Harufi hizi na mfano wa hizi ndizo zikakusanyika kuifanya Qur'ani kuwa ni muujiza ulio washinda watu kuiga mfano wake, ijapo kuwa hizo harufi ndizo wanazo zitamka. Basi mwenye kuitilia shaka hii Qur'ani kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu au la, basi na alete mfano wake. Na hatoweza.
Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao.
Sisi tunaweza kuwaletea muujiza wa kuwalazimisha Imani, wat'ii kwa unyenyekevu amri yake, na yatimie unayo yatarajia. Lakini hatuwaletei, kwa sababu mwendo wetu ni kuwaongoza watu waamini bila ya kuwalazimisha, ili isikosekane hikima ya kujaribiwa kwa mitihani, na yanayo kuja baada yake ya thawabu na adhabu.
Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao.
Wala Mwenyezi Mungu hawaletei watu wako kwa ufunuo wake ya kuwakumbusha Dini ya Haki kuwa ni rehema kwao, ila wao huzua upya upinzani na ukafiri kuukataa. Kwani njia ya uwongofu imekwisha zibwa mbele yao.
Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?
Hivyo hao wanatenda watendavyo katika ukafiri wao na kukadhibisha kwao wala hawaangalii baadhi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu katika hii hii ardhi? Lau kuwa wanaangalia kwa kuzingatia wangeli ongoka. Hebu wazingatie hii mimea ya kila namna yenye manufaa tunayo itoa Sisi kwenye ardhi, na wala hawezi hayo isipo kuwa Mungu Mmoja Muweza.
Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,
Ewe Muhammad! Watajie watu wako kisa cha Musa pale Mola wako Mlezi alipo mwita: Ewe Musa! Nenda kwa Utume kwa watu walio dhulumu nafsi zao kwa ukafiri, na wakawadhulumu Wana wa Israili kwa kuwafanya watumwa na kuwauwa watoto wao wanaume.
Nenda kwa kaumu ya Firauni; kwani hao wamepita mipaka katika dhulma yao. Ama ajabu ya watu hawa! Hawaogopi nini litalo wafika kwa vitendo vyao hivi, wakatahadhari?
Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.
Na mimi nimejaa dhiki kwa kuwa wataniambia mwongo, na ulimi wangu si mkunjufu wa kuweza kuhojiana nao kama ninavyo penda. Basi mtume Jibril ende kwa ndugu yangu aje kuniunga mkono katika hii kazi yangu.
Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.
Na watu hawa wana kisasi juu yangu. Kwani mimi nilimuuwa mtu katika wao. Basi nina khofu watakuja niuwa kwa kisasi kabla sijatimiza kazi yangu. Hayo yananizidisha khofu.
Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.
Mwenyezi Mungu akamwambia: Hawatokuuwa. Na kwa mintarafu ya Haruni nimekukubalia ombi lako. Basi nendeni nanyi mmejizatiti na miujiza yetu. Mimi niko pamoja nanyi kwa ulinzi. Nayasikia yanayo jiri baina yenu na Firauni. Nyinyi mtapata ushindi, na kuungwa mkono.
(Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?
Firauni akamwambia Musa kwa kumsimbulia, naye alimtambua walipo ingia na wakakadimisha Ujumbe wao, kwani alilelewa mle mle katika kasri lake: Hatukukulea sisi ulipo kuwa mtoto? Na ukaishi chini ya ulezi wetu kwa miaka mingi katika umri wako?
Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?
Na ukatenda makosa yako ya jinaya maovu kumuuwa mtu katika kaumu yangu, na ukazikanusha neema zangu nilizo kufanyia, hukuwahifadhi raia zangu, ukaushambulia ungu wetu kwa kudai kuwa wewe ati ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Basi nilikukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi, akanitunukia hukumu, na akanijaali niwe miongoni mwa Mitume.
Nikakukimbieni nilipo khofu kuwa mtakuja niuwa kwa jinaya hii ambayo sikuukusudia. Mola wangu Mlezi akanitunukia fahamu na ilimu, kwa fadhila zake na neema zake, na akanifanya mmoja katika Mitume.
Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?
Musa akaashiria sifa katika sifa ovu kabisa za Firauni, nayo ni kuwa kawafanya watumwa Wana wa Israili, na akiwauwa watoto wao wanaume. Na akakataa kukuita kule kulelewa kwake katika jumba la Firauni kuwa ni neema, kwani yaliyo sabibisha hayo ni yale aliyo kwisha yataja, ndio yeye alitupwa mtoni aokoke asiuliwe. Akaishia kwenye jumba la Firauni. Na lau kuwa si hivyo basi angeli lelewa na wazazi wake.
Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?
Firauni akasema: Na nini hizo sifa za Mola Mlezi wa walimwengu wote ambaye unakithiri kumtaja, na wewe unadai kuwa ni Mtume wake, na hali sisi hatujui lolote khabari zake?
Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.
Musa akasema: Yeye huyo ndiye Mwenye kuzimiliki mbingu na ardhi na kila kilio baina yao. Ikiwa nyinyi mna yakini ya ukweli wa jawabu hii basi mtanafiika, na mtaongoka, na mtajua kuwa ufalme wa Firauni wa kujidai haufui dafu mbele ya Ufalme wake Mwenyezi Mungu. Kwani ufalme wa Firauni haupindukii hata eneo moja katika hii dunia.
Firauni kuonyesha mastaajabu kwa wale walio mzunguka kwa kuwa Musa katika jawabu yake alipo mtaja Mola wake Mlezi na akadhukuru Ufalme wake hakuugusia hata kidogo ufalme wa Firauni, alisema: Mwayasikiaje maneno ya Musa?
(Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.
Musa akiendelea na usemi wake bila ya kujali hasira za Firauni na uchafu wa maneno yake, akasema: Ndiye huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote, aliye kuumbeni nyinyi na baba zenu walio tangulia. Na miongoni mwa hao walikuwako walio dai ungu kama unavyo dai wewe. Na wao wameteketea. Na wewe utateketea, na hayo unayo yadai yatapotelea mbali. Kwani Mungu wa kweli hafi.
Firauni akwaambia watu wake yale yanayo mtibuwa roho na kumghadhibisha, akautaja Utume wa Musa ni kwao wao, wala si kwake yeye, na akambandikiza wazimu, kwa kuwa ati akiulizwa kitu hujibu kingine, na anamsifu Mola Mlezi kwa sifa za kiajabu ajabu. Na kwa hivyo Firauni anawahimiza wamkadhibishe.
. (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.
Musa akasema: Ikiwa nyinyi mna akili, basi uaminini Ujumbe wangu. Kwani kuchomoza jua na kuchwa kwake kwa mpango madhubuti ni dalili wazi ya Mwenye kuumba. Kwa hivyo basi ni nyinyi ndio mnastahiki kuambiwa wendawazimu.
(Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.
Firauni akamwambia Musa: Ukimfuata mungu yeyote badala yangu mimi, utakuwa mmoja katika wanao ijua hali yao mbaya katika magereza yangu. Na yeye Firauni kaangukia kitisho hichi baada ya kushindwa kuondoa athari za kazi za Muumbaji.
Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.
Firauni akasema: Ulete ushahidi utao onyesha Unabii wako kama wewe kweli unasema kweli katika wito wako. Kasema hayo kwa tamaa ya kuwa huenda akapata kipengee cha udhaifu katika hoja zake.
Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.
Musa akautoa mkono wake kutoka mfukoni mwake. Hiyo ni Ishara ya pili. Nao ukawa mweupe, bila ya maradhi, hata wakashangaa watazamaji kwa kumetuka kwake.
(Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.
Firauni akawaambia watu wake: Hakika Musa ni mchawi bingwa katika uchawi wake. Kasema hayo kwa kuchelea watu wake wasiifuate Haki waliyo iona kwa Musa.
Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?
Tena Firauni akasema: Mchawi huyu anataka kunifanyia kahari apate kukutoeni katika hii nchi yenu. Na haya ni uchochezi dhidi ya Musa, kwani katika la dhiki mno katika hayo yaliyo dhiki ni mtu kuiacha nchi yake, na khasa ikiwa kwa kahari. Naye akataka mawazo ya wale walio kuwa wanamuabudu. Kasahau ungu wake kwa nguvu za Ishara za Musa.
Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo.
Watu wake wakamwambia: Akhirisha kukata shauri yao hawa, na uwatume askari wende wawakusanye wachawi katika raia zako. Kwani uchawi hupingwa kwa uchawi.
Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.
Wakazitupa kamba zao na fimbo zao, na watu wakazugwa wakaona kama ni nyoka wanakwenda. Wakaapa kwa utukufu wa Firauni na nguvu zake hapana shaka hawa leo watashinda
Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua.
Musa tena akatupa fimbo yake. Mara ikawa joka kubwa likaingia kuvimeza vile walivyo vizua kwa uchawi, navyo ni kamba na fimbo, wakidanganya kuwa ni nyoka wanao kwenda.
(Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote.
Firauni kwa kukasarika kuwa wale wachawi wamemuamini Musa bila ya yeye kuwapa ruhusa, aliwatishia ya kwamba yeye ndiye mwalimu wao aliye wafunza fani za uchawi, na watakuja jua adhabu itakayo wateremkia. Akawaambia: Nitakata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali, nitakata wa kulia huu kwa wa kushoto huu, na kinyume cha hayo. Na nyote nitakutundikeni juu ya misalaba.
Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
Wachawi wakasema: Hapana la kutudhuru sisi kwa adhabu unazo tutishia, kwani sisi ni wenye kurejea kwenye malipo ya Mola wetu Mlezi. Na Yeye ndiye mbora wa kulipa na mbora wa kuadhibu.
Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.
Na Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Musa a.s. atoke usiku usiku pamoja na Waumini miongoni mwa Wana wa Israili, ilipo kuwa tena haiwi kumsubirisha Musa. Mpango ukawa wa makundi mawili kwamba atangulie Musa na kaumu yake, na Firauni afuatie na kaumu yake, mpaka waingie katika maingilio ya njia ya baharini, na Mwenyezi Mungu awateketeze.
Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo.
Firauni akawatuma askari wake katika miji ya mamlaka yake, wawakusanye wenye maguvu katika kaumu yake, alipo jua kuwa Musa kesha toka na Wana wa Israili, ili awazuie lile walilo kusudia.
Firauni akasema: Hakika hawa Wana wa Israili walio kimbia na Musa ni taifa dogo kwa nguvu zao. Idadi yao ni chache. Anasema hayo kutia mori katika nyoyo za askari wake.
Tukawatoa Firauni na askari wake kwenye nchi yao iliyo fanana na mabustani yapitiwayo na mito kati yao, wakaangamia kwa kujitenga kwao na Haki, na kuchochewa kutaka kumfuatia Musa, kama ilivyo kuja katika Aya tatu zilizo tangulia.
Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.
Ni kutoka kama huku kwa ajabu tulivyo kueleza ndivyo tulivyo watoa, na tukawapa ufalme huo na kila namna ya neema zilizo kuwamo Wana wa Israili, baada ya kuwa masikini hawana mbele wala nyuma.
(Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!
Musa akasema: Hakika mimi ninao uangalizi wa Mwenyezi Mungu unao nifuata kwa kunihifadhi. Na Yeye ataniongoza kwenye Njia ya uwokovu. Amesema hayo ili awatuze kuwa watasalimika, na iwe mbali na mawazo yao fikra ya kutisha kwamba takuja patikana. .
Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.
Tukamuamrisha Musa kwa wahyi, ufunuo, aipige bahari kwa fimbo yake. Ikapasuka bahari njia kumi na mbili kwa mujibu wa idadi ya mataifa ya Wana wa Israili. Kila njia katika hizo njia ilikuwa na kizuizi cha maji yaliyo nyanyuka kama mlima ulio simama imara.
Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.
Wakasema: Hawafanyi lolote katika hayo. Lakini sisi tumewakuta baba zetu wakiyaabudu mfano wa ibada yetu. Basi sisi tukawafwata kwa waliyo kuwa wakiyafanya.
Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Kwani hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni maaadui kwangu mimi na kwenu. Basi mimi siwaabudu hao. Lakini ninaye muabudu na najijongeza kwake ni Muumba wa walimwengu wote, na Mwenye kumiliki mambo yao, na Mwenye kuwalinda.
Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa,
Ambae ndiye aliye nizua kabla sijawa chochote akaniumba kwa bora ya umbo, na akanitunukia uwongofu wa kunifikishia kwenye mafanikio yangu ya duniani na Akhera.
Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema.
Ibrahim a.s. akasema kwa kuomba: Mola wangu Mlezi! Nitunukie ukamilifu wa ilimu na vitendo, ili nipate kustahili kuubeba Ujumbe wako na hukummu kwa waja wako, na niwezeshe niungane pamoja na kundi la watendao wema.
Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.
Na mjaalie baba yangu astahili msamaha kwa kumwezesha kuwa Muislamu. Na yeye alikuwa kamuahidi kusilimu siku alio achana naye, kwani yeye huyo baba alikuwa ameitupa kando njia ya uwongofu na uwongozi.
Na Pepo itajongezwa, na itakaribishwa pahala pa watu wema. Basi wataiendea wale walio jikinga na ukafiri na maasi, na wakaikubali Imani na ut'iifu duniani.
Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?
Badala ya Mwenyezi Mungu, na mnadai kuwa ati ndio itakuombeeni hii leo? Je! Inakufaeni kitu kwa kukunusuruni, au hata inajifaa wenyewe kujisaidia? Hapana lolote. Kwani wao na miungu yao ni kuni za Moto.
Watatumbukizwa katika Jahannamu kifudifudi, wakipinduliwa pinduliwa mpaka waishie ndani kabisa shimoni, wao na walio wapoteza na wakawatia katika madhambi na upotovu.
Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Pale tulipo kufanyeni nyinyi tulio kuabuduni badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ati ni sawa sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote katika kustahiki kuabudiwa, juu ya kuwa hamjiwezi wala hamfai kwa lolote.
Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
Na hakika katika khabari za Ibrahim zilizo tajwa yapo mawaidha na mazingatio kwa mwenye kutaka mawaidha na akazingatia. Na wala si wengi katika watu wako wanao somewa khabari hizi wenye kuitikia wito wako.
Na Mwenyezi Mungu ametaja khabari za Nuhu kwa kauli yake: Kaumu ya Nuhu iliukanusha Utume wake, wakamrudishia mwenyewe. Kwa kitendo hicho ikawa wamewakadhibisha Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wito wao ni mmoja katika asli yake na lengo lake.
Waliukanusha Utume huu pale alipo waambia ndugu yao Nuhu - ndugu kwa makhusiano ya nasaba si kwa Dini - akiwahadharisha: Hamumchi Mwenyezi Mungu, mkaacha kuabudu wenginewe?
Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!.
Hapana wa kuwalipa kwa vitendo vyao na kazi zao ila Mola wangu Mlezi; kwani Yeye ndiye anaye yajua vyema ya undani wao. Kama nyinyi ni watu watambuzi mngeli tambua hayo.
Wala mimi siye wa kuwafukuza watu wanao uamini wito wangu vyovyote itavyo kuwa hali yao ya ufakiri au utajiri, kwa sababu ati ya kukubalieni nyinyi kwa mtakalo ili ndio mpate kuniamini.
Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri.
Mimi si chochote ila ni Mtume niliye toka kwa Mwenyezi Mungu kuwaonya walio wajibikiwa kwa onyo lilio wazi, kwa ushahidi wa kutenganisha baina ya kweli na uwongo, bila ya farka yoyote baina ya mtukufu na mnyonge. Basi vipi itanifalia mimi kuwafukuza Waumini kwa sababu ya ufakiri wao?
Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha.
Nuhu kuonyesha kushikilia watu wake kuukadhibisha wito wake, alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha! Kuthibitisha kuwa wanastahiki maapizo yake.
Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini.
Basi tuhukumie baina yangu na wao, kwa hukumu ya kuwaangamiza wanao pinga Upweke wako, na wakamkadhibisha Mtume wako! Na niokoe mimi na Waumini walio pamoja nami na adhabu ya uasi wao.
Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
Hakika katika yaliyo simuliwa na Qur'ani juu ya khabari za Nuhu ni hoja ya kuthibitisha ukweli wa Mitume na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na katika watu walio somewa hadithi hizi si wengi walio amini.
Kabila ya A'di ilimkanusha Mtume wao Hud a.s. Na kwa hivyo wakawa ndio wamewakadhibisha Mitume wote, kwa kuwa wito wao ni mmoja katika asli yake na lengo lake.
Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili nikuongoeni mfuate uwongozi, na ni mwenye kuulinda ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Naufikisha ujumbe huo kama alivyo niamrisha Mola wangu Mlezi.
Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?
Je! Mnasimamisha juu ya kila pahala palipo nyanyuka katika nchi jengo refu kwa ajili ya kujifakhirisha, na mnakutana humo kwa mambo ya upuuzi na fisadi? Mwenyezi Mungu Subhanahu anataka kwa haya kuwazindua watende yatakayo wanufaisha, na anawatahayarisha kwa kuacha kwao Imani na vitendo vyema.
Mwogopeni Mwenyezi Mungu katika kutumia nguvu, Na fuateni amri yangu katika ninayo kuitieni. Kwani hayo hakika ndiyo yatakayo kukufaeni na ndiyo yatakayo dumu zaidi.
Kama alivyo kupeni mifugo kama ngamia, na ng'ombe, na kondoo, na mbuzi, na wana wenye nguvu, wakukulindieni mifugo yenu, na kukusaidieni katika shida za maisha.
Mimi nina khofu asije Mwenyezi Mungu akakuteremshieni adhabu kali hapa duniani, na Akhera akakutieni katika Moto wa Jahannamu kwa sababu ya ujabari wenu na starehe alizo kustarehesheni Mwenyezi Mungu.
Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
Basi wakaendelea kushikilia kumkanusha. Mwenyezi Mungu akawafanyia haraka kuwateketeza. Hakika katika hayo aliyo wateremshia Mwenyezi Mungu kina A'di kwa kuwa ni malipo kwa ukanushi wao, ni hoja inayo juulisha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na si wengi katika wanao somewa khabari za A'adi walio Waumini.
Kabila ya Thamud ilimkanusha Swaleh katika Ujumbe wake na wito wake, na kwa hivyo ikawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa asli ya Ujumbe ni moja, na lengo ni moja.
Ewe Mtume! Watajie watu wako, wakati ule kina Thamud walipo ambiwa na ndugu yao kwa uzao na uwananchi, si kwa dini, Swaleh: Hamumwogopi Mwenyezi Mungu, mkamuaabudu Yeye tu?
Hakika mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu kwenu kwa mambo yenye kheri yenu na mafanikio yenu. Na mimi ni mwenye kuuhifadhi Ujumbe huu kama nilivyo upokea kwa Mwenyezi Mungu.
Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
Wewe si chochote ila ni mmoja unaye fanana na sisi kwa ubinaadamu, basi yawaje uwe bora kuliko sisi kwa Unabii na Utume? Na ukiwa wewe ni mkweli katika madai yako basi lete muujiza wa kuonyesha uthibitisho wa Utume wako.
Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.
Saleh akawaambia - alipo pewa na Mwenyezi Mungu ngamia jike kuwa ni muujiza wake: Huyu hapa ngamia jike wa Mwenyezi Mungu, amekutoleeni kuwa ni Ishara. Yeye ana sehemu yake ya maji katika siku moja; siku hiyo msinywe nyinyi. Na nyinyi mna sehemu yenu siku nyengine. Kunyweni siku hiyo.
Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
Basi ikawateketeza adhabu aliyo waahidi Swaleh, wala majuto hayakuwakinga na adhabu ya ukosefu wao. Hakika katika kusimulia kisa chao pana dalili ya kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kuwateketeza makafiri na kuwaokoa Waumini. Na si wengi katika watu wako wenye kuamini.
Lut'i alisema: Nyinyi mnastarehea kuwaingilia wanaume mkaacha wanawake? Kwa hayo anakusudia kuyakanya yale waliyo yazoea ya vitendo vichafu. "Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?" Yaani kazi ya liwat'i, ambayo tangu asli yake ni ukosefu muovu, unao chusha hata kuusikia, kinyume na maumbile, unao mteremsha mwanaadamu chini kabisa. Na lau kuwa unaenea basi huharibu sunna ya kuoa, nayo ni sunna ya maumbile, hata uzazi ukatike na ulimwengu usite kuendelea. Na kwa liwat'i huenea maradhi kama yanavyo enea kwa uzinzi kama tego, kisonono, donda ndugu, maradhi ya ngozi kama ukurutu, na hutokea ishara za kudhoofika nyama za nyuma hata ikawa mtu hawezi kujizuia kutokwa na choo ovyo. Na nyuma kwake mtu huchanua kukawa kama mdomo wa tarumbeta. Na huko nyuma hujaa vijidudu vya maradhi na hivyo humuambukiza mwenye kumuingilia na yeye hivyo vijidudu vikenda mletea maradhi mengine ya njia za mkojo. Na huenda huyo mwenye kufanywa mambo hayo akawa mpumbavu hafai kitu, ikiwa kaanza tangu utotoni. Na huenda akajidai kuonesha ujanadume mwingi kuliko kiasi kwa kutaka kuficha upungufu wake wa uume. (Karibuni imedhihiri kuwa maradhi ya khatari kabisa ya AIDS [Ukimwi] yameenea zaidi sana kwa watendao kitendo hichi na watumiao madawa ya ulevi, ijapo kuwa na wazinzi nao hupata!). Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameukemea ukosefu huu katika Aya kadhaa wa kadhaa, na akabainisha hikima ya Mwenye kuhukumu kwa kuharimisha huku, kwa kusema: " Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume? Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!"
Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!.
Na mnaacha aliyo kuumbieni Mwenyezi Mungu ya kustarehe na wake zenu walio halali yenu? Ama hakika nyinyi ni watu mlio pindukia mipaka ya udhalimu katika kufanya maasi.
Mwenyezi Mungu akamuitikia ombi lake, akamwokoa yeye na wale walio fuata wito wake, kwa kuwatoa wote majumbani mwao wakati wa kuteremka adhabu kuwashukia wenye kukanusha.
Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa.
Na Mwenyezi Mungu aliwateremshia wale watu wapotovu mawe kutoka mbinguni, yakawateketeza. Na ilikuwa mvua ya kutisha kwa wingi wake na namna yake. Basi mvua ovu ya walio kwisha onywa ni mvua hiyo, kwani iliteremka kwa uangamizi mkubwa mno!
Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
Hakika adhabu ile iliyo wateremkia watu wale hapana shaka ni hoja yenye kuonyesha utimilivu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Wala si wengi katika watu wako wenye kusadiki hayo.
Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kusifika kwa rehema iliyo kamilika. Huwapa adhabu watendao dhambi, na huwalipa wema Waumini.
Hichi kisa cha Shuaibu pamoja na Watu wa Al Aykat, Machakani, nao ni msitu wenye miti mizuri, karibu na Madian. Kikundi cha watu waliteremkia hapo na wakakaa. Mwenyezi Mungu akawapelekea Shuaibu kama alivyo wapelekea watu wa Madian. Wakamkadhibisha katika wito wake. Na kwa hivi wakawa wamekanusha risala za Mitume wote.
Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Na mimi kwa hivi kukuongozeni na kukufunzeni sikutakini ujira wowote. Mimi sina malipo kaamili kwa sababu ya kazi yangu ila kutokana na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja.
Shuaibu akawaamrisha kutimiza vipimo kwa ukamilifu wanapo pima, kwani ilikuwa ada yao kupunguza kwa pishi na mizani, kupunguza haki za watu kwa kuwapunja na kuwapimia kasoro.
Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.
Na wewe si chochote ila ni mmoja wetu sawa na sisi kwa utu. Basi vipi ujipe ubora kuliko sisi kwa Utume? Nasi tunaamini kuwa wewe ni mwongo wa kubobea.
Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.
Basi hebu tuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni ikiwa ni katika wasemao kweli kwa huu ujumbe wako! Na chini ya shauri hii kwa hakika pana kila namna ya ubishi.
Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda.
Shuaibu akasema: Mola wangu Mlezi ni Mjuzi, upeo wa kujua, wa maasi yote myatendayo, na adhabu mnayo stahiki. Yeye atakuteremshieni hayo kwa wakati wake alio ukadiria. Na huu ndio hadi ya mwisho wa kumwachilia Mwenyezi Mungu kila kitu, na kuwatisha hao makafiri.
Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.
Lakini wao waliendelea kumkadhibisha. Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa adhabu ya joto kuu mno. Wakawa wanatapa tapa hawana pa kukimbilia. Walipo pata kiwingu cha kuwapa kivuli kukinga mwako wa jua walijikusanya chini yake. Mwenyezi Mungu akawateremshia moto, ukawateketeza wote katika siku ya kitisho kikubwa mno.
Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
Hakika adhabu iliyo wateremkia watu wa Machakani kuwa ni malipo ya uasi wao, ni dalili ya ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na hawakuwa wengi wa watu wako wenye kusadiki.
Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Na hakika hii Qur'ani iliyo tajwa ndani yake visa vya kweli imeteremshwa kutoka kwa Mwenye kuumba walimwengu wote, Mwenye kumiliki mambo yao, na Mlezi wao. Basi khabari zake ni za kweli. Na hukumu yake inatimizwa mpaka Siku ya Kiyama.
Juu ya moyo wako ulio tulia kuihifadhi na kuifahamu, na idhibitike katika moyo wako iwe madhubuti isisahaulike, ili upate kuwaonya wakhalifu kwa adhabu ziliomo ndani yake.
Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?.
Je! Hawa wenye inda wanaikataa Qur'ani na hali wao wanayo hoja inayo onyesha ukweli wa Muhammad s.a.w., nayo ni ilimu ya wanazuoni wa Wana wa Issraili juu ya Qur'ani kama ilivyo katika vitabu vyao?
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Watu wa Makka wameghurika na kuchelewesha kwangu kuwaadhibu, basi ndio wanaihimiza? Anakusudia Subhanahu Aliye takasika kuzisafihi akili zao kwa sababu ya kuhimiza kwao adhabu juu ya kuwaonya na kuwatisha.
Kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mema hakutowakinga hata chembe na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani adhabu ya Mwenyezi Mungu itakuja tu, kama si leo kesho. Wala hapana kheri katika neema ambayo khatima yake ni adhabu.
Qur'ani inakataa waliyo yasema makafiri wa Makka ya kwamba Muhammad anafuata majini, nao ndio wanampa Qur'ani. Qur'ani inasema: Mashetani hawakuiteremsha hii Qur'ani.
Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa.
Basi wewe muelekee Mwenyezi Mungu ukiendelea na usafi wako wa ibada, wala usishughulike na fisadi za madai ya washirikina na mwendo wao muovu. Na hivi kutakiwa Mtume s.a.w. awe na ikhlasi ya namna hii ni wito kwa jamii ya watu waliomo katika umma wake.
Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
Na tegemeza mambo yako kwa Mwenye nguvu, Mwenye uweza wa kuwatenda nguvu adui zako kwa utukufu wake, na kukunusuru wewe na kumnusuru kila mwenye kufanya a'mali yake kwa usafi wa niya.
Hakika Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kusikia dua zako na dhikri zako, ndiye Mjuzi wa kujua niya yako na vitendo vyako. Ni kama kwamba Subhanahu anamwambia: Usichukue taklifu kubwa bila ya kiasi katika mashaka ya ibada, kwani uyatendayo yote nayaona na nayasikia Mimi.
Washirikina walisema: Mashetani ndio wanamsomea Qur'ani Muhammad. Qur'ani ikawajibu: Nikupeni khabari watu gani Mashetani ndio wanawateremkia, na wakawashawishi?
Wanamteremkia kila mwenye kubeba dhambi za namna mbaya kabisa za uwongo, na madhambi ya kuchusha kabisa. Nao ni hao makohani mafisadi ambao tabia zao na tabia za Mashetani ni jinsi moja na zimewafikiana.
Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo.
Hao hutega masikio yao kwa Mashetani, na kwao wakapata mambo ya dhana dhana tu. Na wengi wao ni waongo, na huzidisha tena juu ya kauli walizo zipata kwa Mashetani.
Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata.
Makafiri wanasema: Hii Qur'ani ni mashairi, na Muhammad ni mtungaji mashairi. Mwenyezi Mungu ameyavunja haya kwa kuthibitisha kuwa hakika Qur'ani imejaa hikima na hukumu. Mpango wake unapingana na mpango wa mashairi ambao unategemea juu ya kweli na uwongo. Na amebainisha kwamba hali ya Muhammad s.a.w. inapingana na hali ya watungaji mashairi. Yeye anasema kwa hikima, wao wanasema kwa udanganyifu. Na hii ndiyo hali ya wengi katika watungaji mashairi.
Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.
Lakini walio hidika kwa hidaya ya Mwenyezi Mungu, na wakatenda mema mpaka zikatua katika nafsi zao sifa bora, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi mpaka ikathibiti khofu katika nyoyo zao, hawa basi huyafanya mashairi kama dawa ilio sibu kwa ugonjwa wake. Na hupambana kwa ajili ya kuiwania Dini yao na kusimamisha Haki, inapo kuwa Haki inafanyiwa jeuri. Na walio dhulumu nafsi zao kwa shirki na kumkejeli Mtume kwa mashairi, watatafuta wapi pa kuikimbia shari na hilaki wanayo iendea.
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
ผลการค้นหา:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".