ترجمة معاني القرآن الكريم - الترجمة السواحلية - علي محسن البرواني * - فهرس التراجم

XML CSV Excel API
تنزيل الملفات يتضمن الموافقة على هذه الشروط والسياسات

ترجمة معاني سورة: الأحقاف   آية:

سورة الأحقاف - Surat Al-Ahqaf

حمٓ
H'A MIM .
Imeanzia Sura hii kwa baadhi ya harufi kama ilivyo ada ya Qur'ani katika Sura kadhaa wa kadhaa.
التفاسير العربية:
تَنزِيلُ ٱلۡكِتَٰبِ مِنَ ٱللَّهِ ٱلۡعَزِيزِ ٱلۡحَكِيمِ
Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Hii Qur'ani imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima katika ayatendayo.
التفاسير العربية:
مَا خَلَقۡنَا ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ وَمَا بَيۡنَهُمَآ إِلَّا بِٱلۡحَقِّ وَأَجَلٖ مُّسَمّٗىۚ وَٱلَّذِينَ كَفَرُواْ عَمَّآ أُنذِرُواْ مُعۡرِضُونَ
Hatukuziumba mbingu na ardhi wala yaliyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda maalumu. Na walio kufuru wanayapuuza yale wanayo onywa.
Hatukuziumba mbingu na ardhi na vyote vilio baina yake ila kufuatana na sharia zilizo thibiti, kwa makusudio yanayo ambatana na hikima, na kwa muda maalumu ambao baada yake utakwisha. Na wale wanao ukataa ukweli huu wanapuuza yale waliyo onywa kwayo, ya kuumbwa kupya siku watakapo fufuliwa watu kwa ajili ya malipo.
التفاسير العربية:
قُلۡ أَرَءَيۡتُم مَّا تَدۡعُونَ مِن دُونِ ٱللَّهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُواْ مِنَ ٱلۡأَرۡضِ أَمۡ لَهُمۡ شِرۡكٞ فِي ٱلسَّمَٰوَٰتِۖ ٱئۡتُونِي بِكِتَٰبٖ مِّن قَبۡلِ هَٰذَآ أَوۡ أَثَٰرَةٖ مِّنۡ عِلۡمٍ إِن كُنتُمۡ صَٰدِقِينَ
Je! Mwawaona wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba nini katika ardhi; au hao wanayo shirika katika mbingu? Nileteeni Kitabu kilicho kuwa kabla ya hiki, au alama yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
Waambie hao wanao muomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu: Hebu nambieni hali ya hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu. Nijuvyeni wameumba nini katika ardhi, au wana ushirika wowote katika mbingu? Nileteeni Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, au mabaki yoyote kutokana na ilimu za watu wa zamani ambayo mnayategemea kwa madai yenu, ikiwa mnasema kweli.
التفاسير العربية:
وَمَنۡ أَضَلُّ مِمَّن يَدۡعُواْ مِن دُونِ ٱللَّهِ مَن لَّا يَسۡتَجِيبُ لَهُۥٓ إِلَىٰ يَوۡمِ ٱلۡقِيَٰمَةِ وَهُمۡ عَن دُعَآئِهِمۡ غَٰفِلُونَ
Na nani mpotofu mkubwa kuliko hao wanao waomba, badala ya Mwenyezi Mungu, ambao hawatawaitikia mpaka Siku ya Kiyama, na wala hawatambui maombi yao.
Na nani aliye zidi kupotea kuliko anaye muacha Mwenyezi Mungu akaiomba miungu mingine ambayo haitamjibu kitu mpaka mwisho wa dunia, na ambao hao hata hawana khabari ya maombi yao.
التفاسير العربية:
وَإِذَا حُشِرَ ٱلنَّاسُ كَانُواْ لَهُمۡ أَعۡدَآءٗ وَكَانُواْ بِعِبَادَتِهِمۡ كَٰفِرِينَ
Na ambao watu watakapo kusanywa watakuwa maadui zao, na wataikataa ibada yao.
Na watu wakikusanywa kwa ajili ya hisabu Siku ya Kiyama hawa wanao abudiwa kwa upotovu watakuwa ndio maadui wa walio kuwa wakiabudu, na watajitenga nao, na kuwakadhibisha kwa madai yao kwamba wao wanastahiki kuabudiwa. (Katika Injili ya Mathayo inasimuliwa wazi vipi Nabii Isa a.s. atavyo wakataa Wakristo wanao muabudu yeye. Tazama Mathayo 7.22-23. Yesu anasema: "Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.")
التفاسير العربية:
وَإِذَا تُتۡلَىٰ عَلَيۡهِمۡ ءَايَٰتُنَا بَيِّنَٰتٖ قَالَ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ لِلۡحَقِّ لَمَّا جَآءَهُمۡ هَٰذَا سِحۡرٞ مُّبِينٌ
Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, walio kufuru husema juu ya haki inapo wajia: Huu ni uchawi dhaahiri.
Na washirikina wakisomewa Aya zetu zilizo wazi wao husema, kwa ule ukafiri wao na inadi yao, bila ya kuzingatia, kuzisema hizo Aya: Huu ni uchawi dhaahiri!
التفاسير العربية:
أَمۡ يَقُولُونَ ٱفۡتَرَىٰهُۖ قُلۡ إِنِ ٱفۡتَرَيۡتُهُۥ فَلَا تَمۡلِكُونَ لِي مِنَ ٱللَّهِ شَيۡـًٔاۖ هُوَ أَعۡلَمُ بِمَا تُفِيضُونَ فِيهِۚ كَفَىٰ بِهِۦ شَهِيدَۢا بَيۡنِي وَبَيۡنَكُمۡۖ وَهُوَ ٱلۡغَفُورُ ٱلرَّحِيمُ
Au wanasema: Ameizua mwenyewe! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi nyinyi hamwezi kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye anajua zaidi hayo mnayo ropokwa; anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Na Yeye ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Bali wanasema hawa makafiri: Muhammad ameizua hii na akamsingizia Mwenyezi Mungu! Sema kuwajibu: Ikiwa mimi nimeizua hii Mwenyezi Mungu atanipatiliza upesi upesi, wala nyinyi hamwezi kunilinda hata kwa chembe ya adhabu. Yeye peke yake ndiye Mwenye kujua kabisa hayo mnayo ropokwa katika kuzitia kombo Aya zake. Na Yeye anatosha kunishuhudia ukweli wangu, na kukushuhudilieni nyinyi kuwa mnanikadhibisha. Na Yeye pekee, ndiye Mkunjufu wa msamaha kwa mwenye kutubu, Mkubwa wa rehema, kwa kuwapa muhula wenye kuasi ili wadiriki kurejea.
التفاسير العربية:
قُلۡ مَا كُنتُ بِدۡعٗا مِّنَ ٱلرُّسُلِ وَمَآ أَدۡرِي مَا يُفۡعَلُ بِي وَلَا بِكُمۡۖ إِنۡ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰٓ إِلَيَّ وَمَآ أَنَا۠ إِلَّا نَذِيرٞ مُّبِينٞ
Mimi si kiroja miongoni mwa Mitume. Wala sijui nitakavyo fanywa wala nyinyi. Mimi nafuata niliyo funuliwa tu kwa Wahyi, wala mimi si chochote ila ni mwonyaji mwenye kudhihirisha wazi.
Waambie: Mimi sikuwa Mtume wa mwanzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hata ndio muukatae ujumbe wangu. Wala mimi sijui Mwenyezi Mungu atanifanya nini na atakufanyeni nini nyinyi. Mimi sifuati ninayo sema au kutenda ila anayo nifunulia Mwenyezi Mungu. Wala mimi si chochote ila ni mwonyaji miongoni mwa waonyaji.
التفاسير العربية:
قُلۡ أَرَءَيۡتُمۡ إِن كَانَ مِنۡ عِندِ ٱللَّهِ وَكَفَرۡتُم بِهِۦ وَشَهِدَ شَاهِدٞ مِّنۢ بَنِيٓ إِسۡرَٰٓءِيلَ عَلَىٰ مِثۡلِهِۦ فَـَٔامَنَ وَٱسۡتَكۡبَرۡتُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَهۡدِي ٱلۡقَوۡمَ ٱلظَّٰلِمِينَ
Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi mmeyakataa, na akashuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya mfano wa haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu.
Sema: Hebu nambieni, ikiwa hii Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu na nyinyi mkaikataa, na hali ameshuhudia shahidi katika Wana wa Israili kuwa imeshuka mfano wa hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akawa yeye kaamini na nyinyi mkatakabari, basi hapo nyinyi si mtakuwa ni wenye kupotea na wenye kujidhulumu wenyewe kuliko watu wote? Hakika Mwenyezi Mungu hamsaidii kuongoka mwenye kujidhulumu mwenyewe na akapanda kiburi kuikataa Haki.
التفاسير العربية:
وَقَالَ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ لِلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَوۡ كَانَ خَيۡرٗا مَّا سَبَقُونَآ إِلَيۡهِۚ وَإِذۡ لَمۡ يَهۡتَدُواْ بِهِۦ فَسَيَقُولُونَ هَٰذَآ إِفۡكٞ قَدِيمٞ
Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Lau kuwa hii ni kheri, wasingeli tutangulia. Na walipo kosa kuongoka wakasema: Huu ni uzushi wa zamani.
Na walio kufuru walisema kuwakhusu walio amini, kwa kejeli na majivuno juu yao: Ingeli kuwa aliyo kuja nayo Muhammad ni ya kheri, basi wasingeli tutangulia hawa katika kuyaamini. Kwani sisi ndio twenye ubwana, na akili bora! Na ilivyo kuwa hawakuyafuata basi wakaangukia kuyatoa kombo, wakisema: Huu ni uwongo wa zamani unatokana na hadithi za watu wa kale!
التفاسير العربية:
وَمِن قَبۡلِهِۦ كِتَٰبُ مُوسَىٰٓ إِمَامٗا وَرَحۡمَةٗۚ وَهَٰذَا كِتَٰبٞ مُّصَدِّقٞ لِّسَانًا عَرَبِيّٗا لِّيُنذِرَ ٱلَّذِينَ ظَلَمُواْ وَبُشۡرَىٰ لِلۡمُحۡسِنِينَ
Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa chenye uwongozi na rehema. Na hichi ni Kitabu cha kusadikisha na kilicho kuja kwa lugha ya Ki./Arabu, ili kiwaonye walio dhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
Na kabla ya Qur'ani Mwenyezi Mungu aliteremsha Taurati kuwa ni uwongozi na rehema kwa wenye kuitenda. Na hii Qur'ani wanayo ikadhibisha inasadikisha Vitabu vilivyo kwisha tangulia. Mwenyezi Mungu ameiteremsha kwa lugha ya Kiarabu iwe ni onyo jipya kwa wenye kudhulumu, na bishara kwa wenye kusimama sawa juu ya Njia.
التفاسير العربية:
إِنَّ ٱلَّذِينَ قَالُواْ رَبُّنَا ٱللَّهُ ثُمَّ ٱسۡتَقَٰمُواْ فَلَا خَوۡفٌ عَلَيۡهِمۡ وَلَا هُمۡ يَحۡزَنُونَ
Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu; kisha wakatengenea, hawatakuwa na khofu, wala hawatahuzunika.
Hakika wanao sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu peke yake, kisha wakatengenea kwa kufanya vitendo vizuri, watu hao hawana khofu ya kushukiwa la karaha, na wala hawatahuzunika kwa kuyakosa wayatakayo.
التفاسير العربية:
أُوْلَٰٓئِكَ أَصۡحَٰبُ ٱلۡجَنَّةِ خَٰلِدِينَ فِيهَا جَزَآءَۢ بِمَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ
Hao ndio watu wa Peponi, watadumu humo, kuwa ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
Hao wanao sifika kwa kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, na kusimama sawa, ndio walio khusika kuingia Peponi wakikaa humo milele. Mwenyezi Mungu amewapa hayo kuwa ni jaza yao kwa mema waliyo kuwa wakiyatenda.
التفاسير العربية:
وَوَصَّيۡنَا ٱلۡإِنسَٰنَ بِوَٰلِدَيۡهِ إِحۡسَٰنًاۖ حَمَلَتۡهُ أُمُّهُۥ كُرۡهٗا وَوَضَعَتۡهُ كُرۡهٗاۖ وَحَمۡلُهُۥ وَفِصَٰلُهُۥ ثَلَٰثُونَ شَهۡرًاۚ حَتَّىٰٓ إِذَا بَلَغَ أَشُدَّهُۥ وَبَلَغَ أَرۡبَعِينَ سَنَةٗ قَالَ رَبِّ أَوۡزِعۡنِيٓ أَنۡ أَشۡكُرَ نِعۡمَتَكَ ٱلَّتِيٓ أَنۡعَمۡتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَٰلِدَيَّ وَأَنۡ أَعۡمَلَ صَٰلِحٗا تَرۡضَىٰهُ وَأَصۡلِحۡ لِي فِي ذُرِّيَّتِيٓۖ إِنِّي تُبۡتُ إِلَيۡكَ وَإِنِّي مِنَ ٱلۡمُسۡلِمِينَ
Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.
Na tumemuusia mwanaadamu kwa wazazi wake awafanyie wema mkubwa. Kwani mama yake amechukua mimba yake kwa mashaka, na akamzaa kwa mashaka. Na muda wa kuchukuliwa mimba mpaka kuachishwa ziwa ni miezi thalathini. Muda wote huo mama kapitikiwa na kila namna ya machungu. Mpaka huyo mtu alipo fikilia ukamilifu wa nguvu zake na akili yake, na akafikia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Nijaalie niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nijaalie nitende vitendo vyema utavyo viridhi Wewe, na ujaalie huo wema wapate pia dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako kwa kila dhambi, na mimi ni miongoni wa Waislamu, yaani walio zisalimisha nafsi zao kwako. Uchache wa mimba ni miezi sita, kwa kauli yake Mtukufu: " Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini." Na kauli yake Mtukufu: "Na kumwachisha ziwa kwake ni miaka miwili", na kauli yake Mtukufu: "Na wazazi wa kike huwanyonyesha wana wao miaka miwili kaamili, kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha." Basi ukitoa muda wa kuachisha ziwa kutokana na muda wa mimba na kunyonyesha inabakia muda wa mimba ni miezi sita. Na haya yanawafikiana na iliyo thibiti kwa ilimu za sayansi kwamba mtoto mchanga akizaliwa baada ya mimba ya miezi 6 anaweza kuishi.
التفاسير العربية:
أُوْلَٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ نَتَقَبَّلُ عَنۡهُمۡ أَحۡسَنَ مَا عَمِلُواْ وَنَتَجَاوَزُ عَن سَيِّـَٔاتِهِمۡ فِيٓ أَصۡحَٰبِ ٱلۡجَنَّةِۖ وَعۡدَ ٱلصِّدۡقِ ٱلَّذِي كَانُواْ يُوعَدُونَ
Hao ndio tunao wapokelea bora ya vitendo vyao walivyo vitenda, na tunayasamehe makosa yao. Watakuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Miadi ya kweli hiyo walio ahidiwa.
Hao walio sifika kwa sifa hizo ndio tutakao wapokelea a'mali zao njema, na tutawasamehe maovu yao miongoni mwa watu wa Peponi. Itawathibitikia miadi ya kweli walio kuwa wakiahidiwa duniani.
التفاسير العربية:
وَٱلَّذِي قَالَ لِوَٰلِدَيۡهِ أُفّٖ لَّكُمَآ أَتَعِدَانِنِيٓ أَنۡ أُخۡرَجَ وَقَدۡ خَلَتِ ٱلۡقُرُونُ مِن قَبۡلِي وَهُمَا يَسۡتَغِيثَانِ ٱللَّهَ وَيۡلَكَ ءَامِنۡ إِنَّ وَعۡدَ ٱللَّهِ حَقّٞ فَيَقُولُ مَا هَٰذَآ إِلَّآ أَسَٰطِيرُ ٱلۡأَوَّلِينَ
Na ambaye amewafyonya wazazi wake na akawaambia: Ati ndio mnanitisha kuwa nitafufuliwa, na hali vizazi vingi vimekwisha pita kabla yangu! Na hao wazazi humwomba msaada Mwenyezi Mungu (na humwambia mtoto wao): Ole wako! Amini! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na yeye husema: Hayakuwa haya ila ni visa vya watu wa kale.
Na waliwafyonya wazazi wao kwa kuchukia na kuchoka nao, walipo wataka waamini kufufuliwa, na wakawaambia: Mnaniambia tutatoka makaburini na mataifa mangapi yamepita kabla yangu na hapana hata mmoja aliye fufuliwa kutoka makaburini? Na hao wazazi wake wanaomba msaada kwa Mwenyezi Mungu jinsi ya kuona ni makuu makosa ya mwana wao, wakisema kwa kumshikilia aamini: Utaangamia wewe kama hukuamini. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kufufua ni kweli. Naye bado amekakamia kukadhibisha kwa kusema: Hayo mnayo yasema si chochote ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale!
التفاسير العربية:
أُوْلَٰٓئِكَ ٱلَّذِينَ حَقَّ عَلَيۡهِمُ ٱلۡقَوۡلُ فِيٓ أُمَمٖ قَدۡ خَلَتۡ مِن قَبۡلِهِم مِّنَ ٱلۡجِنِّ وَٱلۡإِنسِۖ إِنَّهُمۡ كَانُواْ خَٰسِرِينَ
Hao ndio ambao imehakikikishwa hukumu juu yao kama mataifa yaliyo kwisha pita kabla yao miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa wenye kukhasiri.
Hao wasemao hayo ndio iliyo wathibitikia kuwashukia adhabu sawa sawa na mataifa yaliyo kuwa kabla yao miongoni mwa majini na watu, kwa sababu hakika hao walikuwa ni wenye kukhasiri.
التفاسير العربية:
وَلِكُلّٖ دَرَجَٰتٞ مِّمَّا عَمِلُواْۖ وَلِيُوَفِّيَهُمۡ أَعۡمَٰلَهُمۡ وَهُمۡ لَا يُظۡلَمُونَ
Na wote watakuwa na daraja zao mbali mbali kwa waliyo yatenda, na ili awalipe kwa vitendo vyao, na wala hawatadhulumiwa.
Na wote, Waislamu na makafiri, wana vyeo vyao vinavyo lingana na vitendo vyao walivyo vitenda, ili uadilifu wa Mwenyezi Mungu upate kuonekana kati yao, na ili awalipe jaza ya 'amali zao, nao hawatadhulumiwa, kwa sababu wanastahiki hayo wanayo lipwa.
التفاسير العربية:
وَيَوۡمَ يُعۡرَضُ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ عَلَى ٱلنَّارِ أَذۡهَبۡتُمۡ طَيِّبَٰتِكُمۡ فِي حَيَاتِكُمُ ٱلدُّنۡيَا وَٱسۡتَمۡتَعۡتُم بِهَا فَٱلۡيَوۡمَ تُجۡزَوۡنَ عَذَابَ ٱلۡهُونِ بِمَا كُنتُمۡ تَسۡتَكۡبِرُونَ فِي ٱلۡأَرۡضِ بِغَيۡرِ ٱلۡحَقِّ وَبِمَا كُنتُمۡ تَفۡسُقُونَ
Na siku watakapo letwa walio kufuru kwenye Moto wataambiwa: Nyinyi mlitwaa vitu vyenu vizuri katika uhai wa duniani, na mkastareheshwa navyo. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya fedheha kwa mlivyo kuwa mkitakabari katika ardhi bila ya haki, na kwa sababu mlikuwa mkifanya upotovu.
Na siku watakapo simamishwa walio kufuru kwenye Moto waambiwe: Mmekwisha chukua fungu lenu la vitu vizuri katika maisha yenu ya duniani, na mkavionea raha. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya kufedhehesha kwa mliyo kuwa nayo duniani, ya kujivuna katika nchi bila ya haki, na kutoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
التفاسير العربية:
۞ وَٱذۡكُرۡ أَخَا عَادٍ إِذۡ أَنذَرَ قَوۡمَهُۥ بِٱلۡأَحۡقَافِ وَقَدۡ خَلَتِ ٱلنُّذُرُ مِنۢ بَيۡنِ يَدَيۡهِ وَمِنۡ خَلۡفِهِۦٓ أَلَّا تَعۡبُدُوٓاْ إِلَّا ٱللَّهَ إِنِّيٓ أَخَافُ عَلَيۡكُمۡ عَذَابَ يَوۡمٍ عَظِيمٖ
Na mtaje ndugu wa kina A'di, alipo waonya watu wake kwenye vilima vya mchanga. Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake kuwaambia: Msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nakukhofieni isikupateni adhabu ya siku iliyo kuu.
Mtaje Hud, mwenzao kabila ya A'di, alipo wahadharisha watu wake wanao kaa Ah'qaaf, kwenye vilima vya mchanga. Na Mitume kadhaa walikuja kabla yake na baada yake kwa maonyo kama yake ya kusema: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu. Mimi nakukhofieni isikupateni adhabu yenye vitisho vikuu. Maskani ya kabila hii ilikuwa huko Ah'qaaf, kwenye vilima vya mchanga. Na wapi hapo Ah'qaaf? Zipo khitilafu. Baadhi ya wanazuoni wa taarikh (historia) wanasema kuwa hapo ni baina ya Yaman na Oman mpaka Hadhramaut na Shihr, yaani mashariki ya kusini ya Bara Arabu. Na baadhi ya wachunguzi wa zama za karibu wanaona ni mashariki ya A'qaba, wakitegemea maandishi ya Nabat'ia waliyo yakuta katika magofu ya hekalu walilo livumbua katika mlima wa Arim. Walikuta pembezoni mwa mlima huo mabaki ya siku za Jahiliya za zamani. Wakasahihisha kuwa hapo ndipo ilipo Arim iliyo tajwa katika Qur'ani tukufu. Kisha kabila hiyo ikatoka hapo kabla ya Uislamu, na hapana kilicho baki chao isipo kuwa chemchem ya maji ambayo wafanyi biashara na watu wa misafara wakishukia hapo katika njia yao kwendea Shamu.
التفاسير العربية:
قَالُوٓاْ أَجِئۡتَنَا لِتَأۡفِكَنَا عَنۡ ءَالِهَتِنَا فَأۡتِنَا بِمَا تَعِدُنَآ إِن كُنتَ مِنَ ٱلصَّٰدِقِينَ
Wakasema: Je! Umetujia ili ututenge mbali na miungu yetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
Kaumu ya Hud walisema kwa kumkanya: Hivyo ndio umetujia ili utuachishe kuwaabudu miungu yetu? Basi tuletee hiyo adhabu ikiwa wewe hakika ni mwenye kusema kweli kwa ahadi hiyo.
التفاسير العربية:
قَالَ إِنَّمَا ٱلۡعِلۡمُ عِندَ ٱللَّهِ وَأُبَلِّغُكُم مَّآ أُرۡسِلۡتُ بِهِۦ وَلَٰكِنِّيٓ أَرَىٰكُمۡ قَوۡمٗا تَجۡهَلُونَ
Akasema: Hakika ujuzi uko kwa Mwenyezi Mungu. Mimi nakufikishieni niliyo tumwa. Lakini nakuoneni kuwa nyinyi mnafanya ujinga.
Hud akasema: Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujua wakati wa kuileta adhabu yenu. Mimi nafikisha ujumbe tu nilio tumwa. Lakini naona kuwa nyinyi hamjui chochote katika mambo wanayo tumwa Mitume.
التفاسير العربية:
فَلَمَّا رَأَوۡهُ عَارِضٗا مُّسۡتَقۡبِلَ أَوۡدِيَتِهِمۡ قَالُواْ هَٰذَا عَارِضٞ مُّمۡطِرُنَاۚ بَلۡ هُوَ مَا ٱسۡتَعۡجَلۡتُم بِهِۦۖ رِيحٞ فِيهَا عَذَابٌ أَلِيمٞ
Basi walipo liona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili la kutunyeshea mvua! Kumbe sivyo, haya ni hayo mliyo yahimiza, upepo ambao ndani yake imo adhabu chungu!
Ikawajia adhabu kwa sura ya wingu. Walipo liona limetanda kote juu linaelekea mabondeni kwao, walisema kwa furaha: Wingu hili linatuletea mvua na kheri. Wakaambiwa: Bali hilo ni hayo mliyo yahimiza, nayo ni upepo wenye adhabu kali na chungu, itakayo teketeza kila kitu kwa amri ya Muumbaji wake. Nao ukawaangamiza, yasionekane mabaki yao isipo kuwa nyumba zao. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kutenda kama makosa yao.
التفاسير العربية:
تُدَمِّرُ كُلَّ شَيۡءِۭ بِأَمۡرِ رَبِّهَا فَأَصۡبَحُواْ لَا يُرَىٰٓ إِلَّا مَسَٰكِنُهُمۡۚ كَذَٰلِكَ نَجۡزِي ٱلۡقَوۡمَ ٱلۡمُجۡرِمِينَ
Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake Mlezi. Wakawa hawaonekani ila nyumba zao tu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wakosefu!
Itakayo teketeza kila kitu kwa amri ya Muumbaji wake. Nao ukawaangamiza, yasionekane mabaki yao isipo kuwa nyumba zao. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kutenda kama makosa yao.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ مَكَّنَّٰهُمۡ فِيمَآ إِن مَّكَّنَّٰكُمۡ فِيهِ وَجَعَلۡنَا لَهُمۡ سَمۡعٗا وَأَبۡصَٰرٗا وَأَفۡـِٔدَةٗ فَمَآ أَغۡنَىٰ عَنۡهُمۡ سَمۡعُهُمۡ وَلَآ أَبۡصَٰرُهُمۡ وَلَآ أَفۡـِٔدَتُهُم مِّن شَيۡءٍ إِذۡ كَانُواْ يَجۡحَدُونَ بِـَٔايَٰتِ ٱللَّهِ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُواْ بِهِۦ يَسۡتَهۡزِءُونَ
Na bila ya shaka tuliwaweka vizuri sio kama tulivyo kuwekeni nyinyi; na tuliwapa masikio, na macho, na nyoyo. Na hayakuwafaa kitu masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao kwa lolote. Kwani hao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhara ndiyo yakawazunguka.
Na tuliwaweka kabila la A'di kwa nafasi na nguvu sio kama tulivyo kuwekeni nyinyi watu wa Makka. Na tuliwajaalia masikio, na macho, na nyoyo, lau wangeli taka kunafiika kwayo. Lakini hayakuwafaa hata kitu kidogo masikio yao, wala macho yao, wala nyoyo zao, kwa sababu walikuwa wakizikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi hayo yakapinga baina yao na kunafiika kwa waliyo letewa. Na ile ile adhabu waliyo kuwa wakiifanyia maskhara ikawazunguka.
التفاسير العربية:
وَلَقَدۡ أَهۡلَكۡنَا مَا حَوۡلَكُم مِّنَ ٱلۡقُرَىٰ وَصَرَّفۡنَا ٱلۡأٓيَٰتِ لَعَلَّهُمۡ يَرۡجِعُونَ
Na hakika tuliiangamiza miji ilio jirani zenu, na tulizitumia Ishara ili wapate kurejea.
Enyi watu wa Makka! Tumeiangamiza miji iliyo jirani zenu. Na Sisi tuliwawekea wazi dalili namna mbali mbali, ili wapate kurejea waache ukafiri. Hawakurejea.
التفاسير العربية:
فَلَوۡلَا نَصَرَهُمُ ٱلَّذِينَ ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِ ٱللَّهِ قُرۡبَانًا ءَالِهَةَۢۖ بَلۡ ضَلُّواْ عَنۡهُمۡۚ وَذَٰلِكَ إِفۡكُهُمۡ وَمَا كَانُواْ يَفۡتَرُونَ
Basi mbona wale walio washika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa ati hao ndio wawakurubishe, hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na huo ndio uwongo walio kuwa wakiuzua.
Basi kwani hao walio wafanya miungu badala ya Mwenyezi Mungu ili iwakaribishe kwa Mwenyezi Mtukufu imeweza kuwakinga na maangamizo? Hasha! Bali miungu hiyo iliwakimbia, na hali wao ndio wana haja nayo mno iwanusuru. Na hayo yaliyo wafika, ya kutupwa na miungu yao, na kuwapotea ndio matokeo ya uwongo wao na uzushi wao.
التفاسير العربية:
وَإِذۡ صَرَفۡنَآ إِلَيۡكَ نَفَرٗا مِّنَ ٱلۡجِنِّ يَسۡتَمِعُونَ ٱلۡقُرۡءَانَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوٓاْ أَنصِتُواْۖ فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوۡاْ إِلَىٰ قَوۡمِهِم مُّنذِرِينَ
Na wakati tulipo waleta kundi la majini kuja kwako kusikiliza Qur'ani. Basi walipo ihudhuria walisema: Sikilizeni! Na ilipo kwisha somwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya.
Ewe Muhammad! Taja tulipo kuletea kikundi cha majini waje sikiliza Qur'ani. Walipo hudhiria ilipo kuwa ikisomwa, baadhi yao wakawaambia wenzao: Sikilizeni! Ilipo kwisha timia kusomwa wakarudi kwa haraka kwa wenzao, kuwahadharisha na ukafiri, wakiwataka waamini.
التفاسير العربية:
قَالُواْ يَٰقَوۡمَنَآ إِنَّا سَمِعۡنَا كِتَٰبًا أُنزِلَ مِنۢ بَعۡدِ مُوسَىٰ مُصَدِّقٗا لِّمَا بَيۡنَ يَدَيۡهِ يَهۡدِيٓ إِلَى ٱلۡحَقِّ وَإِلَىٰ طَرِيقٖ مُّسۡتَقِيمٖ
Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilicho teremshwa baada ya Musa, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinacho ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Walisema: Enyi watu wetu! Hakika sisi tumekisikia Kitabu chenye shani kubwa. Kimeteremshwa baada ya Musa, na kinasadikisha Vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyo tangulia, kinaongoza kwenye itikadi ya haki, na sharia ya vitendo iliyo simama sawa.
التفاسير العربية:
يَٰقَوۡمَنَآ أَجِيبُواْ دَاعِيَ ٱللَّهِ وَءَامِنُواْ بِهِۦ يَغۡفِرۡ لَكُم مِّن ذُنُوبِكُمۡ وَيُجِرۡكُم مِّنۡ عَذَابٍ أَلِيمٖ
Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu, na muaminini, Mwenyezi Mungu atakusameheni, na atakukingeni na adhabu chungu.
Enyi watu wetu! Muitikieni mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu anaye ongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na msadikini Mwenyezi Mungu akusameheni madhambi yenu yaliyo tangulia, na akulindeni na adhabu kali iliyo chungu.
التفاسير العربية:
وَمَن لَّا يُجِبۡ دَاعِيَ ٱللَّهِ فَلَيۡسَ بِمُعۡجِزٖ فِي ٱلۡأَرۡضِ وَلَيۡسَ لَهُۥ مِن دُونِهِۦٓ أَوۡلِيَآءُۚ أُوْلَٰٓئِكَ فِي ضَلَٰلٖ مُّبِينٍ
Na wasio mwitikia Mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hao hawatashinda katika ardhi, wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhaahiri.
Na asiye muitikia Mwenyezi Mungu basi hawezi kumshinda Mwenyezi Mungu asimtie mkononi hata akikimbia vipi katika ardhi. Na wala hana isipo kuwa Mwenyezi Mungu wa kumnusuru na kumkinga na adhabu yake. Hao wanao puuza wasimwitikie mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu wamo katika ubabaishi na dhaahiri wako mbali na Haki.
التفاسير العربية:
أَوَلَمۡ يَرَوۡاْ أَنَّ ٱللَّهَ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ وَلَمۡ يَعۡيَ بِخَلۡقِهِنَّ بِقَٰدِرٍ عَلَىٰٓ أَن يُحۡـِۧيَ ٱلۡمَوۡتَىٰۚ بَلَىٰٓۚ إِنَّهُۥ عَلَىٰ كُلِّ شَيۡءٖ قَدِيرٞ
Je! Hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliye ziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwani? Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Wameghafilika wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi, na wala hakushindwa kuziumba, ni Muweza wa kuwafufua maiti? Bali Yeye ni Muweza wa hayo, kwani Yeye Mtukufu ana uweza kaamili juu ya kila kitu.
التفاسير العربية:
وَيَوۡمَ يُعۡرَضُ ٱلَّذِينَ كَفَرُواْ عَلَى ٱلنَّارِ أَلَيۡسَ هَٰذَا بِٱلۡحَقِّۖ قَالُواْ بَلَىٰ وَرَبِّنَاۚ قَالَ فَذُوقُواْ ٱلۡعَذَابَ بِمَا كُنتُمۡ تَكۡفُرُونَ
Na siku watakapo letwa makafiri Motoni wakaambiwa: Je! Haya si kweli? Watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, ni kweli! Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya kule kukataa kwenu.
Na siku watakapo simamishwa walio kufuru Motoni wataambiwa kwa kukemewa: Adhabu hii si jambo la kweli linakubaliana na tuliyo kuonyeni nayo duniani? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, haya ni haki kweli. Atasema: Onjeni kila namna ya adhabu kali kwa kushikilia kwenu ukafiri na ukanushi.
التفاسير العربية:
فَٱصۡبِرۡ كَمَا صَبَرَ أُوْلُواْ ٱلۡعَزۡمِ مِنَ ٱلرُّسُلِ وَلَا تَسۡتَعۡجِل لَّهُمۡۚ كَأَنَّهُمۡ يَوۡمَ يَرَوۡنَ مَا يُوعَدُونَ لَمۡ يَلۡبَثُوٓاْ إِلَّا سَاعَةٗ مِّن نَّهَارِۭۚ بَلَٰغٞۚ فَهَلۡ يُهۡلَكُ إِلَّا ٱلۡقَوۡمُ ٱلۡفَٰسِقُونَ
Basi subiri, kama walivyo subiri Mitume wenye stahmala kubwa, wala usiwafanyie haraka. Siku watakayo yaona waliyo ahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa ulimwenguni ila saa moja ya mchana. Huu ndio ufikisho! Kwani huangamizwa wengine isipo kuwa walio waovu tu?
Ewe Muhammad! Wastahamilie makafiri kama walivyo stahamili Mitume wengine wenye nguvu na imara wakati wa shida. Wala usiwahimizie adhabu. Kwani hiyo itawafika tu, hapana hivi wala hivi, hata ikichukua muda mrefu. Siku watapo kiona kitisho chake watadhani kuwa hawakukaa kabla yake ila saa moja tu ya mchana. Haya uliyo watolea waadhi yatosha. Hawataangamizwa kwa adhabu isipo kuwa walio toka kwenye ut'iifu.
التفاسير العربية:
 
ترجمة معاني سورة: الأحقاف
فهرس السور رقم الصفحة
 
ترجمة معاني القرآن الكريم - الترجمة السواحلية - علي محسن البرواني - فهرس التراجم

ترجمة معاني القرآن الكريم إلى اللغة السواحلية، ترجمها علي محسن البرواني.

إغلاق