Terjemahan makna Alquran Alkarim - Terjemahan Berbahasa Sawahili - Ali Muhsin Al-Barwani * - Daftar isi terjemahan

XML CSV Excel API
Please review the Terms and Policies

Terjemahan makna Surah: Surah Al-Ma'ārij   Ayah:

Surat Al-Ma'arij

سَأَلَ سَآئِلُۢ بِعَذَابٖ وَاقِعٖ
Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea!
Ameita, mwenye kuita, kuhimiza kama kufanya kejeli, iletwe upesi adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo hapana shaka itawashukia makafiri.
Tafsir berbahasa Arab:
لِّلۡكَٰفِرِينَ لَيۡسَ لَهُۥ دَافِعٞ
Kwa makafiri - ambayo hapana awezaye kuizuia .
Wala hapana chochote cha kuzuia adhabu hiyo,
Tafsir berbahasa Arab:
مِّنَ ٱللَّهِ ذِي ٱلۡمَعَارِجِ
Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja.
Kwani hiyo inatoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu, ambako huko ndiko zinatoka nguvu zinazo simama, na hukumu inayo tekelezwa.
Tafsir berbahasa Arab:
تَعۡرُجُ ٱلۡمَلَٰٓئِكَةُ وَٱلرُّوحُ إِلَيۡهِ فِي يَوۡمٖ كَانَ مِقۡدَارُهُۥ خَمۡسِينَ أَلۡفَ سَنَةٖ
Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka khamsini elfu!
Malaika na Jibrili wanapanda kwenda kunako toka amri yake kwa siku ambayo urefu wake ni miaka khamsini elfu kwa mujibu wa hisabu ya miaka ya duniani.
Tafsir berbahasa Arab:
فَٱصۡبِرۡ صَبۡرٗا جَمِيلًا
Basi subiri kwa subira njema.Hakika wao wanaiona iko mbali!
Basi, ewe Muhammad! Subiri uwastahamilie hizo kejeli zao, na kuhimiza kwao adhabu, kwa subira isiyo kuwa na mbabaiko ndani yake wala mashtaka.
Tafsir berbahasa Arab:
إِنَّهُمۡ يَرَوۡنَهُۥ بَعِيدٗا
Hakika wao wanaiona iko mbali!
Hakika hao makafiri wanaiona hiyo Siku ya Kiyama ni kitu cha muhali kutokea.
Tafsir berbahasa Arab:
وَنَرَىٰهُ قَرِيبٗا
Na Sisi tunaiona iko karibu.
Na Sisi tunaona kuwa ni jambo jepesi katika uweza wetu, wala halina uzito wowote.
Tafsir berbahasa Arab:
يَوۡمَ تَكُونُ ٱلسَّمَآءُ كَٱلۡمُهۡلِ
Siku ambayo mbingu zitakapo kuwa kama maadeni iliyo yayushwa.
Siku mbingu itakapo kuwa kama fedha iliyo yayuka,
Tafsir berbahasa Arab:
وَتَكُونُ ٱلۡجِبَالُ كَٱلۡعِهۡنِ
Na milima itakuwa kama sufi.
Na milima itakapo kuwa kama sufi iliyo tiwa rangi na ikapigwa,
Tafsir berbahasa Arab:
وَلَا يَسۡـَٔلُ حَمِيمٌ حَمِيمٗا
Wala jamaa hatamuuliza jamaa yake.
Wala jamaa hamuulizi jamaa yake: Nini hali yako? Kwa sababu kila mmoja kajishughulikia nafsi yake!
Tafsir berbahasa Arab:
يُبَصَّرُونَهُمۡۚ يَوَدُّ ٱلۡمُجۡرِمُ لَوۡ يَفۡتَدِي مِنۡ عَذَابِ يَوۡمِئِذِۭ بِبَنِيهِ
Ijapo kuwa wataonyeshwa waonane. Atatamani mkosefu lau ajikomboe na adhabu ya siku hiyo kwa kuwatoa fidia wanawe,
Watakuwa wakijuulishana wao kwa wao mpaka wajuane baraabara, na ilhali hapana amuulizae mwenzie kitu. Kafiri atatamani lau ange pata kujikomboa nafsi yake na adhabu hiyo Siku ya Kiyama kwa kumtoa mwanawe awe ni fidia yake,
Tafsir berbahasa Arab:
وَصَٰحِبَتِهِۦ وَأَخِيهِ
Na mkewe, na nduguye,
Au mkewe, au nduguye,
Tafsir berbahasa Arab:
وَفَصِيلَتِهِ ٱلَّتِي تُـٔۡوِيهِ
Na jamaa zake walio kuwa wakimkimu,
Au jamaa zake aliyo khusiana nao,
Tafsir berbahasa Arab:
وَمَن فِي ٱلۡأَرۡضِ جَمِيعٗا ثُمَّ يُنجِيهِ
Na wote waliomo duniani, kisha aokoke yeye.
Na wote waliomo duniani, apate kuokoka yeye tu!
Tafsir berbahasa Arab:
كَلَّآۖ إِنَّهَا لَظَىٰ
La, hasha! Kwa hakika huo ni Moto mkali kabisa,
Ewe mkosefu! Wacha hayo unayo yatamani ya kutaka kujikomboa kwa fidia! Hakika huo moto, unawaka kweli!
Tafsir berbahasa Arab:
نَزَّاعَةٗ لِّلشَّوَىٰ
Unao babua ngozi ya kichwa!
Utakubabua mikono yako, na miguu yako, na viungo vyako vyote,
Tafsir berbahasa Arab:
تَدۡعُواْ مَنۡ أَدۡبَرَ وَتَوَلَّىٰ
Utamwita kila aliye geuza mgongo na akageuka.
Utanadi kwa jina la huyo aliye iacha Haki, na akaacha ut'iifu,
Tafsir berbahasa Arab:
وَجَمَعَ فَأَوۡعَىٰٓ
Na akakusanya mali, kisha akayahifadhi.
Na akakusanya mali akayaweka katika mabweta yake, wala hakutoa haki ya Mwenyezi Mungu iliomo katika hayo mali!
Tafsir berbahasa Arab:
۞ إِنَّ ٱلۡإِنسَٰنَ خُلِقَ هَلُوعًا
Hakika mtu ameumbwa na papara.
Hakika tabia ya binaadamu ni papara, mwingi wa kupapatika,
Tafsir berbahasa Arab:
إِذَا مَسَّهُ ٱلشَّرُّ جَزُوعٗا
Inapo mgusa shari hupapatika.
Na kutoridhika akifikiwa na lolote la karaha na uzito,
Tafsir berbahasa Arab:
وَإِذَا مَسَّهُ ٱلۡخَيۡرُ مَنُوعًا
Na inapo mgusa kheri huizuilia.
Na ni mwingi wa kuzuia na kunyima akipata kheri na neema.
Tafsir berbahasa Arab:
إِلَّا ٱلۡمُصَلِّينَ
Isipo kuwa wanao swali,
Isipo kuwa wanao swali,
Tafsir berbahasa Arab:
ٱلَّذِينَ هُمۡ عَلَىٰ صَلَاتِهِمۡ دَآئِمُونَ
Ambao wanadumisha Sala zao,
Ambao wanadumisha Swala zao, hawakikosi hata kipindi kimoja.
Tafsir berbahasa Arab:
وَٱلَّذِينَ فِيٓ أَمۡوَٰلِهِمۡ حَقّٞ مَّعۡلُومٞ
Na ambao katika mali yao iko haki maalumu
Na wale ambao katika mali yao ipo haki iliyo ainiwa
Tafsir berbahasa Arab:
لِّلسَّآئِلِ وَٱلۡمَحۡرُومِ
Kwa mwenye kuomba na anaye jizuilia kuomba;
iliyo wekwa kwa ajili ya masikini mwenye kuomba kutaka msaada, na anaye jizuilia kuomba pia. (Katika wanao zuilika kuomba wanaingia si wenye kustahi na kuona vibaya tu, bali pia wasio weza kuomba kama watoto wachanga, wagonjwa, na wanyama pia.)
Tafsir berbahasa Arab:
وَٱلَّذِينَ يُصَدِّقُونَ بِيَوۡمِ ٱلدِّينِ
Na ambao wanaisadiki Siku ya Malipo,
Na wale wanao isadiki Siku ya Malipo, basi wanajitayarisha kwa ajili yake;
Tafsir berbahasa Arab:
وَٱلَّذِينَ هُم مِّنۡ عَذَابِ رَبِّهِم مُّشۡفِقُونَ
Na ambao wanaiogopa adhabu itokayo kwa Mola wao Mlezi.
Na wale wanao iogopa adhabu ya Mola wao Mlezi basi wanajikinga nayo wala hawajitii katika jambo la kuwaletea adhabu hiyo.
Tafsir berbahasa Arab:
إِنَّ عَذَابَ رَبِّهِمۡ غَيۡرُ مَأۡمُونٖ
Hakika adhabu ya Mola wao Mlezi si ya kuaminika nayo.
Kwani hakika adhabu ya Mola wao Mlezi hapana hata mmoja anaye weza kuaminika nayo isimpate.
Tafsir berbahasa Arab:
وَٱلَّذِينَ هُمۡ لِفُرُوجِهِمۡ حَٰفِظُونَ
Na ambao wanahifadhi tupu zao.
Na ambao wanazihifadhi tupu zao hata hawaemewi na matamanio yao.
Tafsir berbahasa Arab:
إِلَّا عَلَىٰٓ أَزۡوَٰجِهِمۡ أَوۡ مَا مَلَكَتۡ أَيۡمَٰنُهُمۡ فَإِنَّهُمۡ غَيۡرُ مَلُومِينَ
Isipo kuwa kwa wake zao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi
Lakini kwa wake zao na masuria wao hawazihifadhi; kwa sababu hapo hawalaumiwi kuifuata tabia ya maumbile.
Tafsir berbahasa Arab:
فَمَنِ ٱبۡتَغَىٰ وَرَآءَ ذَٰلِكَ فَأُوْلَٰٓئِكَ هُمُ ٱلۡعَادُونَ
Lakini wanao taka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka.
Basi mwenye kutafuta starehe ya maingiliano kwa wasio kuwa wake na masuria, basi hao tena ni wenye kuikiuka halali na kuingia katika haramu.
Tafsir berbahasa Arab:
وَٱلَّذِينَ هُمۡ لِأَمَٰنَٰتِهِمۡ وَعَهۡدِهِمۡ رَٰعُونَ
Na ambao wanazichunga amana zao na ahadi zao,
Na hao wenye kuzihifadhi amana za sharia na amana za waja wa Mwenyezi Mungu, na walio lazimika nayo kwa Mwenyezi Mungu na kwa watu bila ya kukhuni wala kupunja,
Tafsir berbahasa Arab:
وَٱلَّذِينَ هُم بِشَهَٰدَٰتِهِمۡ قَآئِمُونَ
Na ambao wanasimama imara katika ushahidi wao,
Na ambao kwa shahada zao wamesimama sawa sawa kwa haki bila ya kuficha wanalo lijua,
Tafsir berbahasa Arab:
وَٱلَّذِينَ هُمۡ عَلَىٰ صَلَاتِهِمۡ يُحَافِظُونَ
Na ambao wanazihifadhi Sala zao.
Na wanao hifadhi Swala zao wakizisali sawasawa kwa ukamilifu -
Tafsir berbahasa Arab:
أُوْلَٰٓئِكَ فِي جَنَّٰتٖ مُّكۡرَمُونَ
Hao ndio watakao hishimiwa Peponi.
Watu wenye sifa kama hizo nzuri watakuwa ni wenye kuhishimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu huko Peponi.
Tafsir berbahasa Arab:
فَمَالِ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ قِبَلَكَ مُهۡطِعِينَ
Wana nini wale walio kufuru wanakutumbulia macho tu?
Kitu gani kinawapelekea hao walio kufuru kukujia mbio mbio ?
Tafsir berbahasa Arab:
عَنِ ٱلۡيَمِينِ وَعَنِ ٱلشِّمَالِ عِزِينَ
Makundi kwa makundi upande wa kulia na upande wa kushoto!
Kutoka kuliani na kushotoni kwa makundi?
Tafsir berbahasa Arab:
أَيَطۡمَعُ كُلُّ ٱمۡرِيٕٖ مِّنۡهُمۡ أَن يُدۡخَلَ جَنَّةَ نَعِيمٖ
Kwani kila mmoja wao anatumai kuingizwa katika Pepo ya neema?
Je, kwani kila mmoja wao ana tamaa ya kuingia kwenye Pepo yenye neema, baada ya kusikia kuwa Mwenyezi Mungu amemuahidi Mtume wake na Waumini kuwatia Peponi?
Tafsir berbahasa Arab:
كَلَّآۖ إِنَّا خَلَقۡنَٰهُم مِّمَّا يَعۡلَمُونَ
La, hasha! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na wanacho kijua.
Basi nawaache hiyo tamaa yao ya kuingia Peponi. Hakika Sisi tumewaumba wao kutokana na maji ya kudharauliwa.
Tafsir berbahasa Arab:
فَلَآ أُقۡسِمُ بِرَبِّ ٱلۡمَشَٰرِقِ وَٱلۡمَغَٰرِبِ إِنَّا لَقَٰدِرُونَ
Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote na magharibi zote kwamba Sisi tunaweza
Naapa kwa Mola Mlezi wa mashariki zote, na magharibi zote za siku, na sayari na hidaya, kwamba hakika bila ya shaka Sisi tuna uweza wa kuwaangamiza,
Tafsir berbahasa Arab:
عَلَىٰٓ أَن نُّبَدِّلَ خَيۡرٗا مِّنۡهُمۡ وَمَا نَحۡنُ بِمَسۡبُوقِينَ
Kuwabadili kwa walio bora kuliko wao; na Sisi hatushindwi.
Na kuwaleta walio wat'iifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko wao. Wala Sisi hatushindwi kubadilisha huko. Huenda ikawa inakusudiwa kwa "mashariki zote" na "magharibi zote" ni maeneo ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu yote ambayo hayana mpaka kama ilivyo ashiriwa katika Aya 137 ya Surat Al-A'araf: "Na tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa mashariki za nchi na magharibi zake ambayo tuliitia baraka", kuonyesha sehemu zote za hiyo nchi inayo tajwa. Na huenda ikawa makusudio yake ni mashariki za jua na mwezi na nyota zote na sayari, na magharibi zao, kwa ajili ya kuonyesha vile vile ufalme wa Mwenyezi Mungu wote. Na kwa hivyo inadhihirika kwetu kuwa vyombo vinavyo kwenda katika qubba la mbingu vinachomoza kwenye upeo wa mashariki na kuchwa kwenye upeo wa magharibi, au kwa uchache vinazunguka kutoka mashariki kwendea magharibi kuizunguka nyota ya Pole, katika sehemu ya kaskazini ya dunia. Kwani umbali wa Pole kwa nyota ni mdogo kuliko pahala unapo angalia, basi nyota hapo haichomozi wala haichwi, bali hupiga duru ndogo kuizunguka North Pole. Na kwa hiyo Aya inaashiria saa za usiku. Rejea kwenye kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: " Na alama na kwa nyota wao wanaongoka." Na kwa udhaahiri wa kuchomoza na kuchwa ipo ishara ya kuzunguka kwa dunia, na hiyo ni neema kubwa kabisa katika neema za Mwenyezi Mungu juu ya maisha katika sayari hii. Kwani bila ya kuzunguka kwa dunia juu ya msumari-kati wake nusu ya dunia ingeli pigwa na jua mfululizo muda wa nusu mwaka kaamili, na ingeli nyimwa mwangaza kabisa nusu nyengine. Kwa hivyo uhai kama tulivyo uzoea usinge kuwako. Na tukifanya hizo mashariki na hizo magharibi ni za jua peke yake, wachilia mbali nyota nyengine na sayari, basi itakuwa ishara ni kule kuchomoza jua kila siku pahala pengine na kuchwa pahala pengine kila siku, au hata katika kila dakika linapo pita juu ya dunia. Kwani jua kila dakika linakuchwa pahala na linachomoza pahala papili mfululizo. Na haya ni katika mipango ya Mwenyezi Mungu na miujiza ya uweza wake. Tazama pia maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 5 katika Surat Assaffat, na Aya 17 ya Surat Arrah'man.
Tafsir berbahasa Arab:
فَذَرۡهُمۡ يَخُوضُواْ وَيَلۡعَبُواْ حَتَّىٰ يُلَٰقُواْ يَوۡمَهُمُ ٱلَّذِي يُوعَدُونَ
Basi waache wapige porojo na wacheze, mpaka wakutane na siku yao wanayo ahidiwa,
Basi waachilie wakiporojoka katika upotovu wao, na wakicheza na dunia yao, mpaka wakutane na siku yao waliyo ahidiwa kupewa adhabu.
Tafsir berbahasa Arab:
يَوۡمَ يَخۡرُجُونَ مِنَ ٱلۡأَجۡدَاثِ سِرَاعٗا كَأَنَّهُمۡ إِلَىٰ نُصُبٖ يُوفِضُونَ
Siku watakapotoka makaburini kwa upesi kama kwamba wanakimbilia mfundo,
Siku watakapo tolewa makaburini mbio mbio kumwendea huyo ataye waita, kama kwamba wamemweka ufundo na wakimuabudu duniani walivyo kuwa wakimkimbilia badala ya Mwenyezi Mungu,
Tafsir berbahasa Arab:
خَٰشِعَةً أَبۡصَٰرُهُمۡ تَرۡهَقُهُمۡ ذِلَّةٞۚ ذَٰلِكَ ٱلۡيَوۡمُ ٱلَّذِي كَانُواْ يُوعَدُونَ
Macho yao yatainama, fedheha itawafunika. Hiyo ndiyo Siku waliyo kuwa wakiahidiwa.
Macho yameinama chini, hawawezi kuyanyanyua, yamegubikwa na unyonge na udhalili. Hiyo ndiyo siku waliyo kuwa wakiahidiwa duniani na wao wakiikanusha.
Tafsir berbahasa Arab:
 
Terjemahan makna Surah: Surah Al-Ma'ārij
Daftar surah Nomor Halaman
 
Terjemahan makna Alquran Alkarim - Terjemahan Berbahasa Sawahili - Ali Muhsin Al-Barwani - Daftar isi terjemahan

Terjemahan Makna Al-Qur`ān Al-Karīm ke Bahasa Sawahili oleh Ali Muhsin Al-Barwani

Tutup