[1] Herufi hizi "Alif Lam Mim" na herufi nyinginezo za mkato zilizo mwanzoni mwa sura mbalimbali zinaonyesha hali ya ushindi wa Qur-ani. Kwani, washirikina walipewa changamoto kwayo, lakini wakashindwa na hawakuweza kuipinga, ilhali inajumuisha herufi hizi zinazounda lugha ya Kiarabu. Kwa hivyo, kutoweza kwa Waarabu kuleta kitu kama hicho - ingawa walikuwa ndio watu wenye ufasaha zaidi - kunaonyesha kwamba Qur-ani ni ufunuo (wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na wanapokutana na walioamini, husema: 'Tumeamini.' Na wanapokuwa peke yao na mashetani wao, husema: 'Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunafanya dhihaka tu.'
Mfano wao ni kama mfano wa aliyekoka moto, na ulipoangaza vile vilivyo kandokando yake, Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawaacha katika viza mbalimbali, hawaoni.
[1] Ni viziwi kwa sababu hawaisikii heri. Ni mabubu kwa sababu hawaitamki heri. Na ni vipofu kwa sababu hawaioni haki. Kwa hivyo, hawatarejea katika haki kwa kuwa waliiacha baada ya kuijua. Tofauti na mwenye kuiacha haki kwa ujinga na upotovu, yeye yuko karibu zaidi na kurudi katika haki.
Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina viza mbalimbali, na radi, na umeme; wakawa wanatia vidole vyao katika masikio yao kwa sababu ya mapigo ya radi, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazingira makafiri.
Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea mwangaza, wanatembea ndani yake. Na linapowawia giza, wanasimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu, angeliondoa kusikia kwao na kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza mno wa kila kitu.
(Mwenyezi Mungu) ambaye alikufanyieni ardhi hii kuwa kama tandiko, na mbingu kama paa. Na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa mazao yawe riziki zenu. Basi msimfanyie Mwenyezi Mungu wenza, na hali nyinyi mnajua.
Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomteremshia mja wetu, basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni wakweli.
Na wabashirie walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito chini yake; kila watakapopewa matunda humo, watasema: 'Haya ndiyo kama tuliyopewa mbele.' Na wataletewa matunda yaliyofanana; na humo watakuwa na wake waliotakaswa; na wao humo watadumu.
Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walioamini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyotoka kwa Mola wao Mlezi. Lakini wale waliokufuru, husema: 'Ni nini analokusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu?' Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi kwa huo ila wale wavukao mipaka.
Wale wanaovunja agano la Mwenyezi Mungu baada ya kwishalifunga, na wakayakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye hasara.
Yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyo katika ardhi, kisha akaelekea kuziumba mbingu, na akazifanya kuwa mbingu saba, naye ndiye ajuaye mno kila kitu.
Na pale Mola wako Mlezi alipowaambia Malaika: 'Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi)', wakasema: Utaweka humo atakayefanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: 'Hakika Mimi nayajua msiyoyajua.'
Akasema: 'Ewe Adam! Waambie majina yake.' Basi alipowaambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayoyadhihirisha na mliyokuwa mnayaficha?
Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale waliodhulumu.
Lakini Shetani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyokuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makazi yenu na starehe kwa muda.
Kisha Adam akapokea maneno kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi akamkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba, Mwenye kurehemu.
Na aminini niliyoyateremsha ambayo yanasadikisha mliyo nayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze ishara zangu kwa thamani ndogo. Na niogopeni Mimi tu.
Na (kumbukeni) tulipowaokoa kutoka kwa watu wa Firauni, waliokuwa wakikupeni adhabu mbaya, wakiwachinja wana wenu wa kiume, na wakiwawacha hai wanawake wenu. Na katika hayo kulikuwa na mtihani mkubwa kutoka kwa Mola wenu Mlezi.
Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmezidhulumu nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu. Naye akapokea toba yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba mno, Mwenye kurehemu zaidi.
Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na tukakuteremshieni Manna na Salwa; tukakwambieni: 'Kuleni katika vitu vizuri hivi tulivyokuruzukuni.' Nao hawakutudhulumu Sisi lakini walikuwa wakizidhulumu nafsi zao.
Na tuliposema: Ingieni mji huu, na humo mle mpendapo maridhawa, na ingieni katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni: 'Tusamehe!' Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.
Lakini waliodhulumu waliibadili kauli isiyo kuwa waliyoambiwa. Kwa hivyo tukaiteremsha juu ya wale waliodhulumu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya walivyokuwa wakivuka mipaka.
Na Musa alipoomba maji kwa ajili ya watu wake, tukamwambia: 'Lipige jiwe kwa fimbo yako.' Mara zikatimbuka chemichemi kumi na mbili; kila kabila likajua mahali pake pa kunywea. Tukawaambia: Kuleni na mnywe katika riziki ya Mwenyezi Mungu, wala msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.
Na mliposema: 'Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu. Basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyomea katika Ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na vitunguu saumu vyake, na adesi zake, na vitunguu maji vyake.' Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyoviomba. Na wakapigwa na unyonge, na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakufuru maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyoasi na wakapindukia mipaka.
Hakika Walioamini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda mema, basi watapata malipo yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika.[1]
[1] Hii ilikuwa hukumu yao kabla ya utume wa Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na aya hii ilitajwa hapa kwa sababu Mwenyezi Mungu alipowakashifu wana wa Israili kwa dhambi zao, na maovu yao, huenda iliingia katika nafsi za baadhi yao kwamba sio wote waliyafanya hayo. Kwa hivyo, aya hii ikawaondoa wale ambao hawakuhusika katika kashfa hiyo. (Tafsir Assa'adiiy)
Na tulipochukua agano lenu, na tukaunyanyua mlima juu yenu (tukakwambieni): Shikeni kwa nguvu haya tuliyokupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kuokoka.
Na Musa alipowaambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje Ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: "Audhu billah (Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga)."
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni ng'ombe gani? Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba ng'ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyoamrishwa.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie ipi rangi yake? Akasema: Yeye anasema kuwa ng'ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza wanaomtazama.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni yupi? Hakika tunaona ng'ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah (Mwenyezi Mungu akipenda), tutaongoka.
Akasema: Yeye anasema kuwa huyo ni ng'ombe asiyetiwa kazini kulima Ardhi wala kumwagia maji kwenye mimea, mzima, hana baka. Wakasema: Sasa umeleta (jambo la) haki. Basi wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye hayo.
Tukasema: Mpigeni (mtu huyo) kwa kipande chake (huyo g'ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni ishara zake ili mpate kufahamu.
Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, hata zikawa kama mawe au ngumu zaidi; kwani kuna mawe yanayotimbuka mito, na kuna mengine yanayopasuka yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine huanguka kwa sababu ya kumhofu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika mbali na mnayoyafanya.
Na wanapokutana na wale walioamini, husema: 'Tumeamini.' Na wanapokuwa peke yao, wao kwa wao, husema: Mnawaambia aliyokufunulieni Mwenyezi Mungu ili wapate kukuhojieni mbele ya Mola wenu Mlezi? Kwani hamfahamu nyinyi?
Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: 'Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu', ili wanunue kwacho thamani ndogo. Basi ole wao kwa yale iliyoyaandika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayoyachuma.
Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache tu. Sema: Mmechukua agano kwa Mwenyezi Mungu? Kwa hivyo Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na agano lake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyoyajua?
Na tulipofunga agano na Wana wa Israili: 'Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Sala, na toeni Zaka.' Kisha mkageuka isipokuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.
Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani mwao, mkisaidiana (na adui zao) dhidi yao kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni wakiwa mateka, mnawakomboa, na hali mlikatazwa kuwatoa. Je, mnaamini baadhi ya Kitabu na mnamkufuru baadhi yake? Basi ni yapi malipo ya mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila aibu katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika mbali na yale mnayoyatenda.
Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu hoja waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Mtakatifu. Basi kila walipokufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.
Na kilipowajia Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kinachothibitisha waliyo nayo - na wao walikuwa wakiomba ushindi kuwashinda makafiri - yalipowajia yale waliyokuwa wakiyajua, waliyakanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya makafiri!
Kiovu kweli walichoziuzia nafsi zao, nacho ni kule kukataa kwao aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, kwa sababu ya kuona haya kwa kuwa Mwenyezi Mungu humteremshia fadhila yake amtakaye miongoni mwa waja wake. Basi wamejiletea wenyewe ghadhabu juu ya ghadhabu. Na makafiri watapata mateso ya kudhalilisha.
Na wanapoambiwa: Yaaminini aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu. Wao husema: 'Tunaamini tuliyoteremshiwa sisi.' Na huyakataa yasiyokuwa hayo. Na hali ya kuwa hii ndiyo haki inayothibitisha yale waliyo nayo wao. Sema: Mbona mliwauwa Manabii wa Mwenyezi Mungu hapo zamani ikiwa kweli mlikuwa Waumini?
Na tulipochukua agano lenu na tukauinua mlima juu yenu (tukakwambieni): Kamateni kwa nguvu haya tuliyokupeni na sikieni. Wakasema: 'Tumesikia na tumekataa!' Na wakanyweshwa nyoyoni mwao (imani ya) ndama kwa kufuru yao. Sema: Ni uovu mno iliyokuamrisheni imani yenu ikiwa nyinyi ni waumini.
Na hakika utawapata ni wenye pupa ya kuishi kuwashinda watu wote, na kuliko washirikina. Mmoja wao anatamani lau angelipewa umri wa miaka elfu. Wala hilo (la kuzidishiwa umri) haliwezi kumweka mbali na adhabu, ili apewe umri mrefu. Na Mwenyezi Mungu anayaona vyema wanayoyatenda.
Sema: Aliyekuwa ni adui wa Jibril, basi huyo ndiye aliyeiteremsha Qur'ani moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, inayothibitisha yaliyokuwa kabla yake, na ni uongofu na bishara njema kwa Waumini.
Na alipowajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwenye kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale waliopewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui.
Na wakafuata yale waliyosoma mashetani katika ufalme wa Suleiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyoteremshwa kwa wale Malaika wawili, Haarut na Maarut huko Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: 'Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru.' Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumtenganisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka kwa Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yenye kuwadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika, walikwishajua kwamba mwenye kuununua (uchawi), hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walichouza kwacho nafsi zao, laiti wangelikuwa wanajua.
Enyi mlioamini! Msiseme: "Raa'ina", na semeni: "Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.[1]
[1] Neno “ra’ina" linalomaanisha "tutunze hali zetu". Lakini kwa lugha ya mayahudi linamaanisha ugumu. Basi Mwenyezi Mungu akakataza neno hili ili kuufunga mlango huu, na akawaamrisha waja wake waseme badala yake: “Undhurna" yaani "Tutazame, tutunze.” kwa Waarabu na Mayahudi. (Al-Mukhtassr fi Tafsiir)
Waliokufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na washirikina hawapendi mteremshiwe heri yoyote kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa rehema yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.
Ishara yoyote tunayoifuta au tunayoisahaulisha, tunaileta iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza mno wa kila kitu?
Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wangekurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa sababu ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwishawapambanukia haki. Basi sameheni na tupilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu atakapoleta amri yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza mno wa kila kitu.
Na simamisheni Swala na toeni Zaka; na heri mtakazozitangulizia nafsi zenu, mtazikuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona vyema mnayoyafanya.
Sivyo hivyo! Yeyote anayeelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi; wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.
Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo (wanalolifuata). Na Wakristo husema: Mayahudi hawana lao jambo (wanalolifuata). Na ilhali wote wanasoma Kitabu kicho hicho (Biblia). Na kadhaalika walisema wale wasiojua kitu mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakihitilafiana.
Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayezuia misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa ndani yake jina lake, na akajitahidi kuiharibu? (Watu) hao haitawafalia kuingia humo isipokuwa kwa hofu. Duniani watapata hizaya (aibu kubwa maishani), na Akhera watapata adhabu kubwa.
Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnakoelekea, huko Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua mno.
Na ati wanasema: 'Mwenyezi Mungu ana mwana.' Subhanahu (ametakasika na hayo!) Bali vyote vilivyomo mbinguni na duniani ni vyake. Vyote vinamdhalilikia Yeye kwa hofu.
Na walisema wale wasiojua kitu: 'Mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi au zikatufikia Ishara.' Kama hivyo walisema wale waliokuwa kabla yao mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka wazi Ishara kwa watu wenye yakini.
Na Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uongofu. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya yaliyokujia katika elimu, hutapata mlinzi wala msaidizi kando na Mwenyezi Mungu.[1]
[1] Mayahudi na Manaswara hawawaridhii Waislamu kwa chochote isipokuwa kwamba wawafuate katika dini yao. Lakini hayo waliyo nayo ni matamanio tu, siyo dini ya haki. (Tafsir Assa'dii)
Na Mola wake Mlezi alipomjaribu Ibrahim kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza. Akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi wa watu. Akasema: Je, na katika kizazi changu pia? Akasema: Agano langu halitawafikia wenye kudhulumu.
Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahali pa kukusanyikia watu na pahali pa amani. Na alipokuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu.
Na aliposema Ibrahim: Ewe Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya Moto, napo ni pahali pabaya mno pa kurejea.
Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipokuwa wanainyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Tukubalie! Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia mno, Mwenye kujua zaidi.
Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma uliosilimu kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hekima na awatakase. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini, Sisi tulimteua yeye katika dunia. Na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
Na Ibrahim akawausia wanawe hilo, na pia Yaaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteulieni Dini hii. Basi msife ila nanyi ni Waislamu.[1]
[1] Yani iliichagua na akawateulia kama rehema na wema. Basi inapasa kusimama nayo na kusifika kwa sheria zake, na kujipaka maadili yake na kudumu namna hiyo hadi kifo. Kwa sababu, mwenye kuishi juu ya kitu, atakufa juu yake. Na mwenye kufa juu ya kitu, atafufuliwa juu yake. (Tafsir Assa'dii)
Je, mlikuwapo yalipomfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is-hak, Mungu Mmoja tu. Na sisi tunasilimu kwake.[1]
[1] Hii ni hoja dhidi ya Mayahudi (na mfano wao) wanaodai kuwa wanaifuata mila (dini) ya Ibrahim na (Manabii wa) baada yake (kama vile) Yaaqub. Mwenyezi Mungu Mtukufu akawauliza ikiwa waliushuhudia wasia wa mwisho wa Yaqub kwa wana wake. "Je, mtamuabudu nani baada yangu?" Wakasema kuwa watamuabudu Mungu wake, Mungu wa baba zake, ambaye ni Mungu Mmoja tu, na kwamba wao ni wenye kujisilimisha kwake (yani ni Waislamu)." (Tafsir Assa'dii)
Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo ndio mtaongoka. Sema: Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika washirikina.[1]
[1] Mayahudi na Wakristo huwaita Waislamu kuingia katika Dini zao wakidai kuwa huo ndio uongofu. Lakini Mwenyezi Mungu akakanusha hilo, na kwamba mila (dini) ya Ibrahim ndiyo uongofu. Na katika kuipa mgongo mila yake ni ukafiri na kupotea. (Tafsir Assa'dii)
Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa sisi, na yaliyoteremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na watoto wake, na waliyopewa Musa na Isa, na pia waliyopewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutofautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi kwake tumesilimu.
Basi wakiamini kama mnavyoamini nyinyi, itakuwa kweli wameongoka. Na wakikengeuka, basi wao wamo katika upinzani tu. Na Mwenyezi Mungu atakutosheni kukukingeni kutokana na shari yao, na Yeye ndiye Mwenye kusikia mno, ajuaye zaidi.
Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye ni Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.
Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na watoto wake walikuwa Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule aliyeficha ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika mbali na hayo myafanyayo.
Wapumbavu miongoni mwa watu watasema: ‘Ni nini kilichowageuza kutoka kibla chao walichokuwa wakikielekea?’ Sema: ‘Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka.’
Na vivyo hivyo tumewafanya muwe Umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulichokuwa juu yake isipokuwa ili tupate kumjua yule anayemfuata Mtume, na yule anayegeuka akarejea kwa visigino vyake. Na kwa yakini, hilo lilikuwa jambo kubwa isipokuwa kwa wale aliowaongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu kwa watu ni Mpole, Mwenye kuwarehemu mno.
Kwa yakini, tuliona unavyougeuzageuza uso wako mbinguni. Basi, tutakuelekeza kwenye Kibla unachokiridhia. Basi, elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu. Na popote mnapokuwa, zielekezeni nyuso zenu upande wake. Na hakika, wale waliopewa Kitabu wanajua sana kwamba hiyo ndiyo haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika mbali na yale wanayoyatenda.
Na hata ukiwaletea hao waliopewa Kitabu hoja za kila namna, hawatafuata Kibla chako. Wala wewe hutafuata kibla chao. Wala baadhi yao hawatafuata kibla cha wengineo. Na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya kile kilichokufikia katika elimu, wewe kwa hakika hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
Na kila mmoja anao mwelekeo anaoelekea. Basi shindanieni mema. Popote mlipo, Mwenyezi Mungu atawaleta nyote pamoja. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Na kokote uendako, uelekeze uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na hiyo kwa hakika ndiyo haki itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika mbali na mnayoyatenda.
Na kokote uendako, uelekeze uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na popote mlipo, zielekezeni nyuso zenu upande wake, ili watu wasiwe na hoja juu yenu; isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Basi, msiwaogope wao, lakini niogopeni Mimi. Na ili niwatimizie neema yangu, na ili mpate kuongoka.
Kama tulivyomtuma Mtume kwenu anayetokana na nyinyi, anawasomea Aya zetu na kuwatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima, na anawafundisha ambayo hamkuwa mnayajua.
Wala msiseme kuwa wale waliouwawa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti. Bali hao ni hai. Lakini nyinyi hamtambui.[1]
[1] Inajulikana kuwa kipenzi hakiachiwi na wenye akili timamu, isipokuwa kwa ajili ya kipenzi kilicho juu zaidi na kikubwa kukiliko. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu akajulisha kwamba mwenye kuuawa katika njia yake akipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, ili neno la Mwenyezi Mungu liwe ndilo la juu zaidi; na dini yake iwe iliyo dhahiri zaidi. Basi yeye kwa hakika hajakosa uhai alioupenda, bali (alipouawa) alipata uhai mkubwa na kamili zaidi kuliko mnavyofikiria nyinyi. (Tafsir Assa'dii)
Wale ambao ukiwapata msiba, husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.[1]
[1] Wao husema hivyo kwa sababu wanajua kwamba wanamilikiwa na Mwenyezi Mungu, wako chini ya amri yake na uendeshaji wake. Kwa hivyo, hatuna chochote katika nafsi zetu wala mali zetu. Na akitujaribu kwa kitu katika hayo, basi Yeye Mwingi wa rehema atakuwa amewaendesha wamilikiwa wake na mali zake. Kwa hivyo haifai kuwa na pingamizi lolote dhidi yake. (Tafsir Assa'dii)
Hakika, vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi, anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuzunguka kati yake. Na anayetendea mwenyewe heri, basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mwenye kujua hilo mno.
Hakika, wale wanaoficha yale tuliyoyateremsha, nazo ni hoja zilizo wazi na uongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni, hao anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani.
Hakika, katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana. Na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo, akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanaozingatia.
Na katika watu wapo wanaojifanyia waungu wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana. Na laiti waliodhulumu wakajua watakapoiona adhabu kuwa nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu, na kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu!
Na watasema wale waliofuata: 'Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama wanavyotukataa sisi!' Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowaonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni.[1]
[1] Basi matendo yao (ya kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mmoja) yakapotelea mbali. Na hali zao zikaangamia, na ikawadhihirikia kuwa wao walikuwa ni waongo. Na kwamba matendo yao waliyoyatarajia yawanufaishe na wapate matokeo yake yaliwabadilikia yakawa masikitiko na majuto. (Tafsir Assa'dii)
Na wanapoambiwa: 'Fuateni aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu;' wao husema: 'Bali tutafuata tuliyowakuta nayo baba zetu.' Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?
Hakika Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichotajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliyefikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Hakika, wale wanaoficha aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu, na wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali katika tumbo zao isipokuwa moto. Wala Mwenyezi Mungu hatawaongelesha Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao wana adhabu chungu.
Siyo wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii. Na anawapa mali - licha ya kuipenda - jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ukombozi. Na akawa anashika Swala, na akatoa Zaka, na wanaotimiza agano lao wanapoahidi, na wanaovumilia katika shida na dhara na wakati wa vita. Hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wacha Mungu.
Enyi mlioamini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika waliouawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anayesamehewa na ndugu yake chochote, basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kulikotokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakayevuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu.
Mmeandikiwa mmoja wenu anapofikwa na mauti, kama ataacha heri (yani mali), afanye wasia kwa wazazi wake wawili, na jamaa zake kwa wema. Ni haki juu ya wacha Mungu.
Na atakayeibadilisha (wasia) baada ya kuisikia, basi dhambi yake ni juu ya wale watakaoibadilisha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Na mwenye kumhofia muusiaji kwenda kombo au kupata dhambi, na akasuluhisha baina yao, basi hakuna dhambi yoyote juu yake. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
(Mfunge) siku zenye kuhesabika. Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini, basi atimize hesabu katika siku nyingine. Na wale wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga saumu, ndiyo bora kwenu, ikiwa mnajua.
Mwezi wa Ramadhani ndio ambao imeteremshwa Qur-ani ndani yake kuwa uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. Kwa hivyo, atakayeushuhudia mwezi miongoni mwenu, basi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hesabu katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi, wala hawatakii yaliyo mazito, na ili mkamilishe hesabu hiyo, na ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa yale aliyowaongoa ili mpate kushukuru.
Na waja wangu watakapokuuliza kunihusu Mimi, basi Mimi kwa hakika nipo karibu. Ninaitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.
Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu alikwishajua kwamba mlikuwa mkizihini nafsi zenu. Kwa hivyo amewakubalia toba yenu na amewasamehe. Basi sasa changanyikeni nao na tafuteni kile alichowaandikia Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka uwabainikie weupe wa alfajiri kutokana na weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao hali ya kuwa mmekaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya (Ishara) zake watu ili wapate kumcha.
Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo. Sema: Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija. Wala sio wema kwamba mziingie nyumba kwa nyuma yake. Bali mwema ni mwenye kumcha Mungu. Na ingieni majumbani kupitia milangoni mwake. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.
Na waueni popote muwakutapo, na watoeni popote walipowatoa; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua. Wala msipigane nao kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka wawapigie huko. Wakikupigeni huko, basi nanyi pia wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu vitakatifu vimeekewa kisasi. Basi, anayewashambulia, nanyi mshambulieni kwa sawa na alivyowashambulia. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu kwa hakika yu pamoja na wacha Mungu.
Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitupe katika maangamivu kwa mikono yenu. Na fanyeni wema. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaofanya wema.
Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mtazuiwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike mahali pao pa kuchinjiwa. Na atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au ana vya kumuudhi kichwani kwake, basi atoe fidia kwa kufunga saumu au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapokuwa na amani, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiyepata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakaporudi. Hizo ni kumi kamili. Hayo ni kwa yule ambaye jamaa zake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Hija ni miezi maalumu. Basi anayehirimia Hija ndani yake (miezi hiyo), basi asijamiiane wala asipindukie mipaka wala asibishane katika Hija. Na chochote mnachokifanya katika heri, Mwenyezi Mungu anaijua. Na chukueni masurufu. Na hakika, masurufu (yaliyo) bora zaidi ni ucha Mungu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili ya hali ya juu!
Hakuna ubaya wowote juu yenu kutafuta fadhila kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi mtakapomiminika kutoka 'Arafat, mtajeni Mwenyezi Mungu katika Mash'aril Haram (eneo takatifu). Na mtajeni kama alivyowaongoa, ijapokuwa kabla ya hilo mlikuwa miongoni mwa waliopotea.
Na mkishatimiza ibada zenu za Hija, mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu au utajo mkubwa zaidi. Na katika watu kuna wale wanaosema, “Mola wetu Mlezi, tupe duniani!” Naye katika Akhera hana fungu lolote.
Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazohisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka (akarejea) katika siku mbili, basi hakuna dhambi juu yake. Na mwenye kukawia, pia hakuna dhambi juu yake, kwa mwenye kumcha Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake.
Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukupendeza; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyo katika moyo wake, na hali yeye ndiye mgomvi mkubwa mno.
Na akiambiwa, “Mche Mwenyezi Mungu,” hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo kinachomtosha ni Jahannam. Napo hakika ni pahali pabaya mno pa kupumzikia.
Je, wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika, na hukumu iwe imekwishatolewa? Na kwa Mwenyezi Mungu ndiyo hurejeshwa mambo yote.
Waulize Wana wa Israili: 'Tumewapa ishara ngapi zilizo wazi?' Na anayezibadili neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Waliokufuru wamepambiwa maisha ya duniani; na wanawafanyia masihara wale walioamini. Na wale wanaomcha Mwenyezi Mungu watakuwa juu yao Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
Watu wote walikuwa umma mmoja. Kisha Mwenyezi Mungu akawatuma Manabii wenye kupeana habari njema na waonyaji. Na akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale waliyohitilafiana. Na wala hawakuhitilafiana ndani yake isipokuwa wale waliopewa Kitabu hicho baada ya kufikiwa na hoja zilizo wazi, kwa sababu ya husuda ya baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walioamini kuiendea haki katika yale waliyohitilafiana ndani yake. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia iliyonyooka.
Ama mnadhani kuwa mtaingia Bustanini, ilhali bado hamjajiwa na mfano wa (yaliyowajia) wale waliopita kabla yenu? Uliwapata ufukara (shida) na maradhi, na wakatikiswa mpaka Mtume na walioamini pamoja naye wakasema. “Ni lini nusura ya Mwenyezi Mungu (itakuja)?” Jueni kuwa hakika nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.
Wanakuuliza watoe nini? Sema: Chochote mnachotoa katika heri ni kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na msafiri. Na chochote mnachofanya katika heri, basi Mwenyezi Mungu kwa hakika anaijua vyema.
Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinawachukiza. Lakini huenda mkachukia kitu, nacho ni heri kwenu. Na huenda mkapenda kitu, nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.
Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita ndani yake ni dhambi kubwa. Lakini kuzuia watu wasiende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkufuru Yeye, na kuzuilia watu wasiende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni jambo kubwa zaidi kuliko kuua. Wala hawataacha kupigana nanyi mpaka wawatoe katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi atakayeacha Dini yake, na akafa hali ya kuwa ni kafiri, basi hao ndio ambao matendo yao yameharibika katika dunia na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni. Wao humo watadumu.
Hakika, wale walioamini, na wale waliohama na wakafanya juhudi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wanaotarajia rehema za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Wanakuuliza juu ya mvinyo na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi kupatikana. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kutafakari.
Katika dunia na Akhera, na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio heri. Na mkichanganyika nao, basi ni ndugu zenu. Na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Mwenyezi Mungu angelipenda, angelikutieni katika ugumu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mwanamke mshirikina hata akiwapendeza. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mwanamume mshirikina hata akiwapendeza. Hao wanaitia kwenye Moto, naye Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Bustani na maghfira kwa idhini yake. Naye huwabainishia Aya zake watu ili wapate kukumbuka.
Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie: hayo ni madhara. Basi jitengeni mbali na wanawake wakati wa hedhi, wala msiwakaribie mpaka wawe safi. Na wakishajisafisha, basi waendeeni namna alivyokuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu, na huwapenda wanaojisafisha.
Wake zenu ni konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini zitangulizieni heri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape habari njema Waumini.
Wala msifanye Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa kisingizio cha kuacha kufanya wema, na kumcha Mungu, na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Mwenyezi Mungu hawachukulii ubaya katika viapo vyenu ambavyo hamkuvikusudia. Lakini anawachukulia ubaya kwa yale ambayo nyoyo zenu zinachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole.
Na wanawake waliopewa talaka, wazizuie nafsi zao tahara (au hedhi) tatu. Wala sio halali kwao kuficha alichoumba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao ya uzazi, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki zaidi ya kuwarejesha katika muda huo, ikiwa wanataka kufanya suluhu. Nao wanawake wanayo haki sawa na ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa uzuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika kile mlichowapa wake zenu, isipokuwa ikiwa wote wawili watahofia ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkihofia kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu, hapo hakuna ubaya juu yao katika kile ambacho mke atajikomboa kwacho. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi msiikiuke. Na mwenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.
Na akimtaliki (talaka ya tatu), basi yeye si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume asiyekuwa yeye. Na (huyo mwingine) akimtaliki, basi hakuna ubaya kwao (mke na mume wa kwanza) kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu anayoibainisha kwa watu wanaojua.
Na mtakapowataliki wanawake talaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo, ameidhulumu nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa masikhara. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyowateremshia katika Kitabu na hekima anachowaonya kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mno kila kitu.
Na mtakapowataliki wanawake, nao wakamaliza muda wao (wa eda), basi msiwazuie kuoleka kwa waume zao endapo baina yao wamekubaliana kwa wema. Hayo anawaidhiwa kwayo yule miongoni mwenu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni bora zaidi kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua, lakini nyinyi hamjui.
Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na ni juu ya aliyezaliwa mwana huyo chakula chao na mavazi yao kwa wema. Wala halazimishwi mtu isipokuwa kwa kiwango cha uwezo wake. Mama asitaabishwe kwa sababu ya mwanawe, wala yule aliyezaliwa mwana kwa sababu ya mwanawe. Na juu ya mrithi ni mfano wa hivyo. Na kama wote wawili watataka kumwachisha kunyonya kwa kuridhiana na kushauriana, basi hakuna ubaya juu yao. Na mkitaka kuwapa watoto wenu mama wa kuwanyonyesha, basi hakuna ubaya juu yenu ikiwa mtapeana mlichoahidi kwa wema. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona vyema mnayoyatenda.
Na wale miongoni mwenu wanaofishwa, na wanaacha wake, hawa wake wazizuie nafsi zao miezi minne na siku kumi. Na wanapotimiza muda wao (wa eda), basi hakuna ubaya wowote juu yao katika yale wanayojifanyia kwa wema. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyatenda.
Wala hakuna ubaya juu yenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake walio katika eda au mkalificha ndani ya nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu alikwishajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, isipokuwa mseme maneno mema. Wala msiazimie kufunga mkataba wa ndoa mpaka andiko (la amri ya eda) lifike muda wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu kwa hakika anajua yaliyo katika nafsi zenu. Basi jitahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole.
Hakuna ubaya wowote juu yenu mkiwataliki wanawake ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kwa kiwango awezacho na mwenye dhiki kwa kiwango awezacho, maliwazo kwa wema, ni haki juu ya watendao mema.
Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa, na tayari mmeshawakatia mahari mahususi, basi wapeni nusu ya mahari mliyowakatia. Isipokuwa ikiwa wanawake wenyewe watasamehe, au amesamehe yule ambaye fundo la ndoa liko mkononi mwake. Na mkisamehe ndiyo kuwa karibu zaidi na ucha Mungu. Wala msisahau fadhila zilizo baina yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu anayaona vyema mnayoyatenda.
Na mkiwa na hofu, basi (swalini) hali ya kuwa mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapokuwa katika amani, basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafunza yale ambayo hamkuwa mnayajua.
Na wale miongoni mwenu wanaofishwa, na wanawaacha wake, na wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi kwa mwaka mmoja bila ya kuwatoa nyumbani. Na wanawake wenyewe wakiondoka, basi hakuna ubaya wowote juu yenu katika yale waliyojifanyia wenyewe kwa wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Je, hukuwaona wale waliotoka katika maboma yao kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Na Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni! Kisha akawahuisha. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru.
Je, hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipomwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, ilhali tumeshatolewa katika maboma yetu na watoto wetu? Lakini walipoandikiwa kupigana vita, wakageuka, isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema madhalimu.
Na Nabii wao akawaambia: Hakika, Mwenyezi Mungu ameshawateulia Taluti (Sauli) kuwa ndiye mfalme. Wakasema: Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, ilhali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Hakika, Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa elimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
Na Nabii wao akawaambia: Hakika, alama ya ufalme wake ni kwamba awaletee lile sanduku ambalo ndani yake mna kituliza nyoyo zenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na mabaki ya waliyoyaacha watu wa Musa na watu wa Harun, linalobebwa na Malaika. Bila shaka, katika hayo zimo ishara kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.
Basi Taluti alipoondoka na majeshi, alisema: Hakika, Mwenyezi Mungu atawajaribu kwa mto. Hivyo basi, atakayekunywa humo, si pamoja nami. Na yule asiyeyaonja, basi huyo atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka humo kiasi cha kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipokuwa wachache tu miongoni mwao. Na alipovuka mto yeye na wale walioamini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Ni makundi mangapi madogo yalishinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
Na walipotoka ili kupambana na Jaluti na majeshi yake, walisema: Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utunusuru kutokana na watu hawa makafiri.
Kwa hivyo, wakawashinda kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na Daudi akamuua Jaluti. Na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hekima, na akamfundisha katika aliyoyataka. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawazuii watu kwa watu, basi dunia ingeliharibika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu wote.
Mitume hao tumewaboresha baadhi yao juu ya wengineo. Miongoni mwao kuna wale ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na akawapandisha vyeo baadhi yao. Na tukampa Isa mwana wa Maryam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Mtakatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelipigana wale waliokuwa baada yao, baada ya kujiwa na hoja zilizo wazi. Lakini walihitilafiana. Basi miongoni mwao kuna wale walioamini, na miongoni mwao kuna wale waliokufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelitaka, wasingelipigana. Lakini Mwenyezi Mungu hufanya kile akitakacho.
Enyi mlioamini! Toeni katika tulivyowaruzuku kabla haijakuja Siku ambayo hapatakuwapo biashara yoyote, wala urafiki, wala uombezi. Na makafiri ndio madhalimu.
Mwenyezi Mungu - hakuna mungu isipokuwa Yeye, Aliye hai, Msimamizi wa mambo yote milele. Hashikwi na kusinzia wala kulala. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo duniani. Ni nani huyo awezaye kufanya uombezi mbele yake isipokuwa kwa idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao, wala wao hawajui vyema chochote katika elimu yake isipokuwa kwa kile akitakacho. Kursi (mahali inapokanyaga miguu) yake imeenea mbingu na dunia, na wala halemewi katika kuvilinda vyote viwili. Na Yeye ndiye aliye juu zaidi, Mkuu.
Hakuna kulazimisha katika Dini. Kwani uongofu umekwishapambanuka kutokana na upotovu. Kwa hivyo, anayemkufuru Taaghuut na akamwamini Mwenyezi Mungu, basi bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia mno, Mwenye kujua vyema.[1]
[1] Na wala hakuna upinzani baina ya maana hii na Aya nyingi zinazolazimu kuwepo kwa Jihadi. Kwani, Mwenyezi Mungu ameamrisha kupigana vita ili Dini yote iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kuzuia uadui wa wenye kufanya uadui dhidi ya dini. (Tafsir Assa'dii)
Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa walioamini. Huwatoa katika giza mbalimbali kwenda katika nuru. Lakini wale waliokufuru, walinzi wao ni Taaghut. Huwatoa katika nuru kwenda hadi katika giza mbalimbali. Hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu.
Kwani hukumuona yule aliyehojiana na Ibrahim kuhusu Mola wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim aliposema: Mola wangu Mlezi ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia ninahuisha na ninafisha. Ibrahim akasema: Kwa hakika, Mwenyezi Mungu hulileta jua kutokea mashariki, basi wewe lilete kutokea magharibi. Kwa hivyo, akashindwa yule aliyekufuru. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu dhalimu.
Au kama yule aliyepita karibu na mji hali ya kuwa umekwishakuwa magofu tu. Akasema: Vipi Mwenyezi Mungu ataufufua mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu akamfisha yeye (muda wa) miaka mia moja, kisha akamfufua. Akasema: Je umekaa muda gani? Akasema: (Labda) nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akasema: Bali umekaa miaka mia moja. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na mwangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu. Na iangalie mifupa yake hii jinsi tunavyoinyanyua kisha tuivishe nyama. Basi yalipombainikia, alisema: Ninajua kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo mno juu ya kila kitu.
Na Ibrahim aliposema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyofufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akasema: Basi wachukue wanne katika ndege na uwazoeshe kwako. Kisha weka juu ya kila kilima sehemu katika hao, kisha waite, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia moja. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
Wale wanaotoa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishi kile walichotoa masimbulizi wala udhia, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Wala haitakuwa hofu juu yao wala wao hawatahuzunika.
Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi. Kama yule anayetoa mali yake ili kujionyesha kwa watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake kuna udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uwezo wowote juu ya kile walichochuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu ya makafiri.
Na mfano wa wale wanaotoa mali zao kwa kuzitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu. Ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake maradufu. Na hata kama haifikiwi na mvua kubwa, basi manyunyu tu yanatosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona vyema mnayoyatenda.
Je, angependa mmoja wenu kwamba awe na bustani ya mitende na mizabibu ipitayo mito chini yake. Naye humo hupata katika mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia ilhali ana watoto wanyonge. Kisha ikapigwa na kimbunga chenye moto, kwa hivyo ikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia ishara ili mtafakari.
Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma, na katika vile tulivyowatolea katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, ilhali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
Shetani anawatia hofu ya ufakiri, na anawaamrisha machafu. Na Mwenyezi Mungu anawaahidi msamaha kutoka kwake na fadhila. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
Mkizidhihirisha sadaka, basi hilo ni vizuri. Na mkizificha na mkawapa mafakiri kwa siri, basi hilo ni heri kwenu, na yatawaondolea katika maovu yenu. Na Mwenyezi Mungu ana habari ya mnayoyatenda.
Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na chochote mnachotoa katika heri, basi ni cha nafsi zenu. Wala hamtoi isipokuwa kwa kutafuta uso wa Mwenyezi Mungu. Na chochote mnachotoa katika heri, mtalipwa kwa ukamilifu, nanyi hamtadhulumiwa.
Na wapewe mafakiri waliozuiliwa katika njia za Mwenyezi Mungu, wasioweza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiyewajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao; hawawang'ang'anilii watu kwa kuwaomba. Na chochote mnachotoa katika heri, basi hakika Mwenyezi Mungu anaijua.
Wale wanaokula riba, hawasimami isipokuwa kama anavyosimama aliyezugwa na Shetani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa walisema: Hakika, biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi mwenye kujiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akakomeka, basi yake ni yaliyokwishapita. Na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia, basi hao ndio watu wa Motoni, wao watadumu humo.
Hakika, wale walioamini na wakatenda mema na wakashika Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika.
Na msipofanya, basi jitangazieni vita kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilimali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe.
Enyi mlioamini! Mnapodaiana deni hadi muda maalumu, basi liandikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika kama alivyomfunza Mwenyezi Mungu. Basi na aandike, na mwenye deni juu yake aandikishe; na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi, wala asipunguze chochote ndani yake. Na ikiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na washuhudisheni mashahidi wawili katika wanaume wenu. Na ikiwa wanaume wawili hawapo, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika wale mnaowaridhia miongoni mwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao (wanawake hao) atapotea, basi mmoja wao amkumbushe huyo mwengine. Na mashahidi wasikatae pindi wanapoitwa. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo ya uadilifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na ya chini zaidi ili msiwe na shaka. Isipokuwa ikiwa ni biashara ya mkono kwa mkono mnayoifanya baina yenu, basi hapo hakuna ubaya juu yenu msipoiandika. Lakini wekeni mashahidi mnapouziana. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo, basi hakika huko ni kupita mipaka mliko nako. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kila kitu.
Na mkiwa katika safari, na hamkupata mwandishi, basi yatosha kukabidhiwa rehani. Na mmoja wenu akimwekea amana mwenziwe, basi aliyeaminiwa airudishe amana ya mwenzake, na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala msifiche ushahidi. Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kutenda dhambi. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyatenda
Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo katika mbingu na viliomo katika dunia. Na mkidhihirisha yaliyo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi Mungu atawahesabu kwayo. Kisha atamsamehe amtakaye na amwadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza mno wa kila kitu.
Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Waumini vile vile. Wote wamemwamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutofautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola wetu Mlezi! Na marejeo ni kwako.
Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kiwango cha iwezavyo. Faida ya iliyoyachuma ni yake, na hasara ya iliyoyachuma ni juu yake pia. (Semeni) Mola wetu Mlezi! Usituchukulie ubaya tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama uliyowabebesha wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi! Usitutwike tusiyoyaweza, na uyatupilie mbali mabaya yetu, na utusamehe na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi dhidi ya kaumu ya makafiri.
വിശുദ്ധ ഖുർആൻ പരിഭാഷ - സവാഹിലി വിവർത്തനം - റുവ്വാദ് തർജമ സെൻ്റർ - വിവർത്തനങ്ങളുടെ സൂചിക
റബ്വ ഇസ്ലാമിക് ദഅ്വാ ആൻഡ് ഗൈഡൻസ് സെൻററിൻ്റെയും കോൺടെന്റ് ഇൻ ലാംഗ്വേജസ് സർവീസ് അസോസിയേഷൻ്റെയും സഹകരണത്തോടെ മർകസ് റുവാദ് തർജമ വിഭാഗം വിവർത്തനം ചെയ്തത്.
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
തിരയൽ ഫലങ്ങൾ:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".