ترجمة معاني القرآن الكريم - الترجمة السواحلية - علي محسن البرواني * - فهرس التراجم

XML CSV Excel API
تنزيل الملفات يتضمن الموافقة على هذه الشروط والسياسات

ترجمة معاني سورة: الحجر   آية:

سورة الحجر - Surat Al-hijr

الٓرۚ تِلۡكَ ءَايَٰتُ ٱلۡكِتَٰبِ وَقُرۡءَانٖ مُّبِينٖ
Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur'ani inayo bainisha.
Hizi ni Aya za Kitabu cha kusomwa, chenye kubainisha, chenye kuweke wazi.
التفاسير العربية:
رُّبَمَا يَوَدُّ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ لَوۡ كَانُواْ مُسۡلِمِينَ
HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu.
Watapenda, na watatamani sana makafiri wanao zikanya Aya za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, watapo ona adhabu ya Siku ya Kiyama, lau kuwa walisilimu walipo kuwapo duniani, na wakafuata kwa ikhlasi Dini ya Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
ذَرۡهُمۡ يَأۡكُلُواْ وَيَتَمَتَّعُواْ وَيُلۡهِهِمُ ٱلۡأَمَلُۖ فَسَوۡفَ يَعۡلَمُونَ
Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua.
Lakini sasa wamo katika kughafilika, hawazingatii adhabu itakayo wapata Akhera! Basi ukisha wafikishia ujumbe wako, na ukawaonya, waachilie mbali. Wao hawana hamu ila kula, na kustarehe kwa ladha za dunia. Tamaa ya uwongo inawazuga. Na hakika bila ya shaka yoyote watakuja jua yatakayo wapata pale watapo yaona kwa macho yao Siku ya Kiyama.
التفاسير العربية:
وَمَآ أَهۡلَكۡنَا مِن قَرۡيَةٍ إِلَّا وَلَهَا كِتَابٞ مَّعۡلُومٞ
Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu.
Na ikiwa wao wanataka wateremshiwe adhabu ya duniani, kama Mwenyezi Mungu alivyo wateketeza walio kuwa kabla yao, basi wajue kuwa Mwenyezi Mungu hauteketezi mji wowote ila kwa wakati wake maalumu.
التفاسير العربية:
مَّا تَسۡبِقُ مِنۡ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسۡتَـٔۡخِرُونَ
Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa.
Hawatangulii wala hawataakhari.
التفاسير العربية:
وَقَالُواْ يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِي نُزِّلَ عَلَيۡهِ ٱلذِّكۡرُ إِنَّكَ لَمَجۡنُونٞ
Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu.
Na uovu wa hali yao na wingi wa kughafilika kwao hata imefika hadi kumuita Nabii wao kwa kejeli wakisema: Ewe uliye teremshiwa Kitabu cha kukumbusha! Hapana shaka kuwa wewe una wazimu moja kwa moja! Huko kumuita kuwa ndiye aliye teremshiwa Ukumbusho, yaani Mawaidha, hakukuwa ila ni kwa kejeli tu, kumfanyia maskhara.
التفاسير العربية:
لَّوۡمَا تَأۡتِينَا بِٱلۡمَلَٰٓئِكَةِ إِن كُنتَ مِنَ ٱلصَّٰدِقِينَ
Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?
Na hadi ya ukafiri wao walizidisha juu ya matusi hayo na kejeli kwa kusema: Laiti badala ya hicho Kitabu kilicho teremshwa ungeli tuletea Malaika wakawa ndio hoja yenyewe, kama wewe ni msema kweli miongoni mwa wenye kusema kweli!
التفاسير العربية:
مَا نُنَزِّلُ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةَ إِلَّا بِٱلۡحَقِّ وَمَا كَانُوٓاْ إِذٗا مُّنظَرِينَ
Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula.
Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka neno lake aliwajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika ila huwa pamoja nao Haki ya nguvu yenye kuthibiti ambayo haina njia ya kuikataa. Basi wakiikanya huwa tena hawapewi muhula wowote, bali huteremshiwa adhabu ya hapa hapa duniani hapo hapo!
التفاسير العربية:
إِنَّا نَحۡنُ نَزَّلۡنَا ٱلذِّكۡرَ وَإِنَّا لَهُۥ لَحَٰفِظُونَ
Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.
Na hakika, kwa ajili ya kuwa Wito wa Nabii huyu kwendea Haki udumu mpaka Siku ya Kiyama, hatuwateremshi Malaika, bali tumewateremshia hii Qur'ani ambayo kukumbusha kwake kunaendelea daima dawamu. Na Sisi ndio wenye kuilinda isiingiliwe na mageuzo na mabadiliko yoyote mpaka kusimama Kiyama.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ أَرۡسَلۡنَا مِن قَبۡلِكَ فِي شِيَعِ ٱلۡأَوَّلِينَ
Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo.
Na ewe Mtume Muaminifu! Usihuzunike; kwani Sisi tuliwatuma Mitume kabla yako kwa mataifa ambao wameshikilia upotovu kama hao walivyo shikilia. Na wao wamepita pamoja na wa kale walio teketezwa kwa ukafiri wao!
التفاسير العربية:
وَمَا يَأۡتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُواْ بِهِۦ يَسۡتَهۡزِءُونَ
Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli.
Wala mtindo wao hao walio watangulia kwa kushikilia upotovu haukuwa ila kuwafanyia maskhara Mitume wao, Mtume baada ya Mtume, kama wanavyo kufanyia kejeli wewe! Huo ndio mtindo wa wapotovu!
التفاسير العربية:
كَذَٰلِكَ نَسۡلُكُهُۥ فِي قُلُوبِ ٱلۡمُجۡرِمِينَ
Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu.
Kama tulivyo itia Qur'ani katika nyoyo za Waumini ikaingiza mwangaza, basi kadhaalika tumeingiza upotovu katika nyoyo za walio pigwa muhuri wa ukosefu; hali ya katika nyoyo zao ikawa kinyume cha hayo. Upotovu ukatia mizizi katika roho zao.
التفاسير العربية:
لَا يُؤۡمِنُونَ بِهِۦ وَقَدۡ خَلَتۡ سُنَّةُ ٱلۡأَوَّلِينَ
Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale.
Wakhalifu hao hawaamini. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa muhula mpaka waione adhabu chungu ya Siku ya Kiyama ndio kama ulivyo kwisha tangulia.
التفاسير العربية:
وَلَوۡ فَتَحۡنَا عَلَيۡهِم بَابٗا مِّنَ ٱلسَّمَآءِ فَظَلُّواْ فِيهِ يَعۡرُجُونَ
Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda,
Watu hao wanataka wateremshiwe Malaika. Ewe Nabii! Usidhani kuwa ndio wataamini wakiteremshiwa. Bali hata tungeli wafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda huko wakaona maajabu yaliyoko, na wakawaona Malaika,
التفاسير العربية:
لَقَالُوٓاْ إِنَّمَا سُكِّرَتۡ أَبۡصَٰرُنَا بَلۡ نَحۡنُ قَوۡمٞ مَّسۡحُورُونَ
Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa.
Bado wasingeli amini, na wangesema: Macho yetu yamefumbwa tusione, na yamefunikwa. Bali hayo si lolote ila ni uchawi tu, tumerogwa! Basi hapana faida ya ishara yoyote maadamu nyoyo zao zimeenea ukafiri.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ جَعَلۡنَا فِي ٱلسَّمَآءِ بُرُوجٗا وَزَيَّنَّٰهَا لِلنَّٰظِرِينَ
Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
Na Sisi tumeweka mbinguni sayari na nyota, kwa makundi yenye hisabu zake na yenye kukhitalifiana umbo lake na sura yake. Na kadhaalika tukazipamba kwa wenye kuziangalia kwa kutuza na kuzingatia, na kuchunguza kwazo dalili za uwezo wa Muumbaji wao.
التفاسير العربية:
وَحَفِظۡنَٰهَا مِن كُلِّ شَيۡطَٰنٖ رَّجِيمٍ
Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye.
Lakini Sisi tumezihifadhi na kila shetani anaye stahiki kupigwa vimondo na kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
التفاسير العربية:
إِلَّا مَنِ ٱسۡتَرَقَ ٱلسَّمۡعَ فَأَتۡبَعَهُۥ شِهَابٞ مُّبِينٞ
Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana.
Na yeyote katika hao mashetani wanao jaribu kuibia kusikiliza maneno yanayo jiri baina ya wakaazi wa hizi nyote, basi Sisi tunampopoa kwa vijinga vya moto vya mbinguni vinavyo onekana wazi.
التفاسير العربية:
وَٱلۡأَرۡضَ مَدَدۡنَٰهَا وَأَلۡقَيۡنَا فِيهَا رَوَٰسِيَ وَأَنۢبَتۡنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَيۡءٖ مَّوۡزُونٖ
Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake.
Na tumekuumbieni ardhi, na tumekutengenezeeni mpaka ikawa kama busati lilio tandikwa, na tukaweka ndani yake milima iliyo simama imara. Na tumekuotesheeni ndani namna mbali mbali za mimea ya kukufaeni kwa uhai wenu, na tumeifanya kwa vipimo na zama maalumu katika kukua kwake, na faida yake kwa kula, na kwa kadiri ya haja zenu na kwa vipimo vyake, na sura yake kwa umbo na tabia. Aya hii inaeleza uhakika wa uumbaji ambao haukujuulikana ila katika zama za hivi karibuni. Nayo ni kuwa kila kabila ya mimea imefanana kati yao kwa kuonekana na undani wake, hata katika sehemu zake ndogo ndogo, katika viungo vyake vyote vya hiyo mimea. Na hali kadhaalika katika "Khalaya" au "Cells" za hiyo mimea ya kabila fulani, kwa ajili ya kutimiza kazi iliyo kusudiwa kiungo hicho cha mmea. Na pia sehemu za mimea ya hizo kabila zao na vilivyo undwa katika viungo vyake utaona mnasaba wake umethibiti kila mwaka, ukilinganisha kwa wakati ule ule katika miaka mingine
التفاسير العربية:
وَجَعَلۡنَا لَكُمۡ فِيهَا مَعَٰيِشَ وَمَن لَّسۡتُمۡ لَهُۥ بِرَٰزِقِينَ
Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.
Na tumekujaalieni katika ardhi sababu za maisha mema. Kwani ndani yake yamo mawe ya kujengea majumba, na wanyama mnao nafiika kwa nyama yao, au ngozi zao, au manyoa yao. Na yapo maadeni yanayo toka chini ya ardhi, na mengineyo. Kama ilivyo kuwa humo zipo sababu za kukuleteeni nyinyi maisha mema, basi humo pia wanapata maisha wenginewe ambao wapo chini ya mamlaka yenu, kama watoto na wafwasi, ambao Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye waruzuku wao na nyinyi.
التفاسير العربية:
وَإِن مِّن شَيۡءٍ إِلَّا عِندَنَا خَزَآئِنُهُۥ وَمَا نُنَزِّلُهُۥٓ إِلَّا بِقَدَرٖ مَّعۡلُومٖ
Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu.
Na hapana chochote cha kheri ila kiko kwetu kama mahodhi yaliyo jaa, nasi tunakiweka tayari na tunakitoa kwa wakati wake. Na hatuwateremshii waja wetu ila kwa kiasi maalumu, kwa mujibu tunavyo pima kwa hikima yetu ya maumbile.
التفاسير العربية:
وَأَرۡسَلۡنَا ٱلرِّيَٰحَ لَوَٰقِحَ فَأَنزَلۡنَا مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءٗ فَأَسۡقَيۡنَٰكُمُوهُ وَمَآ أَنتُمۡ لَهُۥ بِخَٰزِنِينَ
Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka.
Na Sisi tulipeleka pepo zilizo beba mvua na zilizo beba mbegu za mimea, na tukateremsha maji ya kukunywesheni. Na hayo ni kwa kufuata vile tutakavyo. Na yeyote yule hawezi kuyatenda kama hayo ila awe nayo kwake kama mahodhi au mabirika. Aya hii imeitangulia sayansi kwa kusema kuwa upepo unafanya kazi kubwa katika kubeba pollen, chembe dume za kupandishia mimea, kupelekea sehemu za uke za mimea mingine, na kwa hivyo yakazalikana mazao. Na pia haikujuulikana ila mwanzo wa karne hii tuliyo nayo kwamba upepo unazalisha mawingu yanayo nyesha mvua. Kwani "Nucleons" ambazo juu yake hujumuika sehemu za mvuke wa maji na zikawa chembe chembe za maji ndani ya wingu, ndizo chanzo cha mvua inayo chukuliwa na pepo kupelekwa kwenye majimbo yanayo fikiwa na mawingu. Misingi ya hizo "Nucleons" ni chumvi ya bahari, na vinavyo chukuliwa na upepo juu ya uso wa ardhi, na "Oxides" na vumbi vumbi, n.k. Na vyote hivyo ni lazima kwa ajili ya mvua. "Wala si nyinyi mnayo yaweka". Imethibiti kwa sayansi ya kisasa kuwa mvua inaanza kwa mvuke kutokana na uso wa ardhi na bahari, kisha inarejea hali ile ile tena kama ilivyo tajwa. Ikinya mvua hunywesha kila kilicho na uhai katika ardhi, na huinywesha ardhi yenyewe. Wala haiwezekani kuzuilika, kwa sababu ikichuruzika kutokana na vyote vyenye uhai na katika ardhi ikaingia baharini, tena kisha huanza kuzunguka mara ya pili kwa kupanda mvuke kutoka baharini. Basi hali ni hivyo mzunguko. Hapa ndio inabainika maana ya Aya "Wala si nyinyi mnayo yaweka."
التفاسير العربية:
وَإِنَّا لَنَحۡنُ نُحۡيِۦ وَنُمِيتُ وَنَحۡنُ ٱلۡوَٰرِثُونَ
Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi.
Na ni Sisi tu peke yetu ndio tunavipa vitu vyote uhai, kisha tunavipelekea mauti, kwani uumbaji wote ni wetu.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ عَلِمۡنَا ٱلۡمُسۡتَقۡدِمِينَ مِنكُمۡ وَلَقَدۡ عَلِمۡنَا ٱلۡمُسۡتَـٔۡخِرِينَ
Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua waliotaakhari.
Na kila mmoja wenu ana muda wake alio pimiwa. Sisi ndio tunao ujua. Tunawajua walio tangulia kwa kufa na kuwa hai, na pia wanao taakhari.
التفاسير العربية:
وَإِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَحۡشُرُهُمۡۚ إِنَّهُۥ حَكِيمٌ عَلِيمٞ
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi.
Na hakika walio tangulia na walio taakhari watakusanywa wakati mmoja. Na Mwenyezi Mungu atawahisabia na atawalipa. Na hayo ni kwa mujibu wa hikima yake na ujuzi wake. Na Yeye ndiye anaye itwa Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ خَلَقۡنَا ٱلۡإِنسَٰنَ مِن صَلۡصَٰلٖ مِّنۡ حَمَإٖ مَّسۡنُونٖ
Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.
Na Sisi katika kuumba kwetu walimwengu katika dunia hii, tumeumba namna mbili - Tumemuumba mtu kwa udongo mkavu wenye kutoa sauti ukigongwa.
التفاسير العربية:
وَٱلۡجَآنَّ خَلَقۡنَٰهُ مِن قَبۡلُ مِن نَّارِ ٱلسَّمُومِ
Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto.
Na makhaluku wengine ni majini, ambao tuliwaumba mbele, alipo umbwa asili yake Iblisi kutokana na moto mkali mno unao toka katika tundu za mwili wa mtu.
التفاسير العربية:
وَإِذۡ قَالَ رَبُّكَ لِلۡمَلَٰٓئِكَةِ إِنِّي خَٰلِقُۢ بَشَرٗا مِّن صَلۡصَٰلٖ مِّنۡ حَمَإٖ مَّسۡنُونٖ
Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.
Ewe Nabii! Kumbuka asli ya viumbe. Pale alipo sema Aliye kuumba, Mola Mlezi wa viumbe vyote, kuwaambia Malaika: Mimi nataka kumuanzisha mtu niliye muumba kutokana na udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umebadilika rangi, na una sura.
التفاسير العربية:
فَإِذَا سَوَّيۡتُهُۥ وَنَفَخۡتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُواْ لَهُۥ سَٰجِدِينَ
Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia.
Nikisha kamilisha kumuumba, na nikampulizia roho ambayo ninaimiliki, basi teremkeni kwa nyuso zenu mkimsujudia, kwa kumwamkia na kumhishimu.
التفاسير العربية:
فَسَجَدَ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ كُلُّهُمۡ أَجۡمَعُونَ
Basi Malaika wote pamoja walimsujudia,
Wakasujudu wote kwa kuit'ii amri ya Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
إِلَّآ إِبۡلِيسَ أَبَىٰٓ أَن يَكُونَ مَعَ ٱلسَّٰجِدِينَ
Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu.
Lakini Iblisi alijivuna na akakataa kuwa pamoja na Malaika waliyo it'ii amri ya Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
قَالَ يَٰٓإِبۡلِيسُ مَا لَكَ أَلَّا تَكُونَ مَعَ ٱلسَّٰجِدِينَ
(Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu?
Hapo basi Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: Ewe Iblisi! Kitu gani kilicho kupelekea hata ukaasi na usiwe pamoja na wanyenyekevu walio sujudu?
التفاسير العربية:
قَالَ لَمۡ أَكُن لِّأَسۡجُدَ لِبَشَرٍ خَلَقۡتَهُۥ مِن صَلۡصَٰلٖ مِّنۡ حَمَإٖ مَّسۡنُونٖ
Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unaotoa sauti, unao tokana na matope yenye sura.
Iblisi akasema: Si shani yangu mimi kumsujudia mtu uliye muumba kwa udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umegeuka rangi, wenye kutiwa sura.
التفاسير العربية:
قَالَ فَٱخۡرُجۡ مِنۡهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٞ
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!
Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Ukiwa wewe umekuwa a'asi, umetokana na ut'iifu wangu, basi tokelea mbali kwenye Bustani hii! Kwani hakika wewe umefukuzwa kwenye rehema yangu pahala pa hishima.
التفاسير العربية:
وَإِنَّ عَلَيۡكَ ٱللَّعۡنَةَ إِلَىٰ يَوۡمِ ٱلدِّينِ
Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.
Na Mimi nimekwisha kuhukumia ubaidike na rehema na utukufu mpaka Siku ya Kiyama, Siku ya Hisabu na Malipo. Na hapo ndipo utapo pata adhabu, wewe na wanao kufuata .
التفاسير العربية:
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرۡنِيٓ إِلَىٰ يَوۡمِ يُبۡعَثُونَ
Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapofufuliwa.
Iblisi akasema, hali naye kesha kuwa ni mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu: Ewe Muumba wangu! Nipe muhula, nibakishe usinitwae mpaka Siku ya Kiyama, Siku watapo fufuliwa watu wakawa hai baada ya kufa kwao.
التفاسير العربية:
قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ ٱلۡمُنظَرِينَ
(Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula
Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Wewe utabakishwa, umepewa muhula,
التفاسير العربية:
إِلَىٰ يَوۡمِ ٱلۡوَقۡتِ ٱلۡمَعۡلُومِ
Mpaka siku ya wakati maalumu.
Mpaka wakati niliyo ukadiria, ninao ujua Mimi. Na kama utavyo kuwa mrefu una kikomo.
التفاسير العربية:
قَالَ رَبِّ بِمَآ أَغۡوَيۡتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمۡ فِي ٱلۡأَرۡضِ وَلَأُغۡوِيَنَّهُمۡ أَجۡمَعِينَ
Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,
Akasema Iblisi, mkhalifu, a'asi: Ewe Muumba wangu unaye nibakisha! Umenitakia upotofu, nami nikatumbukia ndani yake. Basi kwa sababu hiyo nahakikisha kuwa nitawapambia wanaadamu maovu wayaone mazuri, na nitafanya kila juhudi kuwapotoa wote!
التفاسير العربية:
إِلَّا عِبَادَكَ مِنۡهُمُ ٱلۡمُخۡلَصِينَ
Ila waja wako walio safika.
Wala hawatoepukana na upotovu wangu ila wale waja wako walio kufanyia ikhlasi Wewe na nisio weza kuzimiliki nyoyo zao kwa zilivyo kuwa imara kwa kukumbuka Wewe.
التفاسير العربية:
قَالَ هَٰذَا صِرَٰطٌ عَلَيَّ مُسۡتَقِيمٌ
Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka.
Hakika usafi wa waja walio isafia niya Dini yao ndio Njia Iliyo Nyooka, na haki yangu nisiikiuke, kwani hao siwezi kuwapotoa. (Tafsiri hii yaonyesha maneno hayo ni ya Iblisi. Lakini Tafsiri nyengine zinasema maneno hayo ni ya Mwenyezi Mungu, kwa mfano ya Abdulla Saleh, Abdulla Yusuf, Pickthall, Razi, Baidhawi, Qurtubi, Zamakhshari, Ibn Kathir, Assad.)
التفاسير العربية:
إِنَّ عِبَادِي لَيۡسَ لَكَ عَلَيۡهِمۡ سُلۡطَٰنٌ إِلَّا مَنِ ٱتَّبَعَكَ مِنَ ٱلۡغَاوِينَ
Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Hakika waja wangu walio nisafia Mimi Dini yao wewe huna uwezo wa kuwapoteza. Lakini wapotovu, walio zama katika upotovu, walio kufuata wewe, basi hao ndio unayo madaraka juu ya nyoyo zao.
التفاسير العربية:
وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوۡعِدُهُمۡ أَجۡمَعِينَ
Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote.
Na hakika Moto mkali mno ndio wameahidiwa hao wote kuwa ndiyo adhabu ya kutia uchungu.
التفاسير العربية:
لَهَا سَبۡعَةُ أَبۡوَٰبٖ لِّكُلِّ بَابٖ مِّنۡهُمۡ جُزۡءٞ مَّقۡسُومٌ
Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa.
Wala huo Moto mkali hauna mlango mmoja tu, bali una milango saba kwa ajili ya wingi wanao stahiki kuingia humo. Na kila mlango una kundi lake makhsusi. Na kila kundi una cheo chake maalumu cha kulingana na uovu wake.
التفاسير العربية:
إِنَّ ٱلۡمُتَّقِينَ فِي جَنَّٰتٖ وَعُيُونٍ
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
Haya ni malipo ya wanao mfuata Shetani. Ama wale ambao Shetani kashindwa kuwapotoa, kwa kuwa wameweka kinga baina yake na nyoyo zao, hao watapata Mabustani yaliyo bora, na chemchem zinazo pita .
التفاسير العربية:
ٱدۡخُلُوهَا بِسَلَٰمٍ ءَامِنِينَ
(Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani.
Mola wao Mlezi atawaambia: Ingieni katika Bustani hizi kwa utulivu na amani. Kwani hapana khofu juu yenu, hamhuzunikii nyakati zenu.
التفاسير العربية:
وَنَزَعۡنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنۡ غِلٍّ إِخۡوَٰنًا عَلَىٰ سُرُرٖ مُّتَقَٰبِلِينَ
Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana.
Na hakika watu wa Imani wataishi katika kheri hii na nafsi zao zimetua. Kwani tumezitoa chuki zilizo kuwamo katika nafsi hizo. Wote hao watakuwa ndugu waketi juu ya viti vya enzi zikitazamana nyuso zao kwa furaha na mahaba, wala hawawi mmoja nyuma ya mwenzie wakichunguliana visogoni.
التفاسير العربية:
لَا يَمَسُّهُمۡ فِيهَا نَصَبٞ وَمَا هُم مِّنۡهَا بِمُخۡرَجِينَ
Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo.
Hawapatwi na machofu huko. Na hiyo ni neema ya daima, wala hawatotoka humo milele.
التفاسير العربية:
۞ نَبِّئۡ عِبَادِيٓ أَنِّيٓ أَنَا ٱلۡغَفُورُ ٱلرَّحِيمُ
Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Ewe Nabii muaminifu! Wape khabari waja wangu wote kwamba Mimi ni Mwingi wa kughufiria na kusamehe kwa mwenye kutubu, akaamini, na akatenda mema. Na kwamba Mimi ni Mwingi wa kuwarehemu.
التفاسير العربية:
وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ ٱلۡعَذَابُ ٱلۡأَلِيمُ
Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu!
Na wape khabari kwamba adhabu ninayo wateremshia wenye kuasi na kukufuru ni adhabu yenye kutia machungu kweli, na adhabu yoyote nyengineyo haihisabiwi kuwa ina machungu mbele ya hii.
التفاسير العربية:
وَنَبِّئۡهُمۡ عَن ضَيۡفِ إِبۡرَٰهِيمَ
Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim.
Ewe Nabii! Waambie pia, katika kubainisha rehema yangu makhsusi katika dunia na adhabu yangu kwa wenye kuasi humo, khabari ya Malaika walio mfikia Ibrahim kama wageni.
التفاسير العربية:
إِذۡ دَخَلُواْ عَلَيۡهِ فَقَالُواْ سَلَٰمٗا قَالَ إِنَّا مِنكُمۡ وَجِلُونَ
Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.
Ewe Muaminifu! Watajie pale walipo ingia kwake, naye akawaogopa. Wao wakamwambia: Amani kwako, na tulia! Yeye akasema: Sisi tunakuogopeni, kwani mmetujia kwa ghafla, sio wakati wa dasturi wa kufika wageni, na hatujui mna nini!
التفاسير العربية:
قَالُواْ لَا تَوۡجَلۡ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَٰمٍ عَلِيمٖ
Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi.
Wakasema: Usiogope, na tuwa moyo! Kwani tunakubashiria mwana, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu atampa siku zijazo za uhai wake ilimu kubwa. Inaonyesha hapa kuwa bishara hii si ya Ismail a.s. Kwani Ismail alikuwa kesha zaliwa, naye na mama yake Haajir walikuwa wapo Makka. Bishara hii ni ya Ibrahim na mkewe, basi kwa hivyo ni ya Is-haq mwana wa Ibrahim na Sara.
التفاسير العربية:
قَالَ أَبَشَّرۡتُمُونِي عَلَىٰٓ أَن مَّسَّنِيَ ٱلۡكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ
Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria?
Akasema: Vipi mnanibashiria mtoto na hali mimi nimekwisha patikana na udhaifu wa ukongwe. Kwa njia gani, basi, mnanibashiria jambo hili la ajabu?
التفاسير العربية:
قَالُواْ بَشَّرۡنَٰكَ بِٱلۡحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ ٱلۡقَٰنِطِينَ
Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa.
Wakasema: Sisi tunakubashiria jambo lilio thibiti, ambalo halina shaka kabisa. Basi usiwe katika wanao kata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
قَالَ وَمَن يَقۡنَطُ مِن رَّحۡمَةِ رَبِّهِۦٓ إِلَّا ٱلضَّآلُّونَ
Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea?
Ibrahim akasema: Mimi sikati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu ila walio potea wasio utambua utukufu wake na uwezo wake.
التفاسير العربية:
قَالَ فَمَا خَطۡبُكُمۡ أَيُّهَا ٱلۡمُرۡسَلُونَ
Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe?
Alivyo kuwa kaanza kuzoeana nao, alisema: Ikiwa mmenibashiria khabari hii nzuri, je mna jambo gani jenginelo mlilo nalo baada ya haya, enyi wajumbe mlio tumwa na Mwenyezi Mungu?
التفاسير العربية:
قَالُوٓاْ إِنَّآ أُرۡسِلۡنَآ إِلَىٰ قَوۡمٖ مُّجۡرِمِينَ
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!
Wakasema hakika sisi tumetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa watu walio fanya ukhalifu katika Haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya Nabii wao, na haki ya nafsi zao wenyewe. Ukhalifu ndio mtindo wao. Watu wenyewe ni kaumu ya Luut'i. Basi tutawateketeza.
التفاسير العربية:
إِلَّآ ءَالَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمۡ أَجۡمَعِينَ
Isipo kuwa walio mfuata Luut'i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote.
Wala hakusalimika na huo ukhalifu na adhabu yake ila ahli zake yeye Luut'i. Basi hao Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuamrisha tuwaokoe wote.
التفاسير العربية:
إِلَّا ٱمۡرَأَتَهُۥ قَدَّرۡنَآ إِنَّهَا لَمِنَ ٱلۡغَٰبِرِينَ
Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma.
Na hatoangamia katika ahli zake ila mkewe, kwani yeye hakumfuata mumewe, bali yu pamoja na hao wakosefu ambao wanao stahiki adhabu.
التفاسير العربية:
فَلَمَّا جَآءَ ءَالَ لُوطٍ ٱلۡمُرۡسَلُونَ
Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut'i,
Wale Malaika walio tumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuteremsha yaliyo ahidiwa, walipo fika nchi ya Luut'i na watu wake,
التفاسير العربية:
قَالَ إِنَّكُمۡ قَوۡمٞ مُّنكَرُونَ
Alisema (Luut'i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana.
Luut'i aliwaambia: Watu nyinyi sikujueni, na nafsi yangu inatishika nanyi. Naogopa msituletee balaa.
التفاسير العربية:
قَالُواْ بَلۡ جِئۡنَٰكَ بِمَا كَانُواْ فِيهِ يَمۡتَرُونَ
Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka.
Wakasema: Usituogope, kwani hatukukujia kwa unalo liogopa, bali tumekujia kwa jambo la kukufurahisha, nalo ni kuwateremshia adhabu hawa watu wako walio kukadhibisha na wakawa wanaitilia shaka hiyo adhabu au wanaikanya.
التفاسير العربية:
وَأَتَيۡنَٰكَ بِٱلۡحَقِّ وَإِنَّا لَصَٰدِقُونَ
Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli.
Nasi tumekujia kwa amri iliyo thaabiti isiyo na shaka, nayo ni kuiteremsha adhabu. Na kutimiza ahadi ni katika sifa yetu, kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
فَأَسۡرِ بِأَهۡلِكَ بِقِطۡعٖ مِّنَ ٱلَّيۡلِ وَٱتَّبِعۡ أَدۡبَٰرَهُمۡ وَلَا يَلۡتَفِتۡ مِنكُمۡ أَحَدٞ وَٱمۡضُواْ حَيۡثُ تُؤۡمَرُونَ
Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao,wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa.
Ilivyo kuwa adhabu itawateremkia, basi wewe na ahli zako mlio andikiwa kuokoka, tokeni baada ya kwisha ingia usiku.
التفاسير العربية:
وَقَضَيۡنَآ إِلَيۡهِ ذَٰلِكَ ٱلۡأَمۡرَ أَنَّ دَابِرَ هَٰٓؤُلَآءِ مَقۡطُوعٞ مُّصۡبِحِينَ
Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali.
Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la alimfunulia Luut'i kwa kumwambia: Sisi tumewahukumia na kuwakadiria wakosefu kuteketea. Watang'olewa itapoingia asubuhi, wala hatobaki hata mmoja wao.
التفاسير العربية:
وَجَآءَ أَهۡلُ ٱلۡمَدِينَةِ يَسۡتَبۡشِرُونَ
Na wakaja watu wa mji ule nao furahani.
Asubuhi kulipo pambazuka waliwaona Malaika kwa sura ya binaadamu wazuri. Wao wale wakawafurahia, wakaja ili wafanye nao vitendo vyao viovu, vya kuwaingilia wanaume.
التفاسير العربية:
قَالَ إِنَّ هَٰٓؤُلَآءِ ضَيۡفِي فَلَا تَفۡضَحُونِ
Akasema: (Luut'i) Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe.
Luut'i akaogopa wasije wakatenda vitendo vyao viovu. Akasema: Hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe kwa vitendo vyenu vibaya.
التفاسير العربية:
وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَلَا تُخۡزُونِ
Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.
Na mwogopeni Mwenyezi Mungu Mtukufu! Msifanye uchafu wenu, mkanipatisha hizaya na madhila mbele yao!
التفاسير العربية:
قَالُوٓاْ أَوَلَمۡ نَنۡهَكَ عَنِ ٱلۡعَٰلَمِينَ
Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote?
Wale wakhalifu wakasema: Kwani si tulikukataza wewe usimkaribishe mtu yeyote, na hivi sasa tena unatuzuia tusifanye nao tunayo yatamani?
التفاسير العربية:
قَالَ هَٰٓؤُلَآءِ بَنَاتِيٓ إِن كُنتُمۡ فَٰعِلِينَ
Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.
Ili kuwanabihisha njia ya maumbile ya kisharia, Nabii wa Mwenyezi Mungu Luut'i akasema: Hawa mabinti wa mji huu, nao ni binti zangu, waoeni ikiwa mnataka kukidhi matamanio yenu.
التفاسير العربية:
لَعَمۡرُكَ إِنَّهُمۡ لَفِي سَكۡرَتِهِمۡ يَعۡمَهُونَ
Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo.
Ewe Nabii Muaminifu! Naapa kwa haki ya uhai wako! Hawa wamo katika mghafala, hawajui yatakayo wateremkia. Wamekuwa kama walio lewa! Hakika wao wamo katika upotovu, wanatapatapa, hawajui wapite wapi.
التفاسير العربية:
فَأَخَذَتۡهُمُ ٱلصَّيۡحَةُ مُشۡرِقِينَ
Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa.
Na walipo kuwa wao wamo katika ulevi wao wa mghafala nyoyo zao na akili zao zikachotwa na ukelele mkali mno wa kutisha, wakati jua lilipo chomoza.
التفاسير العربية:
فَجَعَلۡنَا عَٰلِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمۡطَرۡنَا عَلَيۡهِمۡ حِجَارَةٗ مِّن سِجِّيلٍ
Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni.
Mwenyezi Mungu Aliye takasika katekeleza hukumu yake, akasema: Miji yao tukaifanya juu chini kwa kuivuruga, na tukawateremshia udongo ulio fanyika mawe ukiwateremkia kama mvua. Majumba yao yakaporomoka. Na wakitoka nje hukuta hiyo mvua ya mawe. Kwa hivyo wakawa wamezungukwa kila jiha. (upande)
التفاسير العربية:
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَأٓيَٰتٖ لِّلۡمُتَوَسِّمِينَ
Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi.
Haya yaliyo washukia kaumu Luut'i ni alama wazi ya kuonyesha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo timiza ahadi yake. Wajuao mambo wanayatambua hayo, na wanayaelewa matokeo yake kwa alama zake, kwani kila kitendo chenye sifa ya ukosefu kina alama yake isiyo potea. Matokeo yake ni mfano wa haya, duniani na Akhera.
التفاسير العربية:
وَإِنَّهَا لَبِسَبِيلٖ مُّقِيمٍ
Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa.
Na mabaki ya mji huu yapo yamesalia. Nayo yapo njiani katika njia inayo pitiwa na watu. Anaye taka kuwaidhika kwayo anaweza kuwaidhika.
التفاسير العربية:
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَأٓيَةٗ لِّلۡمُؤۡمِنِينَ
Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini.
Kwa kuwa mabaki yake yapo kwenye njia iliyo wazi ni dalili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutimiza onyo lake, na Waumini wenye kut'ii Haki wanatambua hayo.
التفاسير العربية:
وَإِن كَانَ أَصۡحَٰبُ ٱلۡأَيۡكَةِ لَظَٰلِمِينَ
Na Hakika watu wa kichakani, walikuwa wenye kudhulumu
Kama kaumu ya Luut'i walivyo kadhibisha, kadhaalika wakaazi wa Kichakani kwenye msitu wenye matunda walimkanya Mtume wao. Wakawa madhaalimu wenye kudhulumu mno katika imani yao na maingiliano yao.
التفاسير العربية:
فَٱنتَقَمۡنَا مِنۡهُمۡ وَإِنَّهُمَا لَبِإِمَامٖ مُّبِينٖ
Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia iliowazi.
Tukawateremshia nakama yetu. Na mabaki yao yapo njiani yanaonekana, na mpita njia akiwa ni mtu wa Imani basi anaweza kuzingatia kwayo.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ كَذَّبَ أَصۡحَٰبُ ٱلۡحِجۡرِ ٱلۡمُرۡسَلِينَ
Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume.
Na kama walio tangulia hali kadhaalika wakaazi wa Hijr walimkanusha Mtume wao aliye tumwa kwao, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote. Kwani ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Watu wa Hijr ndio Thamud. Na Hijr ni bonde baina ya Madina na Sham. Tazama maelezo juu ya Aya 73 ya Surat Al-Aa'raaf.
التفاسير العربية:
وَءَاتَيۡنَٰهُمۡ ءَايَٰتِنَا فَكَانُواْ عَنۡهَا مُعۡرِضِينَ
Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza.
Tuliwabainishia hoja zenye kuonyesha uwezo wetu, na Utume wa Mtume wetu, nao wakayapuuza, wala wasiyafikiri.
التفاسير العربية:
وَكَانُواْ يَنۡحِتُونَ مِنَ ٱلۡجِبَالِ بُيُوتًا ءَامِنِينَ
Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani.
Nao walikuwa watu wenye nguvu na wajenzi. Walikuwa wakijenga majumba yao katika milima na wakiichonga hiyo hiyo milima. Na wao walikuwa wakijiamini kuwa wametua na nafsi zao na mali yao.
التفاسير العربية:
فَأَخَذَتۡهُمُ ٱلصَّيۡحَةُ مُصۡبِحِينَ
Basi ukelele ukawatwaa asubuhi.
Walipo kufuru na wakakanya, zikawajia sauti za kutisha, za kuonya kuteketea kwao, wakahiliki wakati wa asubuhi.
التفاسير العربية:
فَمَآ أَغۡنَىٰ عَنۡهُم مَّا كَانُواْ يَكۡسِبُونَ
Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma.
Wala mali waliyo yachuma na majumba waliyo yajenga hayakuwalinda na hilaki iliyo wateremkia.
التفاسير العربية:
وَمَا خَلَقۡنَا ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ وَمَا بَيۡنَهُمَآ إِلَّا بِٱلۡحَقِّۗ وَإِنَّ ٱلسَّاعَةَ لَأٓتِيَةٞۖ فَٱصۡفَحِ ٱلصَّفۡحَ ٱلۡجَمِيلَ
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.
Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yao katika anga, na viliomo ndani yake, watu na wanyama, na mimea na visio na uhai, na vinginevyo ambavyo mwanaadamu havijui, isipo kuwa kwa uadilifu, na hikima, na maslaha ambayo hayaambatani na fisadi ya kudumu isiyo na mwisho. Na kwa hivyo basi ni lazima siku ya kukomesha shari ifike bila ya shaka yoyote. Basi ewe Nabii Mtukufu! Wasamehe hao washirikina adhabu ya duniani, na ingiana nao kwa kuwastahamilia maudhi yao. Na kuwaita wito kwa hikima ni kuingiliana kwa usamehevu na upole.
التفاسير العربية:
إِنَّ رَبَّكَ هُوَ ٱلۡخَلَّٰقُ ٱلۡعَلِيمُ
Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi.
Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu aliye kuumba na akakulea, ni Mwenye viumbe vyote, na anajua hali yako na yao. Yeye anastahiki umtegemezee mambo yako na yao. Naye anajua maslaha yako na yao.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ ءَاتَيۡنَٰكَ سَبۡعٗا مِّنَ ٱلۡمَثَانِي وَٱلۡقُرۡءَانَ ٱلۡعَظِيمَ
Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur'ani Tukufu.
Ewe Nabii Muaminifu, tumekupa Aya saba za Qur'ani, nazo ni Sura ya Al- Fatiha unayo ikariri katika kila Swala, na humo yamo ya kutunyenyekea na maombi ya uwongofu yaliyo kaamili. Na tumekupa Qur'ani Tukufu yote. Na ndani yake mna hoja, na miujiza. Kwa hivyo wewe una nguvu ambazo zinakufalia usamehe.
التفاسير العربية:
لَا تَمُدَّنَّ عَيۡنَيۡكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعۡنَا بِهِۦٓ أَزۡوَٰجٗا مِّنۡهُمۡ وَلَا تَحۡزَنۡ عَلَيۡهِمۡ وَٱخۡفِضۡ جَنَاحَكَ لِلۡمُؤۡمِنِينَ
Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.
Ewe Mtume! Usivitazame kwa kuvitamani na kuvitaka vitu vya starehe ya dunia tulivyo wapa makafiri wa kishirikina, na Kiyahudi, na Kikristo, na Kimajusi. Kwani hivyo ni duni kwa kulinganisha na ulio pewa wewe katika kuwasiliana nasi, na Qur'ani Tukufu. Wala usiwasikitikie kwa sababu ya kuendelea kwao na madhambi. Nawe tulia, na unyenyekee, na wachukue Waumini ulio nao kwa upole. Kwani hao ni nguvu za Haki, na watu wa Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
وَقُلۡ إِنِّيٓ أَنَا ٱلنَّذِيرُ ٱلۡمُبِينُ
Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha.
Ewe Nabii! Waambie makafiri wote: Mimi nakuonyeni na adhabu kali, na nakubainishieni maonyo yangu kwa hoja za kukata.
التفاسير العربية:
كَمَآ أَنزَلۡنَا عَلَى ٱلۡمُقۡتَسِمِينَ
Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa,
Haya ni kama maonyo ya walio igawanya Qur'ani wakaifanya ati ni mashairi, na ukohani, na hadithi za kale na mengineyo. Nao wasiiamini juu ya kusimama hoja juu yao.
التفاسير العربية:
ٱلَّذِينَ جَعَلُواْ ٱلۡقُرۡءَانَ عِضِينَ
Ambao wakaifanya Qur'ani vipande vipande.
Hao waliifanya Qur'ani vipande mbali mbali, nayo hali kuwa haikubali kugawika kwa umuujiza wake na ukweli wake.
التفاسير العربية:
فَوَرَبِّكَ لَنَسۡـَٔلَنَّهُمۡ أَجۡمَعِينَ
Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote.
Ikiwa hiyo hali yao, basi Wallahi kwa Aliye kuumba akakulinda na akakulea, hapana shaka tutawahisabu wote Siku ya Kiyama,
التفاسير العربية:
عَمَّا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ
Kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
Kwa vitendo vyao vya kuudhi, na kufuru, na kejeli.
التفاسير العربية:
فَٱصۡدَعۡ بِمَا تُؤۡمَرُ وَأَعۡرِضۡ عَنِ ٱلۡمُشۡرِكِينَ
Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina.
Basi wewe tangaza wito wa Haki, wala usishughulike na wayatendao washirikina na maneno yao.
التفاسير العربية:
إِنَّا كَفَيۡنَٰكَ ٱلۡمُسۡتَهۡزِءِينَ
Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli.
Na hao washirikina wanao ukejeli wito wako hawatokushinda, wala hawatoweza kukuingilia kati baina yako na wito wako.
التفاسير العربية:
ٱلَّذِينَ يَجۡعَلُونَ مَعَ ٱللَّهِ إِلَٰهًا ءَاخَرَۚ فَسَوۡفَ يَعۡلَمُونَ
Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine.Basi, watakuja jua!
Hao washirikina mawazo yao yamedhoofika, ndio wakafanya kuwa Mwenyezi Mungu anao miungu mingine ya masanamu. Na watakuja jua matokeo ya ushirikina wao itapo wateremkia adhabu chungu.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ نَعۡلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدۡرُكَ بِمَا يَقُولُونَ
Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo.
Nasi tunajua dhiki ya moyo inayo kupata kwa wanayo yasema ya ushirikina na kejeli na dharau.
التفاسير العربية:
فَسَبِّحۡ بِحَمۡدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ ٱلسَّٰجِدِينَ
Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanaomsujudia.
Ikikupata dhiki hiyo mkimbilie Mwenyezi Mungu Mtukufu umwelekee, na umt'ii na umnyenyekee, na utake msaada kwa Sala, kwani humo ndio imo poza.
التفاسير العربية:
وَٱعۡبُدۡ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأۡتِيَكَ ٱلۡيَقِينُ
Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini. (nao ni Mauti)
Na shikilia ibada ya Mwenyezi Mungu aliye kuumba, akakulinda, mpaka ifike amri ya yakini, nayo ni Mauti.
التفاسير العربية:
 
ترجمة معاني سورة: الحجر
فهرس السور رقم الصفحة
 
ترجمة معاني القرآن الكريم - الترجمة السواحلية - علي محسن البرواني - فهرس التراجم

ترجمة معاني القرآن الكريم إلى اللغة السواحلية، ترجمها علي محسن البرواني.

إغلاق