Vinamtakasa Allah Mtukufu Aliyetukuka vyote vilivyo mbinguni na vyote vilivyo Ardhini, na Yeye Peke Yake Ndiye mfalme wa kila kitu, Aliye Mshindi kwenye utawala Wake bila ya mpinzani, Mwingi wa hekima katika kuyapelekesha mambo Yake na utengenezaji Wake.
Allah Mtukufu, kutakasika na kila upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyetuma kwa Waarabu, wasiojua kusoma wala kuwa na kitabu wala kumbukumbu zozote za utume, Mtume aliyetokana na wao aliyetumwa kwa watu wote, awasomee Qur’ani, na awatakase na itikadi mbovu na tabia mbaya, na awafundishe Qur’ani na Sunnah. Na wao, kwa kweli, tangu alipokuwa hajatumwa mtume kwao, walikuwa kwenye ukengeukaji ulio wa wazi, kwa kuwa kando na haki. Na Allah Mtukufu, ametakasika na kila upungufu.
Amemtuma huyu mtume kwa watu wengine pia watakaokuja miongoni mwa Waarabu na wengineo. Na Allah Mtukufu Aliyetukuka, Peke Yake, Ndiye Mshindi mwenye kushinda juu ya kila kitu, Mwingi wa hekima katika maneno Yake na matendo Yake.
kutumwa huko kwa Mtume, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie), kwa ummah wa Kiarabu na wasiokuwa wao, ni wema kutoka kwa Allah Mtukufu, humpa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na Yeye, Peke Yake, Ndiye Mwenye wema na upaji mwingi.
Mfano wa Mayahudi ambao walitakiwa kuifuata Taurati kivitendo kisha wakakosa kuifuata ni kama mfano wa punda ambaye yuwabeba vitabu na hajui yaliyo ndani yake. Ni mfano muovu mno wa watu ambao wamezikataa aya za Allah Mtukufu na wasifaidike nazo. Na Allah Mtukufu Hawaelekezi kwenye wema watu madhalimu ambao wanaikiuka mipaka Yake na wanaotoka nje ya utiifu Kwake.
Sema, (ewe Mtume), uwaambie wale ambao wameshikamana na desturi za kiyahudi zilizopotoka, «Mkidai kiurongo kwamba nyinyi ndio vipenzi vya Allah Mtukufu na si watu wengine, basi tamanini kufa iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu kuwa Allah Mtukufu Anawapenda nyinyi».
Na wala hawa Mayahudi hawatatamani kifo kabisa kwa vile wanavyoyapenda maisha ya duniani kuliko Akhera, na kwa kuogopa kuteswa na Allah Mtukufu, kwa sababu ya yale waliyoyatanguliza ya ukafiri na matendo maovu. Na Allah Mtukufu Anawajua mno madhalimu, hakifichiki Kwake chochote cha udhalimu wao.
Sema, «Kwa kweli mauti mnayoyakimbia hayakimbiliki, kwani ni yenye kuwajia wakati wenu wa kufa utakapofika, kisha Siku ya kufufuliwa mtarudishwa kwa Allah Mtukufu, mjuzi wa yale yaliyofichika na yanayoonekana, na hapo Atawapasha habari ya matendo yenu na Atawalipa nyinyi kwa hayo».