Naapa kwa mbingu yenye Buruj au Manaazil, njia au vituo ambavyo nyota hupitia katika nyendo zake, Buruuj au Manaazil ndio huu mkusanyiko wa nyota unao onekana kwa sura namna mbali mbali mbinguni. Hizo Buruuj zimegawika sehemu kumi na mbili ambazo ardhi inazipitia inapo lizunguka jua.
Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa!
Na hapana walilo lichukia kwa hao Waumini ila ni kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu ambaye adhabu yake huogopwa, Msifiwa anaye tarajiwa thawabu zake.
Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu.
Ambaye, peke yake, ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi anashuhudia yote wayatendayo Waumini na makafiri na atawalipa kwayo.
Hakika walio wafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua.
Hakika walio watia matatani Waumini wanaume na Waumini wanawake kwa maudhi na kuwaadhibu kwa moto, kisha wasitubu na kurejea nyuma watapata Akhera adhabu ya Jahannamu kwa ukafiri wao, na watapata adhabu ya kuunguzwa kwa kule kuwaunguza moto Waumini.
Hakika walio amini na wakatenda mema watapata Bustani zenye mito ipitayo kati yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
Hakika hao walio kusanya kwenye Imani ya Mwenyezi Mungu vitendo vyema watapata Mabustani yapitayo mito kati yake. Neema hiyo waliyo lipwa ni kufuzu kukubwa.