.
Na Ibrahim akawausia wanawe, na pia Yaaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteulieni Dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu.
Na Ibrahim hakutosheka na hayo tu, bali aliwausia wanawe wende mwendo wa uwongofu kama wake. Na mjukuu wake Yaakubu akamuiga, naye akawausia wanawe kadhaalika wafuate mwenendo huo huo. Aliwabainishia wanawe ya kwamba Mwenyezi Mungu amewateulia Dini ya Tawhidi, ya Mungu Mmoja. Na akachukua kwao ahadi kuwa hawatakufa ila nao ni Waislamu, wenye kuthibiti juu ya Dini hii.
Je! Mlikuwapo yalipo mfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is- hak, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake.
Na nyinyi Mayahudi mlidai kuwa nyinyi mnakwenda mwendo wa Dini aliyo kufa nayo Yaakubu. Kwani nyinyi mlikuwapo pale mauti yalipo mjia Yaakubu hata mkajua kuwa alikufa katika mila gani? Basi zindukaneni mjue ya kuwa Yaakubu na wanawe walikuwa Waislamu wenye kumuamini Mungu Mmoja, wala wao hawakuwa Mayahudi kama nyinyi, wala hawakuwa Wakristo. ("Uyahudi" umeanza kuitwa hivyo baada ya Yuda, mwana wa Yaakubu. "Ukristo" ni baada ya Isa Masihi, Yesu Kristo. Ama "Uislamu", yaani unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, ni Dini ya maumbile, ipo milele.) Na mjue ya kuwa Yaakubu alipo kabiliwa na mauti aliwakusanya wanawe na akawaambia: Mtaabudu nini baada yangu? Na wao wakajibu: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako Ibrahim na Ismail na Is-hak, Mungu Mmoja; na kwake Yeye tunanyenyekea.
Hao ni watu walio kwisha pita. Watapata waliyo yachuma, nanyi mtapata mtakayo yachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyo kuwa wakiyafanya wao.
Tena imekuwaje enyi Mayahudi kujadili mambo ya watu hawa? Hao ni watu walio kwisha pita na njia yao. Tena wao peke yao watavuna yale waliyo yatenda katika maisha yao. Nyinyi, basi, hamtaulizwa kitu juu ya vitendo vyao, na wala nyinyi hamtapata faida yoyote katika hayo. Nanyi hamtavuna ila yale matunda ya vitendo vyenu mnavyo vitenda nyinyi wenyewe.
Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo ndio mtaongoka. Sema: Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika washirikina.
Lakini wao hawaachi kuendelea katika ghasia na inda zao. Kila kikundi katika hao hudai kuwa ni dini yao wao tu ndiyo iliyo sawa. Mayahudi hukuambieni: Kuweni Mayahudi mpate kuhidika na kuongokewa kwenye njia sawa. Na Wakristo nao wanasema: Kuweni Wakristo ndio mpate kuongoka kwenye haki iliyo nyooka. Nyinyi wajibuni kuwa sisi hatufuati hii wala hii kwa sababu dini zote hizo mbili zimekwisha potoka na zimeacha ile asli yake ya kweli, na zimeingia ndani yake ushirikina (upagani), na ziko mbali kabisa na mila ya Ibrahim. Bali sisi tunaufuata Uislamu ndio ulio ifanya mila ya Ibrahim kuwa safi iliyo safika.
Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.
Waambieni: Sisi tunamuamini Mwenyezi Mungu, na tunaamini Qur'ani iliyo teremshwa kwetu, na kadhaalika tunaamini waliyo teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-hak, na Yaakub na watoto na wajukuu zao, na tunaiamini Taurati ile Mwenyezi Mungu aliyo mteremshia Musa ambayo iliyo kuwa haijakorogwa, na Injili aliyo teremshiwa Isa na Mwenyezi Mungu, ambayo haikukorogwa, na walio pewa Manabii wote kutokana na Mola wao Mlezi. Sisi hatutafautishi hata mmoja kati yao, tukawa tunawakanusha baadhi na kuwaamini wengineo. Na katika haya sisi tunakuwa ndio Waislamu wenye kunyenyekea amri ya Mwenyezi Mungu.
Basi wakiamini kama mnavyo amini nyinyi, itakuwa kweli wameongoka. Na wakikengeuka basi wao wamo katika upinzani tu. Na Mwenyezi Mungu atakutosheni kukukingeni na shari yao, na Yeye ndiye Msikizi, Mjuzi.
Wao wakiamini imani inayo wafikiana na imani yenu basi kweli wameongoka. Lakini wakikakamia katika inadi yao na kukataa kwao basi hao wamo katika ushindani usio koma, na hawana masikizano nanyi. Mwenyezi Mungu atakutosheni kukulindeni na shari yao, ewe Nabii. Na atakupumzisha na ghasia zao za inadi na upinzani wao. Kwani Yeye ni Mwenye kuyasikia wayasemayo, na Mwenye kuyajua hata yaliomo vifuani mwao.
Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu, na nani aliye mbora wa kupaka rangi kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye kumuabudu Yeye tu.
Waambieni: Hakika Mwenyezi Mungu ametuongoa sisi kwa uwongofu wake mwenyewe, na ametuonyesha hoja zake. Na hapana mbora zaidi kwa uwongofu na hoja kuliko Mwenyezi Mungu. Na sisi hatumnyenyekei ila Mwenyezi Mungu. Na wala hatufuati ila anavyo tuongoa na kutuongoza Yeye. (Hilo ndilo pambo, au batizo, au kutia rangi kwa Mwenyezi Mungu--S'ibghatu Llahi).
Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye ni Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.
Waambieni: Mnajadiliana nasi katika mambo ya Mwenyezi Mungu mkidai kuwa Yeye hakuteuwa Manabii ila kutokana nanyi tu? Na Mwenyezi Mungu ni Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa kila kitu; hawapendelei kaumu fulani akawatupa wengine. Rehema yake humfikia amtakaye, na huwalipa watu wote kwa vitendo vyao, bila ya kuangalia nasaba yao na ukoo wao. Na Yeye ametuongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka katika vitendo vyetu. Na ameturuzuku tumsafie niya na vitendo Yeye.
Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zao walikuwa Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule aliye ficha ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na hayo myafanyayo.
Waambieni: Mnajadiliana nasi katika mas-ala ya Ibrahim, na Ismail, na Is-hak, na Yaakub na watoto na wajukuu zao, mkidai kuwa wao walikuwa Mayahudi au Wakristo kama nyinyi, na ilhali Sisi hatukuiteremsha Taurati na Injili wanazo zitegemea Mayahudi na Wakristo ila baada ya hawa. Na Sisi tulikwisha waelezeni khabari ya hayo. Jee, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Bali hakika Mwenyezi Mungu amekwisha waambieni nyinyi hayo katika vitabu vyenu. Basi msiifiche kweli iliyo andikwa katika hivi vitabu vyenu. Na nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye ificha kweli inayo toka katika kitabu chake ambayo naye anaijua. Na Mwenyezi Mungu atakulipeni kwa upotovu mnao ushikilia, kwani Mwenyezi Mungu haghafiliki na mnayo yatenda.
Hao ni watu walio kwisha pita. Wao watapata waliyo yachuma, na nyinyi mtapata mliyo yachuma, wala hamtaulizwa nyinyi yale waliyo kuwa wakifanya wao.
Tena imekuwaje nyinyi Mayahudi na Wakristo kuyajadili mambo ya watu hawa? Kwani watu hawa wamekwisha pita na njia zao. Wao watapata malipo ya a'mali yao waliyo itenda katika uhai wao, wala nyinyi hamtaulizwa juu ya a'mali zao, wala hamtafaidika kwa lolote katika hayo. Nanyi hamtapata malipo ila kwa vitendo mnavyo vifanya nyinyi wenyewe.
WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo nyooka.
Hakika wale wachache wa akili walio potezwa na pumbao lao wasiweza kufikiri sawa na kuzingatia miongoni mwa Mayahudi, na Wakristo, na washirikina na wanaafiki, watachukizwa kuwaona Waumini wameacha kukielekea kibla cha Beitul Muqaddas (Yerusalemu) walicho kuwa wakikielekea kwanza katika Sala. Na wao wakiona kuwa hicho kinastahiki zaidi kuliko kibla kingine, yaani cha Alkaaba. Basi waambie, Ewe Nabii! Jiha zote ni za Mwenyezi Mungu. Hapana upande ulio bora kuliko mwengine kwa dhati yake, lakini Mwenyezi Mungu ndiye mwenyewe anachagua upande autakao uwe ni kibla cha Sala. Na Yeye kwa mapenzi yake huuongoa kila umma katika wanaadamu kufuata njia iliyo sawa anayo ikhiari Yeye na anayo ikhusisha Yeye. Na sasa umekuja Ujumbe wa Muhammad unafuta risala zote zilizo tangulia, na Kibla cha sasa cha Haki ni hichi cha Alkaaba iliyopo Makka.
Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu.
Na kwa ajili ya kutaka huku ndio tukakuongoeni kwenye Njia Iliyo Nyooka kabisa, na tukakujaalieni muwe Umma wa katikati ulio bora kwa muujibu tulivyo iwafikisha Dini sahihi na vitendo vyema, ili muwe wenye kuthibitisha Haki kwa mnasaba wa sharia zilizo tangulia, na ili Mtume awe mlinzi juu yenu, akikupeni nguvu kwa uwongozi wake kwa muda wa uhai wake, na kwa kufuata njia yake na mwendo wake baada ya kufa kwake. Ama kibla cha Beitul Muqaddas tulicho amrisha kifuatwe kwa muda fulani tulikifanya kuwa ni mtihani kwa Waislamu ili watambulikane wanao t'ii wakielekee kwa ut'iifu, na wenye kuchukuliwa na mori wao wa Kiarabu kwa kufuata nyao za Ibrahim tu waivunje amri ya Mwenyezi Mungu na kwa hivyo wapotelee njia ya upotovu. Na ilikuwa ile amri ya kuelekea Beitul Muqaddas ni katika mambo magumu ila kwa wale ambao wamejaaliwa kupata hidaya ya Mwenyezi Mungu. Ikawa kufuata amri hii miongoni mwa nguzo za Imani. Mwenye kuelekea kibla cha Beitul Muqaddas katika zama ilipo amrishwa hayo hakupoteza Imani yake na ibada yake kwa upole na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.
Na Sisi tulikuona vipi unazichungua mbingu asaa uteremke Wahyi (ufunuo) wa kugeuza Kibla cha Beitul Muqaddas ufuate cha Alkaaba ambacho unakipenda, kwa kuwa ndicho Kibla cha Ibrahim, baba wa Manabii, na baba wa Mayahudi na Waarabu. Na hapo pana Maqaamu Ibrahim, alipokuwa akisimama Ibrahim. Kwa hivyo hichi ni Kibla kilicho kusanya wote, ijapokuwa kinaacha kibla cha Mayahudi. Basi hivi sasa Sisi tunakupa lile ombi lako. Kwa hivyo katika Sala zako elekea Masjidil Haraam (Msikiti Mtakatifu). Na nyinyi Waumini, kadhaalika, elekeeni huko popote pale mlipo. Watu wa Kitabu wanao udhika kwa kukiacha kwenu Kibla cha Beitul Muqaddas wanajua katika vitabu vyao kuwa nyinyi ni watu wa Alkaaba. Na wanajua kuwa amri ya Mwenyezi Mungu inawakhusisha watu wa kila sharia na kibla chao. Na hii ni haki inayo tokana na Mola wao Mlezi. Lakini wao wanataka kukufitinisheni na kukutilieni shaka katika Dini yenu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika nao, na Yeye atawalipa kwa wayatendayo.
Na hao walio pewa Kitabu, hata ukiwaletea hoja za kila namna, hawatafuata Kibla chako; wala wewe hutafuata kibla chao, wala baadhi yao hawatafuata kibla cha wengineo; na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya kukufikia ujuzi, hakika hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhullumu.
Na hakukua kutoridhika kwao Watu wa Kitabu nanyi ni kwa kudanganyikiwa ambako kwaweza kuondoka kwa hoja, bali kuudhika huko ni kwa inadi na kiburi. Kwa hivyo Ewe Mtume! Hata ukiwaletea kila hoja ya kukata kuwa Kibla chako ndicho cha kweli, hawakubali kukifuata Kibla chako. Ikiwa Mayahudi wangali wanatumai kuwa bado utarejea kwenye kibla chao, na wanatoa hiyo ni shuruti ya kusilimu kwao, basi watavunjika moyo, wala wewe hutofuata kibla chao. Na hao watu wa Kitabu kila kikundi chao kina kibla chake mbali. Wakristo hawafuati kibla cha Mayahudi, wala Mayahudi hawafuati kibla cha Wakristo, na kila mmoja kati yao anawaona wengine hawamo katika haki. Basi wewe thibiti hapo hapo kwenye Kibla chako, wala usiyaendekeze matamanio yao. Kwani mwenye kuyafuata matamanio yao baada ya kwisha pata ujuzi kuwa wao ni wapotovu, na kujua kuwa yeye yuko katika haki, basi huyo ni katika walio dhulumu na wenye kubobea katika dhulma. Wanasema wafasiri kuwa Mayahudi wanaelekea kwenye Mwamba katika Beitul Muqaddas na Wakristo wanaelekea Mashariki.
Wale tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto wao; na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.
Na hakika Watu wa Kitabu wanajua kuwa huku kugeuza Kibla ni jambo la haki, na wanakutambua kuwa wewe ndiye Nabii aliye sifiwa katika vitabu vyao, na miongoni mwa sifa hizo kuwa atasali kuelekea Alkaaba. Na kujua kwao Unabii wako na kukijua Kibla chako ni sawa sawa wanavyo wajua watoto wao kwa uwazi kabisa. Lakini baadhi yao wanaificha kweli hii juu ya kuwa wanajua, kwa kufuata pumbao na chuki zao za upotovu kuwania mila zao kwa ajili ya kulinda madaraka yao, na wanatafuta hila za kukupotoeni nyie.
Haki inatoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wanao fanya shaka.
Na hakika Haki ni anayo kutolea Mwenyezi Mungu Mtukufu sio wanayo kupotoshelea watu wa Kitabu. Basi kuweni na yakini nayo, msiwe watu wenye kutia shaka shaka na kubabaika. Na katika hiyo Haki ni hii amri ya Kibla, basi endeleeni nayo wala msiwabali (musiwajali) wapinzani.
Na kila mmoja anao upande anao elekea. Basi shindanieni mema. Popote mlipo Mwenyezi Mungu atakuleteni nyote pamoja. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Hakika Kibla hicho tulicho kuelekeza ndicho Kibla chako na Kibla cha Umma wako. Na hali kadhaalika kila umma una kibla chake unako elekea katika swala yao kwa mujibu wa sharia zilizo kwisha pita. Wala katika haya hapana kupikuana kwa ubora, na ama kupikuana kwa ubora ni kwa kutenda vitendo vya ut'iifu na a'mali za kheri. Basi kimbilieni kwenye kheri na mshindane kwa hayo. Mwenyezi Mungu atakuhisabuni kwa hayo, kwani Yeye atakukusanyeni nyote Siku ya Kiyama kutoka kokote mtapo kuwako. Wala hatamchopoka hata mmoja. Kila kitu kimo mkononi mwake, na katika hivyo ni amana, kuhuisha, kufufua na kukusanya.
Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na hiyo ndiyo Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yatenda.
Basi katika Swala zako popote pale ulipo uelekee Msikiti Mtakatifu, ukiwa upo mjini au umo safarini, popote wendapo. Na hakika haya bila ya shaka ndiyo ya Haki yanayo wafikiana na hikima ya Mola wako Mlezi aliye pamoja nawe. Basi wewe na umma wako yatamanini haya. Kwani Mwenyezi Mungu atakulipeni malipo mema kabisa. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye ujuzi wala hapana katika vitendo vyenu vilivyo fichikana naye.
Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na popote mlipo elekezeni nyuso zenu upande huo ili watu wasiwe na hoja juu yenu, isipokuwa wale walio dhulumu miongoni mwao Basi msiwaogope wao, lakini niogopeni Mimi - na ili nikutimizieni neema yangu, na ili mpate kuongoka.
Jilazimishe kuifuata amri ya Mwenyezi Mungu katika mambo ya kuelekea Kibla, na kuwa na pupa nayo wewe na umma wako. Na uelekeze uso wako uelekee upande wa Msikiti Mtakatifu popote wendapo katika safari zako. Na elekeeni huko popote mtapo kuwapo pande zote za dunia, mkiwa mko safarini au mpo mjini, ili ukatike ule ushindani wa hoja za hao walio khalifu na wanao jadiliana nanyi ikiwa hamkufuata amri hii ya kugeuza Kibla. Mayahudi watasema: Vipi Muhammad anapo sali anaelekea Beitul Muqaddas, na Nabii alielezwa katika vitabu vyetu ni kuwa moja katika sifa zake anaelekea Alkaaba? Na washirikina wa Kiarabu watasema: Vipi anadai kuwa mila yake ni mila ya Ibrahim, naye hafuati Kibla chake? Juu ya vyote hakika hao walio dhulumu walio potoka wakaiacha Haki kutoka pande zote mbili hawatoacha majadiliano yao na upotovu wao, bali watasema: Hakugeuka kuelekea Alkaaba ila kuwa anafuata ile ile dini ya kishirikina ya kaumu yake, na kuupenda ule mji wake. Basi nyinyi msiwabali hao, kwani uchochezi wao hauto kudhuruni. Nanyi niogopeni Mimi, msiikhalifu amri yangu. Kwa amri hii tumetaka kuitimiza neema juu yenu, na Kibla hichi tulicho kuelekezeni ndicho kipelekee kuthibiti kwenu katika uwongofu na kupata tawfiki.
Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana na nyinyi, anakusomeeni Aya zetu na kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hikima na kukufundisheni mliyo kuwa hamyajui.
Na hivi kukuelekezeni kwenye Msikiti Mtakatifu na kwa kuwa tumekutumieni Mtume aliye tokana nanyi, akikusomeeni Aya ni katika kukutimizieni neema yetu, kama tulivyo kutimizieni ile neema - nayo ni Qur'ani - na akusafishieni nafsi zenu zitoke uchafu wa ushirikina na tabia na ada mbovu mbovu, na anakusemezeni kwa njia ya kukufunzeni maarifa ya Qur'ani na ilimu zenye nafuu, na kukufunzeni mambo ambayo mlikuwa hamyajui. Kwani mlikuwa katika ujinga na upotovu ulio mpofu wa kijahilia.
Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru.
Basi enyi Waumini! Nikumbukeni kwa kunit'ii, na Mimi nitakukumbukeni kwa kukupeni thawabu. Na nishukuruni kwa neema nilizo kuvikeni, wala msizipinge neema hizi kwa kuyaasi yale niliyo kuamrisheni.
Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Swala. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.
Na tafuteni kujisaidia, enyi Waumini, katika kila linalo kupateni, kwa kusubiri na kushika Swala. Swala ndio msingi wa ibada zote. Hakika Mwenyezi Mungu kwa uwezo wake wenye nguvu yu pamoja na wanao subiri. Yeye ndiye mlinzi wao, na Yeye ndiye anaye wanusuru daima.
Wala msiseme kuwa wale walio uwawa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti; bali hao ni wahai, lakini nyinyi hamtambui.
Na subira haipelekei ila kwenye kheri na kufanikiwa kote kuwili, duniani na Akhera. Basi msikae nyuma mkaacha kwenda kupigana Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Wala msiogope kufa katika Jihadi, kwani mwenye kufa katika Jihadi huyo si maiti, hakufa, bali yuhai maisha ya juu kabisa, ijapo kuwa hawa tunao waona wahai hawatambui hayo.
Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri,
Subira ni ngao na silaha ya Muumini ambayo kwayo hushindia kila shida na mashaka. Na nyinyi zitakuja kupateni shida nyingi. Tutakujaribuni na kukufanyieni mitihani kwa vitisho vya maadui, kwa njaa, na uchache wa vifaa, na kupungukiwa mali, na watu kufa, na kupotea mazao. Na hapana la kukulindeni katika mtihani huu mkali ila Subira. Basi Ewe Nabii! Wape bishara nzuri wanao subiri kwa moyo na ulimi.
Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.
Wale ambao kwamba yanapo wateremkia machungu ya kuwaumiza wanaamini ya kuwa hakika kheri yote na shari inatokana na mwenyewe Mwenyezi Mungu, na ya kwamba amri yote ni ya Mwenyezi Mungu. Hao husema: Sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na sisi ni wenye kurejea kwake Yeye. Sisi hatuna letu jambo lolote. Na Yeye ni mwenye kustahiki kushukuriwa kwa anacho toa, na juu yetu kusubiri wakati wa kujaribiwa, na kwake Yeye ndiyo zipo thawabu na malipo.
Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.
Basi hao wenye kusubiri, wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, wanapewa bishara njema kuwa watapata maghfira na ihsani ya Mwenyezi Mungu, na wao ndio wenye kuongoka njia ya kheri na uwongozi mwema.
Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi anaye hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anaye jitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mjuzi.
Na kama alivyo kuwa Mwenyezi Mungu ametukuza hadhi ya Alkaaba akaifanya iwe ndiyo Kibla cha Swala, hali kadhaalika ametukuza shani ya vilima viwili viliopo Makka, navyo ni Safaa na Marwa, akavifanya miongoni mwa mahala pa kufanyia ibada ya Hijja. Basi imewajibikia baada ya kuizunguka Alkaaba kwa kut'ufu, kwenda huku na huku baina ya vilima viwili hivyo mara saba. Kwenda huko kunaitwa Sa'yu. Na baadhi yenu labda walikuwa wakiona vibaya kufanya hivyo kwa kuwa kilikuwa kitendo cha siku za jahiliya kabla ya kuja Uislamu. Lakini kweli iliopo ni kuwa hiyo ni ada ya Kiislamu ya tangu zamani. Basi hapana ubaya wowote kufanya Sa'yu baina ya vilima viwili hivi kwa mwenye kunuwiya Hijja na Umra. Na Muumini na afanye jambo la kheri kama awezavyo, kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa ayatendayo, na Yeye atamlipa kwa a'mali yake.
Hakika wale wanao ficha tuliyo yateremsha nazo ni hoja zilizo wazi na uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni -- hao anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani.
Hao wanao kukatalieni Dini yenu wako makundi mawili: kundi moja ni katika Watu wa Kitabu wanao ijua Kweli, lakini wanaificha kwa kujua na kwa inda. Na kundi jengine ni la washirikina ambao nyoyo zao ni pofu, kwa hivyo hawaioni Kweli, na badala ya Mwenyezi Mungu Mmoja wakawa wanaabudu miungu myengineo. Basi Watu wa Kitabu walio jua ushahidi wa ukweli wako wanajua haki ya Dini yako, lakini kisha wanazificha hizo dalili ili watu wasijue. Mwenyezi Mungu atawapatiliza ghadhabu yake, na atawaepusha rehema yake, na kila wanao omba katika Malaika, na Wanaadamu na Majini watawaapiza wasipate rehema ya Mwenyezi Mungu.
Ila wale walio tubu na wakatengeneza na wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
Wala hapana atakaye vuka na laana hiyo katika wao ila aliye tubu na akatenda mema kwa kuacha kuficha Haki, akayadhihirisha aliyo kuwa akiyaficha katika sifa za Mtume na Uislamu. Mwenyezi Mungu atakubali toba yake na atamfutia dhambi zake, kwani Yeye ndiye anaye kubali toba ya waja wake kwa huruma na rehema yake.
Watadumu humo. Hawata-punguziwa adhabu wala hawatapewa muda wa kupumzika.
Na wataendelea katika laana hii na katika Moto, wala hawatapunguziwa adhabu, wala hawatapewa muhula wala haitoakhirishwa. Hata wakiomba muhula na kuakhirishwa hawataitikiwa.
Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
Hakika Mungu wenu anaye stahiki kuabudiwa pekee ni Mmoja. Hakuna mungu mwenginewe, wala hapana utawala ila wake. Tena Yeye amesifika kuwa ni Mwenye rehema, basi Yeye ni Rahim, Mwenye Kuwarehemu waja wake katika kuwaumba na kuwafanya walivyo.
Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayo yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanao zingatia.
Na zipo dalili nyingi na Ishara kwa kila mwenye akili juu ya kuwapo kwake na Ungu wake. Miongoni mwa hizo ni hizi mbingu mzionazo zinazo pitiwa na sayari kwa nidhamu bila ya kuzahamiana wala kugongana, zikiuletea ulimwengu huu joto na nuru. Na pia hii dunia yenye bara na bahari, na kupishana usiku na mchana, pamoja na manufaa yake. Katika Ishara na dalili hizo ni kuzingatia marikebu zipitazo baharini zikibeba watu na vifao vyao, na hapana aziendeshao hizo ila Mwenyezi Mungu. Ni Yeye ndiye anaye zituma pepo zinazo leta mvua. Na mvua ikateremka ikahuisha wanyama na ikanywesha ardhi na mimea. Na hizo pepo kwa mivumo yake ya kila namna, na mawingu yaliyo tundikwa baina ya mbingu na ardhi: Jee, yote haya yamesimama kwa uangalifu namna hii na kwa hukumu kama hizi wenyewe tu? Au vimeundwa na Mwenye Kujua Mwenye Uwezo?
Na katika watu wapo wanao chukua waungu wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walio amini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana. Na laiti walio dhulumu wakajua watakapo iona adhabu kuwa nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu na kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu!
Na juu ya dalili zilio wazi baadhi ya watu walio potelewa na akili wamewafanya miungu mingine isiyo kuwa Mwenyezi Mungu, wakiwat'ii na kuwaabudu kama Mwenyezi Mungu na wakawafanya mfano wa Mwenyezi Mungu. Muumini humuelekea Mwenyezi Mungu tu, na kumt'ii kwake hakuna ukomo. Ama hao ut'iifu wao kwa miungu yao hulegalega wakati wa shida. Hapo basi humkimbilia Allah Subhanahu. Na walio jidhulumu nafsi zao lau wangezingatia adhabu itakayo wapata Siku ya Malipo, utakapo dhihiri Ufalme wa Mwenyezi Mungu, na ut'iifu ukawa wake tu wangeli achilia mbali ukhalifu wao na wangeli sita kutenda dhambi zao.
Walio fuatwa watakapo wakataa wale walio wafuata, na hali ya kuwa wamekwisha iona adhabu; na yatakatika mafungamano yao.
Siku hiyo wafuasi watatamani wakubwa wao wawaokoe na upotofu, nao watawakataa na kujitenga nao wakisema: Hatukukwiteni mtut'ii katika kumuasi Mola wenu Mlezi. Hilo ni pumbao lenu tu na uovu wa vitendo vyenu. Makhusiano baina yao na mapenzi waliyo kuwa nayo duniani yatakatika siku hiyo, na watakuwa maadui wao kwa wao.
Na watasema wale walio fuata: Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama wanavyo tukataa sisi! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyo waonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni.
Na hapa wafuasi itawabainikia kuwa walipotea walipo wafuata viongozi wao katika upotovu, na watatamani warejee duniani wawakatae viongozi wao kama wao walivyo wakataa siku ya leo. Vitendo vyao viovu vitadhihiri wajute, lakini wapi! Vimekwisha watumbukiza Motoni, na wala hawatatoka humo.
Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu aliye dhaahiri.
Enyi watu! Kuleni vyakula alivyo kuumbieni Mwenyezi Mungu katika ardhi vilivyo halali, visivyo harimishwa, vilivyo vizuri, vinavyo pendwa na nafsi. Wala msimfuate Shetani anaye kupendezeni kula chakula cha haramu, au kuharimisha kilicho halali. Nyinyi mmeujua uadui wa Shetani kwenu, na umebainika ubaya wa anayo kuamrisheni.
Yeye anakuamrisheni maovu na machafu, na mumsingizie Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua.
Shetani anakupambieni kiovu kwa dhati na chenye madhara kwa afya yenu, na kibaya ili mkitende. Kwa sababu yake mnafuata dhana na mawazo yasio na msingi. Mkamsingizia Mwenyezi Mungu kuhalalisha na kuharimisha bila ya dalili ya ilimu na yakini.
Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?
Wapotovu walio acha njia ya uwongofu wamezoea kuyashika waliyo yarithi kwa baba zao katika itikadi na vitendo. Wanapo itwa wafuate uwongofu wa Mwenyezi Mungu husema: Hatuachi tuliyo yakuta kwa baba zetu. Katika ujinga mkubwa kabisa ni kukhiari kufuata wazee kuliko kumt'ii Mwenyezi Mungu na kufuata uwongofu wake. Kefu basi inapo kuwa baba zao hawanacho wakijuacho katika Dini, na hawana mwangaza wa kuwanawirisha uwongofu na Imani?
Na mfano wa walio kufuru ni kama mfano wa anaye mpigia kelele asiye sikia ila wito na sauti tu ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawaelewi.
Na mfano wa kuwaita hao makafiri wanao pinga haki na uwongofu na wasiitikie wala wasifahamu wanaitiwa nini ni mfano wa mchunga kondoo anapo wasemeza hayawani. Hawafahamu kitu wala hawasikii ila sauti, wala hawaelewi kinginecho. Basi hao kadhaalika kwa mintarafu ya Haki ni viziwi wa kusikia, vipofu wa kuona, mabubu wa kusema. Hawatamki jema, wala hawatoi la akili.
Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.
Na Sisi tumewaruhusu watu kula kila kilicho halali tulicho waumbia katika ardhi. Na tumewakataza wasifuate nyayo za Shetani. Wakifanya hivyo watakuwa wameongokewa, lakini wakikataa basi Sisi tunawakhusisha Waumini tu kwa uwongofu wetu, na tunawabainishia wao kilicho halali na haramu. Basi enyi Waumini! Mmeruhusiwa kula kila chakula kitamu kilicho chema, sio kichafu. Basi mshukuruni Mwenyezi Mungu aliye kuwekeeni wazi neema ya kumakinika kwa vitu vizuri na kukuhalalishieni, na kwa neema ya ut'iifu na kufuata amri yake ili ibada zenu zitimie. Qurani imeutangulia utibabu wa kisasa kwa kukataza kula mzoga, kwani kifacho kwa ukongwe au ugonjwa husabibishwa na sumu inayo mdhuru mlaji. Kadhaalika cha kunyongwa au maradhi huinajisi damu, na ndani yake huwamo vingi vya kudhuru kama jasho na mkojo. Na nguruwe husabibisha maradhi ya khatari kama TRICHINOSIS ambayo khatimaye huharibu moyo na mapafu na husabibisha mauti.
Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilicho tajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Sio yaliyo harimishwa wanayo zua Washirikina na Mayahudi. Lakini mlicho harimishiwa nyinyi Waumini ni nyamafu, mzoga, yaani mnyama asiye chinjwa, na mfano wake katika kuharimishwa ni nyama ya nguruwe, na nyama ambaye wakati wa kuchinjwa ametajiwa jina lisilo kuwa la Mwenyezi Mungu, kama vile miungu ya uwongo au mfano wake. Juu ya hivyo mtu akilazimika kwa dharura kula kidogo katika vilivyo katazwa kwa ajili ya njaa, na hakupata kinginecho, au kwa kulazimishwa, basi hana makosa juu yake. Lakini ajitenge na mwendo wa kijaahili, kutaka kula vilivyo katazwa kwa kutamani tu, na wala asipite kiasi kula kuliko cha kuondoa njaa tu. Hali ya dharura inaruhusisha kinacho harimishwa, kwa sababu mauti ya yakini yanashinda madhara yanayo weza kustahamilika, na kwamba mwenye kulazimika kwa dharura haimfalii kupindukia mpaka wa dharura, wala asikiuke kile alicho lazimika kukila.
Hakika wale wafichao aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu, wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao isipo kuwa moto, wala Mwenyezi Mungu hatawasemeza Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa. Nao watapata adhabu chungu.
Miongoni mwa watu wanao jua aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu kipo kikundi kinacho ficha baadhi ya maandishi ya ufunuo kwa ajili ya sababu fulani za kilimwengu. Mayahudi, mathalan, wakificha mengi yaliyo kuja katika Taurati ya kueleza sifa za Mtume kwa kukhofu wasije wakasilimu watu wa mila yao na kwa hivyo utukufu wao ukaondoka na wakapoteza mapato yao na vyakula vyao vitamu. Na hakika chakula chao wakilacho kwa njia hii ni kama kula moto, kwani hayo yatawapelekea kuingia Motoni. Mwenyezi Mungu atawatupilia mbali Siku ya Kiyama, wala hatawasafisha uchafu wao, na mbele yao kuna adhabu ya kuumiza kweli.
Hao ndio walio nunua upotofu badala ya uwongofu, na adhabu badala ya maghfira. Ama wavumilivu wa Moto watu hawa!
Hao ndio wenye madhambi walio khiari upotovu wakaacha uwongofu, na kwa hivyo wakastahiki adhabu ya Akhera badala ya kupata msamaha. Watakuwa kama mwenye kununua baat'ili kwa haki, na chenye upotovu kwa chenye uwongofu. Hakika hali yao ni ya kustaajabisha, kwa kuwa wanavumilia kufanya mambo ambayo hayana budi kuwapelekea kwenye adhabu, na tena wakawa wenyewe wakayaonea uzuri hayo yanayo wapeleka huko!
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki. Na wale walio khitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani ulio mbali na haki.
Nao yamewapasa malipo waliyo kadiriwa kwa kukikataa Kitabu cha Mwenyezi Mungu alicho kiteremsha kwa haki na kweli. Na wamekhitalifiana kwacho khitilafu kubwa iliyo wapelekea kupenda kujadiliana na kujitenga na Haki, na kufuata pumbao, wakakigeuza na kukifisidi na kukifasiri kinyume na maana yake ya hakika.
Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Swala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.
Watu wamekithirisha maneno juu ya Kibla kama kwamba wema wote ni hayo tu. Hivi sivyo. Kuelekea upande fulani, mashariki au magharibi, sio msingi wa Dini na kupata kheri, lakini kupata wema ni mambo kadhaa wa kadhaa, baadhi yake ni nguzo za itikadi sahihi, na baadhi yake ni katika misingi ya tabia njema na ibada. La kwanza: kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya kufufuliwa na kukusanywa na kuhisabiwa na yatakayo tokea Siku ya Kiyama; na kuamini Malaika, na Vitabu vilivyo teremka kwa Manabii, na kuwaamini wenyewe Manabii. Na pili: kutoa mali kwa kupenda na kuridhia nafsi kuwapa mafakiri katika jamaa, na mayatima, na wenye shida ya haja, na wasafiri walio katikiwa safari yao wasipate cha kuwafikishia wendako, na walio lazimika kuomba kwa haja walio nayo, na kukomboa watumwa. ( Walio fungwa na kutawaliwa na dhaalimu ni watumwa pia. )Tatu: kushika Swala. Lane: kutoa Zaka iliyo lazimishwa. La tano: kutimiza ahadi bilhali wal maal. La sita: kustahamili maudhi yanayo teremkia roho na mali, mnapo pambana na adui zama za vita. Basi wenye kukusanya imani hizi na vitendo hivi vya kheri ndio walio sadikisha Imani yao, na wao ndio wanao jilinda na ukafiri na mambo machafu na wakayaepuka.
Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu.
Katika Sharia tulizo walazimisha Waumini ni hukumu za mauwaji ya makusudi. Tumewaandikia kisasi kwa mauwaji. Na wala msichukulie dhulma za kijahiliya , walipo kuwa wakimuuwa muungwana asiye uwa kwa ajili ya mtumwa, na wakimuuwa mwanamume asiye uwa kwa ajili ya mwanamke, na mkuu asiye uwa badala ya mwenginewe aliye uwa, akaachiliwa aliye uwa khasa. (Kwa kila ukoo kujiona bora). Yatakikana yule aliye uwa auwawe yeye, akiwa ni muungwana, au mtumwa, au mwanamke. Msingi wa sharia ya kisasi ni kuondoa kufanyiana uadui kwa kumuuwa yule yule aliye uwa ili kuuzima moto wa kulipizana na kuondoa uadui. Walio uliwa mtu wao wakiacha kisasi, wakapendelea kuwasamehe wenzao, watakuwa na haki ya kupewa fidia kwa maiti wao. Na wao inatakikana wawe wasemehevu bila ya kumkahirisha aliye uwa. Na juu ya mwenye kuuwa alipe fidia bila ya kujikurupusha. Katika hukumu ya mauwaji kama tulivyo ilazimisha pana wepesi kwa Waumini ukilinganisha na hukumu ya Taurati inayo lazimisha kisasi tu, na kama ilivyo kuwa ni rehema ukilinganisha na watakavyo wenginewe kuwa muuwaji aachiliwe bure bila ya kumtaaradhi. Basi mwenye kuivuka hukumu hii baada ya hayo atapata adhabu chungu duniani na Akhera. Waarabu zama za jahiliya walikuwa hawafanyi usawa baina ya watukufu na wanyonge. Akiuliwa mwongozi hawatosheki na kumuuwa muuwaji bali huyo huachwa akenda kulipizwa kisasi kwa mwongozi wa kabila ya muuwaji. Kwao roho si sawa, na damu si sawa. Uislamu haukukubali haya, lakini ukapasisha Kisasi, roho kwa roho, mwenye kuuwa huuwawa. Muuwaji yeyote awaye atauliwa akiwa muungwana, mtumwa au mwanamke. Haya ni kwa ajili ya usawa katika damu; hapana mwenye damu tukufu na damu isiyo tukufu. Na inafahamika kwa ishara kuwa nafsi kwa nafsi. Na hii ni sharia ya milele, ilikuwako katika Taurat, na Injil na Qur'ani. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na tuliwaandikia kuwa nafsi kwa nafsi..." (taz. sura Almaida ). Na Mtume s.a.w. amesema: "Damu za Waislamu ni sawa." Na amesema: "Nafsi kwa nafsi". Zingatia: Uislamu kwa sharia ya kisasi ina nadhari nyengine, sio kama kanuni za kutungwa. Imewapa wenye kuuliwa mtu wao haki ya kutaka muuwaji auwawe, kuondoa fitna na umwagaji wa damu mkubwa. Imewapa haki ya kusamehe au kulipwa kisasi, wala haizuilii serikali kumfedhehi aliye uwa ikiona hivyo ni maslaha. Uislamu hauzingatii sababu ya kuuwa, kwani mwenye kuuwa amedhulumu hata ikiwa sababu gani. Na huenda ukitafuta sababu akaonewa huruma mkosa, na kumpuuza mkoswa. Na hayo hupelekea mchafuko wa watu kuchukua kisasi mkononi mwao, na kuzalikana makosa juu ya makosa ya kuuwa, kwa kutoridhika wale walio uliwa mtu wao. Nadharia hii ya Kiislamu sasa inadurusiwa katika vyuo vikuu vya Ulaya.
Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili msalimike.
Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu kwenu ni kubwa kwa hii hukumu ya kisasi. Kwa fadhila ya kisasi jamii yenu ina hakika kupata maisha ya amani na salama. Haya ni kwa kuwa mwenye kutaka kuuwa akijua kuwa naye atauwawa atajizuia kutenda alilo kusudia. Kwa hivyo yeye na yule ambaye angeli uwawa wanahifadhika. Lakini ikiwa kama ilivyo kuwa zama za ujahili akiuliwa mkuu kwa kuuliwa mtu mdogo, na asiye na kosa badala ya mwenye makosa - hapo inakuwa ni kuzua fitna, na kuondoka utulivu na amani. Wenye akili nawazingatie faida ya sharia ya kisasi. Hayo yatawapelekea watambue upole wa Mwenyezi Mungu kwao kuendea njia ya uchamngu, na kuzifuata amri za Mwenyezi Mungu Subhanahu.
Mmeandikiwa -- mmoja wenu anapo fikwa na mauti, kama akiacha mali -- afanye wasia kwa wazazi wake na jamaa zake kwa namna nzuri inayo pendeza. Ni waajibu haya kwa wachamngu.
Kama tulivyo weka sharia ya kisasi kwa maslaha ya umma na kuhifadhi jamii, vile vile tumeleta sharia ya maslaha ya ukoo na kuulinda, nayo ni Sharia ya Wasiya. Basi mwenye kuona kuwa amekabiliwa na mauti naye akawa na mali basi yatatikana awawekee katika mali yake fungu la wazazi wake na jamaa zake, wale jamaa ambao hawamrithi. Katika hayo afuate mwendo unao pendeza na unakubaliwa na wenye akili. Asiwe akampa tajiri na akamwacha fakiri, bali amfadhilishe yule mwenye haja zaidi, wala asiweke sawa ila wale wenye pato sawa. Na faridha hiyo ni haki iliyo mwajibikia mwenye kupenda uchamngu na kufuata amri za Dini.
Na atakaye ubadilisha wasia baada ya kuusikia, basi dhambi yake ni juu ya wale watakao ubadilisha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Ukitoka wasiya basi huo ni haki iliyo waajibu, haijuzu kuugeuza na kuubadilisha ila ikiwa wasiya huo umeacha uadilifu. Mwenye kubadilisha haki akageuza wasiya muadilifu ulio sawa baada ya kujua hukumu hii basi huyo amepanda madhambi yatakayo mletea adhabu. Mwenye kuusia hana kosa kwa yatakayo tokea baada yake, wala hakudhani kuwa atakuwapo atakaye fanya hayo, wala yeye hapatilizwi kwa hayo. Mwenyezi Mungu, hakika, ni Mwenye kusikia na kujua, wala hapana linalo fichikana kwake.
Na mwenye kumkhofia muusiaji kwenda kombo au kupata dhambi akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
Ama ikiwa wasiya umeacha haki na njia iliyo sawa tuliyo kwisha ibainisha, kwa mwenye kufanya wasiya kumharimisha fakiri akampa tajiri, akawawacha jamaa zake akawapa mafakiri wasio rithi watu mbali, basi mwenye kwenda mwendo wa kheri akamrejeza mwenye kufanya wasiya ende sawa, basi hapana dhambi kwa kuugeuza wasiya kwa namna hiyo. Na Mwenyezi Mungu hamchukulii kitu kwa hayo, kwani Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.
Na kama tulivyo kuwekeeni sharia za Kisasi na Wasiya kwa ajili ya maslaha ya jamii zenu, na kuhifadhi mambo ya ukoo, kadhaalika tumeweka sharia za Saumu ili kuzitengeneza nafsi zenu, ziweze kujikinga na matamanio, na kukutukuzeni kuliko wanyama walio baki wanao fuata hisiya za matamanio yao tu. Na huku kufaridhishwa Saumu ni kama walivyo faridhishwa kaumu zilizo tangulia. Basi msilione kuwa ni jambo zito mno hili, kwani watu wote walilazimishwa haya. Kulazimishwa Saumu ni kwa ajili ipate kuleleka roho ya uchamngu, na ili muwe watu madhubuti, na nafsi zenu ziongoke sawa.
(Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.
Mmeamrishwa mfunge siku chache za kuhisabika, na lau Mwenyezi Mungu angependa angeli kufanyieni muda mrefu. Wala hatukulazimisheni katika Saumu jambo msilo liweza. Aliye mgonjwa wa maradhi yanayo dhuriana na kufunga, au aliomo safarini, basi anaweza kula na alipe akisha pona au akirejea safarini. Ama asiyekuwa mgonjwa wala si msafiri, lakini hawezi kufunga ila kwa taabu kwa sababu ya udhuru kama ukongwe, na maradhi yasiyo tarajiwa kupona, yeye pia anaweza kula, na juu yake amlishe masikini ambaye hamiliki hata chakula cha siku moja yake. Na mwenye kujitolea kwa ridha yake kufunga zaidi kuliko faradhi itakuwa ni bora zaidi kwake. Kwani Saumu daima ni bora kwa mwenye kujua ukweli wa ibada.
Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.
Na siku hizi ni za mwezi wa Ramadhani mwezi wenye daraja tukufu kwa Mwenyezi Mungu ndipo ilipo teremshwa Qur'ani ili kuwaongoa watu wote kwa hoja zake zilizo wazi zinazo fikishia kheri, na zenye kutenga baina ya Haki na baat'ili kwa nyakati zote na vizazi vyote. Basi mwenye kuuwahi mwezi huu naye ni mzima, si mgonjwa, yupo mjini si msafiri, yampasa afunge Saumu. Na aliye mgonjwa anaye dhurika kwa kufunga au alioko safarini anaweza kula, na juu yake kuzilipa zile siku alizo kula kwa kufunga utapo ondoka udhuru. Kwani Mwenyezi Mungu hataki kuwapatisha watu mashaka na taklifa bali Yeye anapenda kuwafanyia watu sahala. Na Mwenyezi Mungu amekubainishieni Mwezi wa Saumu, na amekuongoeni ili mpate kutimiza siku za kufunga, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa uwongofu alio kuongoeni, na akakupeni tawfiki njema. Imethibiti kwa matibabu ya kisasa kuwa Saumu kwa namna ya Qur'ani ina faida nyingi, katika hizo ni kuwa inasaidia katika kutibu maradhi ya sukari, inatengeneza matumbo, inapunguza maumivu ya viungo, na maradhi ya moyo, inapumzisha nyama za mwili, na inasafisha uchafu mwingi wenye madhara, na pia inakuwa ni kinga kwa maradhi mengi mengineyo. Je, vipi kwa mtu asiye jua kusoma na kuandika ayajue yote haya?
Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.
Na Mimi nawajua vyema waja wangu, na najua wanayo yafanya na wanayo yawacha. Na Ewe Muhammad! Wakikuuliza waja wangu wakasema: Hivyo Mwenyezi Mungu yupo karibu nasi hata ajue tunayo yaficha na tunayo yatangaza na tunayo yawacha? Waambie: Mimi ni karibu nao zaidi kuliko wanavyo dhani. Na dalili ya hayo ni kuwa ombi la mwenye kuomba linafika wakati huo huo, na Mimi ndiye ninaye pokea hayo maombi wakati huo huo vile vile. Ilivyo kuwa Mimi nimewaitikia maombi yao basi na wao waniitikie Mimi kwa kuamini na kut'ii, kwani hiyo ndiyo njia ya kuongoka kwao na kusibu kwao.
Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.
Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni usiku wa kufunga kuingiana na wake zenu, na wao kuchanganyika nanyi katika maisha na katika malazi. Ilikuwa ni mazito kwenu kujitenga nao, na sasa mmepunguziwa hizo taabu. Mwenyezi Mungu anajua kuwa mlikuwa mkijipunguzia starehe ya nafsi zenu na mkijidhulumu kwa kujizuia msiingiane na wake zenu hata usiku wa Ramadhani. Sasa amekusameheni na kukupunguzieni mikazo. Sasa basi msione vibaya kuchanganyika nao, na stareheni kwa aliyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, na kuleni na mnywe usiku wa Ramadhani mpaka mwone mwangaza wa alfajiri unapo tokeza kutokana na kiza cha usiku. Hapo tena fungeni na mtimize Saumu mpaka linapo kuchwa jua. Na ilivyo kuwa Saumu ni katika ibada zinazo taka mtu kujiepusha na matamanio ya roho na kuingiana na wanawake wakati wa mchana, basi kadhaalika katika ibada ya kukaa Itikafu msikitini inahitaji kujitenga na kuacha kustarehe na wake zenu wakati huo mnapo kuwapo katika Itikafu. Na haya ya sharia za Saumu na Itikafu alizo kuwekeeni Mwenyezi Mungu yashikeni baraabara msikaribie kuyavunja. Na Mwenyezi Mungu ameyaweka wazi haya kwa watu kwa namna hii ili wapate kuyaogopa na waepukane na matokeo yake.
Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.
Mmekatazwa siku zote kula mali ya watu kwa njia isiyo ya haki. Mali ya mtu si halali kwenu ila kwa moja ya njia alizo wekea Sharia Mwenyezi Mungu, kama vile mirathi, au kutunukiwa kwa kupewa na mwenye mali, au kwa mkataba ulio sahihi wenye kuhalalisha kumiliki. Na huenda mmoja wenu hutafuta njia za kumpokonya mwenziwe haki ya mali yake kwa kupeleka kesi mahkamani ili yeye kwa kushirikiana na mahakimu au makadhi na kuleta ushahidi wa uwongo, au uwongo dhaahiri, au kutoa rushwa, wapate kula mali kwa dhulma. Huo ni uovu mno kwa wanao tenda, na malipo yao ni mabaya sana.
Wanakuuliza khabarai ya miezi. Sema: Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija. Wala sio wema kuziingia nyumba kwa nyuma. Bali mwema ni mwenye kuchamngu. Na ingieni majumbani kupitia milangoni. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
Na watu wanakuuliza khabari za mwezi, unaanza mwezi mchanga kama uzi, kisha unakua mpaka unatimia kaamili. Tena unapungua mpaka unakuwa kama ulivyo anza. Haukai katika hali moja kama jua. Nini maana ya kugeuka huku hata inakuwa kila siku 29 au 30 unakuja mwezi mpya? Waambie: Huku kutokea hivi kuandama mwezi na kugeuka yapo ndani yake maslaha ya Dini na dunia pia. Hizi ni alama za kuonyesha nyakati za mambo ya maisha yenu. Zinaonyesha nyakati za Hija, ambayo ni moja katika Nguzo za Dini yenu. Na lau kuwa mwezi ungeli baki namna moja tu kama jua, msingeli tambua nyakati za maisha yenu na Hija zenu. Wala huko kutojua hikima ya kugeuka mwezi kusikupelekeeni kutilia shaka hikima ya Muumba. Wala sio wema kuziingilia nyumba kwa nyuma, kinyume na wafanyavyo watu wote. Lakini wema ni kumchamngu katika nyoyo na kumsafishia niya, na kuziingilia nyumba kwa kupitia milangoni kama wafanyavyo watu wote. Na mtake Haki na dalili iliyo sawa. Basi takeni radhi ya Mwenyezi Mungu, na muiogope adhabu yake na kwa hivyo ndio mtaraji kufanikiwa kwenu, na kufuzu kwenu na kuepuka adhabu ya Moto. Uislamu unahisabu mwezi unapo andama na kugeuka sura kwa watu kupimia nyakati za ibada, na pia kwa mambo yao ya kidunia, kwa sababu hayo ni mambo ya kuonekana, na kwa hivyo taarikhi inajuulikana kwa sura ya mwezi. Mwezi kwa hakika ni kama kioo kinacho onyesha mwangaza wa jua huku duniani. Mwezi ukiwa kati baina ya jua na dunia hauonekani, na baadae mwezi mchanga unaandama na wakaazi wa dunia wanajua kuwa mwezi mpya umeanza. Ukifika mwezi katika upande unao kabiliana baina ya jua na dunia ndio unapo kuwa wakati wa mbaamwezi, mwezi mpevu. Khalafu unaendelea kupungua kama ulivyo kuwa kwanza ukizidi kukua. Kwa hivyo taarikhi inaanza tangu pale ulipo kuwa mwezi mchanga. Pale unapo onekana mwezi mchanga kama uzi ndio mwezi umeandama, huonekana upande wa magharibi, hata kwa dakika chache baada ya kuchwa jua nao hupotea. Hivyo hivyo siku baada ya siku huhisabiwa mpaka zipite siku 29 au 30.
Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui.
Na katika kumcha Mwenyezi Mungu ni kustahamili mashaka katika kumt'ii Yeye, na mashaka makubwa kabisa juu ya nafsi ni kuwapiga vita maadui wa Mwenyezi Mungu. Lakini wakikuvamieni, basi piganeni na hao wavamizi. Na mmepewa ruhusa kuurudi uvamizi wao, lakini nyinyi msivamie kwa kuanza nyinyi, au kwa kumuuwa asiye kupigeni vita wala hana mahusiano na vita; kwani Mwenyezi Mungu hawapendi wavamizi.
Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe popote walipo kutoeni; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala msipigane nao kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka wakupigeni huko. Wakikupigeni huko basi nanyi pia wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
Wauweni walio kuanzeni vita popote mnapowakuta, na watoeni Makka, wat'ani wenu ambao wamekulazimisheni kuutoka. Wala msione vibaya, kwani walio kufanyieni nyinyi ni maovu zaidi kuliko kuuwa msikitini, nako ni kuwafitini Waumini katika Dini yao kwa kuwaadhibu huko Makka mpaka wakauacha mji wao kuhifadhi Dini yao. Na huu Msikiti Mtakatifu una utakatifu wake, basi msiuvunje kwa kupigana ndani yake. Lakini wakikupigeni vita ndani yake basi nanyi pia wauweni, na nyinyi kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu, mtashinda. Na malipo ya makafiri ni kufanyiwa wanayo wafanyia watu.
Lakini wakiacha basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Wakirejea wakaacha ukafiri, wakafuata Uislamu basi Uislamu humuitikia anaye uelekea. Na Mwenyezi Mungu atawasamehe ule ukafiri wao wa zamani kwa fadhila yake na rehema yake.
Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadui ila kwa wenye kudhulumu.
Wapigeni vita walio taka kukuuweni na kukugeuzeni muache Dini yenu kwa maudhi na mateso mpaka ing'oke mizizi ya fitina na isafike Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Wakiuacha ukafiri wao basi wamejiokoa nafsi zao na wataepukana na adhabu. Hapo basi haifai kuwafanyia uadui. Uadui hufanyiwa mwenye kuidhulumu nafsi yake akaiteketeza kwa maasi na akaacha uadilifu kwa maneno na vitendo.
Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu vitakatifu vimeekewa kisasi. Anaye kushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadiri alivyo kushambulieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
Na pindi wakikushambulieni katika mwezi mtukufu msiache kupigana nao, kwani huo ni mtukufu kwao kama ulivyo kuwa mtukufu kwenu. Ikiwa wao watauvunja utukufu wake basi nanyi wakabilini kwa kuzilinda nafsi zenu katika huo mwezi. Na katika mambo matukufu na matakatifu pana sharia ya kisasi na kutendeana mfano kwa mfano. Anaye kushambulieni katika matakatifu yenu nanyi jilindeni na uadui huo kwa mfano wake. Na mcheni Mwenyezi Mungu, msikiuke mipaka katika kulipiza kisasi. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwanusuru wachamngu.
Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
Kupambana na makafiri kunahitaji kutoa roho kama ilivyo kutoa mali. Basi toeni kwa kuandaa vita, na jueni kuwa kupigana na hawa ni kupigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi msikae tu. Toeni mali kwa ajili yake, kwani mkitofanya na mkafanya ubakhili adui atakupandeni na atakudhilini. Hapo itakuwa kama mlio jitokomeza wenyewe kwenye maangamio. Tendeni lilio kuwajibikieni kwa uzuri na vilivyo, kwani Mwenyezi Mungu hupenda anapo fanya jambo mtu alifanye vizuri. Aya 190 mpaka 195 zinaeleza sharia ya vita katika Uislamu. Nazo zinaeleza kwa matamshi yalio wazi haya yafuatayo: 1. Ruhusa ya kupigana imetolewa kwa ajili ya kujilinda na uvamizi wa vita wa vitendo khasa, au zikidhihiri dalili kuwa maadui wanataka vita. Vita havikulazimishwa kwa ajili ya vita wala kwa sababu ya kutaka kuwasilimisha watu kwa kuwauwa na kuwapiga vita. 2. Kunakatazwa kuvamia au kuanza uadui kwa njia yoyote ile. Basi hapana ruhusa kufanyiwa uadui asiye pigana, wala hapana ruhusa kuvuka mipaka ya uadui wakati wa vita: basi hauliwi asiye chukua silaha, wala hakhusiani na vita bali ni mwenye kukumbwa tu na vita. Wala hauliwi mwenye kusalimu amri na akatupa silaha. Wala hapana ruhusa kuwavunjia watu nyumba zao, huko ni kupita mpaka. 3. Mzingatie fadhila iliyo onyeshwa kwa kuamrishwa kuchamngu. Basi msivunje heshima ya wanawake kuwanajisi, hata washirikina wakifanya hayo. Wala msiwakatekate walio uwawa hata ikiwa makafiri wakiwafanyia hayo Waumini. Washirikina walimfanyia hayo Bwana wa Mashahidi, Hamza, wala Mtume s.a.w. hakutoa ruhusa kumfanyia hayo maiti yeyote, bali alikataza akasema:"Tahadharini msiwakatekate maiti". 4. Vita vinakwisha wakiacha washirikina kuwafitini Waumini katika Dini yao, na Dini inakuwa inataka akili na nyoyo zimwelekee Mwenyezi Mungu kwa uhuru. 5. Hapana vita katika mwezi mtukufu, nayo ni miezi ya Hija na Umra. Ikiwa washirikina watapigana katika miezi hiyo, basi Waumini nao yawapasa wapigane. 6. Kuacha kutoka kwenda pigana na maadui wanauwa pasina nasi kupigana nao ni kuipoteza kheri na wema. Kwa haya inadhihiri kuwa vita vya Islamu vina fadhila katika sababu zinazo pelekea kuanza kwake, na vina uadilifu katika kuviendesha. Viwapi hivi na vita vya mataifa mengine ya zamani na ya sasa! Vita vyao hao ni vya uchafu, na vita vya Islamu ni vya Haki na vyenye fadhila.
Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mkizuiwa,basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapo kuwa salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu, wala yasiwe makusudio yenu ya kidunia kama kutaka umaarufu na kadhaalika. Mkiharimia Hija na Umra akakuzuieni adui njiani basi mtatoka katika Ihram yenu kwa kunyoa nywele. Lakini kabla ya hayo mchinje mnyama aliye mwepesi kumpata, kama mbuzi au ngamia au ng'ombe, na kumtoa sadaka kwa masikini. Wala msinyoe mpaka mtimize haya. Mwenye kuharimia akapata maudhi katika nywele zake kwa maradhi au wadudu hapana ubaya kunyoa. Juu yake hapo atoe fidiya kwa kufunga siku tatu, au kutoa sadaka kuwalisha masikini sita chakula cha kutwa, au kuchinja mbuzi na kumtoa sadaka kwa masikini. Na ikiwa mpo katika amani na salama na hakukutokeleeni adui njiani, na mkakusudia Hija na Umra, na mkajistarehesha kwa kufanya Umra kwanza mpaka ufike wakati wa Hija ndio mharimie, basi inakupaseni kuchinja mbuzi kwa ajili ya masikini na mafakiri wa Makka. Asiye pata mbuzi au hamiliki bei yake afunge siku tatu hapo Makka, na siku saba akisha rejea kwao. Haya ni kwa aliye kuwa hana watu wake Makka. Kwa mwenye watu wake Makka hapana kitu akijistarehesha.
Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua. Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamngu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili!
Na Hija inakuwa katika miezi mnayo ijua, kwani jambo hili ni maarufu kwenu tangu zama za Ibrahim a.s. nayo ni miezi ya Mfungo Mosi, Mfungo Pili na Mfungo Tatu. Mwenye kuazimia faridha ya Hija katika miezi hii na akaingia basi afuate vilivyo adabu zake. Katika adabu za Hija ni kuwa mwenye kuharimia ajiepushe na kuingiana na wakeze, na kufanya maasi ya kutukanana na mengineyo, kujadiliana na kubishana na Mahujaji wenziwe, na ajiepushe na kila linalo pelekea chuki na khasama ili atoke katika Ihramu yake naye hali ana hishima yake. Ajitahidi kufanya kheri na kutafuta malipwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kutenda mema, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua hayo na ni Mwenye kulipa vitendo vyema. Na mchukue zawadi za Akhera yenu kwa kuchamngu na kufuata amri za Mwenyezi Mungu na kuyaepuka ayakatazayo. Hiyo, basi ndio zawadi bora. Na kuweni wenye kuhisi khofu ya Mwenyezi Mungu katika yote mnayo yafanya na mnayo yawacha kwa mujibu wa akili na hikima njema. Katika vitendo vyenu vyote msichanganyishe hata chembe na mambo ya pumbao au makusudio ya kidunia.
Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila ya Mola wenu Mlezi. Na mtakapo miminika kutoka A'rafat mtajeni Mwenyezi Mungu penye Masha'ril Haram. Na mkumbukeni kama alivyo kuongoeni, ijapo kuwa zamani mlikuwa miongoni mwa walio potea.
Na walikuwako miongoni mwenu ambao wakiona vibaya kufanya biashara na kutafuta riziki wakati wa msimu wa Hija. Basi mnaambiwa kuwa hapana ubaya kwenu hayo, bali mnaweza kuchuma maisha kwa njia ziliyo ruhusiwa na sharia, na mtafute fadhila na neema za Mwenyezi Mungu. Wakitoka Mahujaji A'rafat baada ya kusimama huko, na wakafika Muzdalifa katika mkesha wa Idi ya Kuchinja, wamtaje Mwenyezi Mungu hapo Masha'ril Haram, napo ndipo kwenye kilima cha Muzdalifa, kwa kusoma Tahlili na kuitikia Labbaika na kusoma Takbir. Na wamtukuze Mwenyezi Mungu wakimhimidi na kumshukuru kwa vile alivyo waongoa kwenye Dini ya Haki na ibada iliyo nyooka katika Hija na Umra, na ilhali kabla ya hapo walikuwa katika walio potea njia ya uwongofu.
Kisha miminikeni kutoka pale wanapo miminika watu, na muombeni Mwenyezi Mungu msamaha: hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Makureshi walikuwa hawasimami na watu wengine katika A'rafat juu ya kuwa wakijua kuwa baba yao Ibrahim akisimama hapo. Na hayo ni kwa kujitukuza wasiwe sawa na wengineo na hali wao ati ni watu wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu na ni wakaazi wa katika pahala patakatifu. Wakidai kuwa hayo ni kuitukuza Makka wasitoke kwenda A'rafat ambako si kutakatifu kama Makka. Mwenyezi Mungu akawalazimisha wazing'olee mbali hizo ada za kijinga, na wasimame katika A'rafat, na watoke huko kama watokavyo watu wote. Kwani hapana yeyote aliye bora kuliko mwengine katika utendaji wa ibada. Na inawapasa wamwombe Mwenyezi Mungu maghfira katika mwahala humu mwenye baraka. Hayo ndiyo yana maelekeo zaidi Mwenyezi Mungu kuwasamehe dhambi na makosa yao, na akawarehemu kwa fadhila yake.
Na mkisha timiza ibada zenu basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyo kuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na wapo baadhi ya watu wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika Akhera hana sehemu yoyote.
Mkisha maliza a'mali za Hija na ibada zake wacheni mliyo kuwa mkiyafanya zama za ujahili ya kutafakhari kwa baba zenu na kukumbusha mambo yao, bali makumbusho yenu na kutukuza kwenu kuwe kwa Mwenyezi Mungu kama mlivyo kuwa mkiwakumbuka baba zenu, bali mtajeni Yeye kwa wingi zaidi kuliko wazee wenu, kwani Yeye ndiye Mwenye kuzitawala neema zenu na neema za baba zenu vile vile. Na humu mwahali mwa Hija ndio khasa mwahala mwa dua na kuombea fadhila na kheri na rehema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu. Na walikuwako baadhi ya Mahujaji wakifupiza dua zao kwa mambo na kheri za dunia tu. Hao hawapati sehemu yoyote ya Akhera.
Na katika wao wapo wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto!
Na wapo watu ambao Mwenyezi Mungu amewawezesha nyoyo zao zikapelekea kuomba kheri ya dunia na Akhera, na wakamwomba Mwenyezi Mungu awaepushe na shari na adhabu ya Moto.
Hao ndio watakao pata sehemu yao kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
Hawa wanapewa kama walivyo jaaliwa kuyachuma kwa kumwomba na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu humlipa kila mtu kama anavyo stahiki, na ni Mwepesi wa kuhisabu na kulipa.
Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo hisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka katika siku mbili (akarejea) si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye kumchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake.
Na mtajeni Mwenyezi Mungu kwa Takbiri na vinginevyo katika siku maalumu, nazo ni siku za kutupa mawe hapo Mina, nazo ni taarikh 11 na 12 na 13. Na si lazima kwa Haji kukaa siku tatu hizi Mina akitupa mawe, bali anaweza kufupiza siku mbili, kwani msimamo wa kheri ni kuchamngu, si idadi. Na daima mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa kwake Yeye mtakusanywa na muulizwe mliyo yatenda. Hayo mawe ni changarawe hutupwa mwahala maalumu katika Mina katika siku ya kuchinja (Idd) na siku tatu zifwatiazo.
Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu.
Ilivyo kuwa kumcha Mwenyezi Mungu ndio msingi, basi khasara ni ya wale watu ambao dhamiri walio nayo nyoyoni mwao ni mbali na maneno yanayo tamkwa na ndimi zao. Wamepewa utamu wa kupanga maneno, hukufurahisha kauli yao katika kujivutia manufaa ya maisha ya kidunia, na kuunga mkono kwa wayasemayo humsingizia Mwenyezi Mungu kuwa anashuhudia kuwa wayasemayo yanatoka nyoyoni mwao. Kumbe wao kwa hakika ndio wakubwa wa ukhasama na ukhabithi kwako wewe.
Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi kwa kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.
Na pindi wakitawalishwa madaraka yoyote haiwi juhudi yao kuleta maslaha, bali ni kuleta ufisadi na kuteketeza mimea, kukata miti na kuuwa wanyama na binaadamu. Na Mwenyezi hawapendi watu kama hawa, kwani Mwenyezi Mtukufu hapendi uharibifu.
Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo kwa mapumziko.
Akinasihiwa amwogope Mwenyezi Mungu huzidi kupanda mori wake na akadhani kuwa hivyo unamvunjia cheo chake, akazidi kupanda madhambi na kuzidi kumchafua na kumwongeza inadi. Mtu huyo hatoshelezeki mpaka aingie Jahannam, na hayo ni makao maovu mno.
Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
Ni farka kubwa baina ya wanaafiki hawa na Waumini wa kweli ambao watayari kuuza nafsi zao kwa sababu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kulitukuza Neno la Haki. Hawa ni kinyume na wale wa kwanza. Hawa wakitawalishwa madaraka kuendesha mambo ya watu inakuwa ni katika upole wa Mwenyezi Mungu kuwafanyia waja wake. Mwenyezi Mungu Mtukufu huwarehemu hao waja wema kwa kuwatawalisha watu wema ili awalinde na wenye shari.
Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.
Enyi mlio amini! Na iwe baina yenu nyote amani na salama,wala msichochee chuki za kijahiliya na mengineyo kuleta sababu za ugomvi na khitilafu. Wala msipite katika njia ya Shetani anaye kupelekeeni kugawanyika, kwani yeye ni adui wenu aliye dhaahiri. Maneno haya ya Qur'ani ni wito kwa Waumini wote iwe baina yao salama na amani, na yanafahamisha kuwa vita na khasama ni katika mwendo wa kumfuata Shetani. Waumini wote wanaitwa wawe katika hali ya salama na wengineo, na wao baina yao kwa wao, wasipigane na wengine wala wasipigane wenyewe kwa wenyewe. Na maneno haya ya Qur'ani yanaonyesha kuwa mahusiano baina ya dola ya Kiislamu na nyenginezo ni salama, na huo ni msingi wa mwanzo wa dini zote za mbinguni. Wakati ilipo kuwa kanuni ya porini ndiyo inayo hukumu baina ya madola na kuwekea mipaka ya mahusiano yao, mwenye nguvu kumla mnyonge, Uislamu ulikuja na huu msingi wa kuamrisha kuwa mahusiano yawe ya Usalama. Pindi vikitokea vita basi viwe kwa ajili ya ulinzi na kuupinga uvamizi. Yaani ni kumlazimisha yule mwenye kufanya uadui awe mwenye usalama. Vita vilivyo ruhusiwa na Uislamu ni kuthibitisha nguzo za amani, na kuhakikisha uadilifu. Vita hivi ni vita vya salama, kwa ajili ya uadilifu na amani.
Na ikiwa mkateleza baada ya kukufikieni hoja zilizo wazi, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Mkigeuka mkaiacha Njia hii mliyo itiwa muifuate nyote baada ya kudhihiri hoja za kukata kuwa ndiyo Njia ya Haki, basi jueni mtapatilizwa kwa kugeuka huko, kwani Mwenyezi Mungu hakika ni Mwenye nguvu, humuadhibu mwenye kuiacha Njia yake, na Mwenye hikima anaye pima kadiri ya adhabu yake.
Je wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika, na hukumu iwe imekwisha tolewa? Na kwa Mwenyezi Mungu ndio hurejeshwa mashauri yote.
Je, hao wanao ukataa Uislamu wanangojea mpaka wamwone Mwenyezi Mungu Mtukufu na Malaika jahara katika mawingu na hukumu ya kuwakatisha tamaa zao imekwisha pitishwa? Kwani hakika mambo yote yamo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Yeye huyasarifu atakavyo, na hukumu yake imekwisha tolewa, na hapana shaka yoyote itatekelezwa tu.
Waulize Wana wa Israili: Tumewapa ishara ngapi zilizo wazi? Na anaye zibadili neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Waulize Wana wa Israili tumewaletea dalili ngapi za kukata za kuthibitisha ukweli wa Mtume! Na hayo ni neema ya kutaka kuwaongoa wamwendee Mwenyezi Mungu. Lakini wapi! Walizikataa hizo dalili na wakashikilia kuzikanusha hadi ya kuyageuza makusudio yake. Baada ya kuwa hizo dalili ni kwa ajili ya uwongofu zikawa kwa ukafiri wao ni sababu ya kuwazidisha upotovu na kutenda dhambi. Na mwenye kugeuza neema ya Mwenyezi Mungu kwa namna hii basi huyo anastahiki adhabu, na Mwenyezi Mungu hakika ni mkali wa kuadhibu.
Walio kufuru wamepambiwa maisha ya duniani; na wanawafanyia maskhara walio amini. Na wenye kuchamngu watakuwa juu yao Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
Na sababu ya kupotoka na kukufuru ni kuitaka dunia. Wale walio kufuru wamepambiwa matamanio ya maisha ya kidunia wakawa wanawakejeli wale walio amini kwa kushughulikia kwao maisha ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu atawaweka walio amini pahala pa juu kabisa kuliko wao katika Akhera. Ama kuwa hawa makafiri wana mali zaidi na mapambo ya kidunia hakuonyeshi ubora wao, kwani riziki ya Mwenyezi Mungu haipimwi kwa mujibu wa kuamini na kukufuru, bali inakwenda kama apendavyo Yeye mwenyewe. Wapo watu huzidishiwa hiyo riziki kwa "Istidraaji" kumpururia kamba tu, na wapo wanao nyimwa neema za dunia kama ni mtihani, majaribio.
Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Hakika watu wana tabia moja ya kuwa wapo tayari kupotoka, na wapo ambao sababu za uwongofu zinakuwa na nguvu kwao, na wengine upotovu ndio unawatawala. Kwa hivyo wakakhitalifiana. Mwenyezi Mungu akawapelekea Manabii kuwaongoa na kuwabashiria kheri na kuwaonya. Na akateremsha kwa hao Manabii Vitabu vyenye kukusanya Haki, ili viwe ndivyo vya kuwahukumu iondoke mizozo baina yao. Lakini wale walio nafiika na uwongofu wa Manabii ndio wao tu walio amini, hao ambao Mwenyezi Mungu amewaongoa kutokana na khitilafu wakafuata Haki. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye wapa tawfiqi watu wa Haki pindi wakisafi niya zao.
Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyo wajia wale walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Mwenyezi Mungu itakuja? Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.
Hivyo mnadhani kuwa mtaingia Peponi kwa Uislamu wa kutamka tu bila ya kupatikana na masaibu mfano wa masaibu yaliyo wasibu walio kuwa kabla yenu? Hao walipata shida na mashaka na mateso, wakatikiswa mpaka ikafika hadi ya kuwa Mtume wao mwenyewe kusema, na wao wakasema vile vile pamoja naye: Lini itakuja nusura ya Mwenyezi Mungu? Mola wao Mlezi basi anawahakikishia kwa ahadi yake kwa kuwajibu kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu
Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayo itoa ni kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na wasafiri. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua.
Waumini wanakuuliza mas-ala ya kutoa. Waambie: Kutoa iwe kutokana na mali mazuri, na wa kupewa ni wazazi wawili, na jamaa, na mayatima, na masikini, na msafiri aliye katikiwa na mali yake na watu wake. Na lolote katika vitendo vya kheri mlitendalo basi hakika Mwnyezi Mungu analijua na atakulipeni kwalo.
Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachusha kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
Ikiwa kutoa kusaidia mayatima na masikini na wengineo ni kuhami jamii ya umma kwa ndani, kadhaalika kupigana vita ni kuuhami umma na adui wa nje. Kwa hivyo enyi Waislamu, mmelazimishwa kupigana vita kuhami Dini yenu, na kulinda nafsi zenu. Hakika hizo nafsi zenu kwa mujibu wa tabia zake zinachukia mno kupigana. Lakini huenda mkachukia kitu na ndani yake ipo kheri kwenu, na mkapenda kitu na ikawa ipo shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua maslaha yenu ambayo yamefichikana, na nyinyi hamyajui. Basi tendeni mlilo amrishwa kulitenda.
Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.
Waislamu walichukia kupigana katika mwezi mtakatifu, ndio wakakuuliza juu yake. Waambie: Naam, kupigana katika mwezi mtakatifu ni dhambi kubwa. Lakini kubwa zaidi ni haya wayatendayo maadui zenu nayo: kuwazuia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, wasende kwenye Msikiti Mtakatifu, na kuwafukuza Waislamu kutoka Makka. Na hayo maudhi na mateso yao kuwafanyia Waislamu ili waache Dini yao ni makubwa zaidi kuliko mauwaji yoyote. Kwa hivyo imehalalishwa kupigana vita katika mwezi mtakatifu kwa ajili ya kupambana na maovu haya. Hichi ni kitendo kikubwa cha kujikinga na lilio kubwa zaidi. Enyi Waislamu! Jueni kuwa mwendo wa watu hawa ni mwendo wa ukhalifu na udhaalimu. Na wao hawakubali kwenu uadilifu wala mambo ya kiakili. Na wala hawatasita kukupigeni vita mpaka wakuachisheni Dini yenu pindi wakiweza. Na atakaye dhoofika kwa mashambulio yao akaacha Dini yake na akafa katika ukafiri, basi watu kama hao watapoteza vitendo vyao vyema vyote vya duniani na Akhera. Na hao ni watu wa Motoni ambako watadumu.
Hakika wale walio amini na wale walio hama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wanao taraji rehema za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
Wenye kuamini imani ya kweli hata wakahama kwa ajili ya kuinusuru Dini na kwa ajili ya Jihadi ili Dini ienee hao wanangojea thawabu kubwa za Mwenyezi Mungu. Na ikiwa wamefanya kasoro kitu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, anasamehe dhambi, Mwenye kurehemu, anawarehemu waja wake kwa uwongofu na kuwalipa.
Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri--
Ewe Muhammad! Wanakuuliza juu ya hukumu ya ulevi na kamari. Waambie kwamba katika yote mawili hayo pana madhara makubwa, kwa kuharibu siha na kupoteza akili na mali, na kuleta chuki na uadui baina ya watu. Pia ndani ya hayo yapo manufaa, kama kujipumbaza na kupata faida ya sahali. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake, basi epukaneni nayo. Na wanakuuliza watoe nini? Wajibu watoe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kilicho chepesi na hakina uzito kukitoa. Hivyo ndio Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri yale yatakayo kurejeeni katika maslaha ya dunia na Akhera. Kifungu hichi cha Qur'ani kinatuwekea wazi makusudio ya sharia ya Kiislamu. Kinatueleza kuwa sharia inataka manufaa ya waja. Chenye kuzidi nafuu yake kuliko madhara kinafaa. Chenye nafuu chache kuliko madhara kinakatazwa. Pia kifungu kinatuonyesha kuwa vitu ulimwenguni vimechanganya mema na mabaya. Hapana ovu lisio kuwa na wema, wala wema usio na uovu. Ulevi, mama wa maovu, unao haribu akili na kumfanya mtu kuwa mnyama, nao una faida pamoja na uovu wake usio na mpaka. Na kamari inayo shughulisha nafsi na akili, ikaleta mpapatiko usio sita, nayo ina nafuu yake pamoja na kuwa na madhambi yanayo fisidi maisha na nyumba za watu, na kila makhusiano bora ya binaadamu.
--Katika mambo ya dunia na mambo ya Akhera. Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Mwenyezi Mungu angeli penda angeli kutieni katika udhia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Na wanakuuliza khabari ya mayatima: katika Uislamu inapasa watendejwe? Sema ni kheri yenu na yao kuwatendea wema. Wawekeni katika nyumba zenu pamoja nanyi, na changanyikeni nao kwa makusudio ya kheri si ya fisadi, kwani wao ni ndugu zenu duniani, wanahitaji kwenu mchanganyiko huu. Na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji katika nyinyi. Basi tahadharini! Na Mwenyezi Mungu angeli penda angeli kupeni taabu, akakulazimisheni kuwaangalia mayatima bila ya kuchanganyika nao, au angeli kuacheni bila ya kubainisha waajibu wanao pasa kutendewa. Kwa hivyo wangeli kulia kuchukia watu, na hayo yange pelekea kufisidika na kuleta shida kwa jamii zenu. Kwani kuwakahirisha mayatima na kuwadhili huwafanya wawachukie hao jamaa wawatendao vibaya. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda katika amri yake, lakini naye ni Mwenye hikima halazimishi katika sharia ila lenye maslaha yenu.
Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka.
Hapana ubaya wowote kuchanganyika na mayatima, lakini kuchanganyika na washirikina ni vibaya. Muumini hana ruhusa kumwoa mshirikina asiye fuata dini ya Kitabu cha mbinguni. Basi msipelekewe kutaka kumwoa mwanamke wa kishirikina kwa ajili ya mali yake, au uzuri wake, au jaha yake, au ukoo wake. Muumini aliye mtumwa ni bora kuliko mshirikina aliye huru mwenye mali, na jamali, na utukufu na nasaba. Wala nyinyi msiwaoeze wanawake walio mikononi mwenu wanaume wa kishirikina wasio amini Vitabu vya mbinguni, wala yasikupelekeeni kumkhiari mshirikina utajiri na cheo chake. Mtumwa Muumini ni bora kuliko huyo. Hao washirikina wanawavutia wenzao kwenda katika maasi na ushirikina, na kwa hivyo wanapaswa kuingia Motoni. Na Mwenyezi Mungu anapo kulinganieni mjitenge na ndoa za washirikina anakulinganieni kwa ajili ya maslaha yenu na mwongoke ili mpate Pepo na maghfira, na mwende katika njia ya kheri kwa taisiri. Na Mwenyezi Mungu anabainisha sharia zake na uwongofu wake kwa watu wapate kujua maslaha yao na kheri yao.
Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wat'ahirike. Wakisha t'ahirika basi waendeeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha.
Na wanakuuliza juu ya kuwaingilia wake zenu wakati wanapo kuwa na damu ya mwezi, hedhi. Waambie kuwa hedhi ni uchafu. Basi jizuieni kuwaingilia wakati wake mpaka wat'ahirike (wasafike). Wakit'ahirika basi ingianeni nao katika njia za maumbile. Na ikiwa mtu amefanya makosa katika haya, basi na atubu, na Mwenyezi Mungu anapenda waja wake wakithiri toba na usafi kutokana na uchafu. Ilimu ya kisasa zimethibitisha kuwa wakati wa hedhi yanaweza kuwa madhara kwa kuwa zalio huweza kupata maradhi pindi likiingiliwa na vidudu vya maradhi, ambavyo ni vyepesi kuingia wakati wa kuingiliana na mwanamume. Maradhi hayo huenda yakasababisha mwanamke asiweze kuzaa. Mwanamume naye huambukia maradhi hayo kutokana na mwanamke kwa kupitia njia za mkojo, na maradhi yakapanda juu mpaka mafigo yakaharibika, na kuathirika vyombo vya uzazi, na mwanamume naye akawa hawezi kutia mimba. Maradhi haya huleta machungu makubwa. Watu walikuwa hawajui, lakini Mwenyezi Mungu anajua kila kitu. Na mwanamke anapo kuwa na damu anakuwa hana raghba ya kuingiliwa, basi kumuingilia wakati huo huenda kukamletea hali ya nafsi mbaya na chuki kwa jambo hilo.
Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini.
Wake zenu ni mwahali mwa kupatia uzazi, kama vile mbegu inavyo toa mmea. Basi ni halali kwenu kuwaingilia vyovyote kwa sharti ya kupitia njia za uzazi. Na mcheni Mwenyezi Mungu wala msimuasi katika kukaa kwenu na wanawake. Na mjue kuwa nyinyi mtakutana naye, na mna jukumu kwake. Furaha ni ya hao wanao simama juu ya mipaka yake Mtukufu na hawaikiuki.
Wala msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa ni kisingizio cha kuacha kufanya wema na kuchamngu na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
Msilichezee jina la Mwenyezi Mungu katika kukithirisha viapo, kwani hivyo inakuwa ni kinyume na kulitukuza jina la Mwenyezi Mungu. Na hakika kujilinda na kukithirisha kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ndio hupelekea vitendo vyema, na kuchamngu, na kuweza kusuluhisha baina ya watu. Mwenye kujilinda hivyo huwa anatukuka cheo katika macho ya watu, na anakuwa anaaminika, na kauli yake hukubalika kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno yenu na yamini zenu, na Mjuzi wa niya zenu.
Mwenyezi Mungu hakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi. Bali anakushikeni kwa yanayo chuma nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.
Mwenyezi Mungu amekusameheni baadhi ya yamini (viapo) zenu. Lilio mpitia mtu ulimini mwake katika viapo bila ya kukusudia wala kulitia moyoni, au akaapa kwa kuamini kuwa limetukia na halikutukia, Mwenyezi Mungu hayachukulii hayo. Lakini anakushikeni kwa mnayo yaazimia katika nyoyo zenu kuwa yamekuwa au hayakuwa, na kwa kusema uwongo pamoja na kuuwapia yamini. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumghufiria mwenye kutubu, ni Mpole, anasamehe lisilo kusudiwa moyoni.
Kwa wanao apa kuwa watajitenga na wake zao, wangojee miezi mine. Wakirejea basi Mwenyezi Mungu hakika ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
Na hawa walio apa kuwa hawatawakaribia wake zao, na wangoje muda wa miezi mine. Wakiwaingilia wake zao mnamo muda huu ndoa itaendelea, lakini juu yao ni kafara kwa yamini yao. Na Mwenyezi Mungu amewasamehe na anakubali kafara kwa rehema yake kuwahurumia.
Na wakiazimia kuwapa talaka basi, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mjuzi.
Na ikiwa hawakuwaingilia wake zao katika muda huu inakuwa hayo ni madhara kwa mwanamke. Basi hapana ila t'alaka tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzisikia yamini zao, na Mwenye kuzijua hali zao, na atawahisabu kwa hayo Siku ya Kiyama.
Na wanawake walio achwa wangoje peke yao mpaka t'ahara (au hedhi) tatu zipite. Wala haiwajuzii kuficha alicho umba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya sulhu. Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Yawapasa wat'alaka wangojee bila ya kufanya pupa ya kuolewa muda wa hedhi tatu , ili kuhakikisha hawana mimba na kujipa nafasi ya kumkinika kurejeana. Wala si halali kwao kuficha mimba au damu ya hedhi. Huo ndio mwendo wa wanawake wanao muamini Mwenyezi Mungu na kukutana naye Siku ya Akhera. Na waume zao wanayo haki kuwarejea katika ule muda wa eda. Na wanaume wanapo tumia haki wakusudie kupatana si kudhuru. Wanawake nao wana haki mfano wa jukumu lilio juu yao katika mambo yasio kuwa kinyume na Sharia Tukufu (2). Na wanaume wana daraja juu yao ya ulinzi na kuyahifadhi maisha ya nyumbani na mambo ya watoto. Mwenyezi Mungu Subhanahu yuko juu ya waja wake, na Yeye ndiye anawatungia sharia zinazo wafikiana na hikima. (1) Zingatia: Khabari ya eda ya mt'alaka limefasiriwa neno "Qurui" na wanazuoni wengi kuwa ni "Hedhi". Na wamefasiri Shafii (na Malik) kuwa ni "T'ahara". Khabari nyengine za eda zitakuja baadae. Sharia ya eda imekuja ili kuhakikisha kuwa ipo mimba au hapana, kwani hayo hayawezi kuhakikishwa ila baada ya kupita hedhi (au t'ahara) tatu, kwani mbegu za uzazi haziwezi kuishi baada ya hedhi tatu. Mwenye mimba kwa kawaida hatoki hedhi, na akitoka ni mara moja au sana mara mbili. Kwani hakika hapo ile mimba huwa imepevuka kwa muda huo hata kufikia kujaza eneo lote la tumbo la uzazi, na kwa hivyo ikazuia kuteremka damu ya mwezi. Hiyo ni kudra ya Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake, na hayakuwa hayo yanajuulikana na Waarabu, na wala hayakuwa yajuulikaane na Nabii asiye jua kusoma. Lakini Mwenyezi Mungu alimteremshia Qur'ani, akamfunza yeye na akaufunza umma wake. Na sababu ya pili ya sharia ya eda ni kumpa fursa ya mt'alaka kurejea kwa mumewe baada ya kuwaza na kufikiri na kutua. Na hapo ni mume kusema: "Nimekurejea". Lakini hii itahisabiwa ni moja katika t'alaka tatu. Mwenyezi Mungu amempa mwanamke haki kama zile zinazo mwajibikia yeye. Na mwanamume amepewa cheo cha ulinzi na kuhifadhi. Na juu yake ni waajibu wa uadilifu. Uislamu ndio ulio mpa mwanamke haki ambazo hakupata kupewa na mila zote zilizo tangulia. Kwa Warumi mwanamke alikuwa ni kijikazi wa nyumba ya mumewe. Ana jukumu, lakini hana haki. Hali kadhaalika kwa Waajemi. (Na vivyo hivyo katika dini za Kiyahudi, Kikristo na Kibaniani.) Paulo ameandika katika 1 Korintho: "Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo. Na wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu kunena katika kanisa." - 1 Korinth. 14.34-35. "Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume. Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume. Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume." 1 Korinth. 11.7.9 "Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna. Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.." 1 Timotheo 2.11-14. Na hapana popote katika Biblia panapo kataza Mayahudi au Wakristo kuoa wake wengi, isipo kuwa kauli moja tu ya Paulo inayo mpendekeza Askofu aoe mke asiye zidi mmoja. Kauli hiyo iko katika Waraka wa Kwanza wa Paulo kwa Timotheo 3.2: "Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, n.k." Je, ni Uislamu au Ukristo ulio mweka chini mwanamke?)
T'alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhaalimu.
T'alaka ni mara mbili. Baada ya kila t'alaka ana haki mume kukaa naye kwa kumrejea kabla ya kwisha siku za eda, au kumrejesha katika dhamana yake kwa kumwoa upya. Na katika hali hiyo inapasa makusudio yake ni kukaa naye kwa uadilifu na kumtendea wema, au kuachana kwa ihsani na heshima bila ya kukhasimiana. Wala si halali kwenu, enyi waume, kuchukua chochote mlicho wapa wanawake ila mkikhofu kuwa hamtoweza kufuata haki za uke na ume alizo kubainishieni Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, na akaku lazimisheni mzifuate. Mkikhofu, enyi Waislamu, kutofuata haki za mume na mke vilivyo kama alivyo eleza Mwenyezi Mungu basi ameamrisha mke atoe mali kwa ajili ya kutokana na mumewe. Na hizi ni hukumu zilizo pitishwa, msiende kinyume nazo, mkazipindukia. Mwenye kufanya hivyo amejidhulumu nafsi yake na amedhulumu jamii anayo ishi kati yake. Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameifanyia sharia T'alaka, na akampa mwanamume kwanza uwezo wa kuacha. Baadhi ya watu wanadhani kuwa haya huleta madhara katika maisha na kusahilisha kuvunjika nyumba za watu. (a) Ama kupewa haki ya kuacha mwanamume kwa hakika hakupewa haki hiyo bila ya masharti yoyote. Katika masharti hayo aliyo wekewa ni: KWANZA hana ruhusa kuacha ila t'alaka moja ya kuweza kurejea, yaani anakuwa na haki ya kumrejea mke kabla ya kwisha eda. Ama amrejee naye yu ndani ya eda au amwache, na hivyo tena ni dalili ya hadi ya kuchukiana, na hapana maisha ya mume na mke tena kuchukiana kumefika hadi hiyo. PILI asimwache wakati wa hedhi, kwani wakati huo mwanamke huwa na hamaki, kwa hivyo huwa hapana utulivu. Na huenda hiyo hedhi ndiyo sababu ya hizo chuki zilizo zidi. Basi asiache mpaka mambo yawe yametua. TATU asimwache naye yumo katika t'ahara aliyo kwisha muingilia, kwani hiyo yaweza kuonekana huko kuchukiana kunatokana na kutokuwa na raghba na mkewe. Basi mambo yakiwa hivi t'alaka inakuwa katika hali ya chuki iliyo na nguvu, na kukatika mapenzi ya daima.
Na kama amempa t'alaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu anayo ibainisha kwa watu wanao jua.
Mume akimwacha mkewe mara ya tatu baada ya T'alaka mbili za mwanzo basi hamhalalikii mpaka yule mke aolewe na mume mwengine aingie harusi. Akimwacha baada ya hapo basi anaweza kufunga ndoa tena na yule mume wa kwanza, na wala hapana dhambi juu yao kuanza maisha mapya kwa ndoa mpya. Lakini yawapasa waazimie kuendesha maisha mema ya mume na mke wakifuata sharia alizo ziwekea mipaka Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la. Na mipaka hii imebainishwa wazi kwa mwenye kuamini sharia ya Kiislamu na anataka ilimu na a'mali njema.
Na mtakapo wapa wanawake t'alaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa maskhara. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima anacho kuonyeni kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Mnapo wawacha wake wakakaribia kumaliza eda zao mnaweza kuwarejea kwa makusudio ya uadilifu na kukaa nao kwa wema bila ya kuwadhuru, na pia mnaweza kuwaacha watimize eda zao kwa kuzingatia muamala mwema ulio laiki wakati wa kufarikiana bila ya kuwatendea mabaya. Wala haijuzu katika kuwarejea ikawa makusudio yake ni madhara na kuirefusha eda. Mwenye kutenda hayo basi mwenyewe amejinyima starehe ya maisha ya mke na mume, na imani ya watu kwake, na anastahiki kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu. Wala msizifanyie maskhara na mchezo na kuwa ni upuuzi hukumu za Mwenyezi Mungu zilizo kuja katika Aya hizi kwa ajili ya kutengeza maisha ya kinyumba, na zikaweka khatamu za ukoo katika mikono ya wakili, naye ni mume, mkawa mnatoa T'alaka bila ya sababu, na mkawapatisha wake zenu madhara na maudhi. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu kwa kukupangieni mpango bora kabisa katika maisha ya ndoa, na pia kwa aliyo kuteremshieni katika Kitabu kilicho bainisha wazi ujumbe wa Muhammad, na ilimu mbali mbali zenye manufaa, na mifano na hadithi za kukuwaidhini na kukuongoeni. Na jikingeni na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa Mwenyezi Mungu anajua siri zenu na mnayo dhihirisha na niya zenu na vitendo vyenu. Naye ni Mwenye kukulipeni kwa myatendayo.
Na mtakapo wapa wanawake t'alaka nao wakamaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema. Hayo anaonywa nayo yule miongoni mwenu anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni bora zaidi kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua, lakini nyinyi hamjui.
Mmnapo waacha wake na zikatimia eda na akitaka mwanamke kuanza maisha mapya kwa kuolewa tena ama na yule mku-mwenziwe au na mwanamume mwengine, basi si halali kwa wazee wala yule mku-mwenza kuwakataza, ikiwa pande mbili zimeridhiana kufanya ndoa mpya kwa kutaka maisha bora yatakayo pelekea masikilizano mema baina yao. Anawaidhiwa hayo anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Mwendo huo unapelekea kukuza mahusiano ya hishima na sharaf katika jamii zenu, na ni usafi zaidi katika nafsi zenu kut'ahirika na uchafu na mahusiano yaliyo maovu. Na Mwenyezi Mungu anajua maslaha ya binaadamu na siri za nafsi zao ambazo wao hawajui vipi kuzipata.
Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlicho ahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayo yatenda.
Ni juu ya kina mama kuwanyonyesha wana wao muda wa miaka miwili iliyo timia kwa maslaha ya mtoto mchanga, akitaka hayo mmojapo au wote kati ya wazazi. Itamlazimu baba, kwa kuwa mtoto ni wake, amkimu mama kwa chakula na nguo kwa uwezo wake bila ya israfu wala uchoyo. Kwani haimlazimu mtu kufanya ila kiasi ya uwezo wake, na wala haitakikani kumletea madhara mama kwa kumnyima haki yake ya kumkimu yeye na kumlea mwana. Kadhaalika haitakikani mtoto awe sababu ya kumletea madhara baba yake kwa kumkalifu zaidi kuliko uwezo wake, au kumharimisha haki yake kwa mwanawe. Na akifa baba au akawa fakiri hawezi kazi kiamu kitakuwa juu ya mrithi wa mtoto ikiwa mtoto ana mali yake. Wakitaka wazazi kumwachisha ziwa mtoto kabla ya kutimia miaka miwili wakakubaliana kwa hayo na huku wakiangalia maslaha ya mtoto basi hapana ubaya. Na nyinyi wazazi mkitaka kumpa mama mwingine kumnyonyesha mtoto pia hapana ubaya - na hapo mtamtolea ujira kwa ridhaa na ihsani. Katika myatendayo muangalieni Mwenyezi Mungu, na mjue kuwa Yeye anayajua myatendayo na atakulipeni kwayo. Qur'ani inawajibisha mama amnyonyeshe mwanawe na asinyonyeshwe na mwingine ila kwa dharura, kwani kunyonyesha yeye ni faida kwa mama na mtoto katika siha. Na kuachisha ziwa kuwe kwa taratibu, na yajuzu kabla ya kutimiza muda ikiwa siha ya mtoto inaruhusu hayo
Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha wake, hawa wake wangoje peke yao miezi mine na siku kumi. Na wanapo timiza eda yao basi hapana ubaya kwao kwa wanao jifanyia kwa mujibu wa ada. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
Miongoni mwenu enyi wanaume, akitokea aliye kufa akaacha mke asiye na mimba, basi mwanamke yampasa akae eda, yaani asiolewe, muda wa miezi mine ya kuandama na siku kumi mchana na usiku, ili kuhakikisha kiliomo tumboni, kama ana mimba au la. Ukisha muda huu, enyi wazee, hapana ubaya kwenu mkiwaachilia kuleta mtu wa hishima kuja mposa. Haifai nyinyi kuwazuilia hayo, na haijuzu kwao kufanya mambo yanayo kataliwa na Sharia, kwani Mwenyezi Mungu anajua vyema siri zenu na anavijua vitendo vyenu, na atakuhisabuni kwa myatendayo.
Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.
Katika muda wa eda hapana dhambi kwenu, nyinyi wanaume, mkiwaonyesha dalili kuwa mnadhamiria kutaka kuwaoa waliomo edani kwa kufiwa na waume zao, lakini hayo yawe ni kudhamiria ndani ya moyo tu. Mwenyezi Mungu hakika anajua kuwa hamwezi kuacha kuwazungumza waliomo edani, kwani ni maumbile baina ya wanaume na wanawake. Kwa hivyo mmepewa ruhusa kuashiria bila ya kubainisha kwa maneno. Basi msiwape ahadi ya kuwaoa ila iwe ishara isiyo ovu wala ya uchafu. Basi msifunge ndoa mpaka baada ya kwisha eda. Na kuweni yakini kuwa Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha ndani ya nyoyo zenu. Basi iogopeni adhabu yake, wala msitende anayo kukatazeni. Wala msikate tamaa na rehema yake pale mnapo ikhalifu amri yake, kwani Yeye ni Mwenye kughufiria mno, na anakubali toba ya waja wake, na anasamehe makosa, kama alivyo Mpole hafanyi haraka ya kuwaadhibu wale wanao vunja aliyo yakataza.
Hapana ubaya kwenu mkiwapa T'alaka wanawake ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo - maliwaza kwa mujibu wa dasturi kuwa ni haki juu ya watendao mema.
Wala hapana dhambi kwenu enyi waume, wala hapana mahari juu yenu mkiwaacha wake kabla ya kuingia harusi na kabla hamjawatajia kiasi cha mahari. Lakini wapeni zawadi kama kuwapoza kuwapunguzia machungu ya moyo. Na hicho mnacho toa kiwe cha kuridhisha na kupendeza moyo. Tajiri atoe kwa kadiri ya wasaa wake, na fakiri kwa kadiri ya hali yake. Na zawadi hiyo ni katika a'mali za kheri wanazo jilazimisha nazo watu wenye muruwa na watu wa kheri na ihsani.
Na mkiwapa T'alaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlio agana, isipo kuwa ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Pindi mkiwapa T'alaka wanawake kabla ya kuingia harusi lakini baada ya kwisha wafikiana mahari, basi ni haki yao hao wat'alaka wapewe nusu ya mahari, ila wenyewe kwa ridhaa yao wakikataa kuchukua kitu. Na wao pia hawapewi zaidi ya nusu ila waume nafsi zao wakasamehe na wakatoa mahari yote kaamili. Na kila mmoja wapo kusamehe ndio ubora zaidi na ni kumridhisha zaidi Mwenyezi Mungu, na ndio mambo yanavyo elekea kwa wachao Mungu. Basi msiache huu mwendo wa kusameheana. Na kumbukeni kuwa kheri iko katika kufadhiliana na kufanyiana ihsani. Hayo ndiyo yanayo pelekea kupendana baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema dhamiri zenu na atakulipeni kwa fadhila mzitendazo.
Zilindeni Swala, na khasa Swala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
Fanyeni hima katika kusimamisha Swala zote na kuzidumisha. Na fanyeni hima kuwa Swala yenu iwe ni Swala bora kwa kuzitimiza nguzo zake na kumsafia niya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu katika Swala. Na timizeni ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mkumbukeni kwa usafi wa moyo na kunyenyekea Utukufu wake.
Ikiwa mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapo kuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyo kufunzeni yale mliyo kuwa hamyajui.
Ukikufikieni wakati wa Swala nanyi mko katika khofu basi msiache kusali, bali swalini kama muwezavyo, ikiwa huku mnakwenda kwa miguu au mmepanda kipando. Ikiondoka khofu swalini kwa kutimiza nguzo zote kama mlivyo jifunza, mkimkumbuka Mwenyezi Mungu katika Swala na mkimshukuru kwa aliyo kufunzeni, na kwa kukujaalieni kuwa katika amani.
Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakawacha wake, na wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi kwa mwaka mmoja bila ya kuwatoa nyumba. Na wanawake wenyewe wakiondoka, basi hapana ubaya kwenu kwa waliyo jifanyia wenyewe kwa mujibu wa Sharia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Wanao kufa miongoni mwenu wakaacha wake zao, Mwenyezi Mungu ameusia hao wanawake wafiwa wabaki nyumbani mwa waume zao muda wa mwaka mzima kwa maliwaza na kuwaondolea ukiwa. Wala hana haki yeyote kuwatoa. Wakitoka kwa khiari yao kabla ya mwaka kwisha basi hamna dhambi nyinyi wenye madaraka mkiwaachilia wajitendee wenyewe wapendalo kwa lisio vunja Sharia tukufu. Na mt'iini Mwenyezi Mungu katika hukumu zake, na tendeni Sharia alizo kutungieni kwani Yeye ni Muweza wa kumuadhibu anaye kwenda kinyume na amri yake, na Yeye ni Mwenye hikima iliyo pita ukomo. Hakuamrishini ila lenye maslaha yenu ijapo kuwa hikima yake imepindukia ujuzi wenu.
Na wanawake walio achwa wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Sharia. Haya ni waajibu kwa wachamngu.
Na wanawake walio pewa T'alaka baada ya kuingia harusi wana haki wapewe mali ya kuwaliwaza. Wapewe kwa wema, kwa kadiri ya utajiri na umasikini wa mume. Kumcha Mwenyezi Mungu kunawajibisha hayo, na pia watu wa Imani wanalazimika na hayo.
Namna hivi anakubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake ili mpate kufahamu.
Mwenyezi Mungu anakubainishieni hukumu zake, na neema zake, na Aya zake, kwa mfano wa bayana hizi na Sharia hizi zilizo wazi zenye kuleta maslaha, ili mpate kuzingatia na mpate kutenda yaliyo kheri.
Hukuwaona wale walio toka majumbani kwao kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni! Kisha akawahauisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru.
Zingatia, ewe Nabii, hichi kisa cha ajabu, na ukijue! Hao watu walitoka wakaacha majumba yao ati wanakimbia Jihadi kwa kuogopa kufa, na hali wao ni maelfu kwa maelfu. Mwenyezi Mungu akawahukumia kifo na udhalili kutokana na maadui zao. Walipo bakia walio bakia wakasimama kupigana Jihadi, Mwenyezi Mungu aliwapa uhai kwa kuwapa nguvu. Hakika uhai huu wenye nguvu ulio kuwa baada ya madhila umekuja kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu, na unastahiki shukrani. Lakini wengi wa watu hawashukuru.
Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi na Mjuzi.
Mlivyo jua kuwa hamwezi kuyaepuka mauti kwa kuyakimbia, basi piganeni Jihadi, na zitumieni nafsi zenu kwa kulitukuza Neno la Mwenyezi Mungu, na kuweni na yakini kuwa Mwenyezi Mungu anayasikia wanayo yasema woga na wanaafiki wanao kimbia, na wayasemayo Mujaahidina wanao pigana, na anayajua anayo dhamiria kila mtu katika nafsi yake. Na kwa lilio kheri atamlipa kheri, na kwa shari atamlipa shari.
Ni nani atakaye mkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema ili amzidishie mzidisho mwingi, na Mwenyezi Mungu hukunja na hukunjua. Na Kwake Yeye mtarejea.
Na Jihadi kwa Njia ya Mwenyezi inhaitaji mali, basi toeni mali yenu. Mtu gani huyo ambaye hatoi mali yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa radhi ya nafsi yake, na hali Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa atamrejeshea mara nyingi sana zaidi? Na riziki zote zimo katika mkono wa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye humkunjia amtakaye na akamkunjulia amtakaye kwa yaliyo na maslaha yenu. Marejeo ni kwake Yeye, naye atakulipeni kwa mujibu mlivyo toa. Na ilivyo kuwa riziki zote ni kwa fadhila ya Mwenyezi na Yeye ndiye mwenye kutoa na mwenye kunyima basi ameitwa yule mwenye kutoa kuwa ni kama mkopeshaji ili kuhimiza na kupendekeza kutoa, na kutilia mkazo kuwa malipo ni mara nyingi sana duniani na Akhera.
Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipo mwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto wetu? Lakini walipo andikiwa kupigana waligeuka, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
Zingatia khabari hii ya ajabu ya baadhi ya Wana wa Israili baada ya zama za Musa. Walimtaka Nabii wao wa wakati ule awawekee mtawala ataye weza kuwakusanya baada ya mfarakano walio kuwa nao, awaongoze chini ya bendera ya kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu na kurejeza utukufu wao. Yule Nabii akawauliza kuhakikisha kama wana ukweli katika jambo hilo: "Je haiwezi kuwa nyinyi mtaingia woga mkatae kupigana pindi mkifaridhiwa mpigane?" Wakakataa hayo wakisema: "Itakuwaje tusipigane kurejeza haki zetu, na hali sisi tumefukuzwa makwetu na adui?" Mwenyezi Mungu alipo waitikia yale wayatakayo na akaandikia vita wakakataa ila kikundi cha wachache tu miongoni mwao. Na kule kukataa kwao ni dhulma kujidhulumu nafsi zao, na Nabii wao na Dini yao. Na Mwenyezi Mungu anayajua hayo kwao, na atawalipa malipo ya madhaalimu.
Na Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu amekuteulieni Twaluti (Sauli) kuwa ni mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.
Nabii wao akawaambia: "Hakika Mwenyezi Mungu amekuitikieni, basi amemkhiari Twaluti awe ndiye mtawala wenu." Wakuu wao wakapinga huo uteuzi wa Mwenyezi Mungu, wakisema: "Kwa nini awe yeye ni wa kututawala na hali sisi ni bora kuliko yeye. Yeye si mtu wa ukoo bora wala hana mali." Nabii wao akawarudi kwa kusema: "Mwenyezi Mungu amemkhiari yeye kuwa ni mtawala wenu kwa sababu ana sifa nyingi za uwongozi, kama mazoezi makubwa katika mambo ya vita, na siyasa ya kutawala, pamoja na nguvu za mwili. Na utawala uko katika mkono wa Mwenyezi Mungu humpa amtakaye katika waja wake, wala yeye hatagemei urithi wala mali." Na fadhila za Mwenyezi Mungu na ujuzi wake umeenea. Yeye huchagua lilio na maslaha yenu.
Na Nabii wao akawaambia: Alama ya ufalme wake ni kukuleteeni lile sanduku ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho kwa Mola wenu Mlezi, na mna mabaki ya waliyo yaacha kina Musa na kina Harun, wanalichukua Malaika. Bila shaka katika hayo zimo dalili kwenu ikiwa nyinyi mnaamini.
Na Nabii wao aliwaambia: "Hakika dalili ya ukweli wangu kuwa Mwenyezi Mungu amemteua Twaluti awe ni mtawala wenu ni kuwa atakurejesheeni sanduku la Taurati mlio nyang'anywa, linalo bebwa na Malaika. Na ndani yake yamo baadhi ya mabaki ya watu wa Musa na watu wa Harun walio kuja baada yao. Na likiletwa sanduku hilo nyoyo zenu zitatua. Katika hayo hakika pana dalili ambazo zitakupelekeeni kumfuata na kumridhia, ikiwa kama kweli nyinyi mnataka Haki na mnaiamini."
Basi Twaluti alipo ondoka na majeshi alisema: Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na asiye kunywa atakuwa pamoja nami: ila atakaye teka kiasi ya kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipo kuwa wachache tu miongoni mwao. Alipo vuka mto yeye na wale walio amini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
Taluti alipo toka nao aliwaambia: "Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa mto ambao mtaukuta njiani mwenu. Msinywe katika mto huo ila tama moja tu. Mwenye kunywa zaidi ya hivyo basi hayumo katika jeshi letu, wala jamii yetu. Kwani amekuwa ameacha kumt'ii Mwenyezi Mungu. Wala asinifuate ila yule ambaye hakunywa ila tama moja tu." Hawakuweza kuvumilia jaribio hili, wakanywa maji mengi, ila wachache tu kati yao. Basi akafuatana na hichi kikundi kidogo akavuka nao mto. Walipoona wingi wa maadui wao walisema: "Hatutoweza hii leo kupigana na Jaluti na askari wake kwa wingi wao na uchache wetu." Baadhi yao wenye nyoyo madhbuti kwa kutaraji kwao malipo ya Mwenyezi Mungu watapo kutana naye, walisema: "Msiogope kitu! Mara nyingi wachache wenye kuamini huwashinda wengi walio makafiri. Subirini, kwani ushindi watapata wenye kusubiri."
Na walipo toka kupambana na Jaluti na majeshi yake walisema: Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utusaidie tuwashinde watu Makafiri.
Waumini walipo songa kupigana na Jaluti na jeshi lake walimwelekea Mwenyezi Mungu wakamnyenyekea na kumwomba awajaze subira, awatie nguvu azma zao, naawaweke imara katika uwanja wa vita, na awape ushindi juu ya maadui zao makafiri.
--Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua, na Daudi akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hikima, na akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawapambanishi watu kwa watu basi dunia ingeli haribika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu wote.
Basi wale Waumini waliwashinda maadui zao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Daudi, mmoja wa askari wa Taluti, akamwuuwa Jaluti amiri-jeshi wa makafiri. Na Mwenyezi Mungu akampa Daudi utawala baada ya Twaluti. Akampa na unabii na ilimu yenye manufaa, na akamfunza kwa ayapendayo Mwenyezi Mungu. Na huo ndio mwendo wake Mwenyezi Mungu - kuwanusuru wale wanao tenda mema duniani wala hawafanyi ufisadi. Lau kuwa Mwenyezi Mungu hawasalitishi askari wake kupambana na mafisadi kwa ajili ya kuondoa ufisadi wao, na akawasalitisha waovu wenyewe kwa wenyewe, ulimwengu usingeli endelea. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye hisani na fadhila daima milele juu ya waja wake.
Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.
Kisa hichi ni katika mafunzo ya kuzingatia tunakusimulia kwa kweli, ili kiwe ni ruwaza kwako na dalili ya ukweli wa Utume wako, na ili ujue kuwa Sisi hakika tutakunusuru kama tulivyo wanusuru Mitume walio kuwa kabla yako.
MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.
Hao ni Mitume ambao baadhi yao tumewataja, wengine tumewatukuza kuliko wenginewe. Wamo kati yao walio semezwa na Mwenyezi Mungu ana kwa ana, kama Musa. Na wengine kati yao Mwenyezi Mungu amewanyanyua kushinda vyeo vya wote, kama Muhammad ambaye akamkhusisha kumpa Ujumbe kwa ulimwengu wote, na kukamilisha Sharia, na kuwa ni Mtume wa mwisho. Na miongoni mwao ni Isa bin Maryam, ambaye Mwenyezi Mungu alimtia nguvu kwa kumpa miujiza kama kufufua wafu, na kuponyesha upofu na ukoma, na akamletea Jibril, Roho Mtakatifu, ili kumtia nguvu. Na Mitume hawa wameleta Uwongofu, na Dini ya Haki, na Ushahidi ulio wazi wenye kuongoa. Kwa haya imewajibikia watu wote wawaamini, wala wasikhitalifiane, wala wasipigane. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasipigane hao watu baada ya kuletewa Mitume na ishara zilizo wazi zenye kuonyesha Haki, pasingetokea kupigana wala kukhitalifiana. Lakini Mwenyezi Mungu hakutaka hayo. Kwa hivyo wakakhitalifiana. Basi kati yao wakawapo walio amini, na wengine walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli uwana wala wasingeli khitalifiana. Bali wangeli kuwa wote katika Haki. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda apendalo.
Enyi mlio amini! Toeni katika tulivyo kupeni kabla haijafika Siku ambayo hapatakuwapo biashara, wala urafiki, wala uombezi. Na makafiri ndio madhaalimu.
Enyi mlio muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho! Toeni baadhi ya tuliyo kuruzukuni kwa ajili ya mambo ya kheri. Fanyeni haraka kwa hayo kabla haijafika Siku ya Kiyama ambayo itayo kuwa yote ni ya kheri, wala hazipatikani sababu za kuzozana. Siku hiyo hamwezi kuyadiriki yaliyo kwisha kupiteni duniani, na hapo haitakufaeni biashara, wala urafiki, wala uombezi wa mtu yeyote bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu. Na siku hiyo dhulma za makafiri zitadhihiri kwa kuwa hawakuitikia Wito wa Haki.
Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu.
Mwenyezi Mungu ndiye anaye stahiki kuabudiwa pekee. Yeye ndiye Mwenye kubaki, Mwenye kuyasimamia mambo ya viumbe daima. Haghafiliki kabisa, wala hanyong'onyei, wala halali wala yanayo fanana na hayo, kwani Yeye hasifiki na upungufu wa chochote. Yeye pekee ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi, wala hana mshirika yeyote katika hayo. Kwa hivyo hapana kiumbe anaye weza kumwombea mwenginewe ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Yeye Subhanahu wa Taa'la anajua kila kitu. Anayajua yaliyo kuwa na yatayo kuwa. Hapana mtu anaye weza kujua kitu katika ilimu ya Mwenyezi Mungu ila atakavyo Yeye ajue na aridhie. Utawala wake umeenea mbinguni na ardhini. Hayamhangaishi Yeye kuyadabiri hayo, kwani Yeye ametukuka, hana upungufu wala kushindwa na jambo, Muadhamu katika utukufu wake na utawala wake. Katika haya upo ushahidi wa kuonyesha ujuzi wa Mwenyezi Mungu wa daima, na Kusimamia kwake kusio koma kwa yote ya mbinguni na duniani. Pia pana ishara ya kuwa Mwenyezi Mungu hapitikiwi na vituko vinavyo zuka.Ilimu ya Sayansi imethibitisha kuwa kulala ni katika sifa ya wanyama na mimea iliyo hai. Ikiwa Mwenyezi Mungu halali basi Yeye ni hai kwa uhai ulio elekeana na dhati yake, lakini sio kama vilivyo hai vinginevyo.
Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Hapana ruhusa kumlazimisha yeyote kuingia katika Dini. Kwa Aya na Ishara zilio zagaa Njia ya Haki imewekwa wazi kutokana na njia ya upotovu. Basi aliye ongoka akafuata Imani na akakataa kufuata chochote kisicho ingia akilini, na kinacho mpelekea kuacha Haki, basi huyo ameshika njia madhbuti kabisa ya kumkinga asiingie katika upotovu, kama yule mwenye kukamata kishikio imara kilicho fungika baraabara kitacho mlinda asitumbukie shimoni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia mnayo yasema, ni Mwenye kuyajua mnayo yatenda, na ni Mwenye kukulipeni kwa vitendo vyenu.
Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao ni Mashet'ani. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.
Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuyaangalia mambo ya Waumini, na ndiye Mwenye kuwasaidia na kuwanusuru. Huwatoa kwenye kiza cha shaka na kudanganyikiwa kuendea kwenye nuru ya Haki na utulivu. Na Makafiri wenye kumkanya Mwenyezi Mungu wanashughulikiwa na Mashetani na wanao lingania shari na upotovu. Wao hao huwatoa kwenye nuru ya Imani walio umbiwa nayo na iliyo zagaa kwa dalili nyingi na ishara, na kuwatia kwenye kiza cha ukafiri na ufisadi. Na hawa makafiri ndio watu wa Motoni, na humo watadumu milele.
Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na kufisha. Ibrahim akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
Humwoni yule aliye pofuka asizione dalili za Imani akajadiliana na Ibrahim, rafiki wa Mwenyezi Mungu, katika uungu wa Mola wake Mlezi na Umoja wake, na vipi alivyo danganyika na ufalme wake alio pewa na Mola wake Mlezi hata akatoka kwenye nuru ya maumbile akaingia katika kiza cha ukafiri? Alipo sema Ibrahim: Mwenyezi Mungu huhuisha na hufisha, kwa kuitia roho katika kiwiliwili na kuitoa, yule mfalme kafiri akasema: Nami nahuisha na ninafisha kwa kusamehe na kuuwa. Basi Ibrahim akamwambia ili kuyakata majadiliano: Mwenyezi Mungu analichomozesha jua mashariki, basi wewe lileta litoke magharibi kama wewe ni mungu kama unavyo dai. Akahizika, na majadiliano yakakatika kwa nguvu za hoja zilizo kashifu udhaifu wake na kughurika kwake. Na Mwenyezi Mungu hawawezeshi wakaidi na wenye inadi kufuata Haki.
Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Kisha zingatia kisa hichi cha ajabu, cha mtu aliye pita kwenye mji uliyo kwisha teketea, sakafu za majumba yake zimeporomoka na zimebomoa viwambaza vyake, na watu wake wameangamia. Akasema huyo mtu: Vipi Mwenyezi Mungu atawahuisha tena watu wa mji huu baada ya kuwa wamekwisha kufa? Mwenyezi Mungu akamfisha yeye na akamweka, naye ni maiti, muda wa miaka mia. Kisha akamfufua, ili amwonyeshe wepesi wa ufufuaji na imtoke shaka. Kisha akamwuliza: Umekaa muda gani nawe maiti? Akajibu, naye hajui urefu wa muda wake: Siku moja, au sehemu ya siku. Akaambiwa: Bali umekaa, nawe ni mfu, muda wa miaka mia. Kisha akaonyeshwa jambo jengine kuwa ni dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Akamwambia: Angalia chakula chako hakikuchacha, na vinywaji vyako havikutaghayari. Aidha muangalie punda wako. Na hayo tumeyafanya ikudhihirikie uliyo dhani hayawi, ya kufufuliwa vilio kufa, na tukufanye wewe uwe ni Ishara ya kuwaonyesha watu ukweli wa kufufuliwa. Kisha Mwenyezi Mungu akaamrisha atazame maajabu ya kuumba kwake vilivyo na uhai, na vipi anairekibisha mifupa, na kuivisha nyama, kisha akaitia roho vikawa vinataharaki. Basi ulipo mfungukia yule mtu uweza wa Mwenyezi Mungu, na wepesi wa kufufua, alisema: Najua kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyo fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
Kitaje pia kisa cha Ibrahim alipo sema: Mola wangu Mlezi nionyeshe vipi unahuisha maiti. Mola wake Mlezi akamuuliza Ibrahim, juu ya imani yake kuamini kufufuliwa wafu, ili ajibu Ibrahim kuondoa shaka kabisa katika imani yake. Mwenyezi Mungu akamwambia: Kwani huamini kufufuliwa wafu? Ibrahim akajibu: Mimi naamini, lakini nimetaka ili moyo uzidi kutua. Akasema Mwenyezi Mungu: Basi wachukue ndege wane uwe nao ili uwajue vilivyo. Kisha uwagawe baada ya kuwachinja, na juu ya kila kilima katika vilima vilio jirani weka sehemu yao. Kisha uwete, watakujia mbio, nao ni wahai kama walivyo kuwa. Na jua kuwa Mwenyezi Mungu hashindwi na lolote. Naye ni Mwenye hikima iliyo pita hadi katika kila kitu. Ametaja Al Fakhri Al Razi na wengineo kuwa yapo maoni mengine juu ya tafsiri ya maneno haya matukufu. Nayo ni kuwa Ibrahim hakuwachinja wale ndege, wala hakuamrishwa kuwachinja. Bali aliamrishwa awakusanye kwa kuwazoesha kukaa naye. Kisha akawagawa akaweka juu ya kila kilima ndege mmoja. Kisha akawaita wakamjia. Na hii ni namna Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo umba, ni kwa amri yake ya "Kuwa" basi huwa, kama alivyo waita wakaja
Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.
Hakika hali ya wale wanao toa mali yao kwa ajili ya kumt'ii Mwenyezi Mungu na kufanya kheri, na wanapata kwa hivyo thawabu za kuzidia mara nyingi, ni kama hali ya mwenye kuatika punje moja katika ardhi yenye rutuba ikamea mmea wenye mashuke saba, katika kila shuke mna punje mia. Hii ni sura ya wingi wa Mwenyezi Mungu anavyo walipa wanao toa katika dunia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakae. Yeye ni Mwenye wasaa wa fadhila, Mwenye kuwajua wanao stahiki na wasio stahiki.
Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishii masimbulizi wala udhia kwa walicho toa, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
Hakika wanao toa mali kwa ajili ya wema unao kubaliwa na sharia bila ya kusimbulia au kutafakhari au kumcheleweshea yule anaye fanyiwa hisani, hao wana malipo bora walio ahidiwa kwa Mola wao Mlezi, wala haiwapati khofu kwa lolote wala huzuni.
Kauli njema na usamehevu ni bora kuliko sadaka inayo fuatiliwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha na Mpole.
Kauli ya kupoza nyoyo na ya kumsitiri hali fakiri usimwambie mwenginewe ni bora kuliko kumpa na baadae ukafuatizia maudhi kwa maneno au vitendo. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la si mwenye kuhitaji watu watoe na huku wanawaudhi mafakiri. Na Yeye anawawezesha mafakiri kupata riziki njema. Wala hafanyi haraka kumuadhibu asiye toa kwa matarajio huenda akaongoka akatoa.
Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Enyi Waumini! Msipoteze thawabu za sadaka zenu kwa kudhihirisha kuwa mnawafadhili wenye haja na kuwaudhi. Hivyo mnakuwa kama wale wanao toa mali zao kwa ajili ya kutafuta umaarufu na kupenda wasifiwe na watu., nao hata hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Hali ya mwenye kuonyesha kutoa kwake ni hali ya jiwe manga lenye udongo. Likateremkiwa na mvua kubwa, udongo wote ukaondoka. Basi kama mvua kubwa inavyo chukua udongo wenye mbolea likabaki jiwe tupu, basi kadhaalika masimbulizi, na maudhi, na kuonyesha watu huharibu thawabu za sadaka. Hayo hayamnufaishi mtu, na hizo ni sifa za makafiri. Epukaneni nazo! Kwani Mwenyezi Mungu hawawafikishi makafiri kupata kheri na uwongozi mwema.
Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa kuitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu; na hata kama haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Hali ya wanao toa mali zao kwa kutaka kumridhi Mwenyezi Mungu na kuzithibitisha nafsi zao juu ya Imani, ni kama hali ya bustani, au kitalu, kwenye ardhi yenye rutuba iliyo nyanyuka (1) inayo faidika kwa maji mengi au kidogo. Ikija mvua kubwa huzaa mazao yake mardufu; na ikitopata mvua kubwa basi hata manyunyu kidogo hutosha kwa vile ardhi ni nzuri yenye kutoa mazao katika hali zote mbili. Basi Waumini wenye nyoyo safi hazipotei a'mali zao. Na vitendo vyenu havifichiki kwa Mwenyezi Mungu. (1) Neno la Qur'ani "ardhi iliyo nyanyuka" linaashiria yaliyo vumbuliwa na ilimu za sayansi za kisasa, kuwa maji ya chini yanakuwa yako mbali na mizizi. Kwa hivyo mizizi haiozi na vijizizi vidogo vinapata kunyonya chakula kwa wasaa na pia kuvuta pumzi. Kwa hivyo mazao yanakuwa mema, kwa mvua ijayo au hata manyunyu. (Nasi twajua mikarafuu au minazi ya bondeni haina maisha wala haistawi.)
Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia naye hali ana watoto wanyonge, kikapigwa na kimbunga chenye moto, kikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Ishara ili mpate kufikiri.
Hapana yeyote katika nyinyi anaye penda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu na mito inapita kati yake na kimezaa kila namna ya matunda ayatakayo, naye hali amekwisha kuwa mkongwe na akawa na watoto wadogo wanyonge hawawezi kazi wala yeye hajiwezi kwa ukongwe wake, kikaja kitalu chake kikakauka kwa upepo mkali wenye moto, na miti ikaungua, wakati ambao yeye mwenyewe na watoto ndio wamo katika shida ya kuhitaji. Basi hali kadhaalika shani ya mwenye kutoa sadaka na akafuatishia masimbulizi na maudhi na riya, kujionyesha kwa watu, ambayo hayo yakapoteza thawabu zote za sadaka zake, na wala hawezi tena kutoa sadaka kwa kujitengezea nafsi yake. Kwa bayana kama hizi ndio Mwenyezi Mungu anakuonyesheni Ishara ili mpate kutafakari na kujifunza. Ilimu ya kisasa inaeleza kuwa katika anga pepo kali hugongana zikatoka radi na umeme na mvua. Huenda ukatokea moto kwa umeme kwa kugongana mawingu, au pengine huweza kutokea vimondo kutokana na volkano (burkani) iliyo karibu ikateketeza miti na chochote kilicho katika sehemu hizo. Qur'ani inaashiria maana zote hizo.
Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.
Enyi Waumini! Toeni bora ya mnacho kipata kwa juhudi yenu, na ambacho mlicho wezesha kukitoa katika ardhi, ikiwa kwa makulima, au maadini au chenginecho. Wala msikusudie kutoa kile kilicho duni na kibaya katika mali, na ilhali nyinyi msinge kubali kuchukua hivyo ila ingeli kuwa mmegubikwa macho au hamuuoni huo ubaya. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu si mwenye haja ya sadaka zenu, na Yeye ni mwenye kustahiki kila sifa njema na shukrani kwa alivyo kuongozeni kuendea kheri na wema.
Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na anakuamrisheni mambo machafu. Na Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na fadhila zitokazo kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
Shetani anakutieni khofu kuwa mtafakirika kwa kutoa, na kazi yake kutia ila kila kitendo chema, ili msitoe kwa ajili ya mambo ya kheri na mghurike na maasi. Na Mwenyezi Mungu aliye Mkunjufu wa kusamehe, ni Muweza wa kukutoshelezeni. Hapana lolote katika mambo yenu linalo fichikana kwake.
Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa hikima bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.
Yeye humpa sifa ya Hikima, kusema na kutenda lilio la haki, ampendaye kati ya waja wake. Na mwenye kupewa hayo basi kapewa kheri nyingi, kwani kwayo ndio hutengenea mambo ya duniani na Akhera. Na wala hawanafiiki kwa waadhi na mazingatio ya amali za Qur'ani ila wale wenye akili sawa inayo tambua ukweli bila ya kupindukia mipaka kwa pumbao la ufisadi.
Na chochote mnacho toa au nadhiri mnazo weka basi hakika Mwenyezi Mungu anajua. Na walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
Na kila mnacho kitoa, ikiwa kwa kheri au shari, au mnacho lazimika kutoa kwa ut'iifu, basi Mwenyezi Mungu anakijua na atakulipeni. Na wale wenye kudhulumu, wanao toa kwa ajili ya kujionyesha kwa watu au wale wanapo toa wanawaudhi masikini za Mungu, au wanao toa kwa ajili ya maasi, hawatakuwa na watu wa kuwanusuru na adhabu ya Mwenyezi Mungu huko Akhera.
Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha mkawapa mafakiri kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi ya maovu yenu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Na ikiwa mtazidhihirisha sadaka zenu, bila ya makusudio ya kutaka kujionyesha kwa watu, ni vizuri kwenu, inapendeza, na kwa Mola wenu Mlezi inasifika. Na pindi mkiwapa mafakiri kwa siri ili msiwatie haya, na kwa kuogopa riya (kujionyesha), basi nayo ni kheri kwenu. Na Mwenyezi Mungu atakusameheni dhambi zenu kwa sababu ya usafi wa niya zenu katika kutoa sadaka zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha na mnayo yadhihirisha, na anazijua niya zenu mnapo dhihirisha na mnapo ficha.
Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na kheri yoyote mnayo toa ni kwa nafsi zenu. Wala msitoe ila kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote mtakayo toa mtalipwa kwa ukamilifu, wala hamtadhulumiwa.
Si juu yako wewe, ewe Muhammad, kuwaongoa hao walio potea au kuwalazimisha watende kheri. Lilio juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na msaada wowote mnao toa kumpa mtu, faida yake inarejea kwenu wenyewe. Mwenyezi Mungu atakulipeni kwayo. Haya ni hivyo ikiwa mnapo toa hamkusudii ila kumridhi Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote mnayo itoa kwa njia hii itarejea kwenu, na mtazipata thawabu zake kwa ukamilifu bila ya kudhulumiwa chochote.
Nawapewe mafakiri walio zuilika katika njia za Mwenyezi Mungu, wasio weza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiye wajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao; hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayo toa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.
Na kutoa huko ni kwa kuwapa mafakiri ambao kwa sababu ya kuwania jihadi hawawezi kujichumia wenyewe, au ambao kwa sababu ya kuumia katika jihadi wameemewa na kuweza kuhangaika katika nchi kutafuta riziki. Na juu ya hivyo wanajizuia na kuomba omba. Asiye wajua huwadhania kuwa ni matajiri, lakini wewe utajua hali yao kwa alama zake. Na kila mtacho kitoa kwa wema, basi Mwenyezi Mungu anakijua, naye atakulipeni malipo ya kutosha.
Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
Wale ambao dasturi yao ni kutoa kwa ukarimu wa nafsi zao usiku na mchana, mbele za watu na katika siri, watapata malipo yao kutokana na Mola wao Mlezi. Hawatofikiwa na khofu yoyote baadae, wala hawatakuwa na huzuni kwa kukosa chochote.
Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu.
Wale kazi yao ni kula riba hawawi katika juhudi yao na mambo yao yote ila ni kuhangaika tu na kushughulika ovyo, kama aliye haribiwa akili yake na Shetani, akawa anateseka na wazimu ulio msibu. Kwani wao hudai kuwa biashara ni kama riba, kwa kuwa zote mbili hizi ni kutoa na kuchuma. Basi yapasa, kwa madai yao, njia zote hizo ziwe ni halali. Mwenyezi Mungu amewarudi hayo madai yao, kwa kubainishia kuwa kuhalalisha na kuharimisha si katika madaraka yao, na huko kufananisha kwao si kweli kabisa. Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara, na ameharimisha riba. Basi mwenye kufikiliwa na amri ya Mola wake Mlezi ya kuharimishwa riba na akaifuata, basi imthibitikie ile riba aliyo ichukua kabla ya kuja amri ya kuharimishwa. Na hukumu yake iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu akitaka kumsamehe. Lakini wenye kurejea kula riba wakaifanya ni halali, baada ya kwisha harimishwa, hao watalazimika kudumu Motoni. Riba iliyo tajwa katika Aya hii ni riba ya kijahiliya, nayo ni ziada juu ya deni kwa sababu ya kuakhirisha kulipa. Hii ni haramu, ikiwa kidogo au nyingi. Amesema Imam Ahmad: Haimfalii Muislamu kukanya haya. Kinyume cha hayo ni faida ya biashara, na hii inathibitishwa na hadithi ya Mtume s.a.w.: Ngano kwa ngano, kama ile ile, mkono kwa mkono. Shairi kwa shairi, kama ile ile, mkono kwa mkono. Dhahabu kwa dhahabu, kama ile ile, mkono kwa mkono. Fedha kwa fedha, kama ile ile, mkono kwa mkono. Na tende kwa tende, kama ile ile, mkono kwa mkono. Mwenye kuzidisha au kutaka kuzidisha basi amekula riba. Wanazuoni wamewafikiana kuwa ni haramu kuzidisha katika kubadilishana kitu cha jinsi moja, na wameruhusu kuzidisha ikiwa vitu vya jinsi mbali mbali. Lakini wameharimisha kuakhirisha katika vitu vya namna hii. Na wamekhitalifiana katika kukisia vitu vingine khitilafu kubwa. Katika rai iliyo karibu mno ni kukisia kama haya kila kinacho liwa kinacho weza kuwekwa kisiharibike. Ama riba ya kijahiliya hapana khitilafu yoyote -- mwenye kukanya basi ni kaafiri. Riba ya kijahiliya humtia dhiki na kiwewe mwenye kula na mwenye kuliwa, kwa wasiwasi na kumshughulisha akili kwa mali aliyo kopesha au aliyo kopa. Mwenye kukopa ana dhiki na kushughulika akili yake hata hawezi kushughulikia kazi yake, na mwenye kukopesha anakuwa na hamu na khofu kuwa hatolipwa. Na baadhi ya madaktari wanaona kuzidi kwa maradhi ya "presha" na moyo ni kwa sababu ya kuzidi riba. Na kuharimishwa riba na Qur'ani kunawafikiana na mafailasufi wa zamani, kama Aristotle alivyo sema kuwa uchumi wa riba si uchumi wa tabia, kwani pesa hazizai pesa. Wataalamu wa uchumi wamethibitisha kwamba njia za uchumi ni nne: Tatu katika hizo ni zenye kuzaa matunda, ama ya nne haizai kitu. Zenye kuzaa ni kibarua, tena inafuatia ufundi na ukulima na kujasirisha katika biashara, kwani katika hiyo ni kuhamisha bidhaa kutoka pahala zilipo undwa kuzipeleka pa kuzitumia, na hiyo kwa hakika imekuwa ni kuzalisha matunda. Ama njia ya nne ndiyo hiyo faida ya riba. Katika kukopesha hajitii mtu khasarani bali ni faida tu, na hapana kuzalisha matunda ila kwa kazi ya yule aliye kopeshwa. Faida yake ni kwa kiasi ya mkopo. Ikiwa sababu yenyewe ni mkopo mwenye kukopesha haingii khatarini kwa kuwa anayo dhamana.
Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukanya na afanyae dhambi.
Mwenyezi Mungu huondoa ile ziada iliyo twaliwa kuwa ni riba juu ya mali yaliyo kopeshwa, na huitilia baraka mali iliyo tolewa sadaka, na huilipia thawabu mara nyingi kuliko kile kilicho tolewa. Na Mwenyezi Mungu hawapendi watu wanao endelea kuhalalisha haramu kama riba, wala wale wanao endelea kuchukua riba.
Hakika wale walio amini na wakatenda mema na wakashika Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
Hakika wale wanao muamini Mwenyezi Mungu, na wakazitimiza amri zake, na wakatenda mema aliyo waamrisha, na wakaacha yaliyo katazwa ya haramu, na wakatimiza Swala kwa njia ya ukamilifu, na wakatoa Zaka kuwapa wanao stahiki, watapata thawabu kubwa mno walio wekewa kwa Mola wao. Na wala hawatakuwa na khofu ya chochote kwa siku zijazo, wala hawatahuzunika kwa lolote walilo likosa.
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini.
Enyi mlio amini! Mwogopeni Mwenyezi Mungu, na wacheni heba yake na khofu yake ijae katika nyoyo zenu, na wacheni kudai hiyo riba iliyo bakia juu ya shingo za watu ikiwa ni kweli nyinyi ni Waumini.
Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe.
Ikiwa hamfanyi aliyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu kuacha riba basi kuweni na yakini kuwa nyinyi mko vitani na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa sababu ya inadi yenu kuipinga amri ya Mwenyezi Mungu. Ikiwa mnataka toba ya kukubaliwa basi haki yenu ni kuchukua ile rasilmali yenu tu. Msichukue kitu zaidi, kidogo au kingi, bila ya kujali sababu ya hilo deni na vipi lilivyo tumiwa. Kwani hiyo ziada mnayo ichukua ni kumdhulumu mtu, kama vile kuacha sehemu ya rasilmali yenu ni dhulma juu yenu.
Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua.
Ikiwa mwenye kukopeshwa ana shida na uzito basi mpeni muhula wa kulipa deni lake mpaka wakati wa kufarijika. Na mkitoa sadaka kwa kusamehe deni au baadhi yake ni kheri yenu kama nyinyi ni watu wenye ujuzi na fahamu kuelewa maneno ya Mwenyezi Mungu anaye kufundisheni murwa na utu.
Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Enyi mlio amini! Mkikopeshana deni kwa muda, inatakikana huo muda ujuulikane. Nanyi muandikiane ili kuhifadhi haki na usitokee mzozo. Na lazima mwenye kuandika awe mtu muadilifu katika uandishi wake. Wala muandishi asikatae kuandika, kwani hivyo ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya ilimu aliyo mfunza naye alikuwa haijui. Basi aandike lile deni kwa mujibu anavyo kubali yule mwenye kukopa. Naye huyo mwenye kukopa amwogope Mola wake Mlezi, asipunguze hata chembe katika deni lilio juu yake. Pindi akiwa mwenye kukopa hawezi kujiendesha, wala hayawezi mambo vilivyo, au ni mnyonge kwa udogo au ugonjwa au ukongwe, au akawa hawezi kuandikisha kwa ajili ya ububu au uzito wa ulimi au kutojua lugha inayo andikiwa huo waraka, basi mlinzi wake wa kisharia au hakimu au aliye mkhiari yeye, awe ndiye naibu wake wa kutoa imla ya kuliandika hilo deni kwa uadilifu ulio timia. Na washuhudisheni deni hilo wanaume wawili miongoni mwenu. Ikiwa hawakupatikana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili, washuhudie ili pindi mtu akirusha waweze kutoa ushahidi wao, na akisahau mmoja mwengine aweze kumkumbusha. Wala haijuzu kujizuia kutoa ushahidi pindi unapo takikana. Wala msipuuze kuandika kidogo na kikubwa maadamu ni deni la kulipwa baadae. Hivyo ndio uadilifu wa sharia ya Mwenyezi Mungu, na ndio kuwa na nguvu zaidi kuwa ni dalili ya ukweli wa ushahidi, na ndio vyema zaidi kuondoa shaka shaka baina yenu. Ila ikiwa jambo lenyewe ni biashara ya mkono-kwa-mkono mnayo uzuiana baina yenu, hapo si lazima kuandikiana, kwani hapana dharura ya hayo. Na inatakikana lakini katika kuuziana pawepo mashahidi ili kuepusha ugomvi. Na tahadharini asipate madhara yoyote mwenye kuandika au mwenye kushuhudia. Hayo itakuwa ni kutokana na ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Na mkhofuni Mwenyezi Mungu, na ogopeni heba yake katika anayo amrisha na anayo yakataza. Hivyo ndio nyoyo zenu zitalazimika kufuata insafu na uadilifu. Na Mwenyezi Mungu anakubainishieni haki zenu na waajibu ulio juu yenu. Naye ni Mjuzi wa kila kitu - vitendo vyenu na vinginevyo. Aya hii inahakikisha misingi ya kuthibitisha. Inahakikisha msingi wa kuandikiana. Hukumu haiwi kwa chini kuliko mashahidi wawili walio wanaume waadilifu, au mwanamume mmoja na wanawake wawili. Na imelazimika mwandishi awe muadilifu, na wawepo mashahidi panapo kuwapo mafungamano. Lakini hapana lazima ya mashahidi ikiwa mua'mala wenyewe wa papo kwa papo, nipe nikupe, mkono kwa mkono. Pia aya inahakikisha kuwa mtu aliye pumbaa, au hawezi kujiendeshea mambo yake mtu mwenyewe, au mnyonge dhaifu, basi lazima awe na mtu kuwa ni wakili wake wa kumtendea badala yake. Na pindi ikiwa ni safarini na hapana mtu wa kuandika, basi yatosha kutoa kitu kiwe rahani akamate mwenye kukopesha
Na mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, yatosha kukabidhiwa rahani. Na mmoja wenu akimwekea amana mwenziwe basi aliye aminiwa airudishe amana ya mwenzake, na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala msifiche ushahidi. Na atakaye ficha basi hakika moyo wake ni wenye kutenda dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayo yatenda.
Ikiwa mko safarini na hamkupata mtu wa kuliandika deni, basi kwa dhamana ya deni wekeni kitu kuwa ni rahani ashike mwenye kukopesha kutokana na mwenye kukopa. Na mtu akipewa dhamana na mwenzie kushika, basi iwe hiyo ni amana ilioko mikononi mwake. Yeye ametegemewa kwa uaminifu wake. Basi inapo takikana amana na aitoe amana ya watu. Na amche Mwenyezi Mungu aliye muumba na kumlea na kumshughulikia kwa uangalifu ili isimkatikie neema ya Mola wake Mlezi duniani na Akhera. Wala msifiche ushahidi unapo takikana. Mwenye kuficha amepata dhambi, na khabithi wa moyo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mnayo yafanya. Atakulipeni kwa mujibu mnavyo stahiki.
Viliomo mbinguni na viliomo duniani ni vya Mwenyezi Mungu. Na mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi Mungu atakuhisabuni kwayo. Kisha amsamehe amtakaye na amuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Jueni kuwa vyote viliomo mbinguni na duniani ni vya Mwenyezi Mungu, naye ana makdara navyo vyote na anavijua vyote. Ni sawa sawa ikiwa mtadhihirisha yaliyomo ndani ya nafsi zenu au mkificha, Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa vyote na mwenye kupata khabari za vyote. Naye Siku ya Kiyama atakuhisabuni kwa hayo, na atamghufiria amtakaye na atamuadhibu amtakaye. Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet'ii. Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.
Hakika aliyo teremshiwa Mtume Muhammad s.a.w. ni Haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Naye amemuamini Mwenyezi Mungu, na pamoja naye wameamini pia Waumini, wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake. Wao wanawaamini Mitume wote wa Mwenyezi Mungu sawa sawa, na wanawatukuza sawa, huku wakisema: Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake. Na wametilia mkazo Imani yao ya moyoni kwa kauli yao ya ulimini huku wakimuelekea Mwenyezi Mungu kumwambia: Mola Mlezi wetu! Tumesikia uliyo yateremsha yenye hikima, na tumeyapokea yaliyo amrishwa. Ewe Mola wetu Mlezi! Tupe maghfira yako. Na kwako Wewe tu pekee ndio tunako kwendea na ndio marejeo.
Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma ni juu yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri.
Hakika Mwenyezi Mungu hawakalifishi waja wake ila kwa kadiri wanavyo weza kuyafanya na kuyafuata. Kwa hivyo kila mwenye kukalifishwa atalipwa kwa vitendo vyake - akitenda kheri atapata malipo ya kheri, akitenda shari atapata shari. Basi enyi Waumini! Nyenyekeeni kwa Mwenyezi Mungu mkimuomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Usituadhibu pindi tukiporonyoka tukasahau ulio tuamrisha, au yakatupata ya kutusabibisha kutumbukia makosani. Mola Mlezi wetu! Usituchukulie kwa shida ukatupa sharia nzito nzito kama ulivyo wafanyia Mayahudi kwa sababu ya inda yao na udhalimu wao. Wala usitukalifishe mambo tusiyo yaweza, na utusamehe kwa ukarimu wako, na tughufirie kwa fadhila yako, na uturehemu kwa rehema yako yenye wasaa. Hakika Wewe ni Mola Mlezi wetu. Tunusuru ewe Mola Mlezi, kwa ajili ya kutukuza Neno lako na kuitangaza Dini yako - tuwashinde kaumu ya wapingaji.
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
የፍለጋ ዉጤቶች:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".