(H'a Mim) Hizi harufi mbili katika harufi za alifbete zilio fungulia Sura hii kama ilivyo ada ya Qur'ani katika Sura nyingi, ili kuzindua watu watanabahi, na pia kuonyesha dalili ya muujiza wa Qur'ani.
Hichi ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanao jua.
Kitabu hichi ni namna ya peke yake kwa uzuri wake kwa matamshi na ibara yake ya utungaji, na kwa maana inavyo pambanua baina Haki na baat'ili, na bishara na onyo, na kuzitengeneza nafsi, na kupiga mifano, na kubainisha hukumu. Nacho kinasomwa kwa ulimi wa Kiarabu, chepesi kukifahamu kwa watu wanao jua.
Kitoacho khabari njema, na chenye kuonya. Lakini wengi katika wao wamepuuza; kwa hivyo hawasikii.
Chenye kuwapa khabari njema Waumini wenye kutenda kuwa watapata neema iliyo andaliwa kwa ajili yao, na kuwakhofisha wanao kanusha kuwa watapata adhabu chungu iliyo andaliwa kwa ajili yao. Lakini wengi walikitupilia mbali, wala wasinafiike nacho, kama kwamba hawakusikia.
Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo tuitia, na masikio yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe lipo pazia. Basi wewe tenda, nasi tunatenda.
Na makafiri wakamwambia Mtume s.a.w.: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko vizito kwa hayo unayo tuitia yaliyo khusu Tawhidi (Upweke) wa Mwenyezi Mungu. Na masikioni mwetu mna uziwi, basi hayasikii hayo unayo tulingania. Na baina yetu na wewe lipo pazia nene linalo tuzuia kukubali hayo uliyo tuletea. Basi fanya utakalo, na sisi tunafanya tutakalo.
Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake msamaha, na ole wao wanao mshirikisha!
Ewe Mtume! Waambie: Hakika mimi si chochote ila ni mtu mfano wenu nyinyi, napata Wahyi (Ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwamba wa kuabudiwa kwa haki na nyinyi ni Mungu Mmoja tu. Basi fuateni Njia Iliyo Nyooka ya kwendea kwake! Na mtake kwake msamaha kwa madhambi yenu. Na washirikina wasio toa Zaka kuwapa wanao stahiki watapata adhabu kali. Na wao tu, si wenginewe, ndio wanao kataa kuwa upo uhai wa Akhera.
Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliye umba ardhi katika siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Ewe Mtume! Waambie hawa washirikina: Ama nyinyi mnastaajabisha! Mnamkataa Mwenyezi Mungu aliye iumba ardhi kwa siku mbili, na huku juu ya hayo, mnamfanyia washirika wa kushirikiana naye huyo Muumba ardhi, Mmiliki wa walimwengu wote na Mlezi wao? Zimetajwa Siku moja au Siku nyingi katika Sura nyengine. Katika Surat Al-Hajj, Aya 47 Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: "Na kwa hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Na katika Surat Assajdah, Aya 5 amesema Mtukufu: "Anapitisha mambo yote yaliyo baina ya mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku moja tu ambayo kipimo chake ni miaka elfu mnayo hisabu." Na katika Surat Al-Ma'arij Mtukufu amesema: "Malaika na Roho hupanda kwake katika siku iliyo kadiri yake ni miaka elfu khamsini." Maoni ya kitaalamu: Vipimo vya wakati wanavyo vitumia watu vimefungamana na dunia na inavyo zunguka juu ya msumari-kati wake na kulizunguka jua. Mtu akitoka kwenye ardhi (dunia) akenda kwenye sayari nyengine za mbinguni vipimo hivyo vya nyakati vinabadilika kwa kuzidi au kwa kupungua. Na hizi Aya tukufu zinaonyesha ishara ya ukweli huu wa ki-ilimu, na ya kwamba zama au nyakati ni jambo la mlinganisho tu. Na bila ya shaka ipo miaka ya ki-ilimu ya Falaki ya kulinganisha yenye kumkinika kuifarikisha baina yao. Mwaka wa ki-jua wa duniani huhisabiwa kwa kupimwa wakati ambao dunia inachukua kulizunguka jua kwa ukamilifu mnamo siku 365, na ilhali sayari zilio karibu na jua kama U't'aarid (Mercury) humaliza safari yake ya kulizunguka jua mnamo siku 88, na upande mwengine sayari ya Blutu (Pluto) ambayo ndiyo sayari iliyo mbali mno na jua, na ndiyo inazunguka taratibu mno inachukua kuzunguka kwake mnamo miaka 250 kwa mujibu wa miaka yetu sisi.
Na akaweka humo milima juu yake, na akabarikia humo na akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa wanao uliza.
Naye Mwenyezi Mungu amesimamisha juu ya ardhi milima iliyo simama imara ili isiyumbe nanyi; na akakithirisha humo kheri nyingi, na akakadiria humo riziki kwa watu wake, kwa mujibu wa hikima yake, mnamo siku nne. Na nyinyi, juu ya haya, mnakwenda kumwekea washirika? Na Yeye amekadiria kila kitu bila ya upungufu wala kuzidi. Kufafanua huku katika uumbaji wa ardhi na vilio juu yake ni maelezo kwa hao wanao uliza.
Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni wat'iifu.
Kisha amekhusisha uweza wake na kuumba mbingu, nazo zilikuwa kama moshi, basi zikawapo. Na kuumba kwake mbingu na ardhi kwa mujibu wa mapendo yake ni jambo jepesi kwake, ni kama kukiambia kitu: Njoo ukipenda usipenda, nacho kikat'ii.
Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na akazipangia kila mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya chini kwa mataa na kwa ulinzi. Hichi ndicho kipimo cha Mwenyezi Mungu Mwenye Kujua.
Na akatimiza kuumba mbingu saba mnamo siku mbili nyengine. Na akaweka katika kila mbingu alicho kiandalia na ilivyo pelekea hikima yake. Na akaipamba mbingu ya karibu na dunia kwa nyota zinazo ng'ara kama taa, kwa ajili ya uwongofu wasisikilize mashetani khabari za walio juu. Kuumba huko vilivyo ni mpango wa Mwenyezi Mungu asiye shindika, Mwenye kuzunguka kila kitu.
Basi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano wa adhabu ya A'di na Thamudi,
Basi washirikina wakipuuza Imani baada ya kuwekewa wazi dalili zake, wewe, Mtume, waambie: Nimekuonyeni msije kupatilizwa kwa adhabu kali kama iliyo wateketeza kina A'di na Thamudi.
Walipo wajia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angeli taka Mola wetu Mlezi bila ya shaka angeli wateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyo tumwa.
Walijiwa A'di na Thamudi na hiyo adhabu walipo watokelea Mitume pande zote. Hawakuacha njia ya kuwaongoza ila waliipitia, na wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu. Wao wakasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli taka kumtuma Mtume basi angeli tuteremshia Malaika. Basi sisi hakika tunakataa hayo ya Tawhidi na mengineyo mliyo kuja nayo nyinyi.
Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!
Ama kina A'di walipandwa na kiburi katika nchi bila ya haki ya kuwa na kiburi hicho. Na walisema kwa kughurika na nafsi zao: Nani huyo anaye tushinda sisi kwa nguvu? Ama ajabu watu hawa! Wanasema hayo na wao hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ana nguvu zaidi kuwashinda wao? Na wao walikuwa wakizikanya Ishara zetu!
Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
Tukawapelekea upepo wenye sauti kali katika siku korofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwafanya wawe madhalili wanyonge katika maisha ya duniani. Na ninaapa kuwa bila ya shaka adhabu ya Akhera itakuwa ya hizaya zaidi, wala wao siku hiyo hawatapata wa kuwasaidia.
Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walipenda upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyachuma.
Na ama kina Thamudi tuliwabainishia njia ya kheri na njia ya shari. Lakini wao walikhiari upotovu kuliko uwongofu, ikawatwaa radi iliyo waunguza kwa madhila na unyonge, kwa sababu ya madhambi waliyo yachuma.
Na siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao wakikgawanywa kwa makundi.
Ewe Nabii! Siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kupelekwa Motoni, wakawa wa mwanzo wao wanakutana na wa mwisho wao, ili ipate hoja ilazimike juu ya wote,
Hata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
Mpaka watakapo ufikilia Moto na wakaulizwa juu ya madhambi waliyo yatenda duniani, na wao wakakataa, yakawashuhudilia masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa waliyo yatenda wao,
Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa.
Na hao maadui wa Mwenyezi Mungu wakaziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Na ngozi zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu aliye tamkisha kila kitu. Na Yeye ndiye aliye kuumbeni hapo mwanzo kabla hamjawa chochote. Na kwake Yeye, peke yake, ndio mtarejea baada ya kufufuliwa, akuhisabieni mliyo kwisha yatanguliza katika vitendo.
Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyo kuwa mkiyatenda.
Wala nyinyi hamkuwa mkiweza kuficha vitendo vyenu viovu hata viungo vyenu visivione na ikawa macho yenu, na masikio yenu na ngozi zenu, vyote hivyo vikakushuhudilieni. Lakini nyinyi mlikuwa mkidhani kuwa Mwenyezi Mungu hajui mengi katika vitendo vyenu, kwa sababu mkivifanya kwa uficho.
Basi wakisubiri Moto ndio maskani yao. Na wakiomba radhi hawakubaliwi.
Basi hata wakijizuia machungu yao, Moto ndio mwisho wao, na makaazi yao ya daima. Na wakitaka kumridhi Mwenyezi Mungu sasa hawakubaliwi hayo matakwa yao.
Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao. Basi ikawathibitikia kauli wawe pamoja na mataifa yaliyo pita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kukhasirika.
Nasi tumewaandalia duniani marafiki waharibifu, na wao wakawazainishia mbele yao mambo ya Akhera, basi wakawaghuri kwamba ati hakuna kufufuliwa wala kuhisabiwa, na wakawapambia pia mambo ya duniani ili wastarehe nayo. Na neno la adhabu lilio wapata mataifa yaliyo kwisha pita miongoni mwa majini na watu walio kuwa kama wao, likawathibitikia na wao kwa sababu ya kukhiari kwao upotovu badala ya uwongofu. Hakika watu hao wote walikuwa katika walio khasiri khasara iliyo timia.
Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda.
Makafiri wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Msiisikilize hii Qur'ani, na inapo somwa nyie leteni porojo lisio kuwa na maana, ili pasiwepo mtu wa kuisikia wala kunafiika kwayo, asaa kwa hivyo mkamshinda Muhammad.
Basi hapana shaka tutawaonjesha hao walio kufuru adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
Tunaapa: Bila ya shaka tutawaonjesha walio kufuru adhabu kali kwa vitendo vyao, na khasa kwa hivi kuipiga vita Qur'ani. Na bila ya shaka tutawalipa malipo maovu kabisa kwa vitendo vyao.
Hayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na maskani ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.
Hizo adhabu zilizo tajwa ni malipo wanayo stahiki maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto walio andaliwa katika makaazi ya kuishi milele, kuwa ni malipo kwa kule kuzikataa mfululizo Ishara za Mwenyezi Mungu na hoja zake.
Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni wa walio chini kabisa.
Na makafiri watasema, nao wamo Motoni: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe hayo makundi ya majini na watu walio tupoteza ili tuwaweke chini ya nyayo zetu, wawe katika watu wa chini kabisa.
Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa.
Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, kwa kuukubali Upweke wake, kisha wakasimama sawa sawa juu ya sharia zake, Malaika watawateremkia mara kwa mara wakiwaambia: Msikhofu kukuteremkieni shari, wala msihuzunike kuwa mtakosa kheri, na furahini kuwa mtapata Pepo mliyo ahidiwa kwa ndimi za Manabii na Mitume.
Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyo vitaka.
Na Malaika watawaambia: Sisi ni wasaidizi wenu katika maisha ya duniani kwa kukuungeni mkono, na Akhera kwa kukuombeeni shafaa na kukutukuzeni. Na huko Akhera mtapata kila cha ladha na kizuri kinacho pendwa na nafsi zenu, na mtapata kila mnacho kitamani kuwa ni takrima, na maamkio yanayo toka kwa Mola Mlezi Mkunjufu wa maghfira na rehema.
Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Na Malaika watawaambia: Sisi ni wasaidizi wenu katika maisha ya duniani kwa kukuungeni mkono, na Akhera kwa kukuombeeni shafaa na kukutukuzeni. Na huko Akhera mtapata kila cha ladha na kizuri kinacho pendwa na nafsi zenu, na mtapata kila mnacho kitamani kuwa ni takrima, na maamkio yanayo toka kwa Mola Mlezi Mkunjufu wa maghfira na rehema.
Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?
Hapana mwenye kauli nzuri zaidi kuliko mwenye kulingania Tawhid ya Mwenyezi Mungu na ut'iifu wake, na pamoja na hayo, akatenda vitendo vyema, na akasema kwa kuungama itikadi yake: Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu, yaani wenye kunyenyekea amri za Mwenyezi Mungu.
Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.
Haziwezi kuwa sawa tabia njema na tabia mbovu. Pinga uovu ukikujia kutokana na adui kwa tabia iliyo bora kuliko yake. Hapo matokeo yake ni huyo ambaye uliye kuwa na uadui naye atakuja kuwa kama mwenzio wa kukunusuru mwenye moyo safi.
Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa.
Na hawaruzukiwi tabia hii, ya kulipa wema kwa uovu, ila wale wenye khulka ya kusubiri, na hawaruzukiwi hayo ila wenye fungu kubwa la tabia ya wema na ukamilifu wa nafsi.
Na Shet'ani akikuchochea kwa uchochezi wewe jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Na akitokea Shetani akakutia wasiwasi kukuachisha hayo uliyo amrishwa, ewe unaye semezwa, basi jilinde naye kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu kusikia kwake na kujua kwake kumezunguka kila kitu. Na Yeye atakulinda naye.
Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.
Na katika dalili za uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni huu usiku na mchana, na jua na mwezi. Msilisujudie jua wala mwezi, kwani hivyo ni katika Ishara zake tu. Bali msujudieni Yeye Mwenyezi Mungu peke yake, aliye umba jua, na mwezi, na usiku, na mchana, ikiwa nyinyi kweli mnamuabudu Yeye peke yake.
Na ikiwa watajivuna, basi hao walioko kwa Mola wako Mlezi wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki.
Ikiwa washirikina watajiona wakubwa hawafai kufuata amri yako, basi wewe usiudhike. Kwani hao walio kwa Mola wako Mlezi kwenye utakatifu wake, nao ni Malaika, wanamtakasa Yeye na kila upungufu katika kila wakati, usiku na mchana, wakimsafia ibada Yeye tu, wala hawachoki kumsabihi.
Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge, lakini tunapo iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliye ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Na katika dalili za uweza wake, Mtukufu, ni kwamba unaona, wewe unaye weza kuona, ardhi kavu. Tukiiteremshia maji inatikisika kwa mimea, na inaumuka na kuja juu. Hakika huyo aliye ihuisha ardhi iliyo kwisha kufa ndiye aliye elekea kuhuisha wafu katika hayawani. Yeye ni mtimilivu wa uweza juu ya kila kitu. Aya hii inabainisha kwamba mawadi za mbolea ambazo ni chumvi chumvi zisio na uhai, pindi zipatapo maji ya mvua, huyayuka, na kwa hivyo husahilika kufikilia kwenye mbegu za mimea na mizizi yake. Hapo hugeuka kuingia katika khalaya (Cells) na mifumo na viungo vilio hai. Na kwa hivyo vinaonekana kuwa ni hai. Na ukubwa wake hukua na kuzidi kwa kuingiana na kukuzwa na mimea.
Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda.
Hakika hao wanao iacha Njia iliyo sawa kwa mintarafu ya Ishara zetu na wakaitupilia mbali kwa kuikadhibisha, mambo yao hayatupotei Sisi wala hayo wanayo yakusudia. Nasi tutawalipa kama wanavyo stahiki. Kwani anaye tupwa katika Moto ni bora au yule anaye kuja naye hali katulia Siku ya Kiyama kwa kuokoka kwake na kila ovu? Kabisa hao hawalingani. Waambie kwa kuwaahidi: Fanyeni mtakavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzunguka kila kitu kwa jicho lake, naye atamlipa kila mmoja kwa a'mali yake.
Kwa hakika wanayo yakataa mawaidha haya yanapo wajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.
Hakika wanao ikataa Qur'ani Tukufu inapo wajia bila ya kuzingatia, watapata adhabu ambayo hapana mtu anaye weza kuikadiria. Wao wameipinga Qur'ani nacho hakika ni Kitabu kisicho kuwa na mfano, kinamshinda kila mwenye kukipinga, hakiingiliwi na upotofu usio kuwa na asli kwake kwa upande wowote ule, kimeteremka kwa kukufuatana kutokana na Mungu aliye takasika na upuuzi, Msifiwa kwa wingi wa sifa kwa neema alizo zitoa.
Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
Hakika wanao ikataa Qur'ani Tukufu inapo wajia bila ya kuzingatia, watapata adhabu ambayo hapana mtu anaye weza kuikadiria. Wao wameipinga Qur'ani nacho hakika ni Kitabu kisicho kuwa na mfano, kinamshinda kila mwenye kukipinga, hakiingiliwi na upotofu usio kuwa na asli kwake kwa upande wowote ule, kimeteremka kwa kukufuatana kutokana na Mungu aliye takasika na upuuzi, Msifiwa kwa wingi wa sifa kwa neema alizo zitoa.
Huambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa kabla yako. Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni Mwenye adhabu chungu.
Ewe Muhammad! Huambiwi wewe na maadui wako ila kama walivyo ambiwa Mitume wa kabla yako na maadui wao, nayo ni matusi na kuambiwa mwongo. Hakika Muumba wako na Mlezi wako ana msamaha mwingi, na ni Mwenye kuadhibu kwa machungu makubwa. Basi Yeye humghufiria mwenye kutubu kwake, na humtesa mwenye kushikilia na inda yake.
Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali.
Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni, kama walivyo pendekeza baadhi ya hao wanao kera, basi bila ya shaka wangeli sema: Lau zingeli bainishwa Aya zake kwa ulimi tunao ufahamu! Kitabu hichi cha lugha ya kigeni, na huyu mkhubiri wake ni Mwaarabu! Yawaje haya? Ewe Mtume! Waambie: Hii Qur'ani ni hivyo hivyo kama walivyo teremshiwa Waumini, si wengineo, kuwa ni Uwongofu na Poza kwa Waumini; kiwaokoe na ubabaishi, na kiwaponyeshe na shaka shaka. Na wasio amini wamekuwa kama katika masikio yao pana kizuizi, uziwi, nayo hii Qur'ani kwao wao ni upofu, hawaoni chochote ndani yake ila fitna tu. Hao makafiri ni kama wanao itwa waiamini kwa umbali kabisa. Hawausikii wito huo.
Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea khitilafu kati yake. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
Ninaapa: Kwa hakika tulimpa Musa Taurati, na watu wake wakakhitalifiana kwayo. Na lau ingeli kuwa hukumu ya Mola wako Mlezi haikuakhirishwa, ewe Muhammad, mpaka muda maalumu kwake, basi hapana shaka pange amuliwa hukumu baina yako na hao kwa kuwang'olea mbali wanao kanusha. Na hakika makafiri katika kaumu yako wamo katika shaka na Qur'ani, na hiyo inawatia dhiki na wasiwasi.
Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja.
Mwenye kutenda vitendo vyema ujira wake ataupata mwenyewe, na mwenye kutenda uovu madhambi yake yatakuwa juu yake. Na Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja wake, hata amtese mtu kwa dhambi za mwengine.
UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu Mwenyezi Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako wapi washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni mwetu anaye shuhudia hayo.
Kwa Mwenyezi Mungu peke yake ndio unarejea ujuzi wa kusimama Saa ya Kiyama. Matunda hayatoki kwenye vifuniko vyake, wala mwanamke hachukui mimba wala hazai ila awe Yeye anajua. Na kumbuka siku ambayo Mwenyezi Mungu atawaita washirikina, kwa kuwakebehi, awaambie: Wako wapi hao washirika wangu mlio kuwa mkiwaomba badala yangu? Watasema kwa kutaadhari: Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakujuvya kuwa sisi hatuna wa kushuhudia kuwa wewe una mshirika yeyote.
Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo mpata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.
Mwanaadamu hachoki kumwomba Mola wake Mlezi kwa kheri za kidunia. Ikimpata shari basi huwa mwingi wa kuikatia tamaa kheri, na kuvunjika moyo hadi, ya kwamba Mwenyezi Mungu hamwitikii dua yake.
Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina mema yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda, na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu.
Tunaapa: Tukimwonjesha mtu neema, kwa fadhila yetu, baada ya dhara kubwa iliyo msibu bila ya shaka husema: Hii neema niliyo ipata ni haki yangu mimi. Wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na ninaapa ikitokea nikarejeshwa kwa Mola wangu Mlezi basi na huko kwake bila ya shaka nitapata malipo mema. Lakini Sisi tunaapa: Hapana shaka tutawalipa walio kufuru, Siku ya Kiyama, kwa vitendo vyao! Na hapana shaka tutawaonjesha adhabu kali iliyo rindikwa juu kwa juu!
Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika upinzani wa mbali?
Ewe Muhammad! Waambie: Hebu nambieni; ikiwa hii Qur'ani imetoka kwa Mwenyezi Mungu nanyi mkawa mnaikataa, basi nani aliye kuwa mbali mno na Ukweli kuliko huyo aliye kinyume na Haki?
Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
Karibuni hivi tutawaonyesha hao wanao zikataa Ishara zetu zenye kuonyesha ukweli wako katika pande za mbinguni na ardhi, na katika nafsi zao wenyewe, mpaka yawadhihirikie ya kwamba uliyo waletea ni Haki tupu si vinginevyo. Je! Wanakataa kuwa Sisi tunawaletea Ishara hizo? Je! Haitoshi kuwa Mola wako Mlezi ni Mwenye kukizunguka kila kitu?
Ama wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi! Ama hakika Yeye amekizunguka kila kitu.
Ama hakika hawa makafiri wamo katika shaka kubwa kukutana na Mola wao Mlezi, kwa sababu ya kuwa hawaamini kufufuliwa. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukizunguka kila kitu kwa ujuzi wake na uweza wake.
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
Hasil pencarian:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".