Kabla yake, viwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha Furqani (Upambanuo). Hakika, wale waliozikufuru Ishara za Mwenyezi Mungu wana adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, na Mwenye kulipiza.
eye ndiye aliyeteremsha juu yako Kitabu hiki. Ndani yake zimo Aya muhkam (zenye maana wazi). Hizo ndizo msingi wa Kitabu hiki. Na zimo nyingine Mutashabihat (zenye maana zisizo wazi). Ama wale ambao katika nyoyo zao umo upotovu, wao wanafuata zile zenye maana zisizo wazi kwa kutafuta fitina, na kutafuta maana yake. Na wala hapana ajuaye maana yake isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na wale waliokita katika elimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki (hayo) isipokuwa wenye akili.
Kama ada ya watu wa Firauni na wale waliokuwa kabla yao. Walikadhibisha Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu akawachukua kwa dhambi zao; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Hakika, mlikuwa na Ishara katika yale makundi mawili yalipokutaka (katika vita). Kundi moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, nalo lingine kafiri likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono amtakaye kwa nusura yake. Hakika, katika hayo kuna mazingatio kwa wenye macho.
Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundo mingi ya dhahabu na fedha, na farasi wazuri zaidi, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani, na Mwenyezi Mungu ana marejeo mazuri.
Sema: Je, niwaambie yaliyo bora kuliko hayo? Kwa waliomcha Mungu kwa Mola wao Mlezi ziko Bustani zipitazo mito chini yake. Watadumu humo, na wake waliotakaswa, na radhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.
Mwenyezi Mungu alishuhudia kuwa hakika hapana mungu isipokuwa
Yeye, na pia (walishuhudia) Malaika, na wenye elimu akisimamisha uadilifu. Hapana mungu isipokuwa Yeye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Hakika, Dini kwa Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na hawakuhitalifiana wale waliopewa Kitabu isipokuwa baada ya kuwajia na elimu, kwa sababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na mwenye kuzikufuru Ishara za Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.
Na wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso wangu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na vile vile walionifuata. Na waambie wale waliopewa Kitabu na wale wasiojua kusoma: Je, mmesilimu? Wakisilimu, basi hakika wameongoka. Na wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.
Hakika, wale wanaozikufuru Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawaua Manabii bila ya haki, na wakawaua wale wanaoamrisha haki katika watu, basi wabashirie adhabu kali.
Je, huwaoni wale waliopewa fungu katika Kitabu? Wanaitwa kukiendea Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kihukumu baina yao; kisha kundi miongoni mwao wanageuka huku wamepeana mgongo.
Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye mmiliki wa ufalme wote! Wewe humpa ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye. Na humtukuza umtakaye, na humdhalilisha umtakaye. Heri yote iko mkononi mwako. Hakika, Wewe ni Muweza wa kila kitu.
Wewe huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku. Na humtoa hai kutokana na maiti, na humtoa maiti kutokana na aliye hai. Na unamruzuku umtakaye bila ya hesabu.
Waumini wasiwafanye makafiri kuwa marafiki wa kuwasaidia badala ya Waumini. Na mwenye kufanya hilo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Isipokuwa ikiwa kwa ajili ya kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anawahadharisha naye mwenyewe. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.
Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au akiyaweka wazi, Mwenyezi Mungu anayajua. Na anayajua yaliyo katika mbingu na yaliyo katika dunia. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza mno wa kila kitu.
Siku ambayo kila nafsi itakuta iliyofanya katika mema yamehudhurishwa, na pia iliofanya katika ubaya. Itapenda lau baina ya hayo (mabaya) na yeye ungekuwepo umbali mrefu. Na Mwenyezi Mungu anawatadharisha na yeye mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atawapenda na atawafutia dhambi zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
Aliposema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi, nimekuwekea nadhiri kilicho katika tumbo langu la uzazi awe mtumishi wako, basi nikubalie. Hakika, Wewe ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Basi alipomzaa, akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi, nimemzaa wa kike - na Mwenyezi Mungu anajua sana aliyemzaa. -Na wa kiume si sawa na wa kike. Na mimi kwa hakika nimemwita Mariam. Nami kwa hakika ninamkinga kwako, yeye na dhuria yake kutokana na Shetani aliyelaaniwa.
Basi Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya alipoingia chumbani kwake, alimkuta na vyakula. Basi alisema: Ewe Mariam! Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika, Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hesabu.
Kwa hivyo, Malaika wakamwita hali ya kuwa amesimama katika chumba akisali kwamba: Mwenyezi Mungu anakupa bishara njema ya Yahya, atakayesadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na ni bwana, na mtawa, na ni Nabii miongoni mwa walio wema.
Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema: Alama yako ni kuwa hutasema na watu kwa siku tatu, isipokuwa kwa kuashiria tu. Na mtaje Mola wako Mlezi kwa wingi, na mtakase jioni na asubuhi.
Hizi ni katika habari za ghaibu tunazokufunulia. Nawe hukuwa nao walipokuwa wakitupa kalamu zao ni nani wao atakayemlea Maryam? Na hukuwa nao walipokuwa wakizozana.
Pale Malaika waliposema: Ewe Maryam! Hakika, Mwenyezi Mungu anakupa bishara njema ya (mwana kwa) neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryam, mwenye heshima katika dunia na Akhera, na ni miongoni mwa waliowekwa karibu (na Mwenyezi Mungu).
Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi kwa hakika nimewajia na Ishara kutoka kwa Mola wenu Mlezi, ya kwamba mimi kwa hakika ninawaundia kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha ninapuliza ndani yake na anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaambia mnachokila na mnachoweka akiba katika nyumba zenu. Hakika, katika haya ipo Ishara kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.
Na ninasadikisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ili niwahalalishie baadhi ya yale mliyoharimishiwa. Na nimewajia na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo, mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi.
Isa alipohisi ukafiri miongoni mwao, akasema: Ni nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu.
Pale Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa! Mimi nitakuchukua, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa kutokana na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha kwangu ndiko marejeo yenu, na nihukumu kati yenu katika yale mliyokuwa mkihitalifiana.
Basi mwenye kukuhoji katika haya baada ya yale yaliyokufikia katika elimu hii, waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote. Wala tusifanyane waungu sisi kwa sisi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi kwa hakika ni Waislamu.
Na kilisema kikundi kimoja katika Watu wa Kitabu: Yaaminini yale waliyoteremshiwa wale walioamini mwanzo wa mchana, na yakufuruni mwisho wake; huenda wakarejea.
Wala msimuamini isipokuwa yule anayeifuata dini yenu. Sema: Hakika uwongofu ni uwongofu wa Mwenyezi Mungu, kuwa apewe mtu mfano wa mliopewa nyinyi au wawahoji mbele ya Mola wenu Mlezi. Sema: Hakika fadhila zimo mkononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa hizo amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
Na miongoni mwa Watu wa Kitabu yupo ambaye ukimpa amana ya mrundo wa mali, atakurudishia. Na miongoni mwao yupo ambaye ukimpa amana ya dinari moja, hakurudishii isipokuwa ukimsimamia kumdai. Haya ni kwa kuwa walisema: Hatuna lawama kwa ajili ya hawa wasiojua kusoma na kuandika. Na wanasema uongo juu ya Mwenyezi Mungu hali ya kuwa wanajua.
Hakika, wale wanaouza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao kwa thamani ndogo, hao hawatakuwa na fungu lolote katika Akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema nao, wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao wana adhabu chungu.
Na hakika wapo miongoni mwao kundi lipindualo ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Nao husema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wala hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wanasema uongo juu ya Mwenyezi Mungu hali ya kuwa wanajua.
Haikumfailia mtu yeyote kwamba Mwenyezi Mungu ampe Kitabu na hekima na Unabii, kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola Mlezi wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma.
Na pale Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi za Manabii: Nikishawapa Kitabu na hekima, kisha akawajia Mtume mwenye kusadikisha yale mliyo nayo, basi hakika mtamuamini na mtamsaidia. Akasema: Je, mmekiri na mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: Basi shuhudieni, na Mimi ni pamoja nanyi katika wanaoshuhudia.
Je, wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu, ilhali kila kilicho katika mbingu na katika ardhi kimejisalimisha kwake kwa kumtii Yeye kwa kupenda na kwa kutopenda, na kwake Yeye watarejeshwa?
Sema: Tumemwamini Mwenyezi Mungu, na yale tuliyoteremshiwa sisi, na yale yaliyoteremshwa kwa Ibrahim, na Ismail, na Is-haak na Yaakub na wana wake, na yale aliyopewa Musa na Isa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi. Hatutofautishi yeyote baina yao, na sisi ni wenye kujisalimisha kwake.
Vipi Mwenyezi Mungu atawaongoa kaumu waliokufuru baada ya kuamini kwao, na wakashuhudia ya kuwa Mtume huyu ni wa haki, na zikawajia hoja zilizo wazi? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu ya madhaalimu.
Hakika, wale waliokufuru, na wakafa hali ya kuwa ni makafiri, haitakubaliwa kutoka kwa yeyote wao fidia ya dhahabu ya kujaza dunia nzima lau wangeliitoa. Hao wana adhabu chungu, wala hawatakuwa na wowote wa kuwanusuru.
Kila chakula kilikuwa halali kwa Wana wa Israili isipokuwa kile alichojiharamishia Israili mwenyewe kabla ya kuteremshwa Taurati. Sema: Ileteni Taurati, na muisome ikiwa nyinyi ni wakweli.
Ndani yake kuna Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibrahim. Na mwenye kuingia humo, anakuwa na amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewawajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezaye njia ya kuiendea. Na atakayekufuru, basi hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu.
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnamzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu aliyeamini mkiitakia ipotoke, ilhali nyinyi mnashuhudia? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayoyatenda.
Na vipi mkufuru hali ya kuwa nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu, na Mtume wake yuko miongoni mwenu? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu, basi huyo hakika ameongolewa kwenye Njia iliyonyooka.
Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msitengane. Na ikumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu: mlipokuwa maadui nyinyi kwa nyinyi, naye akaziunganisha nyoyo zenu; na kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa kwenye ukingo wa shimo la Moto, naye akawaokoa kutokana nalo. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Ishara zake ili mpate kuongoka.
Na uwepo umma miongoni mwenu wanaoilingania heri, na wanaamrisha mema na wanakataza maovu. Na hao ndio waliofaulu.[1]
[1] Watu katika kubadilisha maovu na kuamrisha mema wako katika daraja tatu: 1. Kilicho lazima juu ya wanachuoni ni kuwatanabahisha viongozi na watawala, na kuwahimiza kwenye njia ya elimu. 2. Na kinachowalazimu watawala ni kuyabadilisha kwa nguvu zao na mamlaka yao. 3. Na kinachowalazimu watu waliosalia ni kuwajulisha viongozi na watawala baada ya wao kuyakataza kwa kauli. (Tafsir Ibn Attwiyya)
Siku zitakapokuwa nyuso nyeupe, na nyuso nyingine zikawa nyeusi. Basi, ama wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi (wataambiwa): Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi ionjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.
Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu waliamini, ingelikuwa bora kwao. Miongoni mwao wako Waumini, lakini wengi wao ni wapotovu.
Umepigwa udhalilifu juu yao popote wanapokutwa, isipokuwa kwa kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu. Na walirudi na ghadhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na unyonge umepigwa juu yao. Hayo ni kwa sababu walikuwa wakizikufuru Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakiwaua Manabii bila ya haki. Hayo ni kwa sababu waliasi na walikuwa wakiruka mipaka.
Wanamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaamrisha mema na wanakataza maovu, na wanakimbilia katika mambo ya heri. Na hao wako miongoni mwa walio wema.
Mfano wa vile wanavyovitoa katika uhai wao wa duniani ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalipiga shamba la kaumu waliozidhulumu nafsi zao, basi ukaliharibu. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, bali wao wenyewe wanazidhulumu nafsi zao.
Enyi mlioamini! Msiwafanye wandani wenu kuwa watu wasiokuwa katika nyinyi. Hawataacha kuwafikishia lolote la kuwadhuru. Wanapenda mngepata taabu. Imekwisha dhihirika chuki yao kutoka katika midomo yao. Na yanayofichwa na vifua vyao ni makubwazaidi.
Tumekwisha wabainishia Ishara ikiwa nyinyi mnatumia akili.
Nyinyi ndio hawa mnawapenda watu hao, wala wao hawawapendi. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapokutana nanyi husema: Tumeamini. Na wanapokuwa peke yao, wanawaumia vidole kwa chuki. Sema: Kufeni na chuki yenu! Hakika, Mwenyezi Mungu anayajua yale yaliyo katika vifua.
Ikiwagusa heri, inawawia vibaya. Na ikiwapata shari, wanaifurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkamcha Mwenyezi Mungu, havitawadhuru kitu vitimbi vyao. Hakika, Mwenyezi Mungu ameyazunguka yote wayatendayo.
Makundi mawili miongoni mwenu yalipoingiwa na woga kuwa watashindwa - na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wao. Na kwa Mwenyezi Mungu tu, na wategemee Waumini.
Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamcha Mungu, na hata maadui wakiwajia mara hii, basi hapo Mola wenu Mlezi atawasaidia kwa Malaika elfu tano wenye alama maalumu.
Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya isipokuwa iwe ni bishara kwenu, na ili nyoyo zenu zipate kutua kwa hilo. Na nusura haitoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu, Mwenye hekima.
Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Yeye humfutia dhambi amtakaye na humwadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
Wale ambao hutoa wanapokuwa katika nyakati nzuri na wanapokuwa katika dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
Na wale ambao wanapofanya uchafu au wakazidhulumu nafsi zao, humkumbuka Mwenyezi Mungu; basi wanamwomba kufutiwa dhambi zao. Na ni nani anayefuta dhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu? Na wala hawaendelei na waliyoyafanya na hali ya kuwa wanajua.
Hao malipo yao ni kufutiwa dhambi kutoka kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito chini yake. Humo watadumu, na bora zaidi ni ujira wa watendao (wema).[1]
[1] Neno "hao" limetumika kuashiria kwamba, wako mbali sana na wasiokuwa wao kwa sababu wako kwenye vyeo vya mbali zaidi, na daraja za juu zaidi katika ubora. (Tafsir Abi Su'ud)
Ikiwa mtaguswa na majeraha, basi kwa hakika hao watu wengine walikwisha patwa na majeraha mfano wake. Na siku za namna hii tunawaletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awajue wale walioamini na awateue miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalim.
Na Muhammad si isipokuwa Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akiuawa, mtageuka mrudi kwa visigino vyenu? Na atakayegeuka akarudi kwa visigino vyake, basi huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaoshukuru.
Na haikuwa kwa nafsi kufa isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyoandikiwa muda wake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani, tutampa kwayo. Na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa kwayo. Na tutawalipa wenye kushukuru.
Na ni Manabii wangapi waliopigana vita pamoja nao Waumini wenye ikhlasi wengi! Na hawakulegea kwa yaliyowapata katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakusalimu amri. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanaosubiri.
Na haikuwa kauli yao isipokuwa walisema: Mola wetu Mlezi! Tufutie dhambi zetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe imara miguu yetu na utunusuru dhidi ya kaumu ya makafiri.
Tutatia hofu katika nyoyo za wale waliokufuru kwa vile walivyomshirikisha Mwenyezi Mungu na yale ambayo hakuyateremshia hoja yoyote. Na makazi yao ni Motoni. Na maovu mno ni maskani ya wenye kudhulumu!
Na Mwenyezi Mungu aliwatimilizia ahadi yake, vile mlivyokuwa mnawaua kwa idhini yake, mpaka mlipolegea na mkazozana katika amri hii, na mkaasi baada ya Yeye kuwaonyesha yale mnayoyapenda. Wapo miongoni mwenu wanaotaka dunia, na wapo miongoni mwenu wanaotaka Akhera. Kisha akawatenga nao (maadui) ili awajaribu. Naye sasa amekwisha wasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya Waumini.
Pale mlipokuwa mkikimbia mbio, wala hamumsikilizi yeyote, na Mtume anawaita, yuko nyuma yenu. Basi Mwenyezi Mungu akawapa dhiki juu ya dhiki, ili msisikitike kwa yale yaliyowakosa wala kwa yale yaliyowapata. Na Mwenyezi Mungu ana habari za yote mnayoyatenda.
Kisha baada ya dhiki aliwateremshia utulivu - usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jingine nafsi zao ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyokuwa ya haki, dhana ya kijinga. Wakisema: Je, sisi tuna lolote katika jambo hili? Sema: Jambo hili lote ni la Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyokudhihirishia. Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili, tusingeulia papa hapa. Sema: Hata mngelikuwa majumbani mwenu, basi wangelitoka wale walioandikiwa kufa, wakaenda mahali pao pa kuangukia wafe. (Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyo katika vifua vyenu, na asafishe yaliyo katika nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani.
Hakika, wale waliogeuka wakakimbia miongoni mwenu siku yalipokutana makundi mawili, hakika Shetani tu ndiye aliyewatelezesha kwa sababu ya baadhi ya makosa waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mpole.
Enyi mlioamini! Msiwe kama wale waliokufuru na wakawaambia ndugu zao wanaposafiri katika nchi au wanapokuwa vitani: Lau wangelikuwa nasi, wasingelikufa na wasingeliuwawa. Ili Mwenyezi Mungu afanye hayo kuwa ni majuto makubwa katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu huhuisha na hufisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayoyatenda.
Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndiyo umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee kufutiwa dhambi, na shauriana nao katika mambo. Na ukishakata shauri, basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaomtegemea.
Akiwanusuru (nyinyi) Mwenyezi Mungu, hapana wa kuwashinda. Na asipowasaidia, basi ni nani huyo baada yake atayewanusuru? Na kwa Mwenyezi Mungu tu, basi na wategemee Waumini.
Na haikuwa kwa Nabii yeyote kufanya hiyana. Na atakayefanya hiyana, atakuja Siku ya Kiyama na kile alichofanyia hiyana, kisha kila nafsi italipwa kwa iliyoyachuma kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa.
Je, aliyeyafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni kama yule aliyerudi na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makazi yake yakawa Jahannamu? Napo ndipo pahali pabaya mno pa kurejea.
Hakika, Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini alipowaletea Mtume kutoka miongoni mwao wenyewe, anayewasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hekima, ijapokuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi.
Nyinyi mlipopatwa na msiba ambao nyinyi mmekwisha watia mara mbili mfano wake, mkasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo umetoka kwenu wenyewe. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
Na ili awajue wale waliofanya unafiki, walipoambiwa: Njooni mpigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu au lindeni. Wakasema: Tungelijua kuna kupigana vita, bila ya shaka tungeliwafuata. Wao siku ile walikuwa karibu zaidi na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao yasiyokuwa katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema wanayoyaficha.
Wale waliowaambia ndugu zao, na wao wenyewe walikuwa wamekaa: Lau wangelitutii, wasingeliuliwa. Sema: Ziondoleeni nafsi zenu mauti kama nyinyi ni wakweli.
Wanafurahia yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake, na wanawapa bishara wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.
Wale waliomwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya kwisha patwa na majeraha. Kwa waliofanya wema miongoni mwao na wakamcha Mungu, utakuwa ujira mkubwa.
Wale walioambiwa na watu: Hakika, kuna watu wamewakusanyikia, hivyo waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora zaidi wa kutegemewa.
Basi wakarudi na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na fadhila. Hapana baya liliowagusa, na wakafuata yanayomridhisha Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
Hakika, huyo ni Shetani anawatia hofu marafiki zake. Basi msiwaogope. Bali niogopeni Mimi ikiwa nyinyi ni Waumini.[1]
[1] Ilisemwa: Anayeogopa siyo yule anayelia na kupangusa macho yake. Bali anayeogopa ni yule ambaye huacha kile anachoogopa kwamba anaweza adhibiwa juu yake. (Tafsir Al-Qurtubi)
Wala wasikuhuzunishe wale wanaoukimbilia ukafiri. Hakika, hao hawamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee fungu lolote katika Akhera. Na wana adhabu kubwa.
Wala wasidhani kabisa wale wanaokufuru kwamba muhula huu tunaowapa ni heri kwao. Hakika, tunawapa muhula ili wazidishe dhambi. Na wana adhabu ya kudunisha.
Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaacha Waumini katika hali mliyo nayo mpaka apambanue mbaya kutokana na mwema. Na wala hakuwa Mwenyezi Mungu mwenye kuwajulisha mambo ya ghaibu. Lakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume wake amtakaye. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake. Na mkiamini, na mkamcha Mungu, basi mtakuwa na ujira mkubwa.
Wala wasidhani kabisa wale ambao wanafanya ubahili katika aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni heri kwao. Bali hiyo ni shari kwao. Watafungwa shingoni yale waliyoyafanyia ubahili Siku ya Kiyama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ana habari za yote myatendayo.
Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya wale waliosema: Hakika, Mwenyezi Mungu ni fakiri, na sisi ni matajiri. Tutayaandika yale waliyoyasema, na pia kuwaua kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu ya kuunguza.
Waliosema: Hakika, Mwenyezi Mungu alituusia kwamba tusimwamini Mtume yeyote mpaka atujie na kafara inayoliwa na moto. Waambie: Walikujieni Mitume kabla yangu kwa hoja zilizo wazi na kwa hayo mnayosema. Basi kwa nini mliwaua ikiwa nyinyi ni wakweli?
Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Kiyama. Na atakayeepushwa na Moto, na akaingizwa Peponi, basi huyo hakika amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu isipokuwa starehe ya udanganyifu.
Hapana shaka yoyote mtajaribiwa katika mali zenu, na nafsi zenu. Na bila ya shaka yoyote mtasikia udhia mwingi kutoka kwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu na wale walioshirikisha. Na ikiwa mtasubiri na mkamcha Mungu, basi hakika hayo ni katika mambo ya kuazimia.
Na pale Mwenyezi Mungu alipochukua agano la wale waliopewa Kitabu kuwa: Bila shaka mtawabainishia watu, na wala hamtakificha. Lakini wakakitupa nyuma ya migongo yao, na wakanunua kwacho thamani kidogo. Basi ni kiovu mno hicho wanachokinunua.
Kamwe usiwadhanie wale wanaofurahia yale waliyoyafanya, na wakapenda kwamba wasifiwe kwa yale ambayo hawakuyatenda. Basi kamwe usiwadhanie kuwa watasalimika na adhabu. Na wana adhabu chungu.
Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu hali ya kuwa wamesimama, na wakiketi, na ubavuni kwao. Na hutafakari katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka (umetakasika)! Basi tukinge kutokana na adhabu ya Moto.
Mola wetu Mlezi! Hakika, sisi tumemsikia mwitaji akiita kwenye Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; kwa hivyo, tukaamini. Basi tufutie dhambi zetu, na utufunikie makosa yetu, na utufishe pamoja na walio wema.
Basi, Mola wao Mlezi akayakubali maombi yao akayajibu: Hakika Mimi, sipotezi matendo ya mfanya matendo yeyote miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi waliohama, na waliotolewa katika makazi yao, na wakaudhiwa katika Njia yangu, na wakapigana vita, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafunikia makosa yao; na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayopita mito chini yake. Hizo ndizo thawabu zinazotoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake zipo thawabu njema kabisa.
Lakini wale waliomcha Mola wao Mlezi wana Mabustani yanayopita mito chini yake. Watadumu humo. Hayo ni makaribisho yao yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na vilivyo kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa walio wema.
Na hakika, miongoni mwa Watu wa Kitabu wapo wanaomwamini Mwenyezi Mungu na yaliyoteremshwa kwenu na yaliyoteremshwa kwao, wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawanunui kwa Aya za Mwenyezi Mungu thamani ndogo. Hao wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.[1]
[1] Imani yao ilipokuwa ya ujumla (bila ya kutofautisha baina ya Manabii na Vitabu), na ya uhakika, ikawa ni ya manufaa. Kwa hivyo, ikawafanya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Na katika ukamilifu wa kumnyenyekea kwao Mwenyezi Mungu ni kwamba, "hawanunui kwa Aya za Mwenyezi Mungu thamani ndogo." Kwa hivyo, hawaitangulizi dunia mbele ya dini kama walivyofanya watu wa upotovu, ambao wanaficha yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kununua kwayo thamani ndogo. Na wakajua kwamba katika hasara kubwa zaidi ni kutosheka na kilicho duni badala ya dini. (Tafsir Assa'di)
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
تلاش کے نتائج:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".