Alif Laam Miim Raa.[1] Hizi ni Ishara za Kitabu. Na yale uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki. Lakini wengi wa watu hawaamini.
[1] Herufi hizi "Alif Laam Miim Raa" na herufi nyinginezo za mkato zilizo mwanzoni mwa sura mbalimbali zinaonyesha hali ya ushindi wa Qur-ani. Kwani, washirikina walipewa changamoto kwayo, lakini wakashindwa na hawakuweza kuipinga, ilhali inajumuisha herufi hizi zinazounda lugha ya Kiarabu. Kwa hivyo, kutoweza kwa Waarabu kuleta kitu kama hicho - ingawa walikuwa ndio watu wenye ufasaha zaidi - kunaonyesha kwamba Qur-ani ni ufunuo (wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziinua mbingu bila ya nguzo mnazoziona, kisha akainuka juu ya Kiti cha Enzi, na akatiisha jua na mwezi, kila kimoja kinakwenda kwa muda maalumu. Anaendesha mambo, na anazipambanua Ishara kwa kina ili mpate kuwa na yakini ya kukutana na Mola wenu Mlezi.
Naye ndiye aliyeikunjua ardhi na akaweka humo milima mathubuti na mito. Na katika kila matunda akafanya jozi, cha kiume na cha kike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa kaumu wanaotafakari.
Na katika ardhi vimo vipande vilivyokaribiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isiyochipua kwenye shina moja, nayo inanyweshwa katika maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yake kuwa bora kuliko mingine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa kaumu wanaotia mambo akilini.
Na kama ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo usemi wao: Je, tukishakuwa mchanga, kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio waliomkufuru Mola wao Mlezi. Na hao ndio watakaokuwa na makongwa shingoni mwao, na hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu.
Na wanakuharakisha ulete mabaya kabla ya mazuri, hali ya kuwa zimekwishapita kabla yao adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye msamaha kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mkali wa kuadhibu.
Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake linamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa kaumu mpaka wabadilishe wao yaliyo katika nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anapowatakia kaumu ubaya, basi hakuna cha kuyazuia wala hawana mlinzi yeyote asiyekuwa Yeye.
Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumsifu, na Malaika pia, kwa kumhofu. Naye hutuma mapigo ya radi na kumsibu kwayo amtakaye. Nao wanabishana kuhusiana na Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye Mwenye adhabu kali!
Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanaowaomba badala yake hawawajibu chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji ili yafike kinywani mwake, lakini hayakifikii. Na maombi ya makafiri hayako isipokuwa katika upotovu.
Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi, nao hawajimilikii manufaa yoyote wala madhara? Sema: Je, kipofu na mwenye kuona huwa sawa? Au je, huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika walioumba kama alivyoumba Yeye, na viumbe hivyo vikawachanganyikia? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja, Mwenye kushinda!
Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji kwa kiasi chake. Na mafuriko yakabeba mapovu yaliyokusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mifano ya haki na batili. Basi lile povu linapita kama takataka tu. Na ama kinachowafaa watu hubakia kwenye ardhi. Hivyo ndivyo anavyopiga Mwenyezi Mungu mifano.
Wale waliomuitikia Mola wao Mlezi watapata mazuri. Na wale ambao hawakumuitikia, hata wangelikuwa na vyote vilivyo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya shaka wangelivitoa kujikombolea! Hao wana hesabu mbaya kabisa, na makao yao ni Jahannamu. Na hapo ni mahali pabaya mno pa kupumzikia!
Je, anayejua ya kwamba yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki ni sawa na aliye kipofu? Hakika wenye akili ya hali ya juu tu ndio wanaokumbuka.
Na ambao husubiri kwa kuutaka uso wa Mola wao Mlezi, na wakasimamisha Swala, na wakatoa katika vile tulivyowapa, kwa siri na kwa uwazi, na wanayaondoa mabaya kwa mazuri. Hao ndio wana malipo ya nyumba nzuri ya Akhera.
Nazo ni Bustani za milele, wataziingia wao na wale waliotengenea miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika watawaingilia katika kila mlango.
Na wale wanaovunja agano la Mwenyezi Mungu baada ya kulifunga, na wanakata yale aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya uharibifu katika ardhi, hao wana laana, na wana Nyumba mbaya.
Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humkunjia kwa kipimo. Na waliufurahia uhai wa dunia. Na uhai wa dunia kwa kulinganisha na Akhera si kitu isipokuwa ni starehe ndogo.
Na wanasema wale waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye, na humwongoa anayerudi kwake.
Ndivyo hivyo tulivyokutuma kwa umma ambao zimekwishapita kabla yao umma nyingine, ili uwasomee yale tuliyokufunulia, na wao wanamkufuru Rahmani (Mwingi wa Rehema)! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi. Hakuna mungu isipokuwa Yeye. Juu yake nimetegemea, na kwake ndiyo marejeo!
Na kama ingelikuwako Qur-ani inayoendeshewa milima, na kupasuliwa kwayo ardhi, na kusemeshwa kwayo wafu, (basi ingelikuwa Qur-ani hii). Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua wale walioamini kwamba lau kuwa Mwenyezi Mungu angetaka, bila ya shaka angeliwaongoa watu wote? Na wale waliokufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa yale waliyoyatenda, au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao, mpaka ije ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.
Je, anayeisimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika! Sema: Watajeni. Au ndiyo mnampa habari ya yale asiyoyajua katika ardhi, au ni maneno matupu tu? Bali wale waliokufuru wamepambiwa njama zao na wamezuiliwa njia ya sawasawa. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, basi hana yeyote wa kumwongoa.
Mfano wa Bustani waliyoahidiwa wacha Mungu, kwa chini yake inapita mito, chakula chake ni cha daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa wale waliomcha Mungu. Na mwisho wa makafiri ni Moto.
Na wale tuliowapa Kitabu wanayafurahia yale yaliyoteremshwa kwako. Na katika makundi mengine wapo wanaoyakataa baadhi yake. Sema: Hakika nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu tu, na wala nisimshirikishe. Kwake Yeye ndiko ninaitia na kwake Yeye ndiko marejeo.
Na ndivyo hivyo tumeiteremsha (Qur-ani hii kuwa ni) hukumu kwa lugha ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya elimu hii iliyokujia, hutakuwa na rafiki yeyote wala mlinzi kando na Mwenyezi Mungu.
Na hakika Sisi tulikwishawatuma Mitume kabla yako, na tukawafanya wawe na wake na dhuria. Na haikuwa kwa Mtume yeyote kuleta ishara isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake iliyoandikwa.
Je, hawakuona kwamba tunaijia ardhi tukiipunguza kutokea nchani mwake? Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hakuna wa kurekebisha hukumu yake, naye ni Mwepesi wa kuhesabu.
Na walipanga njama wale waliokuwa kabla yao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye njama zote. Yeye anajua kile inachochuma kila nafsi. Na makafiri watakuja jua ni ya nani nyumba (njema) ya mwisho (huko Akhera)!
Contents of the translations can be downloaded and re-published, with the following terms and conditions:
1. No modification, addition, or deletion of the content.
2. Clearly referring to the publisher and the source (QuranEnc.com).
3. Mentioning the version number when re-publishing the translation.
4. Keeping the transcript information inside the document.
5. Notifying the source (QuranEnc.com) of any note on the translation.
6. Updating the translation according to the latest version issued from the source (QuranEnc.com).
7. Inappropriate advertisements must not be included when displaying translations of the meanings of the Noble Quran.
搜索结果:
API specs
Endpoints:
Sura translation
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/sura/{translation_key}/{sura_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified sura (by its number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114)
Returns:
json object containing array of objects, each object contains the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".
GET / https://quranenc.com/api/v1/translation/aya/{translation_key}/{sura_number}/{aya_number} description: get the specified translation (by its translation_key) for the speicified aya (by its number sura_number and aya_number)
Parameters: translation_key: (the key of the currently selected translation) sura_number: [1-114] (Sura number in the mosshaf which should be between 1 and 114) aya_number: [1-...] (Aya number in the sura)
Returns:
json object containing the "sura", "aya", "translation" and "footnotes".