Harufi hizi zimeanzia baadhi ya Sura kuashiria kuwa Qur'ani ni muujiza ulio tungwa na harufi kama harufi wanazo zitumia Waarabu katika maneno yao. Na juu ya hayo wao wameshindwa kuleta mfano wake. Na pia ni kwa ajili ya kuzindua watu wasikilize na watege sikio. Na washirikina walikuwa wamewafikiana kuwa wawe wanaropokwa maneno ya upuuzi tu ikisomwa Qur'ani wala wasiisikilize.
Wanao shika Swala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na Akhera.
Hao ndio wanao timiza Swala kwa njia ya ukamilifu kabisa, na wanawapa Zaka wanao istahiki; na wao wanayaamini maisha ya Akhera kwa imani yenye nguvu kabisa.
Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio wenye kufanikiwa.
Hao Waumini wanao tenda vyema vitendo vyao, wametua kwenye Uwongofu ulio wajia kutokana na Mola wao Mlezi. Na hao tu - si wengineo - ndio wenye kufuzu kikweli.
Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha.
Na miongoni mwa watu wapo ambao hununua maneno ya uwongo wawasimulie watu wapate kuwatenga na Uislamu na Qur'ani kwa kutojua dhambi zilio juu yao, na wanaifanyia maskhara Dini ya Mwenyezi Mungu na Ufunuo wake. Watendayo hayo watapata adhabu ya kuwatia unyonge na kuwadhalilisha.
Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata adhabu chungu.
Na mpotovu kama huyu akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu huzipuuza kwa kiburi. Hali yake kwa haya ni hali ya ambaye hasikii, kama kwamba ana uziwi katika masikio yake. Basi mwonye kuwa hakika Mwenyezi Mungu amemuandalia adhabu yenye machungu makali.
Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Watabaki humo daima dawamu; Mwenyezi Mungu amewaahidi ahadi isiyo vunjika. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mshindi wa kila kitu, Mwenye hikima katika maneno yake na vitendo vyake.
Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.
Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu zisio na nguzo za nyinyi kuziona. Na juu ya ardhi ameweka milima iliyo simama imara, ili ardhi isikutingisheni. Na humo katika ardhi ametawanya kila namna ya wanyama wanao tambaa na kwenda. Na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha mimea ya kila namna nzuri yenye manufaa katika ardhi. Rejea uangalie maelezo ya kisayansi juu ya Aya 2, Sura ya Ar-Raa'd.
Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo dhaahiri.
Hivi viumbe vya Mwenyezi Mungu vipo mbele yenu, basi hebu nionyesheni walicho umba hao mnao wafanya ni miungu badala yake Yeye hata wawe ni washirika wake! Bali madhaalimu - kwa ushirikina wao - wamo katika upotovu ulio wazi.
Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu. Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliye kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.
Na hakika tulimpa Luqman hikima, na ilimu, na kauli ya kusibu. Tulimwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema aliyo kupa. Na mwenye kushukuru basi hakika huyo anaitafutia kheri nafsi yake. Na mwenye kuzikufuru neema, akazikataa, na asishukuru kwa ajili yake, basi kwa hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuihitaji shukra yake, na Yeye Mwenyezi Mungu ni Mwenye kustahiki sifa zote njema, na ingawa pasiwepo hata mmoja wa kumsifu.
Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa.
Taja pale Luqman alipo mwambia mwanawe: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu na yeyote. Hakika kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni dhulma kubwa, kuwaweka sawa Mwenye kustahiki na asiye stahiki. Waarabu walikuwa wanawajua watu wawili kwa jina hili. Mmoja wapo ni Luqman bin A'adi. Nao walikuwa wakimtukuza cheo kwa werevu wake, uraisi, ujuzi, ufasihi na ujanja. Na walikithiri sana kumtaja na kumpigia mithali, kama inavyo onekana katika vitabu vya Kiarabu vingi. Ama mwengine ni huyo anaye itwa Luqman Alhakim, (Mwenye hikima), aliye kuwa mashuhuri kwa hikima yake na mifano yake, na ambaye Sura hii ya Qur'ani imeitwa kwa jina lake. Na hikima zake zilikuwa zimeenea kwa Waarabu. Ibn Hisham amesimulia kwamba Suwaid bin Ass'amit alifika Makka. Naye alikuwa mtu mtukufu kwa watu wake. Mtume s.a.w. akamtaka asilimu. Suwaid akasema: Huenda labda uliyo nayo wewe ndiyo kama niliyo nayo mimi. Mtume s.a.w. akasema: Nini ulicho nacho? Akasema: Majalla ya Luqman. Mtume s.a.w. akasema: Nisomee. Akamsomea. Tena akasema: Hakika haya maneno mazuri. Na niliyo nayo mimi ni bora zaidi, nayo ni Qur'ani aliyo niteremshia Mwenyezi Mungu, nayo ni Uwongofu na Nuru. Mtume s.a.w. akamsomea Qur'ani na akamtaka asilimu. Na pia Imam Malik ametaja kwa wingi hikima za Luqman katika kitabu chake, Al Muwatt'a. Na baadhi ya vitabu vya Tafsiri ya Qur'ani na Adab (maandishi ya ufasihi wa lugha) vimetaja namna mbali mbali katika hikima hizo. Kisha baadae ikakusanywa mithali kwa visa katika kitabu chenye jina la Mithali za Luqman. Lakini kwa sababu ya udhaifu wa mpango wake, na wingi wa makosa ya nahau na sarfu, na kuwa kutopokewa kitabu cha jina hili katika vitabu vya Waarabu wa kale, yatilia nguvu kuwa hichi kimezuliwa tu katika zama za mwisho. Na maoni yanayo gongana juu ya uhakika wa Luqman Al-hakim: ni kuwa yeye ni Mnubi katika watu wa Abla au Uhabeshi, au mtu mweusi wa Sudan ya Misri, au ni Muibrani. Na wengi walio mtaja wanakubaliana kuwa hakuwa Nabii. Wachache tu ndio wanasema kuwa alikuwa Nabii. Na tunalo weza kutambua katika yaliyo tajwa ni kuwa hakuwa Mwaarabu, kwa sababu wote wamewafikiana kwa hayo. Na kwamba alikuwa ni mtu mwenye hikima, na hakuwa Nabii, na kwamba ameingiza miongoni mwa Waarabu hikima mpya zikawa zinatajwa mara nyingi kama ilivyo onekana baadae katika vitabu.
Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.
Na tumemuamrisha mtu awafanyie wema wazazi wake, na mama yake ampe fungu kubwa zaidi. Kwani yeye alimbeba katika mimba kwa udhaifu unao zidi kila siku kidogo kidogo. Na tena kamnyonyesha muda wa miaka miwili ndipo alipo muachisha ziwa. Na tumemuusia: Mshukuru Mwenyezi Mungu na wazazi wako. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo kwa ajili ya hisabu na malipo.
Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
Na ikiwa wazazi wako wakikushikilia kwa juhudi umshirikishe Mwenyezi Mungu na vitu usivyo vijua kuwa vinastahiki kuabudiwa, basi usiwakubalie. Lakini endelea na kusuhubiana nao duniani kwa wema na ihsani. Na fuata njia ya wanao rejea kwangu kwa Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, na Ikhlasi, usafi wa niya na vitendo. Kisha nyote mtarejea kwangu, na nitakupeni khabari ya mliyo kuwa mkiyatenda, ya kheri na shari, ili nipate kukulipeni kwayo.
Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote.
Ewe mwanangu! Hakika wema au ubaya kwa mtu, hata ukiwa, mathalan, kwa udogo wake kama chembe ya khardali, iliyoko pahali palipo fichikana kabisa, kama ndani ya jabali, au ndani ya mbingu, au chini ya ardhi, Mwenyezi Mungu ataufichua na autolee hisabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, hakifichikani kitu hata kidogo kwake, ni Mwenye khabari ya kujua hakika ya kila kitu.
Ewe mwanangu! Shika Swala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.
Ewe mwanangu! Zihifadhi Swala, na amrisha kila wema, na kataza kila baya, na stahamili kwa shida zinazo kusibu. Hakika anayo usia Mwenyezi Mungu ni katika mambo ambayo yanahitajia kufanyiwa hima na kuyashikilia.
Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha.
Wala usiwageuzie watu uso wako kwa takaburi, wala usitembee katika nchi kwa kujiona na majivuno. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kuringa na kujiona.
Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda.
Na nenda mwendo wa wastani, si mbio mbio mno wala taratibu mno. Na teremsha sauti yako. Kwani hapana sauti mbaya kama sauti ya punda. Inaanzia kwa mngurumo unao ghasi, na inaishia kwa ukenje unao kera.
Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni viliomo mbinguni na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na za siri? Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
Mmeona kwamba Mwenyezi Mungu amekudhalilishieni viliomo mbinguni kama jua, na mwezi, na nyota na vyenginevyo; na viliomo katika ardhi, kama mito, na matunda, na wanyama. Naye amekutimizieni neema zake zilio dhaahiri na zilio sitirika, msizo ziona. Na miongoni mwa watu, wapo wanao jadiliana juu ya dhati ya Mwenyezi Mungu na sifa zake bila ya dalili wala uwongozi ulio pokewa kutokana na Nabii au Wahyi (ufunuo) wenye kumurika kwa mwangaza njia ya Haki.
Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani anawaita kwenye adhabu ya Moto uwakao?
Na pindi wakiambiwa: Fuateni Haki na Uwongofu alio uteremsha Mwenyezi Mungu, wao husema: Bali sisi tunafuata tuliyo wakuta nao baba zetu. Je! Wanawafuata hao, ijapo kuwa Shetani ndio anawaitia wende kwenye upotovu utakao waingizia Motoni?
Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa anafanya wema, basi huyo hakika amekwisha kamata fundo lilio madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyezi Mungu.
Na mwenye kumuelekea Mwenyezi Mungu kwa moyo wake na uso wake, na akamwakilisha Yeye mambo yake yote, naye akawa ni mwenye kutenda vitendo vyema, basi amefungamana na sababu za nguvu kabisa za kumfikisha kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu. Na kwake Yeye, Subhanahu, ndio marejeo ya mambo yote.
Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio yao, na hapo tutawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
Na asiye mtakasia Mwenyezi Mungu dhati yake na nafsi yake, basi usikuhuzunishe upinzani wake na mapuuza yake. Kwetu Sisi peke yetu ndio marejeo yao Siku ya Kiyama. Hapo tutawaonyesha vitendo vyao. Kwani Sisi tumezunguka kwa kuvijua viliomo ndani ya nafsi zao, seuze vitendo vyao vya dhaahiri.
Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
Ewe Nabii! Nakuapia ya kuwa ukiwauliza: Nani aliye umba mbingu na ardhi? Hapana shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, aliye ziweka dalili za Upweke wake hata zikaubomoa ushirikina wao wa kumshirikisha na wenginewe katika ibada. Na lakini wengi wao hawajui ya kuwa kwa kukiri kwao huku, basi wamesimamisha hoja ya kuwapinga wenyewe kwa ubovu wa itikadi yao.
Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
Viliomo katika mbingu na ardhi ni vya Mwenyezi Mungu, kwa kuviumba, na kuvikadiria, na kuvipanga. Basi vipi wao wanaacha kumuabudu Yeye? Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika si mhitaji wa viumbe vyake wala ibada yao. Yeye ni Msifiwa kwa dhati yake. Ni mwenye kustahiki kusifiwa na waja wake.
Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Na lau kuwa miti yote ya duniani ikageuka kalamu, na maji yote ya baharini kwa wingi wake yakageuka wino, kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu, basi zingeli kwisha kalamu na wino ukamalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mwenyezi Mungu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, hashindwi na chochote, Mwenye hikima hakimfutu kitu katika ujuzi wake na hikima yake. Basi hayeshi maneno yake na hikima yake.
Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi moja tu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
Kukuumbeni nyinyi hapo mwanzo na kukufufueni baada ya kufa, mbele ya uweza wa Mwenyezi Mungu si chochote ila ni kama kumuumba na kumfufua mtu mmoja tu. Hakika Mwenyezi Mungu anaisikia kauli ya washirikina wanapo sema ati: Hakuna kufufuliwa. Naye ni Mwenye kuviona vitendo vyao, naye atawalipa kwavyo.
Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na amedhalilisha jua na mwezi? Vyote hivyo vinakwenda mpaka wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Je! Huangalii, ewe mwenye jukumu, kwa maangalio ya mwenye kuzingatia, ya kwamba hakika Mwenyezi Mungu huupunguza wakati wa usiku kwa kadri ya anavyo uongeza mchana? Na anaupunguza mchana kwa kadri ya anavyo uzidisha usiku? Naye amedhalilisha jua na mwezi kwa ajili ya maslaha yenu, na amefanya hayo yafuate mpango wa peke yao. Basi kila moja katika hayo huenda katika njia maalumu ya mbinguni wala haigeuki. Na mwendo huo unaendelea mpaka Siku ya Kiyama. Na hakika Yeye, Subhanahu, anazo khabari za yote myatendayo, na ni Mwenye kukulipeni kwayo.
Hivi ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na hakika wanacho kiomba ni cha uwongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mtukufu na ndiye Mkubwa.
Hayo yaliyo tajwa ni katika ajabu za uundaji wa Mwenyezi Mungu na uweza wake, kwa sababu muundaji wake ni Mungu aliye thibiti Ungu wake, Mwenye kustahiki peke yake kuabudiwa, na kwamba miungu yote mnayo iabudu badala yake ni miungu ya uwongo. Na hakika Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye Mtukufu wa shani, Mkubwa wa utawala.
Kwani huoni kwamba marikebu hupita baharini zikichukua neema za Mwenyezi Mungu, ili kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake? Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru.
Ewe mtu! Huzitazami marikebu, vyombo vinavyo kwenda baharini kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, vikichukua ndani yake bidhaa za kukupeni manufaa, ili Mwenyezi Mungu akuonyesheni baadhi ya maajabu ya uundaji wake, na dalili za uweza wake? Hakika katika hayo zimo Ishara kwa kila mwenye kuvumilia mitihani yake, mwenye kuzishukuru kwa neema zake.
Na wimbi linapo wafunika kama wingu, wao humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo baadhi yao huenda mwendo wa sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini kafiri mkubwa.
Hawa makafiri wanao mkataa Mwenyezi Mungu wakipanda marikebu, na bahari ikawachafukia, na mawimbi yakaja juu mpaka wakaona yatawafunika, na wakawa yakini watazama bila ya muhali, humkimbilia Mwenyezi Mungu, wakimwomba kwa ikhlasi na unyenyekevu, awaokoe. Basi akisha waokoa wakafika nchi kavu wapo kati yao wachache wanao kumbuka ahadi yao, na wakenda mwendo wa sawa. Na wapo kati yao, nao ndio wengi, walio sahau fadhila za Mola wao Mlezi, na wakaendelea na kumkataa. Na wala hakatai fadhila za Mola wake Mlezi na hisani yake ila kila mtu aliye mwingi wa ukhaini, aliye pita mpaka kumkanya Mola wake Mlezi.
Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi Mungu mdanganyifu.
Enyi watu! Fanyeni aliyo kuamrisheni Mola wenu Mlezi, na wacheni aliyo kukatazeni. Na tahadharini na adhabu yake ya Siku ya Kiyama, Siku ambayo kwamba mzazi hatamfaa mwanawe kwa lolote, wala mwana hatamfaa mzazi wake kwa lolote. Hakika Siku hii ndiyo aliyo iahidi Mwenyezi Mungu. Na ahadi yake ni ya kweli, hayendi kinyume. Basi yasikupumbazeni mapambo ya dunia na uzuri wake, mkaacha kujitayarisha kwa ajili ya Siku hiyo. Wala msikhadaike na uchochezi wa Shetani, ukakuachisheni kumuelekea Mwenyezi Mungu na kumt'ii.
Hakika kuijua Saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye anaye iteremsha mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.
Hakika ujuzi wa Saa ya Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu umethibiti. Basi hapana anaye ijua isipo kuwa Yeye tu. Na Yeye huteremsha mvua kwa wakati wake alio uweka. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi, kama wanaume, au wanawake, hivyo viliomo vimetimia au havikutimia mimba. Wala hapana mtu ajuaye, mwema na muovu, atapata nini kesho, kama kheri au shari. Wala hapana mtu ajuaye pahala gani duniani itamfika ajali yake ya kufa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye timia ujuzi wake na kuwa na khabari ya kila kitu. Wala hapana yeyote awezae kujua siri yake.
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
Risultati della ricerca:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".