HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu.
Watapenda, na watatamani sana makafiri wanao zikanya Aya za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, watapo ona adhabu ya Siku ya Kiyama, lau kuwa walisilimu walipo kuwapo duniani, na wakafuata kwa ikhlasi Dini ya Mwenyezi Mungu.
Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua.
Lakini sasa wamo katika kughafilika, hawazingatii adhabu itakayo wapata Akhera! Basi ukisha wafikishia ujumbe wako, na ukawaonya, waachilie mbali. Wao hawana hamu ila kula, na kustarehe kwa ladha za dunia. Tamaa ya uwongo inawazuga. Na hakika bila ya shaka yoyote watakuja jua yatakayo wapata pale watapo yaona kwa macho yao Siku ya Kiyama.
Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu.
Na ikiwa wao wanataka wateremshiwe adhabu ya duniani, kama Mwenyezi Mungu alivyo wateketeza walio kuwa kabla yao, basi wajue kuwa Mwenyezi Mungu hauteketezi mji wowote ila kwa wakati wake maalumu.
Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu.
Na uovu wa hali yao na wingi wa kughafilika kwao hata imefika hadi kumuita Nabii wao kwa kejeli wakisema: Ewe uliye teremshiwa Kitabu cha kukumbusha! Hapana shaka kuwa wewe una wazimu moja kwa moja! Huko kumuita kuwa ndiye aliye teremshiwa Ukumbusho, yaani Mawaidha, hakukuwa ila ni kwa kejeli tu, kumfanyia maskhara.
Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?
Na hadi ya ukafiri wao walizidisha juu ya matusi hayo na kejeli kwa kusema: Laiti badala ya hicho Kitabu kilicho teremshwa ungeli tuletea Malaika wakawa ndio hoja yenyewe, kama wewe ni msema kweli miongoni mwa wenye kusema kweli!
Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula.
Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka neno lake aliwajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika ila huwa pamoja nao Haki ya nguvu yenye kuthibiti ambayo haina njia ya kuikataa. Basi wakiikanya huwa tena hawapewi muhula wowote, bali huteremshiwa adhabu ya hapa hapa duniani hapo hapo!
Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.
Na hakika, kwa ajili ya kuwa Wito wa Nabii huyu kwendea Haki udumu mpaka Siku ya Kiyama, hatuwateremshi Malaika, bali tumewateremshia hii Qur'ani ambayo kukumbusha kwake kunaendelea daima dawamu. Na Sisi ndio wenye kuilinda isiingiliwe na mageuzo na mabadiliko yoyote mpaka kusimama Kiyama.
Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo.
Na ewe Mtume Muaminifu! Usihuzunike; kwani Sisi tuliwatuma Mitume kabla yako kwa mataifa ambao wameshikilia upotovu kama hao walivyo shikilia. Na wao wamepita pamoja na wa kale walio teketezwa kwa ukafiri wao!
Wala mtindo wao hao walio watangulia kwa kushikilia upotovu haukuwa ila kuwafanyia maskhara Mitume wao, Mtume baada ya Mtume, kama wanavyo kufanyia kejeli wewe! Huo ndio mtindo wa wapotovu!
Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu.
Kama tulivyo itia Qur'ani katika nyoyo za Waumini ikaingiza mwangaza, basi kadhaalika tumeingiza upotovu katika nyoyo za walio pigwa muhuri wa ukosefu; hali ya katika nyoyo zao ikawa kinyume cha hayo. Upotovu ukatia mizizi katika roho zao.
Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale.
Wakhalifu hao hawaamini. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa muhula mpaka waione adhabu chungu ya Siku ya Kiyama ndio kama ulivyo kwisha tangulia.
Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda,
Watu hao wanataka wateremshiwe Malaika. Ewe Nabii! Usidhani kuwa ndio wataamini wakiteremshiwa. Bali hata tungeli wafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda huko wakaona maajabu yaliyoko, na wakawaona Malaika,
Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa.
Bado wasingeli amini, na wangesema: Macho yetu yamefumbwa tusione, na yamefunikwa. Bali hayo si lolote ila ni uchawi tu, tumerogwa! Basi hapana faida ya ishara yoyote maadamu nyoyo zao zimeenea ukafiri.
Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
Na Sisi tumeweka mbinguni sayari na nyota, kwa makundi yenye hisabu zake na yenye kukhitalifiana umbo lake na sura yake. Na kadhaalika tukazipamba kwa wenye kuziangalia kwa kutuza na kuzingatia, na kuchunguza kwazo dalili za uwezo wa Muumbaji wao.
Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana.
Na yeyote katika hao mashetani wanao jaribu kuibia kusikiliza maneno yanayo jiri baina ya wakaazi wa hizi nyote, basi Sisi tunampopoa kwa vijinga vya moto vya mbinguni vinavyo onekana wazi.
Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake.
Na tumekuumbieni ardhi, na tumekutengenezeeni mpaka ikawa kama busati lilio tandikwa, na tukaweka ndani yake milima iliyo simama imara. Na tumekuotesheeni ndani namna mbali mbali za mimea ya kukufaeni kwa uhai wenu, na tumeifanya kwa vipimo na zama maalumu katika kukua kwake, na faida yake kwa kula, na kwa kadiri ya haja zenu na kwa vipimo vyake, na sura yake kwa umbo na tabia. Aya hii inaeleza uhakika wa uumbaji ambao haukujuulikana ila katika zama za hivi karibuni. Nayo ni kuwa kila kabila ya mimea imefanana kati yao kwa kuonekana na undani wake, hata katika sehemu zake ndogo ndogo, katika viungo vyake vyote vya hiyo mimea. Na hali kadhaalika katika "Khalaya" au "Cells" za hiyo mimea ya kabila fulani, kwa ajili ya kutimiza kazi iliyo kusudiwa kiungo hicho cha mmea. Na pia sehemu za mimea ya hizo kabila zao na vilivyo undwa katika viungo vyake utaona mnasaba wake umethibiti kila mwaka, ukilinganisha kwa wakati ule ule katika miaka mingine
Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.
Na tumekujaalieni katika ardhi sababu za maisha mema. Kwani ndani yake yamo mawe ya kujengea majumba, na wanyama mnao nafiika kwa nyama yao, au ngozi zao, au manyoa yao. Na yapo maadeni yanayo toka chini ya ardhi, na mengineyo. Kama ilivyo kuwa humo zipo sababu za kukuleteeni nyinyi maisha mema, basi humo pia wanapata maisha wenginewe ambao wapo chini ya mamlaka yenu, kama watoto na wafwasi, ambao Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye waruzuku wao na nyinyi.
Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu.
Na hapana chochote cha kheri ila kiko kwetu kama mahodhi yaliyo jaa, nasi tunakiweka tayari na tunakitoa kwa wakati wake. Na hatuwateremshii waja wetu ila kwa kiasi maalumu, kwa mujibu tunavyo pima kwa hikima yetu ya maumbile.
Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka.
Na Sisi tulipeleka pepo zilizo beba mvua na zilizo beba mbegu za mimea, na tukateremsha maji ya kukunywesheni. Na hayo ni kwa kufuata vile tutakavyo. Na yeyote yule hawezi kuyatenda kama hayo ila awe nayo kwake kama mahodhi au mabirika. Aya hii imeitangulia sayansi kwa kusema kuwa upepo unafanya kazi kubwa katika kubeba pollen, chembe dume za kupandishia mimea, kupelekea sehemu za uke za mimea mingine, na kwa hivyo yakazalikana mazao. Na pia haikujuulikana ila mwanzo wa karne hii tuliyo nayo kwamba upepo unazalisha mawingu yanayo nyesha mvua. Kwani "Nucleons" ambazo juu yake hujumuika sehemu za mvuke wa maji na zikawa chembe chembe za maji ndani ya wingu, ndizo chanzo cha mvua inayo chukuliwa na pepo kupelekwa kwenye majimbo yanayo fikiwa na mawingu. Misingi ya hizo "Nucleons" ni chumvi ya bahari, na vinavyo chukuliwa na upepo juu ya uso wa ardhi, na "Oxides" na vumbi vumbi, n.k. Na vyote hivyo ni lazima kwa ajili ya mvua. "Wala si nyinyi mnayo yaweka". Imethibiti kwa sayansi ya kisasa kuwa mvua inaanza kwa mvuke kutokana na uso wa ardhi na bahari, kisha inarejea hali ile ile tena kama ilivyo tajwa. Ikinya mvua hunywesha kila kilicho na uhai katika ardhi, na huinywesha ardhi yenyewe. Wala haiwezekani kuzuilika, kwa sababu ikichuruzika kutokana na vyote vyenye uhai na katika ardhi ikaingia baharini, tena kisha huanza kuzunguka mara ya pili kwa kupanda mvuke kutoka baharini. Basi hali ni hivyo mzunguko. Hapa ndio inabainika maana ya Aya "Wala si nyinyi mnayo yaweka."
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi.
Na hakika walio tangulia na walio taakhari watakusanywa wakati mmoja. Na Mwenyezi Mungu atawahisabia na atawalipa. Na hayo ni kwa mujibu wa hikima yake na ujuzi wake. Na Yeye ndiye anaye itwa Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto.
Na makhaluku wengine ni majini, ambao tuliwaumba mbele, alipo umbwa asili yake Iblisi kutokana na moto mkali mno unao toka katika tundu za mwili wa mtu.
Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.
Ewe Nabii! Kumbuka asli ya viumbe. Pale alipo sema Aliye kuumba, Mola Mlezi wa viumbe vyote, kuwaambia Malaika: Mimi nataka kumuanzisha mtu niliye muumba kutokana na udongo mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umebadilika rangi, na una sura.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!
Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Ukiwa wewe umekuwa a'asi, umetokana na ut'iifu wangu, basi tokelea mbali kwenye Bustani hii! Kwani hakika wewe umefukuzwa kwenye rehema yangu pahala pa hishima.
Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.
Na Mimi nimekwisha kuhukumia ubaidike na rehema na utukufu mpaka Siku ya Kiyama, Siku ya Hisabu na Malipo. Na hapo ndipo utapo pata adhabu, wewe na wanao kufuata .
Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapofufuliwa.
Iblisi akasema, hali naye kesha kuwa ni mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu: Ewe Muumba wangu! Nipe muhula, nibakishe usinitwae mpaka Siku ya Kiyama, Siku watapo fufuliwa watu wakawa hai baada ya kufa kwao.
Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,
Akasema Iblisi, mkhalifu, a'asi: Ewe Muumba wangu unaye nibakisha! Umenitakia upotofu, nami nikatumbukia ndani yake. Basi kwa sababu hiyo nahakikisha kuwa nitawapambia wanaadamu maovu wayaone mazuri, na nitafanya kila juhudi kuwapotoa wote!
Wala hawatoepukana na upotovu wangu ila wale waja wako walio kufanyia ikhlasi Wewe na nisio weza kuzimiliki nyoyo zao kwa zilivyo kuwa imara kwa kukumbuka Wewe.
Hakika usafi wa waja walio isafia niya Dini yao ndio Njia Iliyo Nyooka, na haki yangu nisiikiuke, kwani hao siwezi kuwapotoa. (Tafsiri hii yaonyesha maneno hayo ni ya Iblisi. Lakini Tafsiri nyengine zinasema maneno hayo ni ya Mwenyezi Mungu, kwa mfano ya Abdulla Saleh, Abdulla Yusuf, Pickthall, Razi, Baidhawi, Qurtubi, Zamakhshari, Ibn Kathir, Assad.)
Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Hakika waja wangu walio nisafia Mimi Dini yao wewe huna uwezo wa kuwapoteza. Lakini wapotovu, walio zama katika upotovu, walio kufuata wewe, basi hao ndio unayo madaraka juu ya nyoyo zao.
Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa.
Wala huo Moto mkali hauna mlango mmoja tu, bali una milango saba kwa ajili ya wingi wanao stahiki kuingia humo. Na kila mlango una kundi lake makhsusi. Na kila kundi una cheo chake maalumu cha kulingana na uovu wake.
Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
Haya ni malipo ya wanao mfuata Shetani. Ama wale ambao Shetani kashindwa kuwapotoa, kwa kuwa wameweka kinga baina yake na nyoyo zao, hao watapata Mabustani yaliyo bora, na chemchem zinazo pita .
Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana.
Na hakika watu wa Imani wataishi katika kheri hii na nafsi zao zimetua. Kwani tumezitoa chuki zilizo kuwamo katika nafsi hizo. Wote hao watakuwa ndugu waketi juu ya viti vya enzi zikitazamana nyuso zao kwa furaha na mahaba, wala hawawi mmoja nyuma ya mwenzie wakichunguliana visogoni.
Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Ewe Nabii muaminifu! Wape khabari waja wangu wote kwamba Mimi ni Mwingi wa kughufiria na kusamehe kwa mwenye kutubu, akaamini, na akatenda mema. Na kwamba Mimi ni Mwingi wa kuwarehemu.
Na wape khabari kwamba adhabu ninayo wateremshia wenye kuasi na kukufuru ni adhabu yenye kutia machungu kweli, na adhabu yoyote nyengineyo haihisabiwi kuwa ina machungu mbele ya hii.
Ewe Nabii! Waambie pia, katika kubainisha rehema yangu makhsusi katika dunia na adhabu yangu kwa wenye kuasi humo, khabari ya Malaika walio mfikia Ibrahim kama wageni.
Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.
Ewe Muaminifu! Watajie pale walipo ingia kwake, naye akawaogopa. Wao wakamwambia: Amani kwako, na tulia! Yeye akasema: Sisi tunakuogopeni, kwani mmetujia kwa ghafla, sio wakati wa dasturi wa kufika wageni, na hatujui mna nini!
Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi.
Wakasema: Usiogope, na tuwa moyo! Kwani tunakubashiria mwana, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu atampa siku zijazo za uhai wake ilimu kubwa. Inaonyesha hapa kuwa bishara hii si ya Ismail a.s. Kwani Ismail alikuwa kesha zaliwa, naye na mama yake Haajir walikuwa wapo Makka. Bishara hii ni ya Ibrahim na mkewe, basi kwa hivyo ni ya Is-haq mwana wa Ibrahim na Sara.
Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea?
Ibrahim akasema: Mimi sikati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu ila walio potea wasio utambua utukufu wake na uwezo wake.
Alivyo kuwa kaanza kuzoeana nao, alisema: Ikiwa mmenibashiria khabari hii nzuri, je mna jambo gani jenginelo mlilo nalo baada ya haya, enyi wajumbe mlio tumwa na Mwenyezi Mungu?
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!
Wakasema hakika sisi tumetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa watu walio fanya ukhalifu katika Haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya Nabii wao, na haki ya nafsi zao wenyewe. Ukhalifu ndio mtindo wao. Watu wenyewe ni kaumu ya Luut'i. Basi tutawateketeza.
Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka.
Wakasema: Usituogope, kwani hatukukujia kwa unalo liogopa, bali tumekujia kwa jambo la kukufurahisha, nalo ni kuwateremshia adhabu hawa watu wako walio kukadhibisha na wakawa wanaitilia shaka hiyo adhabu au wanaikanya.
Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali.
Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la alimfunulia Luut'i kwa kumwambia: Sisi tumewahukumia na kuwakadiria wakosefu kuteketea. Watang'olewa itapoingia asubuhi, wala hatobaki hata mmoja wao.
Asubuhi kulipo pambazuka waliwaona Malaika kwa sura ya binaadamu wazuri. Wao wale wakawafurahia, wakaja ili wafanye nao vitendo vyao viovu, vya kuwaingilia wanaume.
Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.
Ili kuwanabihisha njia ya maumbile ya kisharia, Nabii wa Mwenyezi Mungu Luut'i akasema: Hawa mabinti wa mji huu, nao ni binti zangu, waoeni ikiwa mnataka kukidhi matamanio yenu.
Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo.
Ewe Nabii Muaminifu! Naapa kwa haki ya uhai wako! Hawa wamo katika mghafala, hawajui yatakayo wateremkia. Wamekuwa kama walio lewa! Hakika wao wamo katika upotovu, wanatapatapa, hawajui wapite wapi.
Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni.
Mwenyezi Mungu Aliye takasika katekeleza hukumu yake, akasema: Miji yao tukaifanya juu chini kwa kuivuruga, na tukawateremshia udongo ulio fanyika mawe ukiwateremkia kama mvua. Majumba yao yakaporomoka. Na wakitoka nje hukuta hiyo mvua ya mawe. Kwa hivyo wakawa wamezungukwa kila jiha. (upande)
Haya yaliyo washukia kaumu Luut'i ni alama wazi ya kuonyesha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo timiza ahadi yake. Wajuao mambo wanayatambua hayo, na wanayaelewa matokeo yake kwa alama zake, kwani kila kitendo chenye sifa ya ukosefu kina alama yake isiyo potea. Matokeo yake ni mfano wa haya, duniani na Akhera.
Na Hakika watu wa kichakani, walikuwa wenye kudhulumu
Kama kaumu ya Luut'i walivyo kadhibisha, kadhaalika wakaazi wa Kichakani kwenye msitu wenye matunda walimkanya Mtume wao. Wakawa madhaalimu wenye kudhulumu mno katika imani yao na maingiliano yao.
Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume.
Na kama walio tangulia hali kadhaalika wakaazi wa Hijr walimkanusha Mtume wao aliye tumwa kwao, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote. Kwani ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Watu wa Hijr ndio Thamud. Na Hijr ni bonde baina ya Madina na Sham. Tazama maelezo juu ya Aya 73 ya Surat Al-Aa'raaf.
Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani.
Nao walikuwa watu wenye nguvu na wajenzi. Walikuwa wakijenga majumba yao katika milima na wakiichonga hiyo hiyo milima. Na wao walikuwa wakijiamini kuwa wametua na nafsi zao na mali yao.
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.
Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo kati yao katika anga, na viliomo ndani yake, watu na wanyama, na mimea na visio na uhai, na vinginevyo ambavyo mwanaadamu havijui, isipo kuwa kwa uadilifu, na hikima, na maslaha ambayo hayaambatani na fisadi ya kudumu isiyo na mwisho. Na kwa hivyo basi ni lazima siku ya kukomesha shari ifike bila ya shaka yoyote. Basi ewe Nabii Mtukufu! Wasamehe hao washirikina adhabu ya duniani, na ingiana nao kwa kuwastahamilia maudhi yao. Na kuwaita wito kwa hikima ni kuingiliana kwa usamehevu na upole.
Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu aliye kuumba na akakulea, ni Mwenye viumbe vyote, na anajua hali yako na yao. Yeye anastahiki umtegemezee mambo yako na yao. Naye anajua maslaha yako na yao.
Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur'ani Tukufu.
Ewe Nabii Muaminifu, tumekupa Aya saba za Qur'ani, nazo ni Sura ya Al- Fatiha unayo ikariri katika kila Swala, na humo yamo ya kutunyenyekea na maombi ya uwongofu yaliyo kaamili. Na tumekupa Qur'ani Tukufu yote. Na ndani yake mna hoja, na miujiza. Kwa hivyo wewe una nguvu ambazo zinakufalia usamehe.
Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.
Ewe Mtume! Usivitazame kwa kuvitamani na kuvitaka vitu vya starehe ya dunia tulivyo wapa makafiri wa kishirikina, na Kiyahudi, na Kikristo, na Kimajusi. Kwani hivyo ni duni kwa kulinganisha na ulio pewa wewe katika kuwasiliana nasi, na Qur'ani Tukufu. Wala usiwasikitikie kwa sababu ya kuendelea kwao na madhambi. Nawe tulia, na unyenyekee, na wachukue Waumini ulio nao kwa upole. Kwani hao ni nguvu za Haki, na watu wa Mwenyezi Mungu.
Haya ni kama maonyo ya walio igawanya Qur'ani wakaifanya ati ni mashairi, na ukohani, na hadithi za kale na mengineyo. Nao wasiiamini juu ya kusimama hoja juu yao.
Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine.Basi, watakuja jua!
Hao washirikina mawazo yao yamedhoofika, ndio wakafanya kuwa Mwenyezi Mungu anao miungu mingine ya masanamu. Na watakuja jua matokeo ya ushirikina wao itapo wateremkia adhabu chungu.
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
સંશોધનના પરિણામો:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".