Hayo hayakuwa ila ni majina mliyo wapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuleta uthibitisho wowote juu ya hayo. Hawafuati ila dhana tu na kipendacho nafsi. Na kwa yakini uwongofu ulikwisha wafikia kutoka kwa Mola wao Mlezi.
Hayo masanamu yenu si chochote ila ni majina tu yasiyo na maana yoyote ya kiungu. Mmeyatunga nyinyi na baba zenu kwa kufuata pumbao lenu la upotovu. Mwenyezi Mungu hakuteremsha nayo hoja yoyote ya kusadikisha huo uzushi wenu mnao wadaia. Na hawa hawafuati ila ni dhana tu, na kipendacho nyoyo zao zilio potoka na kuacha maumbile yaliyo sawa. Na hakika yalikwisha wajia kutoka kwa Mola wao Mlezi yenye uwongofu, laiti wangeli ufuata huo!
Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautafaa chochote isipo kuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.
Na malaika wengi wa mbinguni, juu ya ubora wa vyeo vyao, haufai kitu uombezi wao isipo kuwa baada ya kupewa idhini huyo mwombezi na Mwenyewe Mtukufu, na kumridhia huyo mwenye kuombewa.
Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, ili awalipe walio tenda ubaya kwa waliyo yatenda, na walio tenda mema awalipe mema.
Na ni vya Mwenyezi Mungu pekee vyote viliomo katika mbingu na ardhi, kwa kuviumba na kuvidabiri, ili awalipe walio potea wenye kufanya viovu vitendo vyao, na awalipe walio hidika watu wema kwa malipo yaliyo mema.
Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vichafu, isipo kuwa makosa khafifu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkunjufu wa maghfira, naye anakujueni sana tangu alipo kuumbeni kutoka kwenye ardhi, na mlipo kuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijisifu usafi. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga na maovu.
Wema hao ndio wale wanao jitenga na madhambi yenye adhabu kubwa kubwa, na yanayo chukiza mno. Lakini Mwenyezi Mungu husamehe dhambi ndogo ndogo. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkuu wa kughufiria, naye anajua vyema hali zenu. Kwani Yeye ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi, na mlipo kuwa mimba matumboni mwa mama zenu katika hali zenu mbali mbali za kukua na kugeuka. Basi msikae mkijisifu nafsi zenu kuwa mmesafika kwa kujigamba na kujifakhari. Na Yeye ndiye Mjuzi mkubwa kabisa wa kila mwenye kumcha na akajisafisha nafsi yake kweli kweli kwa uchamngu wake.
Kutokana na manii yanayo miminwa. Makusudio ya Aya hii tukufu ni kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba Yeye ameumba waume na wake katika wanaadamu na wanyama wote kutokana na tone ya manii ambayo humo humo mna ume na uke. Na juu ya udogo wake na udhaifu wake ndio chemchem ya uhai. Umuujiza wa Qur'ani unadhihirika katika Aya hii tukufu ukikumbuka kuwa ulimwengu ulikuwa haujui mpaka hivi karibu kuwa katika maji ya mwanamume ndio zimo mbegu "sperms" na katika maji ya mwanamke mna vijiyai "ova", ndio vikikutana vijidudu vya manii ya mwanamume na vijiyai vya mwanamke vikawa kitu kimoja ndio hiyo huwa mimba. Ukweli huu ulitajwa na Qur'ani kabla ya kuvumbuliwa na ilimu za Sayansi.
Na kwamba hakika Yeye ndiye Mola Mlezi wa nyota ya Shii'ra.
Na hakika Yeye ndiye Mola Mlezi wa hii nyota kubwa inayo itwa Shii'ra (Sirius, Dog Star). Makusudio hapa ni Nyota hiyo inayo itwa Ash-shi'ra Alyamaaniya, au wanavyo ita Wazungu Sirius au Dog Star. Nyota hii inang'ara kwa nguvu zaidi kuliko nyota zote ziliomo katika kikundi cha nyota kinacho itwa Alkalbu l-akbar, kwa Kizungu Canis Major au Greater Dog. Nyota hiyo ndiyo inayo zagaa sana mbinguni, na huonekana kusini ya mstari wa kati wa mbinguni kiasi ya daraja 18. Na kwa jina hilo la Nyota ya Mbwa ikijuulikana hata miaka elfu tatu ilio pita. Katika mabaki ya michoro ya Mafirauni wa Misri imeashiriwa pia. Mwenyezi Mungu ameitaja khasa kwa kuwa Waarabu walikuwa wakiiabudu hapo kale, na pia Wamisri wa zamani, kwani kutokea kwake upande wa mashariki katikati ya mwezi wa Julai kabla ya kuchomoza jua kulikuwa kunawafikiana na wakati wa mafuriko ya Misri ya kati, yaani katika tukio muhimu kabisa katika ulimwengu huo wa kale. Na tukio hili huenda ndilo lilio fanya kuanzisha kuwekea kiwango urefu wa mwaka katika dunia nzima. Kwani kudhihiri Nyota ya Shiira kabla ya kuchomoza jua hakutokei ila mara moja tu katika mwaka. Basi huu ndio mwanzo wa mwaka mpya.
Na kabla yao kaumu ya Nuhu. Na hao hakika walikuwa ni madhaalimu zaidi, na waovu zaidi;
Na aliwaangamiza kaumu ya Nuhu kabla ya kuwaangamiza A'di na Thamudi. Hakika hao walikuwa wamekithiri kudhulumu, na wamezidi kwa uasi kuliko A'di na Thamudi.
Basi msujudieni Mwenyezi Mungu aliye iteremsha Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu wote, na muabuduni Yeye tu peke yake Mwenye kutukuka kwa utukufu wake.